Mzimu wa Uchaguzi kuitafuna Zanzibar


Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein

Na Enzi T. Aboud – Imechapwa 25 April 2016

MZIMU wa ubaguzi kwa misingi ya rangi, mtu alikotoka, kuzaliwa na uchama wa vyama mfu vya kale, vya upinzani; Hizbu (ZNP) na chama cha watu wa Unguja na Pemba (ZPPP), sasa unakitafuna Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar.

Baadhi ya makada wa CCM na wazee mashuhuri wa chama hicho wamesisitiza kukisafisha chama chao, lakini wakiwa na chembe za ubaguzi zinaoonekana dhahiri.

Katika kutekeleza zoezi hilo, makada hao wameapa kuwaondoka ndani ya chama wanachama wanaowaita “wasaliti,” ambao wanahusishwa, kwa njia moja ama nyingine na vyama hivyo vya upinzani.

Ma-Hizbu na Ma-CUF, kama wanavyoitwa ndani ya chama hicho, wanatuhumiwa kukihujumu na pia kuihujumu serikali yake ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Serikali hiyo iliyoundwa hivi karibuni kwa mbinde na kususiwa na CUF na vyama vingine, imo katika majaribio makubwa ya kiuongozi kutokana na kutengwa na vyama vyote hivyo vya upinzani.

Kama hilo halitoshi, Rais Ali Mohamed Shein amenyooshewa kidole na baadhi ya makada wa CCM wenye msimamo mkali kwa hatua yake ya kumteuwa Hamad Rashid, kiongozi wa chama kidogo cha upinzani (ADC) kuwa waziri wa kilimo. Pia rais huyo aliwateua viongozi wawili wengine; Said Soud wa chama cha wakulima (AFP) na Juma Khatibu wa chama cha Tadea, ambao wamewateuliwa kuwa mawaziri wasiokuwa na wizara maalum.

Makada hao wa CCM wanapingana waziwazi na uteuzi huo wa viongozi wa upinzani, wakidai kuwa hawatamsaidia rais kutokana na misimamo yao ya kupinga sera za CCM na Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964.

Wamebainisha kuwa Hamad Rashid alifukuzwa CCM miaka ya 80 pamoja na wenzake saba, akiwemo Maalim Seif Sharif Hamad walipobainika kuwa hawakubaliani na sera za CCM na muundo wa Muungano wa serikali mbili.

Pia viongozi hao walituhumiwa kujikita zaidi katika siasa za upinzani za kuitetea Zanzibar kupata hati zake ndani ya Muungano na kuwa mamlaka kamili.

Aidha, Rais Shein analalamikiwa kwamba hakufanya uchunguzi wa kina au washauri wake hawakumpa ushauri ipasavyo katika hatua za mwanzo kabla ya kufanya uteuzi wa mawaziri wa serikali yake mpya.

Inaelezwa kwamba CCM Zanzibar imekasirishwa na uteuzi wa Moulding Castico kuwa waziri kwa maelezo ya kutokuwa mzaliwa wa Zanzibar na siyo raia wa kuzaliwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Imedaiwa kuwa Moulding ni raia wa kuzaliwa nchini Zambia ambaye aliwahi kuolewa na hayati Joseph Castico, Mzanzibari aliyefariki dunia miaka ya 90 na aliwahi kuwa Mkurugenzi wa mila, utamaduni na sanaa katika wizara iliyokuwa ya habari wakati wa utawala wa Rais (mstaafu) Dk. Salmin Amour na Dk. Amani Karume.

Katka mazingira hayo ya siasa za majungu, chuki za ubaguzi na kutuhumiana kwa mambo yasiyokuwa na tija ndani ya CCM, imethibitika kuwa hali hiyo ya udhaifu imeanza kuzoeleka na kuota mizizi.

Mbali na Moulding Castico kutiliwa shaka kwa kutuhumiwa kuwa siyo raia wa Tanzania, pia mwingine aliyenyooshewa kidole kwa tuhuma kama hizo ni spika mpya wa Baraza la Wawakilisha, Zubeir Ali Maulid.

