Moyo amtaka Jecha atangaze matokeo, si kurudia uchaguzi

Mzee Hassan Nassor Moyo aliyefukuzwa uanachama hivi karibuni na Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Mzee Hassan Nassor Moyo aliyefukuzwa uanachama hivi karibuni na Chama Cha Mapinduzi (CCM)

Mwanasiasa Mkongwe Zanzibar, Hassan Nassor Moyo, amesema mgogoro wa uchaguzi mkuu wa Zanzibar hauwezi kumalizwa kwa kurudiwa, badala yake ukamilishwe wa Oktoba 25, mwaka jana na mshindi wa urais, atangazwe.

Moyo alitoa kauli hiyo zikiwa zimebakia siku tisa kabla ya uchaguzi wa marudio Machi 20, mwaka huu, baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, kufuta matokeo ya Oktoba, mwaka jana.

Akizungumza na Nipashe jana, Moyo alisema uchaguzi wa Oktoba 25, ulikuwa huru na wa haki, hivyo hakuna sababu za msingi za kurudiwa kwa uchaguzi huo.

“Hakuna sababu za msingi za uchaguzi wa Zanzibar kurudiwa wakati wananchi wanafahamu nani alikuwa mshindi katika uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana,” alisema.

Moyo ambaye aliwahi kuwa Waziri wa kwanza wa Katiba na Sheria baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, mwaka 1964, alisema kinachotokea Zanzibar ni watu wachache kushindwa kuheshimu misingi ya demokrasia, lakini Zanzibar italazimika kuingia katika mgogoro wa kikatiba na kiuchumi na watakaoumia zaidi ni wananchi wanyonge.

“Mimi naamini uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka jana, ulikuwa huru na wa haki, tume waukamilishe tu watangaze mshindi badala ya kurudia uchaguzi mwingine,” alisema.

Alisema CCM lazima wakubali mabadiliko ya kiutawala kama wananchi wameamua kufanya mabadiliko ya kiutawala kwa njia halali za kidemokrasia.

Alisema hakuna kifungu cha Katiba ya Zanzibar au sheria kinachotoa mamlaka kwa mwenyekiti kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu na kama kulikuwa na kasoro zilitakiwa kurekebishwa katika uchaguzi huo.

Alisema aliyeshinda katika uchaguzi huo lazima haki yake apewe badala ya kurudia uchaguzi ambao unaweza kuleta matatizo ya kikatiba na kuteteresha misingi ya umoja wa kitaifa kwa wananchi wake.

Moyo alisema tangu kuibuka mgogoro wa uchaguzi Zanzibar chuki na uhasama wa kisiasa zimerejea upya na kuvuruga misingi ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Moyo ambaye alifukuzwa uanachama wa CCM kutokana na kile kinachodaiwa kuwa misimamo yake ya kukosoa siasa za muungano hadharani, alisema tayari amefanya mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Amani Karume, lakini alisema ni mapema kuweka hadharani ajenda waliozungumza na mafanikio yake na kusisitiza madhumuni ya mazungumzo yao ilikuwa ni kuangalia mwelekeo na mustakibali wa Zanzibar kisasa kabla ya kufanyika uchaguzi wa marudio na baada ya kufanyika.

Hata hivyo, alisema amekwama kufanya mazungumzo na viongozi wa CCM Zanzibar kwa sababu wamekuwa hawataki kukutana naye akiwamo Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.

“Nitaendelea kufanya mazungumzo ya kutafuta muafaka wa mgogoro wa uchaguzi mkuu wa Zanzibar hata kama uchaguzi mkuu wa marudio, utakuwa umefanyika Zanzibar,” alisema.

Alisema anaendelea kufanya mipango ya kukutana viongozi wastaafu akiwamo Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba na Joseph Butiku.

Alisema leo anatarajia kukutana na Butiku kuzungumzia mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar baada ya mazungumzo ya marais wastaafu kushindwa kupata muafaka Zanzibar kutokana na kuwamo watu wasiokuwa na nia njema kushirikishwa katika mazungumzo hayo.

Hata hivyo, alisema kuwa katika mpango kazi wake wa mazungumzo ameamua kumuweka kando Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kwa kile alichodai kuwa ameonekana hana nia ya kusadia mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar.

Chanzo: NIpashe

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s