Kwa nini Jecha anavikwepa vyombo binafsi vya habari?

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Bw. Jecha Salim Jecha
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Bw. Jecha Salim Jecha

Febuari 21, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha ametoa taarifa kwa umma kuhusu Uchaguzi Mkuu wa marudio unatarajiwa kufanyika Machi 20, mwaka huu visiwani humo. Katika ofisi za ZEC zilizopo Maisara mjini Unguja, Jecha alikaririwa akisema maandalizi ya uchaguzi huo wa rais, wawakilishi na madiwani yamekamilika na utoaji elimu kwa wasimamizi umeanza.

Vilevile, alisema ugawaji wa vifaa na makaratasi ya kupigia kura utaanza kufanyika hivi karibuni baada ya kupokelewa na ZEC. Hata hivyo, Jecha katika taarifa yake alisema wagombea wengi hasa wa Chama cha Wananchi (CUF) licha ya kuandika barua za kujitoa katika ofisi za ZEC wilaya na makao makuu, hakuna barua hata moja aliyefuata utaratibu wa kisheria na kwa mantiki hiyo, ZEC ina wahesabu wagombea hao ni halali katika uchaguzi huo wa marudio.

Lakini, utaratibu uliotumika wa utoaji wa taarifa hizo siyo ule wa kawaida ambao umezoeleka kwa waandishi wa vyombo vya habari nchini wa kuitwa na tume hiyo kusikiliza taarifa iliyotaka kuhabarisha au kuelimisha umma, kisha kuulizwa maswali na wahusika kuyajibu.

Utaratibu huu mpya ambao umebuniwa na kutumika kwa sasa siyo wa kutenda haki kwa vyombo vya habari vyote, bali ni wa kubagua baadhi ya wanavyovitaka na wasivyovitaka hupewa taarifa kwa kupelekewa kwa kuwa hutolewa bila ya wao kuwapo na kuvikosesha uhuru wa kuuliza maswali na kupata taarifa ambazo chombo husika kinahitaji kuhabarisha umma.

Ni kwamba ZEC huitisha vyombo vya habari vya Serikali pekee nao siyo kwamba wanakwenda waandishi wote, bali huitwa mpigapicha mmoja kutoka Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na ofisa wa tume hiyo ambaye hupeleka taarifa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC). Chini ya utaratibu huo, mwenyekiti huyo hurekodiwa taarifa yake yote, kisha hataki kutoa ruhusa ya kuulizwa swali hata moja na kuwaomba wapigapicha hao waondoke na waandishi wengine kutakiwa kuzifuata taarifa hizo baada ya Jecha kumaliza kurekodiwa.

Kama kuna waandishi wengine wamekaa nje wakisubiri taarifa hizo, wataitwa wakachukue na kama hawapo, atapewa mwandishi mmoja azisambaze kwenye vyombo vingine vya habari ili ziufikie umma kupitia magazeti, redio na televisheni.

Hili siyo tukio la kwanza kwa Jecha kuamua kutumia utaratibu huo, bali ni mara ya tatu, hata Oktoba 28, 2015 alitumia utaratibu huo kwa kujifungia na kutoa taarifa za kufutwa kwa uchaguzi huo hadi hapo alipotangaza kuwa utarudiwa Machi 20 kwa kuita vyombo vya Serikali.

Januari 22, kuanzia asubuhi ulinzi uliimarishwa katika maeneo yote ya Mji wa Zanzibar na ilipofika mchana Jecha akatoa taarifa kupitia Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), akitangaza siku ya kurejewa kwa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.

Utaratibu huo pia ulitumika siku ile ya Oktoba 28, 2015 wakati wananchi wakisubiri kwa shauku kubwa kutangaziwa matokeo ya uchaguzi huo katika kituo cha kujumlishia kilichokuwa katika Hoteli ya Bwawani mjini Unguja.

