Zanzibar wasikubali kupelekeshwa – Job Lusinde

Balozi Mstaafu Job Lusinde na  Mwenyekiti wa Baraza la wazee Mkoa wa Dodoma.
Balozi Mstaafu Job Lusinde na Mwenyekiti wa Baraza la wazee Mkoa wa Dodoma.

MWANDISHI Wetu GRACE CHILONGOLA, amefanya mahojiano na Mwanasiasa Mkongwe nchini na Waziri wa kwanza wa Serikali za Mitaa, Balozi Job Lusinde, kuhusu uchaguzi wa marudio Zanzibar unaotarajia kufanyika Machi 20, mwaka huu pamoja na maoni yake kuhusu mwenendo wa Serikali ya Awamu ya Tano

.
Raia Mwema: Kama mwanansiasa mkongwe nchini unazungumziaje sintofahamu ya uchaguzi wa marudio Zanzibar?

Lusinde: Wazanzibar waangalie maslahi ya Taifa kwanza, Tanzania na Zanzibar katika lolote wanalotaka kulifanya, na wasiangalie habari ya mimi ndio kiongozi au nani awe kiongozi.

Waangalie jinsi wenyewe walivyopata kuwa na serikali ya mseto, walikuwa na sababu nzuri ya kuwa na umoja wa kitaifa hivyo wanapaswa kulipa nafasi.Katika hilo lazima watazame lipi lenye faida kwao katika hali waliyonayo sasa baada ya uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana kufanyika na kufutwa, wanapaswa kujihoji sasa wanakwenda wapi.

Wameona kuna haja ya kurudia uchaguzi, anawaunga mkono kwani inaweza kuwaletea mapatano mazuri kwa nchi yao.Wanaotaka kujitoa anawaomba wajitafakari na kurudi kufanya uchaguzi, waangalie changamoto zilizojitokeza kwenye uchaguzi uliopita ili zisijitokeze tena na uchaguzi uende vizuri, atakayeshinda kashinda.

Nategemea viongozi wa pande zote watatumia busara zao, hata kama wana mpango wa kujitoa nawaomba washiriki kwenye uchaguzi.

Raia Mwema: Iwapo Chama cha Wananchi (CUF ) hakitashiriki uchaguzi huo wa marudio kama ambavyo kimesema nini kinaweza kutokea?

Lusinde: Kwa kawaida mahali ambapo chama kimoja kinakataa kushiriki uchaguzi, vyama vingine vikashiriki, matokeo yatakayotoka ndiyo yatakayofuatwa.

Kama wanadhani wao (CUF) ndio wenye maslahi ya Taifa washiriki uchaguzi wa marudio, wasiposhiriki na wenzao wakashiriki wataunda serikali na wao watasubiri miaka mitano mingine.

Tunaomba kama hawashiriki, tafadhali wasilete fujo, wasiwatishe watu na badala yake wawahimize waende wakapige kura kwa utulivu kumchagua rais wanayemtaka. Unaweza ukawashawishi watu na wanachama wako wasiende kupiga kura, lakini hawapaswi kuwazuia wanaotaka kwenda kupiga kura, kupiga kura ni haki yao ya msingi ya kuchagua kiongozi.

Raia Mwema: CUF kimekuwa kikidai kuwa kiliongoza kwenye uchaguzi uliofutwa, je unadhani wakishiriki katika uchaguzi wa marudio sintofahamu hiyo inaweza kujitokeza tena?
Lusinde: Kwa sababu sijui undani wa hayo unayoyasema nitakuwa sina majibu, mimi ninachojua ni kuwa mtu mmoja kajitangazia ushindi ambaye sio kazi yake, mwenye jukumu la kutangaza matokeo akaamua kuyafuta na sasa ametangaza tarehe nyingine ya uchaguzi wa marudio.

Kusema walinyimwa haki siwezi kuwasemea kwa sababu sijui undani wake, kwa yote yaliyotokea waende kwenye uchaguzi. Watazamaji wa mwenendo wa uchaguzi wajitokeze kwa wingi kama ilivyokuwa awali, wafike 400 kama awali wote waende wakashuhudie uchaguzi Zanzibar kwenye kila kituo atakayeshinda atakuwa ameshinda.

Raia Mwema: Migogoro inayoendelea Zanzibar inachangia kwa namna gani kuvuruga amani ya nchi iliyojengeka kwa muda mrefu?

Lusinde: Amani ya nchi lazima ilindwe, tunawaomba wananchi wa Zanzibar wasikubali kupelekeshwa mpaka wafike kuwe na uvunjifu amani.

Viongozi wote waweke maslahi ya nchi mbele kwa kutofanya lolote ambalo litavuruga amani. Waende wakafanye uchaguzi, waliopo kihalali kwenye daftari la wapiga kura wajitokeze kupiga kura, sidhani kama matokeo yatakuwa tofauti sana.

Mahali pengine unakuta watu wengi kuliko waliojiandikisha pale, sasa wametoka wapi, vitu kama hivyo ni vyema wakaviangalia mapema ili uchaguzi wa marudio visijitokeze tena na kuvuruga uchaguzi. Zanzibar wameshaona vurugu nyingi za uchaguzi tunaomba zisirudiwe.

