Bado tuna safari ndefu


Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Issa Shivji

Na Awadh Ali Said

Baada ya kumsoma Prof. Issa Shivji katika makala iliyochapishwa hivi karibuni katika Gazeti la Raia Mwema, nimezidi kuthibitisha ile dhana kuwa Tanzania ina nakisi kubwa ya mchango wa Wanazuoni katika kuleta MABADILIKO NA USTAWI mwema katika jamii yetu. Wengi wao (ukiacha baadhi yao ambao wamejipambanua kuwa wanaitambua dhima yao) huwa wanastaajabisha kwa jinsi wanavyokuwa ni sehemu ya kuunga mkono uovu kwa mtindo wa aina yake. Na moja ya njia zao ni kuelekeza lawama kwa MABEBERU kwa kila jambo linaloashiria kushindwa kwetu. Wanazuoni wetu hawa wamekuwa wakiendeleza tabia ya makusudi ya kujaribu kutuondoa kwenye tatizo la msingi na ambalo ndio kiini cha kushindwa kwetu na kutupiga mzubaisho kuwa kiini cha matatizo yetu ni UBEBERU.

Ukweli ni kuwa matatizo yetu mengi sana ni matokeo ya tabia, nyenendo na udhaifu wetu wenyewe katika kujipangia na kujiendeshea mambo yetu . Badala yake Wasomi wetu hao wamekuwa wabunifu stadi wa kutuelekeza pahala pa kurushia lawama zeru (UBEBERU ); na kwa kufanya hivyo, sio tu kwa madhumuni ya kunusuru TAWALA zetu ambazo ndio khasa zinazostahiki lawama, bali kutufanya tuzionee huruma na tuamshe hamasa za uzalendo. Ni kama mtu anayeamua kufanya mambo kinyume na maamrisho ya Dini yake, halafu akamsingizia IBILIS. Kwa hivyo, IBILIS/BEBERU ndio inayotumika kama sababu au kinga ya kushindwa kwetu?

Kwa mfano, hebu tuchukuliye hili suala la MCC. Kama tutaliangalia kwa makini suala hili, tunaweza kujiuliza kuna ubeberu gani hapa? Aliyevuruga mambo ni BEBERU au Mzee JECHA na wenzake? Profesa wetu kakwepa kwa makusudi kabisa kugundua kiini cha kadhia hii. Hio ndio aina/mtindo wa mzubaisho wanaoutumia Wasomi wetu hao daima. Ndugu zetu “tuliowapa” madaraka wanafanya ufisadi uliokithiri, wanakandamiza demokrasia, wanavunja haki za binadamu, wanaingia mikataba mibovu, kulindana, upendeleo, wizi wa wazi wazi, upindishaji mambo, ukosefu wa nidhamu, almuradi mambo mchafukoge. Matokeo yake, nchi haina maendeleo, huduma za kijamii ziko duni – halafu, ati unaambiwa kuwa tatizo ni UBEBERU.

Kazi kubwa ya Wanazuoni wetu hawa ni kuenzi na kuwalinda WATAWALA; na pale wanapoamua kukosoa, basi hukosoa baada ya miaka 30 ya MTAWALA kuondoka; huwaoni wala huwasikii kusimama kidete kupaza sauti zao wakati ule ambapo mambo yako motomoto yanaharibika.

Kwa kweli, tuna safari ndefu.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s