Uhasama wa kisiasa wakwamisha maziko

Uhasama wa kisiasa wakwamisha maziko
Kwa ufupi

Wazikaji watunishiana msuli kuzuia msikiti usitumike kuswalia maiti

Pemba. Ubaguzi unaoendelea visiwani hapa kutokana na makovu ya uchaguzi mkuu uliopita, juzi ulichelewesha kwa saa kadhaa maziko ya mwanachama wa CUF, Achia Khatib wa Kijiji cha Wingwi Mjini wilayani Micheweni, baada ya msikiti uliokuwa utumike kuswalia mwili huo kufungwa.

Akizungumza na gazeti hili jana, mmoja wa wanafamilia aliyejitambulisha kwa jina la Said Omar Said, alidai hali hiyo ilitokea baada ya mtoto wa marehemu, Abdalla Kombo ambaye ni Mwenyekiti wa CCM kufika kijijini hapo kwa ajili ya kumzika baba yake.

Alisema wanakijiji waliojitokeza kuja kumzika mzee huyo walisema hawako tayari kushiriki maziko hayo hadi mtoto huyo atakapoondoka mahali hapo.

“Unajua mzee wetu alikuwa mfuasi wa CUF, lakini sasa mtoto wake mkubwa ni mwanaCCM na ni kiongozi, waliofika mazikoni pale wengi ni wafuasi wa CUF hawakutaka mwana CCM yeyote ashiriki msiba ule,” alidai ndugu huyo aliyeonekana kusikitikia kitendo hicho.

Hata hivyo, Sheha wa Shehia ya Mjini Wingwi, Sheikh Yussuf Hamad alisema wananchi hao walitaka pia kuzuia makaburi yasitumike kumzika marehemu, lakini Serikali ya kijiji ililazimika kuingilia kati. “Huu msiba uligubikwa na visa tele, mtoto mmoja wa marehemu aliamua naye kuficha sindano ya kushonea sanda na kuificha wakati kazi ya ushonaji wa sanda hiyo ukiendelea, washonaji walilazimika kwenda kuazima sindano zingine vijiji jirani vya Micheweni na Majenzi ambako walitoa pia na kitanda cha kubebea mwili,” alisema Sheha huyo.

Imamu wa Msikiti wa Ijumaa katika Shehia hiyo, Bakar Abdallah alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, alikana kuufunga msikiti na hata taarifa za kuvunjwa kufuli la msikiti huo alidai hajazisikia.

Kamati ya Ulinzi na Usalama ikiongozwa na Mwenyekiti wake Abeid Juma Ali, ilifika kwenye msiba huo na kuzungumza na wazee waliokuwapo msibani na kuamua kuvunja kufuli na kuruhusu mwili uswaliwe.

Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia mkuu wa wilaya hiyo, alilaani kitendo hicho na kuwataka wananchi kuacha kubaguana katika shughuli za kijamii.

Pia, alikemea nyumba za ibada kutumika kwa masuala ya kisiasa na kuahidi kulitafutia ufumbuzi suala hilo kwa kukutana na mashekhe na maimamu wa misikiti yote wilayani hapa.

Chanzo: Mwananchi

One Reply to “Uhasama wa kisiasa wakwamisha maziko”

  1. vitendo hivi kwa ndugu zetu wa visiwani ni kawaida. ubaguzi kwao ni sehemu ya maisha yao. Tangia ukoloni walikua wakibaguana kati ya waswahili na Waarabu.. leo ni kama mwendelezo tu wa ubaguzi kwa kisingizio cha tofauti za kisiasa. Mungu awarekebishe

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s