Raia Mwema: Unadhani Serikali ya Muungano itaongozwaje iwapo uchaguzi wa marudio utampa ushindi mgombea Urais wa Chama cha Wananchi (CUF)?

Lusinde:Tusubiri tuone, kama Maalim Seif atachaguliwa basi kutakuwa na namna ya kushirikishana uongozi, mfumo wa utendaji kwa upande wa Zanzibar hakuna tatizo anayechaguliwa ndio anakuwa Rais.

Changamoto itakuwa Serikali ya upinzani ndani ya Muungano, ikitokea litazungumzwa na mfumo utatengenezwa, mfano kuwa Muungano ulipoanza Hayati Abeid Karume alikuwa makamu wa rais wa kwanza na hayati Rashid Kawawa akawa makamu wa pili wa rais, kwa mujibu wa Katiba, Karume alikuwa Makamu wa kwanza wa Rais hivyo chaguzi nyingine zilipotokea Karume aliendelea kuwa Makamu wa kwanza wa rais.

Rais wa Zanzibar si Makamu wa rais wa Muungano hivyo hata akiwa wa upinzani hawezi kuwa makamu wa Muungano, Rais wa Zanzibar ni sehemu ya Muungano na anaingia kwenye vikao vya baraza la mawaziri.

Tofauti ni pale anapokuwa ametoka upinzani hawezi kuingia kwenye baraza kwa sababu hatoki kwenye Chama kilichoshinda kwenye Muungano. Kwa Zanzibar kuwa na rais kutoka upinzani hakuwezi kubadilisha muundo wa serikali.

Raia Mwema: Ni kwa namna gani Ukawa inachangia migogoro ya kisiasa inayoendelea Zanzibar?

Lusinde: Wanatafuta maslahi zaidi kuliko mustkabali wa nchi, kule Zanzibar CUF ina nguvu kuliko Chadema, Lowasa anaisaidia CUF na si Chadema kwa Zanzibar. Wanasababisha migogoro isiyo na maslahi kwa nchi.

Raia Mwema: Unazungumziaje utendaji wa serikali ya awamu ya tano?

Lusinde: Nampongeza Rais John Magufuli kwa staili yake ya uongozi, Mungu amzidishie afya njema, busara na hekima ili aweze kuweka muundo wa serikali katika maono yake na taifa.

Anataka Taifa lenye maadili,siku za nyuma yalikuwepo lakini sehemu nyingine yalilegea lakini sasa lazima yarejeshwe ili Taifa liwe na maadili na nidhamu.

Tayari ameanza na katika muda wa miezi sita hadi mwaka atakuwa ameliweka taifa kwenye maadili mapya na mazuri yaliyoota mizizi.

Rais anasisitiza kuchapa kazi za serikali kwa saa 8 zenye tija na sio saa mbili unafanya kazi za serikali halafu unahamia sehemu nyingine binafsi. ‘Hapa kazi tu’ inarudisha nidhamu kazini.

Ukwepaji wa kodi umeanza kudhibitiwa na makusanyo yameanza kuongezeka ambapo ni jambo jema maana kodi isipokusanywa maendeleo hayawezi kupatikana, ujenzi wa reli na barabara utashindikana., kama Taifa linahitaji kufanya mambo mengi hivyo Rais na watendaji wake wanapaswa kupongezwa kwa hatua waliyoanza nayo kwa upande wa kodi Serikali yeyote inayotaka kuendelea ni lazima ikusanye kodi na watu walipe kodi, naona nidhamu ya kulipa kodi inaanza kuja hivyo katika muda mfupi ujao tutakua tumefika kilele cha watu kukumbuka kulipa kodi na sio kukwepa na nidhamu kuingia kazini na Taifa.

Rushwa ilifikia mahali pabaya pa kuwaaminisha watu kuwa bila kutoa rushwa hawawezi kupata huduma inayofaa kwenye maeneo mbalimbali ya upatikanaji wa huduma ikiwemo hospitalini na sehemu za kazi, wakati huduma hiyo hiyo wangeweza kuipata bila kutoa rushwa.Tabia hiyo ni lazima ivunjwe.

Suala la kulindana, hasa kulinda uhalifu lilikuwa kubwa, kwenye ujangili, ndani ya ofisi na kwenye vyama, sasa vinahitaji kusawazishwa na hilo linawezekana kwa mtu mchapakazi kama Rais Magufuli na wenzake aliowachagua.

Litachukua muda kubadilika lakini inawezekana. Sambamba na kuingiza adhabu kali kwa muda wa kati ya miaka mitatu hadi mitano ili changamoto za rushwa na kulindana ziweze kupungua.

Rushwa ipo hata kwenye Biblia imeandikwa, ili kuikomesha adhabu lazima ziwe kali kwenye baadhi ya sheria na kuipunguza sambamba na elimu kutolewa na kwamba itafika mahali rushwa haitakuwa na nguvu tena kwani kila mtu atatimiza wajibu wake.

Chanzo: Raia Mwema

One Reply to “Zanzibar wasikubali kupelekeshwa – Job Lusinde”

  1. Mtihani . Lusinde anaangalia upande wa kwake tu.Leo,Schein ametuhakikishia kuwa Muungano na mapinduzi lazima yalindwe kwa hali yoyote ile. Haya twendeni tutafika.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s