Unapopuuza yako ukashughulikia jirani

Mpiga kura akitumbukiza karatasi yake ya kura ndani ya sanduku la kura za udiwani baada ya kukamilisha hatua za kupiga kura
Mpiga kura akitumbukiza karatasi yake ya kura ndani ya sanduku la kura za udiwani baada ya kukamilisha hatua za kupiga kura

WATU wengi nchini na nje wanauliza maana ya Zanzibar kuendesha uchaguzi wa marudio baada ya ule wa 25 Oktoba 2015 kufutwa katika mazingira yaliyojaa utata kuhusu mamlaka ya kisheria aliyokuwanayo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.

Wanauliza kama uchaguzi wa marudio itakuwa ni hatua inayokuza au kuviza demokrasia Zanzibar.

Unapoliangalia suala hili juujuu utaona kama ni gumu, lakini kwa undani, huioni haja wala faida isipokuwa kupoteza fedha za wananchi na kupalilia uhasama wa kisiasa katika sehemu hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika kuliangalia suala hili ni busara kuukubali ukweli kwamba:

Uchaguzi ulifanyika na kukamilika. Kura zilihesabiwa, washindi wakatangazwa na kupewa hati za kuthibitisha kushinda kwao na fomu za matokeo kubandikwa kwenye kuta za vituo vya uchaguzi nchi nzima. Kwa maana hiyo kilichofutwa si uchaguzi, bali matokeo.

Hapakuwepo taarifa yoyote ya mgombea wa nafasi yoyote, au chama chochote kilichoshiriki uchaguzi kulalamikia ukiukaji taratibu, lakini kilichotokea ni kwamba Mwenyekiti Jecha, ndiye aliyekuwa mlalamikaji, msikilizaji malalamiko na hakimu wa kuyaamua malalamiko hayo.

Hapana kifungu cha sheria kinachompa Mwenyekiti wa ZEC au tume mamlaka na madaraka kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi Na.11 ya Zanzibar ya kufuta matokeo au uchaguzi.

Baada ya Jecha kutoa tangazo la “kufuta” uchaguzi, badala ya kusema anafuta matokeo, umma uliambiwa huo ulikuwa uamuzi wa Tume.

Kama ni hivyo mbona haijaelezwa wazi siku gani kulifanyika kikao cha Tume cha kutoa uamuzi alioutangaza, nani walihudhuria (paoneshwe kumbukumbu za kikao), fomu ya mahudhurio kabla ya tangazo la Jecha kufuta uchaguzi?

Haijawahi hata wakati mmoja Jecha kutoa tangazo muhimu la Tume akiwa peke yake na katika mazingira yanayoonesha usiri. Jecha alitangaza kwa kurekodiwa ndipo kanda ikarushwa na televisheni ya Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC).

Nini kilichosababisha Jecha asitoe tangazo lake katika ofisi zilizokuwa zikitumiwa na Tume wakati wote wa uchaguzi mkuu zilizopo Hoteli ya Bwawani ambako ZEC kwa kusaidiwa na UNDP, ilifungua kituo maalum cha habari na mawasiliano. Wakati wote waandishi wa habari wa Tanzania na nje pamoja na waangalizi wa uchaguzi walikuwa hapo kufuatilia matokeo ya uchaguzi.

Jingine la kuzingatia ni kwamba katika uchaguzi panakuwa na anayeshinda na anayeshindwa. Tatizo ni viongozi wa CCM kusema mara nyingi tena hadharani kuwa hawatakubali kushindwa na wengine kutamba kwamba hata wakipata kura moja jimboni wao ndio wataongoza serikali na si upinzani.

Katika hali kama hii kwa nini uchaguzi urejewe wakati mmoja wa washiriki wakuu haamini katika utamaduni wa kukubali kushindwa?

Mbali na hayo, viongozi kadhaa (si mmoja si wawili) wa CCM wamewahi kusema katika mikutano na hata kwenye Bunge na Baraza la Wawakilishi kuwa mabadiliko ya uongozi wa serikali Zanzibar yasitarajiwe kupatikana kwa njia ya kura. Sababu waliyotoa ni kuwa serikali iliopo ilipata madaraka kwa kubeba silaha na kupindua katika mapinduzi ya Januari 1964.

Kwa hivyo, wale wanaotaka kuongoza hawatapata nafasi labda tu nao watakapotumia silaha za moto na jadi kupindua waliopo kama ilivyotokea 1964. Sasa kama CCM haipo tayari kushindwa ndani ya mfumo wa siasa za ushindani, kwanini kutumike fedha kuitishwe uchaguzi ambao CCM watajitangazia ushindi?

Kuna jingine, mmoja wa washindani wakuu katika uchaguzi Zanzibar, Chama cha Wananchi, kimeamua hakitoshiriki uchaguzi.

Sasa ni nafasi kwa CCM iliyoapa kutokabidhi madaraka kwa kura, kuendelea kutawala; yanini basi kupoteza fedha za umma na kusumbua wananchi kwa uchaguzi?

Uchaguzi huo utasimamiwa na Jecha yuleyule aliyeufuta kibabe uchaguzi halali. Hakuwa tayari kumtangaza Maalim Seif Shariff Hamad mshindi, atawezaje leo kupitia uchaguzi mpya?

