Wanaibeba CCM kuitusi demokrasia

Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Jaji George Masaju akitoa hotuba yake katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji George Masaju akitoa hotuba yake katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo kwa hakika ni Rais John Magufuli, imefanya uamuzi kwamba ni lazima Wazanzibari – wananchi wa Unguja na Pemba – wafanye tena uchaguzi wa viongozi wa kuwawakilisha kwa miaka mitano mingine ijayo.

Kwa hivyo, inaposema bado kuna nafasi ya mazungumzo katika kupata suluhisho la mgogoro wa kisiasa Zanzibar, inadanganya wananchi hao, umma wa Watanzania, na ulimwengu mzima.

Inasikitisha zaidi kuona uongozi wa jamhuri unadanganya kwa njia ya kejeli pia – kule kusema watu wengi wangependa Chama cha Wananchi (CUF) kithibitishe kukubalika kwake kwa njia ya sanduku la kura kwa kushiriki kiitwacho “uchaguzi wa marudio” uliopangwa tarehe 20 Machi 2016.

Kauli hii inayoendana na msimamo wa uamuzi uliokwishafanywa na Rais Magufuli, ni kielelezo cha waziwazi kuwa yeye binafsi, yeye katika wadhifa alionao, na yeye katika uhusiano wake wa kindakindaki na Chama Cha Mapinduzi (CCM), hawana nia njema ya kuona mgogoro unatatuliwa kwa mujibu wa sheria.

Ndivyo ninavyoona kwa sababu nyingi. Kwanza, wakati kiongozi huyu wa jamhuri – ambayo inaundwa na Tanganyika na Zanzibar – anataka CUF ishiriki uchaguzi, wasaidizi wake serikalini walitangulia kumpotosha kwa kauli za kukanganya.

Februari 5 bungeni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju alisema si sahihi wabunge kumtaka Rais Magufuli kuingilia mgogoro wa Zanzibar kwa sababu hana mamlaka maana Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) inazaliwa na Katiba ya Zanzibar ambayo (anasema) si jambo la Muungano.

Sina elimu ya sheria lakini ninajua uchaguzi ni suala la kisiasa pia la kisheria/kikatiba. Ni suala la Muungano, vinginevyo Zanzibar ingekuwa ina vyama vyake kwa sheria ya Baraza la Wawakilishi ambayo ingetambua msajili wa vyama hivyo.

Lakini pia huyu rais ni sehemu mojawapo (ya mbili) ya Bunge, na kama bunge lina wabunge kutoka Zanzibar, wakiwemo watano wanaotokana na Baraza la Wawakilishi, unamtengaje na Zanzibar na kukatalia wabunge kumbana ashughulikie suala linalohusu uchaguzi wa Zanzibar.

Kadhalika, Katiba ya Zanzibar inatambuliwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano maana ndio mkataba wa Wazanzibari na mamlaka mojawapo ya zile mbili (serikali) zinazotambuliwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Katika mkazo wa nukta hii, labda basi Wazanzibari waelezwe kwa ufasaha leo kuwa wao si mali kitu katika kukamilisha wajibu wao wa kutoa mamlaka inayompa ridhaa Rais wa Jamhuri wakati wa uchaguzi.

Hapa najiuliza ndio maana ametangazwa mshindi bila ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuzingatia kura zao (Zanzibar) baada ya uchaguzi wao kufutwa tarehe 28 Oktoba 2015?

AG Masaju ametaja ibara Na.4 na vifungu vyake vinne, ambavyo vinaongeza uzito wa mfungamano wa Rais wa Jamhuri na watu wa Zanzibar na mamlaka ya serikali ya Zanzibar na namna vile inavyotekeleza majukumu yake, likiwemo la kupatikana viongozi.

Lakini hayo yote yawe upuuzi, mwenyewe amesema “masuala ya ulinzi na usalama ndiyo ya Muungano na ndiyo sababu ulinzi umeimarishwa (Zanzibar) kuhakikisha nchi hiyo inakuwa salama.”

Ni kweli Zanzibar ulinzi umeimarishwa, lakini ajue hata ofisi za Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) zilizoko Maisara, mjini Zanzibar, zinalindwa na majeshi hao. Kwa hivyo ni sahihi majeshi kulinda Tume isiyozaliwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano bali ya Zanzibar? Zikitaki mbichi hizi!

Labda mimi sijui, hivi AG anajua kwamba Rais wa Wazanzibari analindwa na majeshi (angalia yule mpambe nyuma yake) ambayo amiri wake ni Rais wa Jamhuri? Anajua kuwa Rais pia ana ulinzi wa Mamlaka ya Usalama wa Taifa (TISS) ambayo nayo inawajibika kwa Rais wa Jamhuri?

