Historia mpya Zanzibar

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mh. Jecha Salim Jecha akitoa taarifa za uchaguzi
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Mh. Jecha Salim Jecha akitoa taarifa za uchaguzi

BAADA ya siku 144 za utata, fadhaa, taharuki na sintofahamu, Wazanzibari Jumapili hii watafanya uchaguzi wa aina yake. Uchaguzi huo umepachikwa jina la ‘uchaguzi wa kimya’ kwa vile hakukuwa na kampeni wala shamrashamra zozote za kawaida zinazohusishwa na chaguzi zote zilizowahi kufanyika hapa nchini.

Tayari Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imetangaza kurekebisha mapungufu yaliyopo kwenye karatasi za kupigia kura kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Marudio uliopangwa kufanyika Jumapili hii, Raia Mwema limeambiwa.

Karatasi za kupigia kura ambazo ziliwasili wiki iliyopita zilionekana na mapungufu kadhaa yakiwamo ya kukosewa kwa majina ya wagombea; jambo ambalo lingeweza kubatilisha uchaguzi huo.

Kupitia taarifa iliyosambazwa kwa vyombo vya habari juzi jioni (Jumatatu Machi 14) na Zec kupitia kwa Mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha, karatasi zilizofanyiwa marekebisho zitawasili kesho Alhamisi kutoka Afrika Kusini.

Mmoja wa wagombea urais katika uchaguzi huo, Hamad Rashid Mohamed, aliliambia gazeti hili mapema wiki hii kuwa amezungumza na ZEC kuhusu kasoro hizo na wamemuahidi kuwa watarekebisha.

“ Mimi wameniambia kwamba matatizo yaliyojitokeza yametokana na wachapaji wa karatasi hizo na kwamba wenyewe ndiyo watagharamia karatasi mpya na zitawasili kabla ya uchaguzi, alisema Hamad anayewania urais kupitia chama chake cha Alliance for Democratic Change (ADC).

Hamad aliliambia gazeti hili kwamba ana matarajio makubwa ya kushinda na kwamba tayari amejiandaa kwa ajili ya kuapishwa kuwa Rais mpya wa Zanzibar. “ Wazanzibari wanafahamu sera zangu hasahasa katika eneo la ujenzi wa viwanda na biashara ya mwani.

Wanafahamu kuwa ADC ndiyo chama pekee kinachoweza kuleta tofauti katika jamii na siasa za Zanzibar. “ Siasa za chuki, hadaa na uhasama zifike mwisho. ADC si CCM wala si CUF. Hiki ndicho chama kilichotabiriwa na akina Abdulrahman Babu kuwa kitakuja kuleta tofauti inayotakiwa,” alisema.

Alipoulizwa kama tayari ameandaa suti maalumu kwa ajili ya shughuli ya kuapishwa, Hamad ambaye ni mmoja wa wanasiasa wakongwe wa upinzani nchini alijibu kwa kucheka kwamba; “ kwa bahati nzuri nina suti za kutosha tangu nikiwa mbunge.

Naweza kuvaa yoyote”. Vyovyote itakavyokuwa, Zanzibar itaingia katika historia mpya ya kufanya Uchaguzi Mkuu wa Marudio.

Hatua hiyo inakuja ikiwa ni karibu miezi mitano baada ya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, alipotangaza kuyafuta matokeo yote ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.

Licha ya waangalizi wa ndani na nje pamoja na jumuiya ya kimataifa kupongeza kwa namna mchakato huo ulivyotawaliwa na amani, huru na haki, Jecha alitangaza kuufuta uchaguzi huo siku ya Jumatano, mchana wa Oktoba 28, 2015, kwa kile akichodai ni kasoro nyingi zilizojitokeza ambazo zimelazimisha kufutwa kwa uchaguzi huo.

Alizitaja sababu tisa zilizosababisha uchaguzi huo kufutwa kuwa ni; Makamishna wa Uchaguzi katika tume hiyo walipigana na kufikia kuchaniana mashati kutokana na tofauti zao, katika vituo vyengine, hususani kisiwani Pemba, kura zilizopigwa zilikuwa zaidi ya idadi ya watu walioandikishwa.

Alitaja sababu nyingine kuwa ni kutopewa ulinzi kwa masanduku ya kupigia kura, kufukuzwa kwa mawakala wa vyama katika vituo, vijana kuvamia vituo vya kupigia kura wakiwa na lengo la kuzua ghasia, vyama vya siasa kuingilia majukumu ya tume kwa kutoa mashinikizo na pia kujitangazia ushindi hali ambayo ingeweza kuzua machafuko, kutochukuliwa kwa kadi za kupigia, lakini watu wamepiga kura, fujo katika vituo vya kupigia kura zilijitokeza katika majimbo yaliyopo kisiwa cha Pemba ikiwemo Micheweni, Tumbe na Konde.

