Vuai: CUF wanafanya maandalizi kimyakimya

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai

Zanzibar. Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai amesema ana matumaini makubwa kuwa CUF watashiriki kwa hiari uchaguzi wa marudio utakaofanyika visiwani hapa Machi 20 kwa kuwa wanafanya maandalizi kimyakimya.

Vuai aliliambia gazeti hii katika mahojiano maalumu hivi karibuni kuwa anawafahamu vyema viongozi wa chama hicho kikuu cha upinzani visiwani hapa kuwa wana tabia ya kubadilibadili uamuzi.

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Mazrui alisema chama chake kinaendelea kushikilia msimamo wa kutoshiriki uchaguzi huo wa marudio kwa kuwa ‘biashara’ ilikwisha tangu Oktoba 25, 2015 wakati Uchaguzi Mkuu ulipofanyika nchini.

Uchaguzi wa marudio uliitishwa tena Januari 22 mwaka huu na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha baada ya kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 28, 2015 akisema kulikuwa na uvunjwaji wa sheria na taratibu za uchaguzi.

Vuai alisema mbali na CUF vyama vyote vya upinzani vilivyotangaza kususia uchaguzi wa marudio vitashiriki kikamilifu tofauti na watu wanavyofikiri kwa kuwa sheria na Katiba pia vinawataka kufanya hivyo.

“Naamini CUF watashiriki uchaguzi. Nawajua sana wale ndugu zangu. Kwa taarifa tulizo nazo wanafanya maandalizi ya chinichini ili siku wakiibuka iwe kama shtukizo, tunawakaribisha,” alisema na kuongeza:

“Tunajiandaa tukijua CUF wanashiriki uchaguzi. Sisi tunajua hivyo ama wanashiriki uchaguzi ama wanafanya jambo jingine, tutalijua mbele.”

Alisema mfano mzuri wa CUF kubadili mtazamo ni kitendo cha mgombea wake wa urais, Maalim Seif Sharif Hamad alivyoomba maridhiano baada ya matokeo ya uchaguzi huo kufutwa, kuwa wa kwanza kujitoa na sasa anaomba tena vikao vya maridhiano kwa kutoa masharti.

Imani ya Vuai kwa CUF kushiriki uchaguzi na vyama vingine vilivyotangaza kususia, inaenda sanjari na tamko la Jecha alilotoa juzi kuwa hadi sasa vyote 14 vitashiriki uchaguzi huo kwa kuwa hakuna hata kimoja kilichofuata taratibu za kisheria kujitoa.

Jana, Mazrui aliendelea kupigilia msumari msimamo wao kuwa anayedai CUF itashiriki uchaguzi “ni mwongo” na hakuna maandalizi yoyote ya chinichini.

Alisema amefanya ziara hivi karibuni na wanachama wote, viongozi na wagombea waliokuwa wakishiriki Uchaguzi Mkuu wanaunga mkono uamuzi wa chama kutoshiriki uchaguzi wa marudio.

“Sisi tumeshaiandikia barua ZEC wataoe majina ya wagombea wetu kwenye uchaguzi wa marudio, wao hawataki. “Tumewaachia CCM wafanye uchaguzi wao, wachague Serikali yao sisi tutabaki kuwa waangalizi tu na hakuna jambo lolote baya ambalo tunapanga kwa sababu biashara tulishaimaliza Oktoba 25,” alisema Mazrui.

Katika mahojiano hayo, Vuai alisema maandalizi ya CCM katika uchaguzi huo wa marudio yanaendelea vizuri kwa kufuata taratibu zote zilizotangazwa na ZEC Alipoulizwa iwapo wanaridhia uamuzi wa ZEC kutangaza uchaguzi wa marudio bila kampeni, Vuai alisema CCM wamesikitishwa kwa sababu unawabana kuwakumbusha wananchi sera zao, lakini hawana namna zaidi ya kutii mamlaka hayo yaliyopo kisheria.

“Kwa mujibu wa sheria tume ina nguvu ya kuratibu uchaguzi na sisi tulishatoa maelekezo kwa wanachama wetu kuwa tunatii taratibu na maagizo yote ya tume,” alisema. Tangu Jecha atangaze kufutwa kwa uchaguzi wa mwaka jana baadhi ya vyama vya siasa takriban 10 vikiongozwa na CUF vilitangaza kujitoa kushiriki uchaguzi wa marudio.

Hali hiyo imekuwa ikizua hofu huenda CCM ikabaki peke yake katika kinyang’anyiro hicho na kupunguza uhalali wa kisiasa kwa mgombea wa wake wa urais, Dk Ali Mohamed Shein iwapo atashinda uchaguzi huo.

Hata hivyo, Vuai alisema ushiriki wa vyama vya siasa katika uchaguzi ni hiari kisheria na kikatiba, hivyo siyo lazima vyote vishiriki. Akiongea kwa kujiamini, alisema Katiba ipo wazi na kwamba dhamira ya kila chama cha siasa ni kushika dola, hivyo anaamini vyama vyote vina malengo hayo pia.

“Hata kama vikiwepo vyama viwili au kama vyote vikijitoa lakini kwa sababu vyote vilishaweka wagombea tukienda kwenye uchaguzi bila kujitokeza, aliyeshinda uchaguzi atatangazwa.

“Baada ya matokeo ndiyo tutajua kitakachofuata kwa mujibu wa sheria na iwapo kuna kasoro na kwa kuwa Baraza la Wawakilishi litakuwepo litatafuta namma ya kutatua utata huo,” alisema Vuai.

Alisema suala hilo bado halina haja ya kulifanyia utabiri kwa kuwa uchaguzi bado na vyama vyote viliweka wagombea, hivyo uwezekano wa CCM kubaki pekee yake hautakuwapo.

Alipoulizwa iwapo anaridhishwa na sababu za kurudiwa uchaguzi huo, alisema kwa hali ilivyokuwa taratibu nyingi na sheria zilivunjwa na CCM walitoa malalamiko ya mawakala wao kunyimwa vitambulisho tangu saa 4:00 asubuhi siku ya uchaguzi wa mwaka jana

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s