Sasa huu mfungamano wa rais kwa baadhi ya mambo tu, lakini akawa hapaswi kujihusisha na suala muhimu la uchaguzi ambalo huwapa haki ya kikatiba wananchi wa Zanzibar ya kuchagua viongozi wao, una mantiki gani? Au ndiyo kielelezo kingine cha mtanziko wa Muungano wa Tanzania wa 1964?

Pili, aliibuka Mwenyekiti wa Tume inayosimamia uchaguzi wa Rais wa Jamhuri, wabunge na madiwani wa Tanzania Bara, Jaji Damian Lubuva aliyetoa uamuzi wa kumzuia Rais Magufuli kuingilia suala la Zanzibar. Eti naye anasema hana mamlaka ya kushughulikia tatizo linaloisumbua sehemu moja ya jamhuri.

Kama msimamo wake huo ni halali, nimwambie Jaji Lubuva kwamba pamoja na hayo niliyoyaeleza kumhusu AG Masaju, muda mfupi kabla ya Mwenyekiti mwenzake wa tume ya Zanzibar, Jecha Salim Jecha kuufisidi uchaguzi halali wa Zanzibar, siku ile ya 28 Oktoba, 2015, kituo cha habari na matangazo ya matokeo ya uchaguzi kilichokuwa Hoteli ya Bwawani, kilizingirwa na majeshi ambayo ni amri ya Rais Magufuli.

Na hata waliofika pale kumchukua kwa njia ya kumteka nyara Makamu Mwenyekiti Jaji Abdulhakim Ameir Issa, na kumpeleka kizuizini kwa muda wa saa tatu makao makuu ya Jeshi la Polisi Zanzibar yaliyoko Ziwani, walikuwa askari wa JWTZ pamoja na Polisi.

Kama Rais Magufuli hahusiki kushughulikia mgogoro wa Zanzibar eti akishauriwa si suala la Muungano, ni nani basi aliamrisha majeshi haya mawili yasaidie kuhujumu maamuzi ya Wazanzibari?

Kwa hivyo suala la uchaguzi wa Zanzibar lisiwe la kumlazimu Rais Magufuli kuhangaikia ufumbuzi, bali yeye yeye awe sawa kuamuru majeshi yaliyo chini yake kuuhujumu uchaguzi unaosimamiwa na Tume ambayo AG Masaju amesema si jambo la Muungano?

Kielelezo kingine cha mkanganyiko katika Muungano wa Tanzania.

Ila katika hili linalohusu msimamo wa Jaji Lubuva nataka kuamini kuwa anajitia pambani kwa kuhofia uingiliaji kati wa Rais Magufuli waweza kugusa kura za kumhalalisha kuchaguliwa ingawa anajua amemtangaza kwa kuzijaliza kura za Wazanzibari.

Kura hizi aliziona sukari na sio shubiri kama zilivyoonekana za uchaguzi wa Rais wa Zanzibar ambazo zimepigwa katika mfumo mmoja wa uchaguzi, kupitia shahada ileile ya uandikishwaji iliyotolewa na ZEC wala si NEC, wapigakura walewale na daftari lilelile.

Tatu, akaibuka Balozi Augustine Mahiga mbele ya mabalozi wageni akiomba wasaidie kumshawishi Maalim Seif Shariff Hamad akubali kushiriki uchaguzi wa marudio. Ni usaliti CUF kushtaki Marekani na Ulaya bali serikali kuwaomba hao wamlainishe Maalim Seif ni sahihi.

Ujanja wa bure, serikali zinatumwa na CCM kulazimisha uchaguzi wa marudio kwa kudai ndio njia sahihi ya kutatua mgogoro, wakidharau kurudi kwenye hoja ya ubatili wa amri ya Jecha kuufuta uchaguzi uliokuwa mzuri.

Chanzo: MwanaHalisi

Advertisements

One Reply to “Wanaibeba CCM kuitusi demokrasia”

  1. Kila mwana CUF, kila mpenzi wa CUF na kila mpenzi wa Zanzibar na kila anaeamini juu ya umoja wa wazanzibari lakini na hasa yule anaeamini kuwa kuna kufufuliwa na kuwa kuna malipo siku ya Kiama basi kilichobora kabisa kwake ni KUTOKSHIRIKI KABISA KUPIGA KURA YA KUTAWALIWA YA TAREHE 20/3/16. Kura hii maana yake ni kuizizimisha kabisa Zanzibar na kufisidi Dini yetu na kumdharau Mwenyezi Mungu . Kwa maana Magufuli na Mkapa wanaendeleza wito wa mtume wao Nyerere juu ya Jihadi ya KUIKATOLISHA ZANZIBAR na watu wake. OGOPA MAGUFULI KULIKO YAHUDI. Ndugu Usiende kabisa kupiga kura. Na ikitokezea kulazimishwa kwa sababu wewe ni kitumwa chao yaani ni mfanyakazi basi HARIBU KURA YAKO.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s