Jecha aliteuliwa kukidhi matakwa ya CCM

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Bw. Jecha Salim Jecha
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Bw. Jecha Salim Jecha

Na Enzi T. Aboud

UCHAGUZI wa marudio ulioitishwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kufanyika 20 Machi mwaka huu unazidi kukabiliwa na vikwazo kutokana na matamko ya wanasheria wabobezi kuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jecha Salim Jecha hana uhalali wa kuiongoza tume kwa sasa.

Sababu inatajwa kuwa yeye ndiye aliyevuruga uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba 2015 akitumia amri isiyokuwa halali kisheria.

Wanasema hana sifa ya kushika nafasi hiyo kwa kuwa si mtu anayefaa kuwa jaji kama inavyoelezwa na Kif. (2) ambacho kinasema Mwenyekiti wa Tume awe na sifa ya ujaji wa Mahakama Kuu au Jaji wa Mahakama ya Rufaa, yenye misingi ya taratibu za Jumuiya ya Madola, na pia awe na sifa ya heshima iliyotukuka katika jamii.

Kwa kuwa Jecha hana sifa zote hizo, wanasheria wabobezi wanabainisha kuwa uongozi wake na utendaji wake hapo ni batili.

Ina maana mamlaka iliyomteua imefanya hivyo kisiasa zaidi kwa mkakati maalum wa kukiwezesha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupata upendeleo wa kushinda uchaguzi kupiku vyama vya upinzani visivyokuwa na mchango wowote katika uteuzi wa viongozi, jukumu ambalo kwa nchi za kiafrika, hufanywa bila kuangalia vigezo halisi.

Watawala wasioheshimu Katiba na sheria mara zote husababisha migogoro na mizozo katika uratibu na usimamizi wa wa uchaguzi, kwa vile wanaongoza zoezi hilo hawana sifa.

       Jecha amevuruga uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba mwaka jana kwa kuufuta akitii shinikizo la mamlaka ndio maana ameungwa mkono nao pamoja na dola nzima. Kukosekana haki, uwazi na uadilifu kulizima ufanisi, lakini anafanya dharau na dhihaka na kuhujumu kwa makusudi majukumu aliyokabidhiwa.

       Ujinga wa kutokujua sheria umemuingiza Jecha mashakani, ametengwa na jamii, hasa kundi kubwa la wafuasi wa upinzani wanaofikia asilimia 89 na kwa takwimu ya idadi yao hasa Chama cha Wananchi (CUF), ni dhahiri kuwa amejijengea uadui wa kudumu na mustakbali hasi mbele ya wafuasi wa upinzani.

Kama hilo halitoshi, Jecha ameirudisha Zanzibar nyuma katika mkabala wa kisiasa ambao umerudisha chuki na uhasama kisiasa na kuwatia hofu na woga mkubwa si tu wafuasi wa upinzani, bali wananchi pia wanaolilia usalama wa maisha yao na mali zao kwa kuwa uzoefu wa Zanzibar katika uchaguzi wa aina hiyo haikuwa salama.

Katika uchaguzi wa Juni 1961 hali kama hiyo ilijitokeza kwa watawala wa kikoloni waliwaweka baadhi ya wajinga wasiojua sheria ya uchaguzi ambao walisimamia matokeo katika vituo vya uchaguzi, na ilipobainika haki haikutendeka katika baadhi ya majimbo, ghasia ziliibuka katika uchaguzi huo wa 1961 eneo la Mabatini karibu na Darajani ambako kulienea ghasia na watu 62 wakapoteza maisha na wengine 250 kujeruhiwa.

Kutojikumbusha yaliyotokea nyuma, kuyaelewa na kuchukua tahadhari, ni upungufu kwa watawala. Wanajikuta katika ule usemi usio na mashiko, eti yaliyopita si “ndwele tugange yajayo.”

Ni usemi wa falsafa isiyohai, sawa na kukataa historia yenye mafundisho mazuri na mabaya yaliyopita maana yaliyotokea wakati wa mapinduzi ya mwaka 1964 yaliyokuwa mabaya hayana maana kuyasema, yanafukua makaburi ambayo mwisho wa siku maafa yanawarudia watenda mabaya.

Jecha hakujali yote hayo. Ameamua tu kuganga yajayo kwa kuandaa uchaguzi wa marudio ambao utaipitisha CCM na kuvipiga ngeu vyama visivyo na ufuasi.

