Sumaye: Urais Z’bar angepewa Maalim Seif

Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye
Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Frederick Sumaye

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye amesema ingekuwa busara kumpa ushindi mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na CCM irudi nyuma kujipanga upya kwa kuwa tofauti ya ushindi baina ya pande hizo mbili ni ndogo.

Mtendaji huyo mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu pia ameonya kuwa bila ya CUF, hakutakuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) na kama itaundwa baada ya kurudiwa kwa uchaguzi Machi 20, haitaendeleza mshikamano.

Kauli ya Sumaye pia imekuja katika kipindi ambacho Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha ametoa tamko kuwa pamoja na vyama kutangaza kutoshiriki, hakuna kilichofuata taratibu za kujitoa, kauli inayokosolewa na wanasiasa na wanasheria. Sumaye, ambaye amehamia Chadema, alitoa rai hiyo katika mahojiano maalumu na Mwananchi ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Waziri mkuu huyo wa zamani alisema kwa mujibu wa matokeo yaliyokuwa yameshatangazwa, inaonekana yeyote ambaye angeshinda, angepishana kidogo kwa kura na mpinzani wake na hivyo wote kuwa na nafasi inayolingana serikalini.

“Kwa utaratibu huu wa mseto uliopo na kwa matokeo yaliyokuwa yameshatangazwa, ile sehemu ambayo ilikuwa imeshatangazwa, ilikuwa inajulikana kwa jimbo nani ameshinda. (Hivyo) Serikali ya Zanzibar; atawale CUF, atawale CCM ni 50 kwa 50 ilikuwa.

“Sasa kama imefika 50 kwa 50, hivi mnauana nini hasa? Tunauana nini? Pride (majivuno) tu ya kusema mpinzani hatawali? Why? “Kwa hiyo, ndiyo kitu ambacho mimi nasema; ningekuwa na mamlaka hayo na madaraka hayo, ningesema tu miaka mitano si mbali.

Huyo, kama kweli Seif alishinda, ambayo ni kweli alishinda uchaguzi, mpeni. Halafu tujipange huko mbele ya safari. Si tutapiga tena uchaguzi,” alidai Sumaye ingawa matokeo ya Zanzibar hayajawahi kutangazwa.

Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha alifuta matokeo ya uchaguzi wa rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani Oktoba 28, siku ambayo alitakiwa atangaze mshindi wa kinyang’anyiro cha urais.

Wakati akitangaza, tayari matokeo ya majimbo 31 yalikuwa yameshatangazwa huku majimbo mengine tisa yakiwa yameshahakikiwa na kusubiri kutangazwa. Pia siku hiyo, tayari washindi wote wa viti vya ubunge, uwakilishi, na udiwani walishatangazwa na kupewa hati za ushindi isipokuwa kwenye maeneo yaliyokuwa na matatizo.

Sumaye alisema uamuzi huo wa Jecha haueleweki. Alisema kuna maneno mengi ya ubishani ambayo yamekuwa yakisemwa kwamba Zanzibar wana tume yao na Bara iko Tume ya Taifa ambayo ni NEC na kwamba visiwani kuna katiba yao tofauti na huku. Alisema maneno hayo hayasaidii.

“Tunaangalia jinsi uchaguzi unavyosimamiwa,” alisema. Alisema anayesimamia uchaguzi wa Zanzibar ni ZEC kwa kuwa inakuwa imekasimiwa madaraka na NEC.

“(Kwa) wapigakura ambao wanasimamiwa na ZEC, mtu anachukua karatasi tano; tatu zinapigia Zanzibar, mbili zinapigia Jamhuri. lakini ni mtu huyo huyo, wakatio huohuo, na masanduku yapo pale yamepangwa,” alisema.

“Si kama inavyozungumzwa kana kwamba hawa watu siku ya kwanza walipigia ya Zanzibar, au siku ya kwanza walipigia ya Jamhuri mambo yakawa mazuri, siku ya pili ya Zanzibar, kukawa na vurugu. Hakuna kitu cha namna hiyo.”

Alisema hata makamishna wa ZEC hawakwenda kwenye majimbo kuhakiki, bali walipata taarifa kutoka kwa wasimamizi, ambao waliona kuwa hakukuwepo na kasoro zozote hadi wakatangaza washindi. “Yule anayesimamia pale hakulalamika.

Hii ZEC na si ZEC yote sasa. Mwenyekiti anafumuka na kusema ziko taratibu za hovyo zimetumika, amezitoa wapi?” alihoji. Alisema hadi sasa hakuna anayejua hitilafu hizo, na hata Maalim Seif amekuwa akiwauliza kwenye vikao vyao, lakini hawajamuonyesha.

“Nadhani kinachotokea Zanzibar ni kwamba tu, mimi kwa jinsi ninavyoona, chama tawala kimeamua hakuna chama cha upinzani kutawala popote,” alisema Sumaye. CUF imesema kufuta uchaguzi si halali kikatiba na hivyo haitashiriki uchaguzi wa marudio kwa kuwa ni batili.

