Masikini Dk. Kitine, kopo tupu kihistoria

Hassy Kitine

Na Rashid Abdallah

NIMEMSOMA Daktari Hassy Kitine ambaye ni Mkurugenzi wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) akisema, ni ndoto Maalim Seif kuiongoza Zanzibar.

Katika habari aliyonukuliwa, kwa hakika naona ametoa maelezo yanayopotosha hali halisi ya historia ya mapinduzi ya Januari 1964.

Anasema watu wengi wanashabikia mgogoro wa Zanzibar bila ya kujua kiini chake.

Labda anayeshabikia. Aliye mkweli na huru kimawazo, atakuwa anajua kiini cha mgogoro wa Zanzibar. Kwa urahisi tu atasema tatizo ni viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokubali kuachia madaraka hata kuthubutu kutumia vikosi vya usalama kudhibiti upinzani.

Na wapo viongozi waliotoka hadharani na kuapa nchi haitatolewa kwa vikaratasi na kama wapinzani – na hapa wakilengwa hasa Chama cha Wananchi (CUF) – wakitaka madaraka basi nao wapindue kama ilivyokuwa 1964.

Dk. Kitine anasema, “wenzetu (Zanzibar) wamepata uhuru wao kwa kumwaga damu, tofauti na sisi huku (Tanganyika) ambako Mwalimu Nyerere alitumia meza ya mazungumzo kusaka uhuru.”

Si kweli kuwa Zanzibar uhuru ulipatikana kwa njia ya kumwaga damu. Uhuru wa Zanzibar ambao ulitoka kwa Uingereza, ulipatikana kwa amani 10 Disemba 1963. Ikaundwa serikali ya kiraia ya umoja wa kitaifa chini ya Waziri Mkuu Mohamed Shamte.

Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoongozwa na John Okello, aliyekuwa raia wa Uganda, sio uhuru. Mapinduzi yalipindua serikali ya uhuru ambayo viongozi wa Afro-Shirazi Party (ASP) waliipinga kwa kuona wamepikuliwa baada ya Chama cha ZNP (Zanzibar Nationalist Party), kuungana na Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP).

Mapinduzi yalikuwa ni matokeo ya chuki za kigozi na uchu wa madaraka, zilizosababisha kutapakaa damu kila kona ya Zanzibar baada ya wananchi walioandaliwa kwa makusudi na ASP na mshirika wake TANU au angalau kiongozi wake Mwalimu Nyerere, kupewa silaha za jadi na moto na kuelekezwa kuvamia na kuua watu kikatili.

Anaposema “Historia ya Zanzibar inawahusisha Waarabu (mabwana) na Waswahili (watwana),” Dk. Kitine anakanganya. Kwanza kiasili, Wazanzibari ni watu waliotoka Yemen, Oman, Iran, Comoro na maeneo mbalimbali ya Bara la Afrika. Visiwa siku zote huwa ni mahamizi ya watu waliotoka kwingineko.

Baadaye watu waliojikuta hapo, wakawa Waswahili kwa sababu ya lugha moja waliyozungumza na eneo la kijiografia wanaloishi, wakawa Waafrika kwa sababu ya bara wanaloishi.

Itakuwa ni ajabu kuwaita wale wenye asili ya Asia kuwa ni Waarabu na hawa wengine wakawa ndio wenyeji wakati wote walihamia tu. Huo utakuwa ni ubaguzi.

Washirazi wenye asili ya Pashia (Iran ya zamani), ukawaita Waafrika ambao ndio wanatajwa na wapotoshaji wa historia kuwa ndio Waafrika wa asili japo si kweli, kiasili Washirazi wanatoka Mashariki ya Kati – Waarabu pia ambao walipitia Shirazi-Iran kabla ya kuingia Afrika Mashariki.

Sasa anaposema mwenye asili ya Kiarabu atabaki kuwa Mwarabu lakini mwenye asili ya Kiajemi, Kingazija, atabadilika kuwa Mswahili-Muafrika wakati wote ni wahamiaji, huko ni kuchanganya mada. Kama ni kubadilika basi wote wamebadilika.

Ukisema Waswahili wa Zanzibar halafu ukawatoa Waarabu, hueleweki hata kidogo, wakati lugha na mazingira yameshawakubali kuwa wao ni Waswahili japo kila mtu atabaki na asili yake.

Anasema, “Abeid Amani Karume alipochukua uongozi wa Zanzibar na kuruhusu Waswahili kuoana na wanawake wa Kiarabu,” anathibitisha jinsi anavyoitazama historia kishirikina. Ni debe tupu.