Hali hiyo ya kufuta Uchaguzi Mkuu kwa kiasi kikubwa ikaibua taharuki ya kisiasa visiwani Zanzibar na imeiacha Zanzibar katika hali mbaya kiuchumi –shughuli za kiuchumi zikawa zinakwenda kwa kusuasua hadi leo.

Wakati hayo yakiendelea, tayari vyama zaidi ya tisa kati ya vyama 14 vilivyosimamisha wagombea katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana, vimetangaza rasmi kutokushiriki katika uchaguzi huo ambao wanasema ni batili kwa mujibu wa Katiba na tangazo la Jecha halina uhalali wa kisheria, kimamlaka wala kikatiba.

Chama kikuu cha upinzani visiwani Zanzibar, CUF wameweka wazi na kusisitiza msimamo wao kuwa, kamwe hawawezi kushiriki kuhalalisha uchaguzi huo waliouita haramu.

Uchaguzi huu unafanyika baada ya kushindikana kwa mazungumzo ya mwafaka baina ya pande hizo mbili; CUF na CUF, kutokana na kila upande kushikilia msimamo wake.

Bado hali ya Zanzibar ni ya taharuki kutokana na matukio mbali mbali ambayo yanaendelea kutokea wakati tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa Marudio ikikaribia.

Hivi karibuni kumekuweko na matukio ya kuvamiwa kwa baraza (vijiwe) za CUF, kuvunjwa, kuchomwa moto na kupigwa kwa wafuasi wake wanaokutwa katika baraza hizo.

Matukio hayo yanaendeshwa na kikundi cha watu wanaotumia magari ambayo wakati mwingine hayana hata namba za usajili, wakiwa na silaha za moto na za jadi kama vile mapanga, misumeno na marungu huku wakiwa wamefunika nyuso zao, makundi haya maarufu kwa jina la “mazombi” yamekuwa yakiendesha uharamia huo huku Jeshi la Polisi wakikana kuwatambua.

Matukio ya kuchomwa nyumba moto katika kijiji cha Wawi, Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba, Kangagani, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, kituo cha Afya cha Kuiyu Munungwini, maskani za CCM, kuchomwa moto baraza za CUF za Kilimahewa (Mjini Unguja), Mkanyageni (Mkoani, Pemba), Kiwapwa (Ziwani, Pemba), Kiuyu Minungwini (Kojani, Pemba), Wingwi Ofisi ya Jimbo (Wingwi, Pemba) na Baraza ya Kinowe (Tumbe, Pemba).

Aidha kumeripotiwa kuwepo kwa ubaguzi wa kisiasa wanaofanyiwa wafuasi wa CCM kisiwani Pemba kwa kususiwa katika shughuli za kijamii ikiwemo kubaguliwa katika usafiri wa visiwa hivyo likiwemo tukio la hivi karibuni lililoripotiwa kisiwani Panza huko Pemba.

Ubaguzi huo umejitokeza katika vyombo vya usafiri ambapo baadhi ya manahodha wa vyombo vinavyovusha wananchi kutoka Panza kwenda Chokocho kisiwani Pemba wameanza kugoma kuwavusha wananchi kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kuwepo kwa itikadi tofauti za kisiasa.

Tukio la karibuni kabisa ni mripuko wa bomu ambao bado polisi hawajathibitisha kuwa ni bomu la kivita au la kienyeji lililoripuka usiku wa saa sita kuamkia Ijumaa ya Machi 4, mwaka huu, katika eneo marufu la maskani ya CCM, Kisonge, eneo la Michenzani, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.

Taharuki hiyo ilizuka katika siku ambayo Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, alikuwa amewasili visiwani Zanzibar akitokea nchini India alipokwenda kufanyiwa matibabu.

Mfululizo wa matukio hayo ambayo ni wazi yanaelekea kuvirudisha visiwa hivi katika siasa za chuki na ubaguzi yanaonekana kuwafurahisha wahafidhina wachache bila kujali ni gharama gani imetumika kuwatoa Wazanzibari katika siasa za aina hiyo.

Kwa hali ilivyo sasa, kuna dalili kuwa huenda CCM watashinda uchaguzi huo kwa kura nyingi na kuunda serikali ya peke yao, kwa vile ADC haionekani kuwa na nguvu sawa na CUF na hivyo kuna uwezekano mkubwa kusiwe na Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Chanzo: Raia Mwema

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s