Uamuzi huo unaungwa mkono na takriban vyama nane kati ya 14 vilivyosimamisha wagombea urais kwenye uchaguzi wa Oktoba 25. CCM imesema itashiriki. Kuhusu suala hilo, Sumaye alisema iwapo utasusiwa halafu ukaendelea kufanyika, tafsiri yake ni kuwa hakuna demokrasia.

Alisema Wazanzibari walishafikia mahali pazuri ndio maana wakaunda serikali ya mseto, lakini ule ustaarabu ulioletwa na serikali ya mseto, sasa unavurugika. SUK iliundwa baada ya CUF na CCM kufikia maridhiano yaliyorasimishwa kwa kurekebisha katiba na hivyo kuanza kufanya kazi rasmi baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Dk Ali Mohamed Shein akiwa rais na makamu wake wa kwanza akiwa Maalim Seif.

“Kwa hiyo tusidanganyane hapa; bila ya CUF hakuna mseto Zanzibar,” alisema Sumaye. “Najua wanataka kuingiza vyama vingine, sijui ADC, sijui nini. Bila ya CUF, mnaweza kupata mseto wa jina, lakini hautaweka mshikamano ndani ya nchi. Kwa hiyo kuna umuhimu kabisa, wanaohusika waone hilo.”

Sumaye alisema hali ya kisiasa Zanzibar baada ya marudio ya uchaguzi, haieleweki kwa kuwa hakuna anayejua kitakachotokea. “Siwezi kusema nchi itaingia kwenye mapambano, siwezi kujua.

Mimi sitaki kutabiri mabaya, lakini hali inaweza isiwe nzuri sana, hatuwezi kujua,” alisema. “Inawezekana Wazanzibari wakanyamaza kimya wakasema ‘ah bwana, wacha tu lipite’. Tutamshukuru Mungu kama ikiwa hivyo.

Lakini wakisema ‘bwana sisi hapana’, tutaingia kwenye matatizo makubwa. Na kama tunavyosema siku zote, Zanzibar kukiwa na vurugu, Bara hatuwezi kuwa salama.”

Alisema kuvuruga amani ni kitu kidogo sana, lakini ikivunjika haitulizwi kwa mabomu wala mitulinga. “Ukisema vurugu ikitokea utapiga mabomu au utaleta zana nzito kiasi gani za kupiga watu, haisaidii sana,” alisema. “Hata ukiua wangapi bado utakuwa haujatatua tatizo.

Nawaomba sana tumwombe Mungu aweke busara kwa viongozi wetu, waliamue jambo hili bila kusababisha vurugu.” Jecha akosolewa Visiwani Zanzibar jana, viongozi wa kisiasa na wanasheria wamesema Jecha amezidi kujichanganya kwa kauli yake kuwa hakuna mgombea aliyemtaarifu kujitoa kihalali kwenye uchaguzi wa marudio.

Wadau hao wamesema Jecha amefanya hivyo kwa lengo la kujenga taswira kwamba uchaguzi huo umefuata taratibu. Waliotoa kauli hiyo ni pamoja na Naibu Katibu wa ACT­Wazalendo Zanzibar, Juma Said Sanani aliyewaambia waandishi wa habari kuwa ZEC ilishafuta uchaguzi, hivyo ilifuta kila kitu.

“Kwa nini ZEC ilituletea tena barua ya kutaka tuthibitishe wagombea, walitaka tuthibitishe nini? Sisi tuliwaandikia barua kwamba hatutashiriki uchaguzi wa marudio,” alisema Sanani.

“Tunachosema ni kuwa uchaguzi ulishafanyika na ndiyo msimamo wa chama chetu. Mimi nadhani Jecha na wenzake wanatafuta namna ya kuendelea tu na huo uchaguzi. Alisema ZEC inapodai vyama nane kati ya 14 vilivyojitokeza awali, vitashiriki uchaguzi, hivyo vilivyojitoa vimetumia utaratibu gani.

Sanani alisema hata kama aliyekuwa mgombea wao wa urais, Khamis Iddi Lila, amejipeleka ZEC kutaka kushiriki, haiwakilishi ACT kwa kuwa chama kilishasitisha na kumvua uanachama.

Pia Naibu Katibu Mkuu wa APPT­Maendeleo, Faki Hamad Faki alisema msimamo wa chama chake, ambacho kilimuunga mkono mgombea wa CUF kwa mwamvuli wa Ukawa, Maalim Seif, ni kutoshiriki uchaguzi wa marudio.

Pia Masoud Fakih Masoud, ambaye ni mwanasheria, alisema tamko la Jecha linazungumzia uchaguzi wa Oktoba 25. Masoud alisema kuwa Jecha alitangaza kasoro zilizojitokeza kuwa ni pamoja na kuzidi kwa idadi ya kura, lakini ameshindwa kuubainishia umma marekebisho ya Daftari la Wapigakura yaliyofanywa.

“Kwa mantiki hiyo Tume isijaribu kupoteza muda, ikae pamoja kukamilisha kazi ya kumtangaza mshindi wa urais wa Uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 ili aweze kuapishwa”.

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s