Jecha aacha vumbi Zanzibar

jecha

Dar es Salaam. Hatimaye Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ameshaapishwa na sasa ameshaanza kutekeleza majukumu yake ya kipindi cha pili, lakini kilichoacha gumzo kubwa ni vumbi lililobakia nyuma na sura mbili za mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha.

Jecha alifuta matokeo ya uchaguzi wa rais wa Zanzibar, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani Oktoba 28, 2015 siku ambayo alitakiwa atangaze mshindi wa urais. Utoaji wa tamko hilo ulikuwa wa kipekee; Oktoba 27 hakuonekana kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Bwawani ambako alikuwa akitangazia matokeo hayo huku wasaidizi wake wakiendelea kuyatangaza, hakuonekana tena Bwawani siku iliyofuata.

Badala yake alionekana kwenye kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) akitangaza kufuta matokeo hayo. Uamuzi huo umeacha kilio na furaha, CUF ikiwa imesusia uchaguzi na CCM ikifurahia baada ya kupata ushindi wa viti vyote vya Pemba, ambako ni nadra chama hicho kushinda.

Hali hiyo imezidisha uhasama baina ya wafuasi wa CCM na CUF na kufanya vikosi vya ulinzi na usalama kuongeza idadi ya askari kwenye visiwa vya Pemba na Unguja. Uamuzi huo pia ulifuatiwa na Marekani kutangaza kutosaini mkataba wa Malengo ya Milenia (MCC), ambao ulikuwa ukitoa fedha kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa barabara, umeme na maji.

Lakini, kitu cha pekee ni jinsi Wazanzibari wanavyomuangalia Jecha kabla ya kutangaza uamuzi wa kufuta matokeo. Wakazi wa Zanzibar walioongea na gazeti la Mwananchi wanasema tangu siku alipotangaza kufuta matokeo ya uchaguzi, Jecha amebadilika na kuwa mtu tofauti; adimu, mpweke asiyekaribiana na watu wengine kwenye mazungumzo ya kawaida, ana ulinzi wakati wote na sasa ana dereva.

Mwandishi mmoja wa habari wa Zanzibar (jina linahifadhiwa) alisema kabla ya tukio la kufuta uchaguzi walikuwa wakikutana na Jecha kama kawaida na wala hakuwa na makuu na si mzungumzaji sana. Alisema hali ilibadilika baada ya tangazo la kufuta matokeo na sasa si rahisi tena kumfikia.

Mkazi mmoja wa Zanzibar aliungana na mwandishi huyo kuwa Jecha sasa si rahisi kupatikana. “Sikumbuki ni lini nilimuona Jecha kwa mara ya mwisho,” alisema Hassan Ibrahim Hassan, mkazi wa mtaa wa Saateni uliopo Wilaya ya Mjini mkoani Mjini Magharibi ambako pia ni makazi ya Jecha.

“Lakini kabla ya kufuta uchaguzi alikuwa mtu wa kawaida akiendesha gari mwenyewe na hakuwahi kuwa na dereva. Tamko lake la kufuta uchaguzi lilimfanya apewe ulinzi na pia gari na dereva.” Hassan aliongeza kuwa hivi sasa hawajui Jecha anaishi wapi, anaswali wapi hata familia yake imekuwa ni siri.

Waandishi wa Zanzibar nao wamekuwa wakinung’unikia ugumu wa kumuona Jecha, wakisema namba zake za simu zilizokuwa zikitumika wakati wote kabla ya kufutwa kwa uchaguzi, sasa hazipatikani. “Haijulikani kama Jecha ana simu nyingine ya mkononi na inadhibitiwa na nani.

Mmoja wa makamishna wa ZEC aliwahi kuliambia gazeti hili kwamba ana muda mrefu hajawasiliana na mwenyekiti wake, kwa kuwa namba alizokuwa anatumia haziko hewani. Mmoja wa waandishi waandamizi wa gazeti la Serikali ya Zanzibar ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini, alisema Jecha alikuwa mtu wa kawaida kabla ya kutangaza kufuta matokeo, lakini baada ya hapo alibadilika sana na kuwa adimu.

“Kabla alikuwa anajumuika na watu kwenye maongezi, anaonekana msikitini wakati wa swala na anapatikana kirahisi waandishi wakimtafuta, lakini baada ya lile sakata amekuwa kama ameji­isolate (amejitenga),” alisema mwandishi huyo.

