Kuwalazimisha watumishi wa umma kupiga kura sio sahihi

jecha

Salma Said

Wananchi wa Zanzibar wiki ijayo Machi 20 wanatarajiwa kupiga kura katika uchaguzi wa marudio ambao ndiyo utakaoamuwa miongoni mwa wagombea 14 waliojitokeza katika kuwania nafasi hiyo ya urais wa Zanzibar kwa miaka mitano ijayo.

Tayari Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imeshachapisha majina ya wagombea 14 ambao watapigiwa kura na wananchi mbali mbali katika Visiwa Vya Unguja na Pemba, licha ya baadhi ya vyama vya siasa kukataa kushiriki katika uchaguzi huo wa marejeo.

Uchaguzi wa marudio unafanyika kufuatia kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana  na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Jecha Salum Jecha kwa kile kilichoelezwa  kujitokeza kwa kasoro mbali mbali ambazo zingeufanya uchaguzi huo kutokuwa huru.

Lakini wakati Tume ya uchaguzi na serikali ikishindikiza kufanyika kwa uchaguzi huo kwa madai ya kuwa umekumbwa na kasoro tayari waangalizi wa uchaguzi huo kutoka nchi mbali mbali na jumuiya za kimataifa na mashirika na taasisi za ndani nan je ya nchi zilizotoa taarifa zake za awali walisema kwamba uchaguzi wa Octoba 25 ulikuwa wa uhuru, haki na uwazi.

Tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 hapa Zanzibar vyama viwili tu vya siasa ambavyo vimekuwa na ushindani mkubwa na kutawala siasa za Zanzibar ambavyo ni CCM na CUF vyenye uwezo wa kunyakuwa majimbo ya uchaguzi ya Unguja na Pemba.

Uchaguzi wa marudio umepata msukosuko mkubwa ambapo baadhi ya vyama vya siasa ikiwemo chama kikuu cha upinzani Chama Cha Wananchi (CUF) kususia uchaguzi huo kwa madai kwamba uchaguzi wa Oktoba 25 umefanyika kwa uhuru kama ilivyothibitishwa na waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje ya nchi waliokuja kushuhudia.

Kujitoa kwa Chama Cha CUF katika uchaguzi huu wa marudio na vyama vyengine 10 kumeleta changamoto kubwa katika uchaguzi huu ambapo wananchi nao wamekuwa na khofu ya kushiriki kutokana na sababu mbali mbali.

Wakati wanachama wa chama cha mapinduzi na vyama vyengine ambavyo havina wafuasi wa kutosha wakijiandaa na uchaguzi wa marudio kitandawili kikubwa kipo kwa wafanyakazi wa taasisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na mashirika yake kuhusu kutumia haki ya kupiga kura katika uchaguzi huo.

Jee wafanyakazi wa serikali watashiriki kikamilifu katika uchaguzi wa marudio na watatumia haki yao ya kidemokrasia kwa wale watakaoshindwa kupiga kura hatma yao ikoje hawataonekana ni wafuasi wa CUF walioamuwa kususia zoezi hilo?.

Ni moja ya swali kubwa na zito ambalo wafanyakazi wamekuwa wakijiuliza hivi sasa ambapo katika kipindi hichi suala la kupiga kura linaonekana kuwa ni la lazima kwa watendaji wa serikali.

Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kupitia wizara ya utumishi bado haijatowa waraka kwa watumishi wake kuhusu suala la kupiga kura katika uchaguzi wa marudio ingawa jambo hilo lipo chini chini kwa watendaji wa kuu katika kutoa maagizo ya kuwataka wafanyakazi kuwasilisha baadhi ya nyaraka za upigaji kura.

Kwa mfano katika kisiwa cha Pemba wafanyakazi wa taasisi za serikali wote wametakiwa kuwasilisha shahada za kupiga kura pamoja na vitambulisho vyao na kituo cha kupiga kura kwa ajili ya kuhakikiwa zaidi huku wakitakiwa kuwasilisha namba za kitambulisho cha mzanzibari mkaazi, kitambulisho cha kupigiwa kura pamoja na kutaja kituo cha upigaji kura.

