Kikwete amesahau wosia wake mgogoro wa Zanzibar?

Rais Jakaya Kikwete, akifurahia jambo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, walipokutana kwa mazungumzo ya faragha Ikulu jijini Dar es Salaam jana. Picha: Adam Mzee
Rais Jakaya Kikwete, akifurahia jambo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, walipokutana kwa mazungumzo ya faragha Ikulu jijini Dar es Salaam jana. Picha: Adam Mzee

By Yusufu Ahmadi,Mwananchi

Kimaumbile kwa mwanadamu yeyote yule kusahau ni suala la kawaida, kwani hata baadhi ya mafundisho ya dini yanatwaambia kwamba, tusingeitwa binadamu ila ni kwa kusahau, hivyo haishangazi kwa mtu kusahau jambo.

Hivyo, kwa muktadha huo, leo naomba nimkumbushe nami pia, kujikumbusha wosia wa Rais wangu mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alioutoa kwa Watanzania katika sherehe za maadhimisho ya miaka 52 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Desemba 9, mwaka 2013.

Itakumbukwa kuwa mwezi huo ndiyo alikuwa amefariki dunia, Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela na raia wa nchi hiyo walikuwa katika majonzi ya kumpoteza kiongozi waliyempenda.

Kikwete alitumia fursa hiyo kumzungumzia Mandela na kuwataka Watanzania kumuenzi kwa kuiga mambo mema aliyoyafanya.

Rais aliyotutaka Watanzania tuige busara za Mandela za kutobeba kinyongo cha kulipiza kisasi kwa maadui zake (makaburu), ambao walimfunga jela miaka 27, wakati kiongozi huyo akiwa katika jitihada za kutafuta uhuru wa taifa lake la Afrika Kusini chini ya chama cha Africa National Congress (ANC).

Mzee Mandela alitolewa jela mwaka 1990 na baadaye kuwa Rais wa Afrika Kusini huru, hakutaka kulipa kisasi kwa
Badala yake, Mandela aliunda tume ya maridhiano iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Askofu Desmond Tutu, ikiwa na lengo la kuwaleta Waafrika Kusini pamoja, kusameheana na kufungua ukurasa mpya wa maisha usiokuwa na visasi na chuki.

Hizo ndizo busara ambazo Kikwete alituusia kwa dhati tuzibebe katika mioyo yetu popote twendako, ili kuhakikisha Watanzania tunaishi kwa amani na uvumilivu bila ubaguzi.

Ushauri huo ulikuwa mzuri ikizingatiwa kwamba Taifa limekuwa na majeraha yaliyotokana na chaguzi mbalimbali tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa nchini mwaka 1992.

Inaonekana Rais wangu mstaafu Kikwete ameshasahau wosia wake huo na busara za mzee Mandela, kwani hivi karibuni wakati akihutubia katika sherehe za kuadhimisha miaka 39 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Singida, akiwa pia, ndiyo mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, amewataka wafuasi wa CCM Zanzibar kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa marudio Machi 20, mwaka huu.

Rais wangu mstaafu huyo, Kikwete ambaye aliwahi kusaidia kutanzua mgogoro nchini Kenya mwaka 2008 uliosababishwa na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007 na pia, kwenda kusaidia kuvikomboa Visiwa vya Comoro, ameshindwa kulitazama suala la marudio ya Uchaguzi wa Zanzibar kwa jicho la tofauti.

Uchaguzi umesusiwa

Ukiachia mbali suala la utata wa kikatiba na kisheria unaogubika uchaguzi huo, tangu kufutwa kwake hapo mwaka jana na mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha na kutangazwa kufanyika tena na mwenyekiti huyo, mustakabali wa visiwa vya Zanzibar kwa sasa unahitaji kufikiwa kwa maafikiano ya Wazanzibari wote.

Visiwa hivyo vinaingia katika uchaguzi wa marudio uliosusiwa na chama kikuu cha upinzani, Chama cha Wananchi (CUF) huku ukiwa umegubikwa na dalili za wazi za kibaguzi kutokana na matamshi ambayo yalitolewa hivi karibuni na baadhi ya viongozi wa CCM-Zanzibar na wafuasi wake.

Mfano ni lile bango la wafuasi wa CCM lililoonyeshwa katika sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi Zanzibar likiwataka machotara wajijue wao ni wageni visiwani humo kwani hivyo ni visiwa vya Waafrika.

Sijui niseme ni bahati mbaya au la, wakati hisia za visasi zikionekana kuchipuka tena visiwani humo, Rais mstaafu Kikwete ‘anayeumizwa’ na matatizo ya nchi za wengine, kama alivyofanya nchini Kenya, Visiwa vya Comoro, haonekani kuguswa na hali hiyo inayoweza kuja kuwa chungu hapo baadaye, badala yake anawatia shime wafuasi wa chama chake huko Zanzibar wajitokeze kwa wingi katika uchaguzi wa marudio.

Kwa mtu kama Kikwete aliyejijengea haiba ya kidiplomasia nje ya nchi na akiwa mwenyekiti Taifa wa CCM nilitarajia kumuona akichukua jitihada kadri awezavyo kuhakikisha kwanza viongozi wa visiwa hivyo wanaunda tume ya maridhiano na usawa ili kuzima hisia za visasi na ubaguzi zinazofukuta visiwani humo ili Uchaguzi Mkuu huo unaporejewa, Wazanzibari wawe wamoja, wasio na chuki wala visasi.

Tume ya maridhiano

Suala la kuundwa kwa tume ya maridhiano visiwani Zanzibar siyo jipya, kwani mwaka 1964 chini ya Rais wa kwanza, Abeid Amani Karume kulitolewa amri ya Rais (Presidential decree) namba 6 inayojulikana kama ‘Usawa, maridhiano na umoja wa watu wa Zanzibar’, ambayo lengo lake kuu lilikuwa kuondoa ubaguzi, uadui uliokuja kutamalaki baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Utekelezaji wa suala hilo haukuishia kwenye makaratasi, bali mzee Karume alionyesha anaongozwa na dhamira ya dhati ya kuondoa ubaguzi na uadui, alimteua Salum Rashid (chotara), hizbu aliyekuwa mfuasi wa chama cha Umma kuwa katibu mkuu wa Baraza la Mapinduzi.

Pamoja na kwamba ubaguzi na visasi viliendelea kuwapo mambo yalikuja kubadilika baada ya kuanza tena kwa mfumo wa vyama vingi visiwani humo ambapo CUF ilionekana bado kama ni mtoto wa vyama vya Waarabu vya ZNP na ZPPP.

Hivyo basi, Rais Kikwete kama alivyotuhusia sisi kuacha mambo ya kulipizana visasi naye angepaswa kutumia busara za mzee Mandela na Karume ili kuhakikisha tume ya maridhiano inaundwa visiwani ili kuwaleta pamoja Wazanzibari na kuzika hisia za kubaguana na kulipizana visasi, lakini yeye na chama chake wamekimbilia katika uchaguzi wa marudio.

Rais mstaafu Kikwete, lazima afahamu kuwa hata kama chama chake cha CCM kitashinda katika uchaguzi huo wa marudio, kitakuwa kikiendesha Serikali na nchi ambayo watu wake wamegawanyika.

Jambo hilo linainyima Serikali sifa ya uadilifu na kupunguza imani kutoka kwa wananchi wake kusaidia maendeleo.

Mwandishi wa makala hii ni mwaandishi wa habari. Anapatikana kwa simu, 0658010594 au barua pepe: maoni@mwananchi.co.tz .

Chanzo: Mwananchi

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s