Mafuriko yaua, kubomoa nyumba Manispaa Z’bar

Mvua Znz

Kamanda Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Mkadam Khamis, alimtaja mtu aliyefariki dunia kuwa Salim Mohamed, mkazi wa Migombani ambaye aliangukiwa na ukuta nyumbani kwake alfajiri kuamkia jana.

Kamanda Mkadam alifafanua kuwa Salim alitoka nje ya nyumba yake kuangalia mazingira ya mvua zilizokuwa zikinyesha, lakini ghafla ukuta ulibomoka na kumuagukia na kusababisha kifo chake.

Alisema katika mkoa wake, familia nyingi zimepoteza makazi yao. Hata hivyo, alisema tayari serikali imeamua kufungua kambi ya muda ya kuwahifadhi waathirika katika Shule ya Msingi Mwanakwerekwe C.

“Tunaendelea kukusanya taarifa, lakini mtu mmoja amefariki dunia na familia nyingi hazina makazi baada ya nyumba zao kukumbwa na mavuriko na nyingine kubomoka,” alisisitiza Kamanda Mkadam.

Aliongeza kuwa barabara kuu ya kuingia na kutoka mjini katika eneo la Mwanakwerekwe, imeufungwa kwa sababu za kiusalama baada ya mkondo wa maji kujaa na magari kushindwa kupita katika eneo hilo la daraja.

Alisema polisi imewataka wataalam wa miundombinu kushirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Magharibi Unguja kufanya ukaguzi wa daraja linalopitisha maji katika mkondo huo kabla ya kuanza kutumika ili kufahamu usalama wake.

Nyumba nyingi zilizoathirika na mafuriko ya maji zile zilizojengwa katika vyanzo vya maji na mabondeni.

Maeneo yaliyoathirika zaidi ni Kinuni, Migombani, Mpendae Chumbuni Mwakwerekwe, Kwahani na Mtoni Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Wakizungunza na Nipashe kwa nyakati tofauti, baadhi ya waathirika katika eneo la Chumbuni, walisema mafuriko ya hayo yaliyanza kutokea saa 9:00 usiku wa kuamkia jana na kuwapa wakati mgumu wa kuokoa mali katika nyumba zao.

Rukia Omar, mkaazi wa Chumbuni, alisema wanahitaji msaada wa vifaa yakiwemo mahitaji ya watoto ya shule, vifaa vya ujenzi kama saruji pamoja na vyakula.

Alisema wamepoteza vitu vingi yakiwamo magodoro, vyombo vya nyumbani na hadi kufikia jana, walikuwa hawafahamu sehemu ya kuishi pamoja na serikali kufungua kambi ya kuwahifadhi.

“Mpaka sasa sifahamu pakulala nikiwa na watoto 10, vitu vingi vya matumizi ya nyumbani vimepotea,” alisema Rukia.

Kwa upande wake, Masoud Mohamed Abdallah, mkazi wa Chumbuni, alisema msaada wa haraka unahitajika kutoka serikalini kwa wazee na watoto baada ya makaazi yao kuathiriwa na mafuriko hayo.

Alisema nyumba nyingi katika eneo hilo zimebomoka na watu wengi walipoteza mali baada ya kushindwa kuokoa kutokana na mazingira ya mafuriko hayo kutokea majira ya usiku.

Hafidh Haji Othman, mkazi wa Chumbuni, aliomuomba Rais wa Zanzibar, Dk, Ali Mohammed Shein na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli, kuwasadia watu walioathirika kutokana na mazingira magumu wanayoishi.

Hafidh aliitaka serikali iwapatie hifadhi maalum waathirika kutokana na nyumba zao kubomoka wakiwa na familia wakiwamo watoto.

Mafuriko hayo pia yameathiri nyumba ya Sheha wa Chumbuni pamoja na vyoo kuathirika huku ugonjwa wa kipindupindu ukiripotiwa kuwa umeua watu 34 na 2,705 kuugua tangu kuibuka Septemba, mwaka jana.

Mbunge wa Jimbo la Chumbuni, Ussi Salum Pondeza, alisema katika jimbo lake, nyumba 360 zimeathirika na familia 100 zimehamishwa kutokana na mafuriko hayo.

Alisema mafuriko ya mwaka huu makubwa na yameleta madhara makubwa kwa wananchi wa shehia mbili katika jimbo hilo ikiwamo Shehia ya Mwembe Makumbi na Chumbuni, lakini hadi jana walikuwa wakishirikiana na serikali kusadia wathirika katika mkasa huo.

Hata hivyo, katika maeneo ya Mpendae, Chumbuni na Kinuni, kumelalamikiwa kuathiriwa na vitendo vya wizi baada ya vibaka waliokuwa wakijifanya kusadia kuokoa mali za waathirika laki wakatoweka na mali zao.

“Tumepoteza mali nyigi, lakini vitu vingi vimechukuliwa na vijana ambao tulidhani wasamaria wema kumbe wezi hasa vijana watumiaji wa dawa za kulevya hawana utu wa ubinadamu,” alisema Aisha Seif, mkazi wa Mpendae.

Matatizo ya mali kuibiwa baada ya kujitokeza mafuriko hayo pia yamejitokeza huko katika mji mdogo wa Kinuni Mkoa wa mjini Magharibi Unguja.

Mafuriko hayo yanatokea huki Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa katika mpango wa kupima viwanja 580 kuwapatia watu wanaoishi mabondeni na katika vyanzo vya maji kabla ya kuhamishwa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud, alisema familia 300 zinatarajia kunufaika na mpango huo.

Alisema tathmini inayoendelea kufanyika imebainika kuwa wathirika wakubwa wa mafuriko kila mvua inaponyesha watu waliojenga katika vyanzo vya maji pamoja na katika mikondo ya kupitisha maji mabondeni.

Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa urasimu wa upatikanaji wa viwanja vya kujenga nyumba za makazi, umeathiri kwa kiwango kikubwa ramani ya mipango miji na wananchi wanyonge kuamua kujenga mabondeni na katika vyanzo vya maji na hivyo kuhatarisha maisha yao kila mvua zinaponyesha.

Chanzo: Nipashe

One Reply to “Mafuriko yaua, kubomoa nyumba Manispaa Z’bar”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s