Makamu Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Abdulhakeem Ameir Issa akiwa na baadhi makamishna wa tume hiyo wakiendelea kutangaza matokeo ya majimbo ya uchaguzi, ghafla hali ikabadilika katika hoteli hiyo baada ya idadi ya wanajeshi wanaolinda eneo hilo kuongezeka.

Kila mmoja alishangaa kuona wanajeshi wamezingira hoteli hiyo, baadhi wakiwa wamelala chini, wengine wakilinda lango la kuingilia na kutokea na kuwaamuru watu waliokuwapo ndani wasitoke nje na kupiga marufuku waliokuwa nje kuingia ndani.

Kwa muda mfupi wananchi wachache, waandishi wa habari na waangalizi wa ndani na nje ya nchi wa uchaguzi huo walishuhudia amri za kijeshi zikitumika “ rudi, toka hapa, ingia ndani, hakuna ruhusa kutoka” .

Nyakati hizo hizo, ikasikika sauti ya Jecha kupitia ZBC, akitangaza kufutwa kwa uchaguzi huo kutokana na kasoro zilizojitokeza. Kama ni filamu au mchezo wa kuigiza , kila mmoja alikuwa amepigwa butwaa na hakuna aliyeamini, lakini ndiyo imetokea.

Wakati huo baadhi ya waandishi wa habari walipigiwa simu wakitakiwa kuondoka Bwawani kwa kuambiwa kwa kifupi “Ondokeni hapo hakuna kinachoendelea rudini nyumbani”.

Na waandishi hao wakahimizana kuondoka huku wengine tuliobaki tukikumbana na majeshi tukabaki heee!. Tukashangaa, lakini tulibaki hapo hapo. Waandishi wengi wanauliza ni kwa nini ZEC inatumia utaratibu huo mkongwe ambao uliwahi kutumika mwaka 2000 wakati wa kumtangaza mshindi wa urais, Amani Abeid Karume wakati huu wa uwazi?

Nakumbuka mwaka 2000 wakati wa kumtangaza rais waandishi kadhaa wa vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi tuliachwa kwenye lango la ofisi ya ZEC tukisubiri kuitwa, lakini kilichotokea ni waandishi wa vyombo vya Serikali pekee ambavyo ni TVZ na (Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ) ndivyo vilivyoingizwa ndani na kupewa matokeo ya mshindi wa uchaguzi huku wengine wakiambiwa nendeni mkasubiri saa 9:00 alasiri atatangazwa mshindi huyo kupitia vyombo hivyo.

Tunafahamu ZEC ilipewa mafunzo na Shirika la Maendeleo la Kimataifa (UNDP) tangu mwanzo wa mchakato mzima wa uchaguzi na kutakiwa kuendesha mambo yao kwa uwazi na kuwashirikisha wadau wote wa uchaguzi wakiwamo wanasiasa, asasi za kiraia ambazo zinawashirikisha watu wenye ulemavu, vijana, wanawake na waandishi wa habari.

Mwanzo walianza vizuri kwa wadau wote kushirikishwa kikamilifu kwa shughuli hizo kufanywa kwa uwazi tokea kuanza kwa mchakato wa kutangaza siku za uchaguzi, kampeni, kuchukua fomu wagombea, kupokelewa kwa vifaa vya uchaguzi.

Hata wakati wa kupokea makaratasi ya kura waandishi wa habari walikesha na maofisa wa ZEC, akiwamo Mkurugenzi, Salum Kassim Ali, Mwenyekiti Jecha, makamishna na maofisa wa tume hiyo tangu saa 3 usiku hadi saa 10 alfajiri uwanja wa ndege wakisubiri kutoka Afrika ya Kusini.

Tunaweza kujiuliza ni nini kimezidi hata ikawa Jecha na ZEC wanavitenga vyombo vya habari binafsi na kuvialika vile vya Serikali pekee? Je, kuna kosa ambalo vimekosa au ni kitu gani kisichozungumzika?

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s