Jecha amepoteza imani na washiriki wa uchaguzi, na kuendelea kwake kuongoza Tume kunafanana na kuiambia timu ya mpira ishiriki katika mashindano inayojua kwa vyovyote vile itashindwa, uchaguzi unafanyika ili kuamua watafungwa kwa mabao mangapi.

Naona uamuzi wa kuitisha uchaguzi wa marudio, kama vile inavyoonekana kwenye mashindano ya kandanda ya mtindo wa ligi wenye mchezo mmoja wa nyumbani na mwengine wa ugenini, hautofautiani na mchezo maarufu wa kuchezesha karagosi ili kufurahisha watoto uliokuwa ukifanyika katika viwanja vya Mnazimmoja wakati wa sherehe za sikukuu ya Idd.

Lakini wanaochezesha karagosi wajuwe badala ya kufurahisha watu wanajenga mazingira ambamo kunaashiria kuitumbukiza Zanzibar shimoni.

Mwenendo wao umetengeneza tatizo kubwa la kiusalama hasa kwa kutilia maanani kauli za fitna, uchochezi na ubaguzi zinazotolewa na viongozi wa CCM na vitendo vya askari wa serikali kugeuza migongo ya wananchi kama ngoma katika mchezo wa Kiluwa.

Naendelea kushuhudia baadhi ya wanasiasa waliopo madarakani wanavyofadhili vitendo vya watu kutukanwa, kubaguliwa na kupigwa huku wahusika wakilindwa na vyombo vya dola.

Hata mawaziri kutoka CCM wanasikika wakidanganya umma kuwa hawana taarifa za vitendo hivyo vya kinyama. Ninawasikitikia wanaofadhili au watekelezaji vitendo hivyo kwa kutojali madhara yake.

Watu wasijidanganye na kudanganya wengine kwamba Zanzibar ni shwari. Nchi imo katika mgogoro wa kisiasa, zipo dalili zote za hatari ya machafuko iwapo maamuzi ya wananchi yatakandamizwa.

Kinachohitajika ni kufanya juhudi za kuzuia kufika huko kwenye janga.
Kutunishiana misuli na ubabe hakutasaidia na hapa tujiulize kwa nini waliounga mkono kufutwa uchaguzi uliosifiwa na waangalizi wa ndani na wa kimataifa, wanakuwa mstari wa mbele kutaka uchaguzi wa marudio?

Watu hawa wanajijua umma hauna imani nao na ndio maana hawatoi ushahidi wa madai yao ya uchaguzi ule kuharibika.

Zanzibar ipo katika hali tete mfano wa mgonjwa mahututi anayehitaji msaada wa dharura kutoka kwa mtu mwingine. Huyu tabibu lazima atoke nje ya Zanzibar na labda kwa kuanzia atoke Bara ambako inaonekana wapo wenye busara ya kutatua mgogoro kwa majadiliano sio mabavu.

Lakini ninavyofikiri ndivyo wafikiriavyo viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wakiwemo wastaafu? Nahisi wanajali zaidi kusuluhisha migogoro ya nchi jirani kama Burundi.

Hii ni sawa na yale masikitiko ya mshairi maarufu wa Mombasa, nchini Kenya, aliyesema: Ninajenga kwa wenzangu kwangu kukiporomoka.

Tubadilike na tukubali kuwa Zanzibar lipo tatizo, tena kubwa. Wanasema usipoziba ufa utajenga ukuta, lakini kwa hali ilivyo Zanzibar, huenda nyumba ikaporomoka kukabaki kiwanja tu.

Chanzo: MwanaHalisi

Advertisements

One Reply to “Unapopuuza yako ukashughulikia jirani”

  1. Potelea mbali nyumba iporomoke na kibakiye kiwanja. Uchaguzi halali umefanyika 25/10/15 na matokeo yanajulikana mshindi wa Uraisi ni CUF na wawakilishi viti 27/27 baina ya ccm na Cuf. Kikwete kaufuta uchaguzi kwa makusudi ili kuendeleza ajenda ya Nyerere ya kuvikalia na mwishowe kuvihodhi kabisa visawa vya Zanzibar kwa kuwatumia Waafrica wahamiaji CCM Zanzibar. Ili waibe Raslimali za Zanzibar na kufisidi Dini Na uchumi wa Zaznibar. Nyinyi wanasheria na wanadiplomasiya hata muandike lugha ya Shakespear au lugha ya Shaban Robert wanyama hawa hawasikii. Hawa wanaweza kusikia lugha moja tu ,nayo nikuwatia ghasara za kiuchumi kule kwao Tanganyika . pamoja na balozi zao zilizo nchi za nje. Hapo huenda wakaanza kusikia.Sisi huku Zaznibar wanatabia ya kutujengea dharau bila sababu huku wakijua kwamba wao wana kasoro nyingi hasa za kimaadili na utu. Mungu wetu ni mmoja tutakutana huko huko uwanja wa mahkama, tutetee Zanzibar yetu kwa njia yeyote ile na popote mtu alipo kwa ajili ya kukomesha uvamizi .

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s