Rais Magufuli amepata sababu ya kutotekeleza wajibu Zanzibar?

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli

Kuna kitu kinaitwa ‘visingizio’ au ‘excuses’ kwa Kiingereza. Visingizio ni sababu ambazo mtu anatoa kwa kushindwa kufanya kitu fulani, ingawa ukweli ni kwamba hataki kufanya kitu hicho. Wanasiasa wanatumia visingizio.

Hata Rais John Magufuli ameanza kutoa visingizio. Baada ya kuahidi kuutafutia suluhu mgogoro wa Zanzibar, Rais Magufuli hatimaye kapata kisingizio cha kukwepa kazi hiyo kwa kisingizio cha kuheshimu sheria na uhuru wa tume.

Akihutubia wazee wa Jiji la Dar es Salaam hivi karibuni, Dk Magufuli alikataa kuingilia mgogoro wa Zanzibar kwa sababu anaheshimu sheria inayoipa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) uhuru wa kuamua mambo yake.

Alisema, “Naheshimu sheria, ZEC inao uhuru wa kuamua mambo yake, haiwezi kuingiliwa na yeyote…kama kuna mtu anataka tafsiri ya sheria aende mahakamani. Mahakama iko hapo, hutaki kwenda, halafu unamwambia Magufuli ingilia, siingilii na nitaendelea kukaa kimya.

Yeyote atakayeleta fyokofyoko ajue vyombo vya ulinzi vitamshughulikia.” Hata hivyo, kauli yake ilikatisha tamaa Watanzania waliokuwa na mategemeo makubwa kwa Rais Magufuli kuwa angetafuta suluhu ya mgogoro wa Zanzibar kutokana na kauli yake aliyoitoa Novemba 20 wakati akifungua Bunge la Kumi na Moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rais Magufuli alisema:

“Kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wadau wa siasa hususan vyama vya CUF na CCM tutahakikisha kuwa yanayoikabili Zanzibar yanamalizika kwa salama na amani. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujalie busara na hekima tumalize kwa utulivu na amani.”

Nawashangaa wanaomshangaa Kauli ya Dk Magufuli ambaye anasifika kwa uadilifu, aliyoitoa kukwepa majukumu ya kusaidia kutafuta suluhu Zanzibar ilishangaza wengi, ingawa baadhi yetu kilichotushangaza ni wale walioishangaa kauli yake kuliko kumshangaa Rais Magufuli.

Ambao hatukushangaa ni wale ambao hatukuwa tumesahau kuwa pamoja na umahiri wake wa kutumbua majipu na ‘kumwaga data’, Magufuli ni rais kwa sababu yeye ni mwanasiasa.

Ambao hatukushangaa ni wale tuliojua kuwa kama mwanasiasa, Rais Magufuli anawajibika kwa taasisi iliyomteua kugombea urais, CCM na kwamba sikio kamwe haliwezi kukua likakizidi kichwa.

Kama mwanasiasa, siyo kwamba Rais Magufuli hajui kuwa kauli yake kuwa hawezi kuingilia mgogoro wa Zanzibar siyo sahihi. Siyo kwamba Rais Magufuli hajui kuwa anao uwezo wa kuingilia suala la Zanzibar kisiasa.

Anajua vyema ila mazingira ya kisiasa ndani ya chama chake yanamlazimisha kufanya alivyofanya. Katika hotuba yake, Rais Magufuli alizungumzia suala la kuingilia uchaguzi kiujumla ujumla. Hata hivyo, ‘kuingilia’ suala la uchaguzi kuna maana pana.

Ni kweli kwamba Rais Magufuli hana mamlaka kisheria kuingilia mchakato wa uchaguzi kwa maana ya shughuli za tume katika mchakato mzima wa kusimamia uchaguzi ikiwamo kuandikisha wapigakura, kusimamia uteuzi wa wagombea waliopendekezwa na vyama vyao, kuratibu kampeni, kusimamia upigaji kura wenyewe na kutangaza matokeo.

Rais Magufuli anaweza kuingilia kisiasa kwa maana ya kuongea na viongozi wenzake wa Zanzibar na kuwasihi uchaguzi usogezwe mbele na kushawishi mazungumzo ya pande mbili husika yaanze upya, kwa masilahi ya taifa na hususan kwa masilahi ya usalama wa nchi.

