Siasa za Zanzibar ni hatua moja mbele, kumi nyuma

Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein (kushoto) na aliyekuwa Makamu  wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Shariff Hamad
Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein (kushoto) na aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Shariff Hamad

KWA wale wasioijua Zanzibar ambayo imezungukwa na Bahari ya Hindi, siasa ni kila kitu na imekuwa ikitumika kwenye mzunguko wote wa maisha iwe katika shughuli za kijamii, kiuchumi au kimaendeleo. Hali hii imesababisha kwamba karibu kila siku kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana haipiti bila kusikia tukio la kushangaza au kufurahisha.

Vituko vingi vimekuwa vikiripotiwa Unguja na Pemba katika shughuli za huzuni au furaha kwa mfano mazishi au harusi na shughuli nyingine za kijamii ambapo watu hufarakana na hata kupigana kutokana na tofauti zao za kisiasa.

Lakini tukio la hivi karibuni baada ya mlipuko wa maradhi ya kipindupindu Zanzibar inawezekana ikawa ni tukio kubwa zaidi na kushangaza au kusikitisha baada ya baadhi ya watu kuhusisha kipindupindu na siasa.

“Kipindukipindu hakiwezi kuisha Zanzibar mpaka Maalim Seif apewe nchi kwani maradhi hayo ni pigo kwa kumpora ushindi wake,” hizo ni kauli za baadhi ya wananchi wakati watalamu wa afya walipofika katika maeneo mbalimbali kutoa elimu ya afya kujikinga na kipindupindu.

Ofisa Afya kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, Khadija Hussein, akitoa ushuhuda wa changamoto anazokumbana nazo katika kutoa elimu ya afya kuhusu kujikinga na kipindupindu, anasema baadhi ya wananchi wanahusisha maradhi hayo na siasa jambo ambalo siyo zuri kwa afya na uhai wa binadamu.

Anasema kipindupindu hakichagui wafuasi wa vyama vya siasa, jinsia wala kabila hivyo jamii inapaswa kubadilika na kuachana na fikra potofu ambazo haziwezi kujenga jamii imara.

Anasema wakati walipokuwa wakitoa elimu ya afya ili kujikinga na maradhi ya kipindupindi baadhi ya wananchi ambao wanamrengo mmoja wa chama cha kisiasa walikuwa wakitoa kauli ambazo zilijikita zaidi katika siasa.

“Mtu unampa elimu kuhusu kipindupindu anakwambia kipindupindu hakiwezi kuondoka kwa sababu rais anayeongoza Zanzibar hawamtambui na wengine wanasema kipindupindu hakiwezi kuondoka mpaka Maalim Seif apewe nchi,” anaeleza ofisa huyo.

Anawasihi wananchi wabadilike na siyo kila jambo kuliingiza katika siasa kwani kipindupindu kipo na kinaendelea kuteketeza wananchi kama jamii haijawa tayari kubadilika.

Watalamu wa afya waeleza sababu za kuwapo kwa kipindupindu visiwani hapa na kufafanua kuwa ugonjwa huo haufungamani na masuala ya kisiasa kama baadhi ya watu wanavyofikiria.

Uchunguzi uliofanywa na watalamu hao wa Wizara ya Afya Zanzibar umegundua katika visima mbalimbali vya maji kisiwani Pemba, vina vimelea vya ugonjwa wa kipindupindu.

Ofisa uendeshaji kinga kisiwani humo, Shaib Itibar Mzee, anasema pia visima hivyo vimebainika kuwa na vimelea vyingine vya magonjwa ya kuharisha.

Wizara hiyo imefanya utafiti huo kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwamo mamlaka ya maji Zanzibar (Zawa) na visima 17 kati ya 32 vilivyochunguzwa, vimeonekana kuwa na vimelea hivyo.

Anasema katika uchunguzi huo, maji yanayotoka katika mifereji (bomba), hayakuonekana kuishi wadudu hao.

Anafafanua zaidi kuwa maji ya visima ni hatari kwa matumizi ya binadamu hasa kipindi hichi, kwani wadudu wanaosababisha maradhi ya kipindupindu na mengine ya kuharisha, wamefanya makazi yao humo.

“Wizara inaandaa mikakati mbalimbali ya kukabiliana na tatizo la kipindupindu, ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kutia dawa katika maji au kuyachemsha na kuyaweka katika sehemu salama,” anasema Ofisa huyo.

