Ukawa waibua utata wa uchaguzi Zanzibar katika Bajeti ya Ulinzi

Msemaji wa kambi rasmi ya upinzani wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Juma Hamad Omar akiwasilisha maoni ya kambi hiyo mjini Dodoma jana. Picha: Mwananchi
Msemaji wa kambi rasmi ya upinzani wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Juma
Hamad Omar akiwasilisha maoni ya kambi hiyo mjini Dodoma jana. Picha: Mwananchi

Dodoma. Matumizi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika uchaguzi uliofutwa na kurejewa Zanzibar jana yalitikisa Bunge huku upande wa upinzani ukidai limetumika kuiweka CCM madarakani.

Katika mjadala huo, Mbunge wa Chambani, Yusuph Salim Hussein (CUF), alilazimika kufuta kauli yake kuwa JWTZ limefanya mapinduzi Zanzibar, baada ya Spika, Job Ndugai kumtaka aifute.

Baada ya kufutwa kwa uchaguzi huo na kurejewa, Chama cha Wananchi (CUF) na mgombea wake wa urais, Maalim Seif Shariff Hamad walikataa kushiriki na kutangaza kutomtambua Dk Ali Mohamed Shein kama Rais.

Hoja ya Zanzibar iliibuliwa na Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Juma Hamad Omar akisema kila inapofikia kipindi cha uchaguzi, Zanzibar inakuwa kama iliyovamiwa kijeshi kwa vikosi vya JWTZ, polisi na mgambo kutoka Tanzania Bara kupelekwa huko.

“Kumezuka tabia ya watawala kuitumia JWTZ katika masuala ya ndani ya kisiasa ili kutimiza matakwa yao ya kisiasa. Tabia hii ni mbaya kwa sababu inaliondolea jeshi letu sifa ya maadili,” alisema.

Alisema ulinzi wa raia na mali zao unafanywa na polisi, JWTZ inaweza kuongeza nguvu ikiwa tu nchi iko vitani au kama hali ya hatari imetangazwa. “Tunalaani kitendo cha Serikali ya Muungano kutumia nguvu za kijeshi kutisha wananchi wa Zanzibar na kutumia mwanya huo kuiweka CCM madarakani kwa nguvu,” alisema Omar.

Kambi ya upinzani imesema kulishirikisha jeshi katika mchakato wa kutwaa madaraka ya dola kwa njia za kiujanjaujanja ni hatari na demokrasia inatakiwa iachwe ichukue mkondo wake.

Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alisema Serikali ifahamu kuwa watu wanapokandamizwa sana wanajengewa fikra za kufanya mambo ambayo walikuwa hawayafanyi. “Kwa hiyo unapoona mwenzio ananyolewa wewe tia maji. Kina Al Shabaab, kina Boko Haram hawakuanza hivihivi.

Ni watu walikandamizwa kama inavyotokea Zanzibar. “Haiingii akilini watu wenye tamaa ya mamlaka wanalazimisha kubaki Zanzibar kwa kutumia Jeshi wakati Wazanzibari hawajawachagua,” alisema Mdee huku akishangiliwa na wabunge wa upinzani.

Mbunge wa Chambani ndiye aliyechafua hali ya hewa baada ya kudai kuwa JWTZ ilifanya mapinduzi Zanzibar na kuiweka CCM madarakani. Baada ya kutoa kauli hiyo, Ndugai alimweleza kuwa maneno hayo yanampa tabu, hivyo kumtaka kurekebisha kauli hiyo ili aweze kueleweka.

Alipopewa fursa alisema Oktoba 25, mwaka jana kulikuwa na uchaguzi Zanzibar, wananchi wakaichagua CUF lakini uamuzi wao ukapinduliwa. Alipomaliza kuchangia, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenister Mhagama aliomba mwongozo kuhusu kauli hiyo ya Jeshi kupindua Zanzibar akisema maneno kwamba “JWTZ imefanya mapinduzi” hayana ukweli.

Baada ya maelezo hayo, Spika alimtaka mbunge huyo kufuta kauli yake hiyo, lakini alikataa akisema anao ushahidi wa kituo kwa kituo kuonyesha kwamba CUF ilishinda uchaguzi huo. Hata hivyo, Spika alisimama na kumweleza kuwa alichojibu sicho, kwa kuwa anazungumzia kwamba chama chake kilishinda, lakini kiti kinamtaka afute kauli kuhusu Jeshi kupindua Zanzibar.

Alipopewa nafasi ya mwisho alikubali kufuta kauli yake na Spika akaagiza kauli hiyo ifutwe kwenye kumbukumbu rasmi za Bunge (Hansard). Mbunge wa Mfenesini (CCM), Masoud Ali Hamis, alisema wapo wabunge ambao hawafurahi bila kuizungumza Zanzibar, akisema wanaosema vifaru viliingia mitaani, hawavijui vifaru.

“Tusipotoshe wananchi tukawaambia majeshi sasa yanaingia mitaani. Mimi nilikuwa mwanajeshi. Mazoezi yote ya jeshi yanafanyika porini unaposema vifaru vimeingia mitaani mimi sikuelewi.

“Kama kuna mtu au taasisi yoyote leo inayoweza kumuondosha Dk Shein ifanye, lakini nawaambia Dk Shein atakuwa Rais wa Zanzibar kwa miaka mitano na hakuna mtu wa kumuondoa,” alisema.

Mdee ahoji bilioni za Museveni Katika hatua nyingine Mdee alimtaka Waziri wa Ulinzi na JKT, Dk Hussein Mwinyi kutoa maelezo ya mahali zilipo Sh59 bilioni zilizotolewa na Serikali ya Uganda.

Mdee alisema fedha hizo zilitolewa kama kifuta jasho na Serikali ya Uganda kwa wanajeshi waliopigana vita ya kumuondoa Idd Amin Dada mwaka 1978, lakini fedha hizo ziliyeyuka.

“Tulisema hiki kufuta jasho tutawapa wanajeshi wetu hawa wastaafu lakini miaka saba baadaye mmechikichia na mkwanja wa watu. Naomba leo mtujibu zile fedha zimekwenda wapi,” alisema.

Kubena amzulia jambo Dk Mwinyi Akichangia bajeti hiyo, Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea alivitaka vyombo vya dola kumchunguza Waziri Mwinyi, akidai anajengewa nyumba binafsi na kampuni ya Henan Guoji Industry Investment ya China ambayo pia imeingia mkataba na JWTZ au iko katika mchakato wa kuendeleza kiwanja namba 1255 kilichopo Masaki na itakimiliki kwa miaka 40.

“Mjenzi huyuhuyu ndiye atajenga nyumba ya Dk Mwinyi, huu si mgongano wa kimasilahi? Jeshi letu linaingizwa katika mkataba wa kinyonyaji kwa sababu naye ananufaika,” alisema Kubenea.

Akijibu hoja madai hayo, Dk Mwinyi alisema tuhuma hizo hazina hata punje ya ukweli na zimemsikitisha. Alilitaka Bunge kumtaka Kubenea athibitishe madai yake na iwapo atafanya hivyo atajiuzulu

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s