Hatua hiyo imelalamikiwa na wafanyakazi wa serikali na kuwatia wasiwasi mkubwa ambayo lengo lake kubwa ni kutaka kuwabaini wafanyakazi waliosusia zoezi la kupiga kura katika uchaguzi wa marudio.

Wakuu wa mikoa wamekuwa wakitoa taarifa za kuwataka wafanyakazi kuwasilisha vitambulisho hivyo nilivyovitaja hapo juu lakini baada ya kuulizwa jee hatua hiyo haitowaleta fitna na sio sababu ya kuwatisha wafanyakazi kwa kuwatafutia sababu ya kuwafukuza kazi?.

Mkuu wa mkoa wa kaskazini pemba alisema lengo la kuitisha vitambulisho ni kuwahakiki na kutaka kujua wafanyakazi wa serikali wapo wangapi katika mkoa wake jambo ambalo limezusha masuali mengi ikiwemo ni kwa nini iwe wakati huu?

Katika mtego huo mfanyakazi wa serikali ambaye hatoshiriki katika uchaguzi wa marudio moja kwa moja ataonekana wazi wazi kwamba ni mfuasi wa chama cha CUF ambacho kimewataka watu wake kutoshiriki katika zoezi hilo.

Licha ya kuwepo kwa demokrasia ya uhuru wa kuchagua chama unachokitaka lakini kwa upande wa Zanzibar wafanyakazi wa Zanzibar ambao wenye kukiunga mkono chama cha wananchi CUF wamekuwa wakijificha na huogopa kujionesha hadharani na hata pale panapofanyika uchaguzi huwa wanafanya ni siri kubwa ili wasijulikane kama wao ni waungaji mkono wa CUF.

Mbali na wafanyakazi wa taasisi za serikali lakini hata waajiriwa wa vikosi vya serikali ya mapinduzi Zanzibar nao wanaingia katika mkumbo kama huo hasa kwa kuzingatia uchaguzi uliopita wa Octoba 25 idadi kubwa ya kura zilizopigwa na vikosi zimeonekana kuunga mkono CUF na kusababisha baadhi ya watendaji na wafanyakazi hao kutiliana fitina.

Taarifa za ndani na za uchunguzi zinaonesha kwamba hata kutolewa vipeperushi ndani ya vikosi vya SMZ limetokana na kutofautiana kwa wafanyakazi ambapo baadhi ya wafanyakazi walimpinga waziri wao wazi wazi, Haji Omar Kheri kwa uamuzi wake wakimshutumu kutoa agizo la kuagiza sare za wafanyakazi zinazofanana na jeshi jambo ambalo limekanushwa na Makamo Mwenyekiti wa Idara Maalum, Kamishna wa Zimamoto Zanzibar, Ali Abdalla Malimussy.

Taarifa hizo zenye ujumbe usemao “Mfumo wako hatuutaki” zinazodaiwa kuandikwa na kusambazwa na baadhi ya vikosi hivyo ambao unamhusisha moja kwa moja Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalumu za SMZ Haji Omar Kheir.

“Kwa kweli jambo hili sisi limetusikitisha sana na tunaamini kwamba limetayarishwa kwa makusudi na kwa lengo maalumu na mtandao wa watu wanaotumiwa na wanasiasa wasioitakia mema nchi yetu “alisema Kamishna.

Uamuzi wa kuwataka wafanyakazi wa serikali kuwasilisha shahada za kupiga kura pamoja na kituo ni kitendo ambacho kinakwenda kinyume na haki ya kidemokrasia ya maamuzi ya kisiasa.

Unaweza kuthubutu kusema ni utaratibu wa zamani sana uliowahi kutumiwa katika mwaka 1995 katika uchaguzi mkuu wa kwanza mara baada ya watu kupiga kura wakaaza kufuatilia kura zao walikipigia chama gani cha siasa.

Utaratibu huo matokeo yake yalikuwa mabaya sana ni kupelekea kufukuzwa kwa watumishi wengi wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar baada ya kubainika kwamba wamekipigia chama cha upinzani zaidi katika kisiwa cha Pemba.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s