Baada ya mapinduzi kutekelezwa, hakukuwa na ruhusa ya hiyari ya Waafrika kuwaoa watoto wa Kiarabu. Kilichotokea ni wakubwa wa ASP kuanzisha utaratibu wa ndoa za nguvu kwa mabwana wa kimapinduzi kujichagulia watoto weupe (Waarabu, Wahindi, Washirazi, n.k) na kuwaoa kwa nguvu.

Ni utaratibu huu ulisababisha zinaa kwa baadhi ya mabwana hao kuchukua hata wanawake waliokuwa wameolewa na kuwafanya wake zao. Mabwana walipojulishwa mtoto fulani mweupe ameolewa, kulitoka amri ya kusakwa huyo mume mtu na baadhi ya waliokutwa, waliuliwa ili mabwana wajihalalishie ndoa za nguvu.

Historia inaonesha baadhi karibu mawaziri wote wa serikali ya Rais Karume walipata wake kwa njia hii haramu kwa sababu Kiislam, ndoa inaidhinishwa na walii wa anayeolewa. Wao mabwana waliozeshana kienyeji.

Ni vema Dk. Kitine akaelewa kwamba anaposikia makada wenzake wa CCM wakichukia “machotara” kwa kusema si Waafrika wana kwao, baadhi yao ndio watoto waliozaliwa kutokana na hizi ndoa za nguvu.

Hili ni jambo linalofahamika sana Zanzibar na wakubwa wa ki-ASP wakati ule, na baadaye CCM, wanajivuna kwa mafanikio hayo.

Anaposema “Wapo watu wa ndani na nje ya nchi wanatamani mfumo wa kitwana na kibwana urudi visiwani,” Dk. Kitine anajidharau kifikra.

Utwana na ubwana? Tuseme anakusudia watu waliokuwa wanakwenda Zanzibar kutafuta vibarua. Kama amelenga kuzungumzia utumwa angeeleweka. Utwana, ubwana, utumwa ni mambo tofauti.

Historia ya watu kufanya kazi ya kibarua kwa matajiri jambo la wazi na lipo hadi leo. Wapo Watanzania wenzetu Wasukuma, Wanyamwezi na makabila mengine wanakwenda Zanzibar kutafuta kibarua. Sasa sijui mtu huyu utamwitaje mtwana wakati kaenda mwenyewe? Pengine utamwita kwa tafsiri ya kilugha.

Wasaka kazi walikuwepo Waswahili wa makabila yote, hata Waarabu masikini, ambao nao walikuwa wanajitafutia riziki kwa kufanya kazi katika mikarafuu na maeneo mengine kama watu wengine.

Kama kumtumikia mtu kwa sababu ya kutafuta chejio ni “utwana”, basi Tanzania kuna Watwana wengi, watu hawapati mishahara ya kila mwezi kama hawajatumikia au kutumwa na watu.

Kama anazungumzia umiliki wa watumwa – haukuwa kwa watu wenye asili ya Yemen na Oman tu, hata Washirazi kutoka Shirazi (Iran) walikuwa wanamiliki watumwa pia. Familia za Kizanzibari walimiliki watumwa hata hao wanaoitwa Waafrika.

“Ndiyo maana wanahangaika huku na kule kutafuta uongozi jambo ambalo haliwezekani kwa sababu nchi hiyo haikukombolewa kwa makaratasi.”

Sasa anaposema nchi haitolewi kwa vikaratasi, tafsiri yake anahimiza mapinduzi ya pili? Sijui kama anajua matokeo ya mapinduzi?

“Hivi hamjiulizi ni kwanini Unguja hakuna shida, badala yake Pemba ndio kuonekane kugumu. Kuna historia nzito inayohusu usultani hapo katikati.”

Labda kwanza nielewe “shida” gani anayoikusudia Dk. Kitine; kama ni za kimaisha, mbona hizi zipo pande zote?

Shida gani hizo? Kwani Sultani alikuwepo Pemba au Unguja? Kama shida ni usultani katikati, basi shida iweko Unguja sio Pemba. Ananivuruga!

Anamalizia hoja akisema, “Kitendo cha kufuta Historia ya Mapinduzi ya Zanzibar hakikubaliki, na hakuna mtu makini atayekubali kufanya hivyo.”

Si lazima kuifuta historia ya mapinduzi, waumini wanaamini kila mtu atalipwa kwa matendo yake siku ya mwisho. Waliofanya mauaji, ubakaji na utesaji kwa kisingizio cha mapinduzi wakati Sultani alishakimbia nchi, ipo siku kila mtu atabeba mzigo wake mbele ya aliyemuumba ambaye ameapa atamuadhibu vilivyo aliyedhulumu hata tone tu la damu ya mwenzake.

Wacha tushabikiane duniani bali mbele twendako kila mtu na lake, na wala historia haitofutwa maana ukweli ilishaandikwa, haifutiki. –

0773526254

Chanzo: MwanaHalisi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s