“Sasa ana ulinzi, haonekani kwenye mazungumzo ya kawaida na saa zote ana ulinzi. Imekuwa vigumu kumuona tofauti na awali. Hata mimi nikitaka kumuona mpaka nifanye jitihada kubwa ndipo nimpate. Jecha amebadilika. Ninavyoona ulinzi ataendelea kuwa nao kwa muda mrefu ujao.”

Mwandishi mwingine kutoka chombo cha habari cha serikali, alisema anamuona Jecha kama mtu aliyepata ahueni baada ya Rais kuapishwa.

“Sasa anaonekana ana nuru usoni, hata nilipomuona jana (juzi) wakati akitembea baada ya shughuli za kuapisha kumalizika, alionekana kama ametua mzigo hivi,” alisema mwandishi huyo.

“Lakini hapa katikati alipoteza nuru kabisa. Nashangaa kwa nini hali ilikuwa vile. Siku moja alikuwa anahojiwa na ZBC, mahojiano yaliyozaa habari iliyoandikwa na gazeti kuwa Jecha aibua madudu ya uchaguzi, lakini alikuwa haonyeshwi sura.

Tulikuwa tunasikia sauti zaidi kuliko kumuona,” alisema mwandishi huyo. “Siku hiyo alisema mengi, mambo makubwa, nachoshangaa kwa nini alikuwa haonyeshwi.”

Waandishi wa habari wa gazeti hili wameshajaribu mara kadhaa kumpata Jecha hadi kijijini kwake, lakini haikuwezekana. Tangu afute matokeo ya uchaguzi Oktoba 28, Jecha amekuwa akionekana kwa nadra hadharani na amekuwa akitumia kituo cha televisheni cha ZBC kutoa matamko yake ya kufuta uchaguzi, kutangaza tarehe mpya na kufafanua kuhusu kasoro za uchaguzi.

Alionekana tena hadharani Januari 12, 2016 siku ya sherehe za mapinduzi na kuibuka kwenye Hoteli ya Bwawani Machi 21 wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi wa marudio na Alhamisi Machi 24 alionekana Uwanja wa Amaan wakati wa kuapishwa kwa Dk Shein.

Siku ya kumtangaza mshindi wa uchaguzi wa marudio, Jecha aliingia ukumbini saa 4:45 asubuhi akiwa amevalia balaghashia kichwani kama ilivyo kawaida yake, na koti la rangi nyeusi akiwa na walinzi wawili wenye maumbile ya miraba minne.

Ndani ya ukumbi Jecha alikuwa lulu akishangiliwa na watu waliokuwa wamevalia vizibao vya njano vyenye mistari ya kijivu vikiwa vimeandikwa observers (waangalizi).

Jecha awa gumzo Wakati baadhi wakishangaa kubadilika kwa Jecha, wakazi wengine wa Zanzibar wanamuona Jecha kama mtu ambaye amekuwa maarufu baada ya kufuta uchaguzi.

Juma Makame Haji, dereva teksi anayeegesha gari lake eneo la Darajani, alisema huko nyuma hakuwa anamfahamu Jecha, lakini tangu afute matokeo ya uchaguzi uliopita jina lake limekuwa maarufu.

Haji alisema kuwa wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi wa marudio watu wengi walijumuika kwenye televisheni wengi wakitaka kumuona Jecha.

Jina lake sasa linahusishwa na kila kitu kinachofutwa au kisichopendeza watu kiasi cha kutaka kisiwepo. Jina lake linahusishwa na neno “futa” kwamba kila panapotea utata fulani, vijana husema “aitwe Jecha afute”.

Kitu kingine kilichosababisha Jecha awe gumzo ni namna alivyoacha utaratibu uliozoeleka wa kutangaza matokeo ya urais kadiri yalivyoingia na badala yake aliamua kuja kumtangaza mshindi kwa kufika na matokeo ya mwisho.

Wakati hadi Oktoba 28, 2015, ZEC ilikuwa haijakamilisha kupokea, kujumlisha na kutangaza matokeo yote ya uchaguzi mkuu wa rais wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, 2015, ilimchukua saa chache kupokea, kujumlisha na kutangaza matokeo ya uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, 216.

Jumatatu ya Machi 21, Jecha akiwa na matokeo yote aliingia ukumbini saa 4:45 asubuhi na alianza kuzungumza saa 5:49 ambapo alitumia dakika 20 kutoa nasaha hadi kumtangaza mshindi na alimaliza saa 6:09 mchana.

Chanzo: Mwananchi

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s