Mabomu Zanzibar yazua maswali

Kamishna wa polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame
Kamishna wa polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame

Wakati matukio ya mfululizo wa milipuko ya mabomu Zanzibar yakizua maswali mengi, tukio lingine kama hilo limetokea tena baada ya nyumba ya Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame, kulipuliwa kwa bomu.

Maswali haya yanaibuka kutokana na ukweli kwamba tangu kuanza kwa matukio hayo, hakuna madhara kwa binadamu wala wahusika wa moja kwa moja kutiwa mbaroni.

Tukio la kurushwa kwa bomu katika nyumba ya Kamishna wa Polisi Zanzibar ambaye bila shaka ana ulinzi wa kutosha, pia limezidi kuzua maswali mengi.

Hilo sasa limefanya idadi ya matukio ya mabomu Zanzibar kufikia manne tangu kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka jana.

Bomu hilo la kutupwa kwa mkono lilirushwa juzi saa 5:15 usiku na watu wasiojulikana katika paa la nyumba yake, mtaa wa Kidichi, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Mlipuko wa kwanza wa bomu ulitokea katika uzio wa transfoma mbovu, mita 30 kutoka kituo kidogo cha Polisi cha Mkunazini na kufuatiwa katika Baraza ya CUF Michenzani na maskani ya CCM Kisonge, mkoa wa Mjini Magharibi.

Akizungumza na waadishi wa habari ofisini kwake,  Ziwani mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Makame alithibitisha kutokea kwa shambulio hilo lakini hakuna mtu aliyejeruhiwa.

Alisema mlipuko huo wa bomu umeleta madhara baada ya paa la nyumba yake kufumuka pamoja na sehemu ya dari ndani ya nyumba hiyo.

Hata hivyo, alisema mlipuko huo unafanana na ule uliotokea katika maskani ya Kisonge, baada ya watu wasiofahamika kutega bomu katika sehemu ya kontena wanalotumia kujipumsisha wanachama wa CCM na kuhifadhi vitu vyao.

Alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa mlipuko huo pamoja na kuwasaka watu waliohusika ili kuhakikisha wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

“Kuna kazi kubwa imefanyika na tumeweza kuibua mambo mengi tangu kuanza kutokea milipuko hiyo,” alisema.

Alisema la polisi hawajashindwa kupambana na watu wanaofanya vitendo hivyo nas kwamba wanaofanya uhalifu huo siku zao zinahesabika

Pamoja na vitendo hivyo, alisema Polisi wameimarisha ulinzi, ikiwamo kuongeza vifaa na askari kutoka Tanzania Bara ili kuhakikisha uchaguzi wa marudio unafanyika kwa amani.

Alisema vitendo vinavyojitokeza Zanzibar, haviwezi kuachiwa na kuahidi kuwachukulia wahusika hatua na kusisitiza kuwa vitendo wanavyofanya ni  “sawa na mtu kubonyeza swichi ya umeme ndani kwa kidole.’’

Taarifa Zaidi zinasema mlipuko wa bomu hilo ulitokea muda mfupi baada ya Kamishna kurudi na kuingia ndani ya nyumba yake.

Kwa mujibu wa mtoa habari wetu, baada ya kutokea mlipuko huo, Kamishna na familia yake walihamishwa ndani ya nyumba hiyo kutokana na sababu za kiusalama.

Alisema kwamba shambulio hilo limetokea wiki mbili nyuma tangu Kamishina kufiwa na mkewe lakini watoto wote waliokuwemo katika nyumba hiyo hakuna aliyejeruhiwa.

Imelezwa kuwa walinzi wakati tukio hilo linatokea walikuwamo ndani ya nyumba iliyozugushiwa uzio, lakini majirani wanasema walisikia sauti ya pikipiki (Vespa) kabla ya kutokea mlipuko

Wengine walisema kuwa walisikia mshindo mkubwa lakini walishindwa kufahamu kilichotokea na kulazimika kujificha na watoto ndani ya nyumba.

Hata hivyo, askari wawili waliokuwa wakilinda nyumba hiyo walikataa kuzungumza chochote, baada ya mwandishi kutaka kufahamu mazingira ya shambulio hilo.

Chanzo: Nipashe

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s