Aidha, aliwataka wananchi kudumisha usafi katika maeneo yao, kwani kinyume na hivyo maradhi hayo hayawezi kuondoka kwa haraka.

Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dk. Mohammed Dahoma, anasema ili ugonjwa wa kipindupindu umalizike inategemea zaidi maamuzi ya familia na jamii kwa jumla kukubali kubadilika.

Anasema desturi potofu na tabia za wananchi zinachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa maambukizi ya kipindupindu Zanzibar.

Dk. Dahoma anawataka waandishi wa habari kutoa elimu zaidi kwa jamii ili wajue sababu zinazochochea ugonjwa huo na njia za kujikinga.

Anasema bado wananchi wanakuwa wagumu kubadili mfumo wao wa maisha licha ya juhudi zinazochukuliwa na Jumuiya za kimataifa, taasisi za Serikali na binafsi pamoja na vyombo vya habari.

“Bado watu wanaishi katika mazingira machafu, wengine hawana vyoo na wapo hawataki kuyatibu maji ya kunywa, mambo yanayochangia mambukizi ya kipindupindu,” anasisitiza Dk. Dahoma.

Akitoa takwimu ya maradhi ya kipindupindu tokea yalipoanza mwezi Septemba mwaka jana, alisema zaidi ya wananchi 3,700 wameugua maradhi hayo na 46 kati yao wamefariki na Wilaya ya Magharibi inaongoza kwa kutoa wagonjwa wengi zaidi.

Aidha alisema imebainika kuwa Nyumba 150 katika Wilaya ya Magharibi Unguja hazina vyoo, hali ambayo imechangia mripuko wa maradhi ya kipindupindu hasa wilayani humo.

Idadi hiyo imefahamika baada ya zoezi lililofanywa na wizara ya afya kukagua nyumba 303 za Wilaya hiyo.

Dk. Mohammed Dahoma, alieleza kuwa kutokana na hali hiyo, wakazi wa nyumba hizo wanajisaidia maeneo yasiyo salama kwa afya zao.

Anasema sababu hiyo ndiyo inayoyafanya mazingira katika maeneo mengi ya wilaya hiyo kuwa machafu.

Aliyataja baadhi ya mitaa ambayo nyumba zake nyingi hazina vyoo kuwa ni Kihinani, Chuini, Daraja bovu na Kinuni ambayo ni maeneo baadhi ya wakazi wake wanaohusisha kipindupindu na siasa.

Mkurugenzi huyo anasema bado juhudi mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa na Serikali na watu binafsi kuhamasisha jamii kujikinga na maradhi hayo.

Hata hivyo, aliwasisitiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo ambao ni hatari ili usije ukaleta maafa.

Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, anasema wakati wa siasa umekwisha na wananchi wanapaswa kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo na kuchukua tahadhari ya kipindupindu kwani kasi imeongezeka.

Alitoa takwimu kwamba watu 56 wameshafariki dunia tangu kilipoanza kipindupindu Septemba mwaka jana hadi sasa; na aliwanasihi wananchi kufuata maelekezo ya serikali na watalamu wa afya katika kuimarisha usafi wa mazingira.

“Lazima kuzingatia nasaha zinazotolewa na watalamu wa afya lazima kuimarisha usafi, kuchemsha maji ya kunywa au kuyaweka dawa, tusifanye biashara za chakula tukifanya hivyo kipindupindu kitachelewa kutoka,” alisema.

Aliwataka wananchi kushirkiana na serikali na kuchukua hatua zote kupambana na janga la maradhi ya kipundupindu kwa kufuata maelekezo ya watabibu kwani ugonjwa huo unapoteza nguvu kazi ya Taifa.

Tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana Wazanzibari wamegawika pande mbili na upande mmoja ukionekana kutoridhika na hatua ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta uchaguzi huo na kisha kutangaza uchaguzi mwingine wa marudio ambao ulifanyika Machi 20, mwaka huu na CUF kususia uchaguzi huo.

Hali hiyo imesababisha ufa kati ya wafuasi wa CUF na CCM, ambavyo ndivyo vyama vyenye upinzani mkubwa Zanzibar kiasi cha kufikia hatua ya kutoshirikiana katika maziko, harusi, shughuli za kibiashara na shughuli za kiserikali.

Chanzo: Nipashe

 

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s