Dk. Mashinji: Muungano unakabiliwa na mgogoro wa aina mbili

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Vincent Mashinji
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Vincent Mashinji

APRILI 04, mwaka huu, Rais John Magufuli, alitangaza kuahirisha shamrashamra za maadhimisho ya siku ya Muungano na kuelekeza fedha zilizokuwa zimepangwa kwa ajili ya vinywaji, vyakula, gwaride, halaiki na burudani mbalimbali zitumike kuanzisha upanuzi wa barabara ya uwanja wa ndege Mwanza.

Fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya shughuli hizo zilikuwa zaidi ya Sh. bilioni mbili. tangazo hilo la mkuu wa nchi, lilitekelezwa jana ambayo ilikuwa siku ya mapumziko kama kawaida, lakini isiyo na shamrashamra zilizozoeleka.

Jana, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulitimiza miaka 52 tangu nchi hizo mbili zilipoungana Aprili 26, 1964.

Akizungumzia Muungano, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Vincent Mashinji, anasema unakabiliwa na mgogoro wa aina mbili ambao ni wa kiitifaki na kimantiki. Aidha, anasema unakabiliwa pia na utashi wa dhati wa kisiasa katika kutafuta suluhu ya matatizo yaliyopo.

Anasema kiitifaki, Muungano hauonyeshi mpaka wa Rais wa Zanzibar wala wa Tanzania Bara, akitolea mfano uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu.

Anasema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye ndie Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama, alikuwa ana uwezo wa kutatua mgogoro wa uchaguzi, lakini haikufanyika hivyo.

Anasema Rais John Magufuli, aliombwa ashughulikie tatizo la Zanzibar kama kiongozi wa nchi, lakini hakufanya hivyo kwa maelezo kuwa hana mamlaka wakati yeye ni kiongozi wa nchi.

Anasema: “Kama Mkuu wa nchi, inashangaza kuona kwamba anaweza kuingilia uchaguzi wa jiji la Dar es Salaam, lakini anashindwa kushughulikia tatizo la Zanzibar.”

Anasema wakati Rais Magufuli akiingilia uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam alikuwa anajua kuna sheria, hivyo hana sababu za msingi za kutoshughulikia mgogoro wa Zanzibar kwa kisingizio cha kukosa mamlaka.

Anasema kiitifaki, Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini kimantiki, visiwa hivyo vinaonekana kama ni nchi huru yenye mamlaka kamili.

Anasema ndio maana rasimu ya pili ya Katiba ilipendekeza Muungano uwe wa serikali tatu ili kuondoa mgongano huo, lakini Chama Cha Mapinduzi (CCM), kiliyakataa mapendekezo ya wananchi wakati wa Bunge Maalum la Katiba.

“Kumekuwa na ukiukaji mkubwa wa Katiba ya Zanzibar pamoja na Katiba ya Jamhuri…na kwa historia ya Zanzibar tangu uchaguzi wa mwaka 1995, uwezekano wa kushinda kwa asilimia 91 haupo,” anasema Dk. Mashinji.

Anasema kasoro hizo ndizo zilizosababisha wadau mbalimbali wakiwamo washirika wa maendeleo kukosoa uchaguzi wa marudio na iliposhindikana, walisusia kuchangua bajeti ya serikali.

Anasema wakati serikali ikiwakejeli washirika wa maendeleo ikiwamo Jumuiya ya Ulaya na Marekani, ambao wamesusia bajeti; taarifa alizonazo ni kwamba imeingia makubaliano ya kupata ufadhili wa bajeti kutoka China, ambayo amesema imetoa masharti magumu zaidi.

Anasema sharti mojawapo ni kuilazimisha serikali iwalipe kwanza makandarasi wa Kichina wanaoendesha shughuli zao nchini, akisema kuwa huo ni ubaguzi kwa kuwa hata makandarasi wa kizalendo wanaidai serikali.