Huyu anatuhumiwa kwamba siyo raia wa Tanzania, bali ni mzaliwa wa Uganda.

Kushuka na kupanda kwa Moulding Castico katika ulingo wa siasa Visiwani, kumetokana na mazingira ya majungu ya kisiasa na kupanda kwake kumetokana na ushiriki wake mzuri katika harakati za kijamii hasa za kuwapigania wanawake na uwezo wake wa kisiasa.

Kwa mara ya kwanza Moulding Castico aliteuliwa kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na baadaye kuteuliwa kuwa Katibu wa Mkoa wa Arusha.

Nafasi nyingine alizowahi kushika katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni mkurugenzi katika wizara iliyokuwa ya habari, mila na utamaduni wakati wa uongozi wa Dk. Salmin Amour, ingawa uteuzi wake ulitenguliwa baada ya kubainika kwamba hakuwa Mzanzibari na hakuwa raia wa Tanzania. Kwa miaka yote hiyo aliyoishi Zanzibar alikuwa ni mke wa hayati Joseph Costico aliyekuwa Zanzibar na raia wa Tanzania wa kuzaliwa.

Imekuwa ni kawaida kwa Zanzibar kuwapokea wageni na kuweza kuishi nchini bila kufuatiliwa kisheria na hata kufikia kushika nafasi za juu katika uongozi wa chama cha siasa hata katika nafasi za uongozi katika Serikali.

Utamaduni huu wa kutojali kuwahakiki wageni wanapoingia Visiwani, hasa wale wanaotoka nchi za jirani za Afrika Mashariki kama vile Kenya, Uganda, Zambia na Malawi, imekuwa ni jambo la mazoea.

Mwanya huo umekuwa ukitumiwa miaka mingi, hata baadhi ya viongozi wa kundi la kamati ya watu kumi na nne (14) waliofanya Mapinduzi mwaka 1964, yaliongozwa na John Okello aliyejivika cheo cha Field Marshall, alibainika kuwa ni raia wa Uganda.

Aidha, mjumbe mwingine wa kamati hiyo alikuwa Egunas Injin, raia ya Kenya.

Wakati CCM Zanzibar kinaishi kwa hofu ya mzimu wa chama cha kale, kilichokufa cha ASP, CCM Bara inasumbuliwa na hofu inayotokana na Katiba mbovu ya Muungano, inayozua maswali mengi kuliko majibu kuhusiana na uhalali wa Muungano wenyewe na namna ya kutoa fursa kwa vyama vyengine vya upinzani kwa upande wa Zanzibar.

Swali linakuja hapa- “je kama chama cha CUF kingeshinda uchaguzi wa mwaka jana wa Oktoba 25 na kiongozi wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Rais wa Zanzibar na Dk. John Magufuli kuwa Rais wa Tanzania, hali ya kisiasa ingekuwaje kwa vyama viwili tofauti kutawala sehemu mbili tofauti ya Tanzania?

Kinachoonekana sasa Wazanzibari bado wanabaguana kwa misingi ya vyama vya siasa vilivyo hai vya CCM na CUF na vyama mfu vya ASP, ZNP na ZPPP.

Fikra hovyo za makada wa CCM zilizojikita katika ndoto hewa za kurudi utawala wa sultani wa kiarabu nazo pia zinajumuisha matatizo ya kudumu ya kisiasa yasiyoweza kutatuka.

Hii pia imeonekana katika siasa zilizojitokeza na kuvunjwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ambayo inahusishwa na utawala wa kisultani.

Njia pekee ya kuondokana na mzimu wa vyama mfu katika utawala wa Zanzibar na katika siasa za mfumo wa vyama vingi ndani ya visiwa hivyo ni kufanya juhudi za kurudisha maelewano wa vyama vikubwa hivi viwili vya CUF na CCM na kutoa wigo mpana wa kugawana madaraka.

Lakini juhudi hizo zitaweza kufanikiwa pale tu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hasa Rais Magufuli kuziangaza upya haki za Zanzibar na kuwajali Wazanzibari katika kusimamia uhuru na haki ya Zanzibar

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s