Anafurahia utokee ushindi huo kwa matumaini kuwa Serikali ya Umoja wa Kitafa ambayo imekuwa ikiandamwa na makada wa CCM ifutwe, ni dhahiri sasa muelekeo huo uko njiani na kwa vyovyote vile kutoshiriki kwa CUF katika uchaguzi wa marudio kunahatarisha kuwepo serikali hiyo.

CCM kimeshasema hata kama CUF haitoshiriki uchaguzi, serikali ya umoja itaundwa kutumia vyama vilivyothibitisha kushiriki, na chama kitakachopata angalau asilimia 10 ya viti katika Baraza la Wawakilishi, ndicho kitakuwa mshirika wa CCM katika kuunda serikali ya umoja.

Pamoja na kauli hiyo ya CCM lengo lao hasa ni kumzuia Maalim Seif Shariff Hamad asiwe Rais, lakini pia asiwemo serikalini. Ndoto yao zaidi ni kuhakikisha CUF inapotea katika ramani ya siasa na hiyo kuwa mafanikio ya kuzima upinzani wa maana Zanzibar.

Lakini katika hali inayoonekana, hasa kwa upande wa kisiwa cha Pemba ambako ni ngome isiyotetereka ya CUF, yumkin wananchi hawana imani na CCM, hawatakuwa tayari kuona chama chao kinafutika.

       Vita vya kisiasa chini kwa chini vinavyoshupaliwa na makada wa CCM ni kuitumia Tume kufanya kila mbinu ili ionekane CCM inakubalika Pemba, japokuwa ni wazi haitofaulu na inapoteza raslimali ambazo ingezitumia kujiimarisha kwa maeneo mengine hasa kwa kuwa kwa Pemba, hakuna zaidi ya CUF.

       Uchaguzi wa marudio utapuuzwa Pemba na katika hali hiyo, swali linakuja kwamba je, Serikali itakayoundwa itapata uhalali gani kuongoza Pemba? Utafiti mdogo uliofanywa na wanaharakati wanaofuatilia masuala ya kisiasa, umeona ombwe la utengano baina ya wafuasi wa CUF kisiwani Pemba ambao ni wengi kuliko wale wa CCM hawatokuwa na uhusiano mzuri baada ya uchaguzi wa marudio na kutarajiwa kuibua upya uhasama miongoni vyama hivyo.

Hivi sasa maduka kadhaa kisiwani Pemba yanayofikiriwa kuwa ni ya wafuasi wa CCM yanagomewa. mambo kama hayo ambayo yanarudi kwa nguvu ksiwani Pemba ambayo yaliwahi kufanyika miaka 50 na 60 sio tu katika kisiwa cha Pemba na hata katika maeno mbali mbali ya mji wa Unguja.

       Uchaguzi wa marudio hautasimama katika mezania ya kukubalika na vyama vyote hasa vya upinzani kutokana na udhaifu wa kuaminiana na kuna madai kuwa baadhi yake vinatumiwa na CCM. Kampeni inayoendelea ya nyumba kwa nyumba na mtaa kwa mtaa inafanywa na vyama vya upinzani kuhamasisha wananchi kutotoka kupigakura.

       Jecha amesema wanaohusika watachukuliwa hatua. Kwa kuanzia amewafuta wasimamizi wanaofikia 500 katika majimbo yote 54 ya uchaguzi na kutangaza nafasi hizo kwa watu wengine ambao kwa muono wake wataweza kusimamia vyema uchaguzi.

Jecha ameitia shimoni Zanzibar kwa uamuzi wake kupanda mbegu za kuchochea siasa za shari ambazo zimejenga hofu na woga mkubwa, sio tu kwa watiifu wa upinzani, bali pia kwa wananchi ambao baadhi wameanza kuondoka Zanzibar kwa kukimbia hatari ya machafuko.

Jecha anaweza kuja kufikishwa katika vyombo vya sheria siku za mbele kwa hoja inayoweza kujitokeza kwamba ameendesha uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015, na uchaguzi wa marudio Machi 2016 huku akiwa hana sifa ya kushika nafasi hiyo.

Chanzo: MwanaHalisi

Advertisements

One Reply to “Jecha aliteuliwa kukidhi matakwa ya CCM”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s