“Huu ndio unaoitwa ukoloni wa kiuchumi. Lakini kwa nini tunawakejeli washirika wetu ambao sharti lao ni jepesi la kututaka tuheshimu maoni ya wananchi wetu kupitia sanduku la kura…tunakubali sharti linaloleta ubaguzi,” anasema.

Dk. Mashinji anaongeza kuwa: “Tunapodaiwa na nchi moja (China), ni hatari kwa usalama wan chi yetu. Lakini pia tunakoelekea hatukujui kwa sababu hatujui wale wanaokandamizwa kule Zanzibar watajitetea kwa njia gani.”

Anasema kwa hali ya Muungano ilivyo sasa ni lazima viongozi wa kisiasa kutafuta njia za kuwaleta wananchi wa pande zote pamoja kwa kuheshimu maoni yao na kutenda haki kwa serikali zilizopo madarakani.

Aidha, anasema nchi sasa inaongozwa kwa matamko ya viongozi badala ya misingi ya kisheria, kanuni na taratibu.

Anasema kinachotakiwa kufanyika ni viongozi kujenga utashi wa kutafuta suluhu ya kweli ya matatizo yaliyopo na kwamba njia pekee ya kushughulikia tatizo ni mazungumzo na siyo kukwepa ukweli.

Kero Viporo

Wakati Muungano ukitimiza miaka 52, bado kuna kero sugu ikiwamo ile ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asili ambayo imekuwa ikiibua mjadala mpana kwenye mikutano hasa ya Bunge.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia ni suala la Muungano. Hata hivyo, taarifa zinaonyesha kuwa suala hili limeondolewa kwenye orodha ya mambo ya Muungano na kinachofanyika sasa ni namna ya kugawana mapato ya rasilimali ya mafuta na gesi asilia itakapopatikana.

Ili kutatua kero hiyo, kinachofanyika ni kuchambua ripoti ya mshauri mwelekezi ambaye ni kampuni ya AUPEC wa Uingereza na kwa kwamba kwa kuwa kampuni ya AUPEC ilikamilisha kazi hiyo na kuwasilisha mapendekezo kwa SMZ na SMT ambazo zinasubiri maelekezo kutoka ngazi za juu za uongozi ili kupatiwa ufumbuzi.

Aidha, iliundwa timu ya wataalamu ikiongozwa na Wanasheria Wakuu wa SMT na SMZ ili kuandaa Utaratibu wa Mapendekezo ya Sera na Sheria zitakazoruhusu SMZ iendelee na matayarisho ya Utafutaji wa Mafuta na Gesi asilia.

Kero nyingine ni taarifa ya mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha ambayo ilifanya tafiti mbalimbali na kutoa mapendekezo kwa Serikali zote mbili (SMT na SMZ) mwaka 2006. Mapendekezo hayo yanajumuisha vigezo vya kuchangia gharama na kugawana mapato ya Muungano.

Hata hivyo, SMZ imekamilisha kupitia mapendekezo ya Tume ya pamoja ya fedha juu ya uchangiaji wa gharama na mgawanyo wa mapato ya Muungano kutoka ngazi ya Wizara hadi Baraza la Mapinduzi, japokuwa utekelezaji haujaanza.

Kero nyingine ambazo hazijapatiwa ufumbuzi ni mgawanyo wa mapato na usajili wa vyombo vya moto.

Kazi ya kuanza kushughulikia kero za Muungano ilianza mwaka 2006, Serikali chini ya Rais Jakaya Kikwete, kuanzisha Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ chini ya uwenyekiti wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Taarifa zinaonyesha kuwa kuanzia mwaka 2006 hadi 2011 jumla ya hoja kumi na tano (15) ziliwasilishwa na kujadiliwa na Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ.

Kati ya hizo, hoja kumi na mbili (12), zimepatiwa ufumbuzi na hoja tatu (3) zipo katika hatua mbalimbali ya kutafutiwa ufumbuzi.

Chanzo: Nipashe

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s