Pamoja na ukweli kuwa rais angeweza kufanya walau jitihada za aina hiyo, Rais Magufuli ameamua hatoingilia mgogoro huo kwa sababu chama chake kishapiga hesabu zake za kisiasa na kugundua mazungumzo ya kisiasa hayana masilahi kwao.

Magufuli asamehewe hata kwa kauli yake aliyoitoa kwa makosa awali ya kuahidi kusaka suluhu kwa sababu bila shaka alikuwa hajakielewa chama chake. Baada ya kukielewa chama na kuelewa siasa za Zanzibar, rais ameamka kutoka usingizini na kugundua kuwa ni rahisi kwake kulinda usalama kwa kuwashughulikia watakaoleta ‘fyokofyoko’ kuliko kuingilia katika kutafuta utatuzi wa mgogoro wenyewe.

Wanasema ndege mjanja hukimbiza bawa lake, woga wa Rais Magufuli wa kuingilia mgogoro wa Zanzibar umekuja baada ya kugundua kuwa mgogoro huo ni sawa na maji yenye kina kirefu yanayohitaji ujuzi na ujasiri kuogelea.

Kinachogombewa Zanzibar siyo namna ya utekelezaji wa demokrasia. Demokrasia yenyewe ndiyo tatizo. Wahafidhina wa CCM waliokamata ‘mpini’ wanataka demokrasia ya aina ya kimapinduzi, yaani demokrasia inayofaidisha wachache.

Ni katika demokrasia ya kimapinduzi ndiyo masilahi ya CCM yalipolala. Ukifanya mazungumzo, hata kama CCM hawatatangazwa washindi, walau mazingira ya usimamizi wa uchaguzi yataboreshwa yawe ya haki zaidi na hivyo kuisaidia CUF.

Hivyo basi, tunaomtaka Rais Magufuli kuingilia mgogoro wa Zanzibar kimsingi tunamtaka rais aende kinyume na masilahi ya chama chake.

Masilahi ya Chama cha Mapinduzi yapo katika kurudia uchaguzi tena katika mazingira yaleyale ya uchaguzi uliofutwa hususan uwapo wa mwenyekiti wa tume yuleyule wanayeweza kumdhibiti. CCM wangekuwa wanataka kuumaliza mgogoro huo kwa nia ya dhati wangeshauri walau tume ibadilishwe.

Katika mazingira yaleyale ya uchaguzi, CCM wanajua CUF hawatashiriki kwa sababu ni mtu asiyefikiri vyema ndiye anaweza kuingia kwenye uchaguzi kama huo wa marudio wakati mazingira yaliyoharibu ule wa kwanza hayajabadilika.

Matokeo ya hali hii ni kuwa CCM watashinda viti vyote na watatawala visiwani humo raha mustarehe miaka mitano ijayo. CUF watalalamika lakini hawawezi kufanya kitu chochote zaidi ya kupeleka fitina kwa wafadhili!

Hiyo ndiyo fikra ya CCM. Rais Magufuli ameanza kuelewa kuwa mambo ya uadilifu na haki anayoyahubiri yana ukomo wake katika utekelezaji. Kwa mfano, hizo nadharia hazina nafasi Zanzibar na jitihada yoyote ya kuzilazimsha ni kutengeneza uadui na kundi la wahafidhina ndani ya chama chake, wakati huohuo akiwa katikati ya vita nyingine kubwa zaidi ya kutumbua majipu.

Nina hakika Rais Magufuli atakuwa amejifunza kutokana na kampeni ya bomoabomoa ambayo iliijengea Serikali uadui na watu wengi ambao ndiyo hasa waliombeba na kumuunga mkono wakati wa uchaguzi.

Kwa mtazamo mwingine, uamuzi wa Magufuli unathibitisha zile kauli zilizowahi kutamkwa na mmoja wa mawaziri wake kuwa muungano na Zanzibar ni kwa ajili ya masilahi ya kiusalama ya Tanzania ambayo ni kuzuia makundi ya wenye misimamo mikali kuingia visiwani humo.

Angalia hata suluhisho ambalo rais alilolitoa baada ya kugoma kuingilia mgogoro huo na kuahidi kupeleka majeshi yakalinde usalama na kuwashughulikia watakaofanya ‘fyokofyoko na hilo ndiyo muhimu.

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s