Balozi Dk. Mahiga amekwenda kombo

Dr-Augustine-Mahiga

Na Enzi Talib Aboud

KWA hili la mgogoro unaozidi kuizonga hatima ya Zanzibar, Balozi Dk. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, amekwenda kombo.

Aonavyo yeye, mgogoro uliopo ni wa Chama cha Wananchi (CUF) na Zanzibar peke yake, na anathubutu kutaka wahisani wamshauri  Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa CUF na mgombea urais wa Zanzibar, kushiriki uchaguzi wa marudio ulioitishwa 20 Machi 2016, kwa vile eti (wahisani) ndio wanaosikilizwa zaidi na chama hicho, sio serikali.

Dk. Mahiga anafanya kazi ya CCM na anavyofanana na Jaji Mstaafu Damian Lubuva, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), inaonesha wametumwa kupaisha ajenda ya CCM ya kulazimisha uchaguzi huo maana itakidhi matakwa yao.

CCM imelenga kuhakikisha Zanzibar hainyanyuki. Ibaki ikitumikia sera kandamizi na visa vya wahafidhina wasiotaka demokrasia ya kweli kustawi. Haitoi nafasi kwa nchi hii kujinasua na uchumi duni, hivyo kuzorotesha ukuaji wa huduma za kijamii.

Kuzuia uhuru wa wananchi kuchagua kiongozi wamtakaye ni moja ya mbinu zinazotumika. Kwao, kiongozi awe yule wanayemtaka wao, watasimamia huyo ndio aongoze.

Dk. Mahiga ni mweledi wa masuala ya kidiplomasia, mbinu za upatanishi na ubobezi kwenye nyanja ya usalama wa taifa, lakini anakosa ufahamu mpana na yakinifu wa siasa za Zanzibar, asili ya mivutano na migogoro sugu isiyokwisha inayojitokeza kila unapofanyika uchaguzi.

CCM inazidi kuamini ni haki yake kutawala peke yake, kwa hivyo, unapotokea mwanya wa upinzani kupewa ridhaa na wananchi, kinazuia mabadiliko.

Ndivyo ilivyofanya tarehe 28 Oktoba, 2015 ilipobaini imeshindwa uchaguzi mkuu uliofanyika 25 Oktoba, Zanzibar uliopata sifa zote za uhalali. Ilimbana Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, ambaye ni kada wake, ikamuagiza kuufuta.

Sababu kwamba uchaguzi uliharibika kisiwani Pemba, zilitengenezwa, ndio maana katika vikao vya majadiliano ya kutatua mgogoro, imeshindwa kutoa ushahidi. Viongozi wao wanajua vizuri historia ya uchaguzi Pemba haijaipa nafasi serikali tangu Zanzibar ilipokuwa chini ya hifadhi ya Waingereza.

Kabla ya 1964, Afro-Shirazi Party (ASP) ilinyimwa kura Pemba, historia iliyo mbichi hadi leo, miaka 23 baada ya mfumo wa vyama vingi kuruhusiwa tena mwaka 1992. Pemba ndio ngome kuu isiyotetereka ya Chama cha Wananchi (CUF).

Pemba imechukuliwa kichuki. Watu wake wanabaguliwa, na sababu mojawapo hawakushiriki mapinduzi. Ni wapi mapinduzi yalimshirikisha kila mtu? Wananyimwa fursa sawa za ajira na watoto wanabaguliwa kuendelezwa kielimu.

Zanzibar iko katika mkwamo wa kisiasa uliosababishwa na Tume kwa nia ya kuikomoa CUF ili kiongozi wake asiwe Rais kutokana na dhana ileile ya ubaguzi na chuki. Balozi Mahiga hakuliona hilo na akaegemea zaidi na muono wa kusadikika kuwa CUF ni chama korofi na kiongozi wake huyo anakusudia kuvunja Muungano.

Dk. Mahiga hapaswi kuficha ukweli kwamba watawala wahafidhina popote duniani hawajali demokrasia, wanatusi katiba na kupuuza haki za wananchi. Tanzania inajipatia sifa kwa hili.

Mambo yanayofanyika Zanzibar kwa muumini wa katiba na demokrasia hayafai. Sababu ya ubabe ya watawala hao, wahafidhina wanaendelea kufanya watakavyo, sanjari na kuunga mkono ZEC kwa kurudia uchaguzi ambao bila ya shaka hauna mustakabali mzuri kwa usalama na utulivu wa wananchi.

Ingawa kunaonekana ukimya, kuna visa na vitisho dhidi ya wananchi vinaendeshwa na vikosi vya serikali.

Makamishna wa ZEC ambao baadhi yao ni wanasheria wamesema kuna umuhimu wa kupatikana msuluhishi wa kimataifa atakaezikutanisha pande mbili zinazovutana.

Hatua hiyo wanasema ndio itakayosaidia suluhu ya kudumu Zanzibar kuliko ilivyo sasa kwa ZEC na baadhi ya viongozi wa CCM na Serikali zake kung’ang’ania uchaguzi wa marudio.

Makamishna Nassor Khamis Mohamed na Ayoub Bakari Hamad walitoa rai hiyo wakiangalia kiini cha mgogoro kinavyoakisi asili ya siasa za Zanzibar; bila ya kuwepo mtu wa tatu, si rahisi kurudisha maelewano.

Tume imekosa muelekeo na ushirikiano na wadau muhimu wa uchaguzi kutokana na baadhi ya vyama vya siasa navyo kutangaza kususia uchaguzi. Mashirika na kimataifa yaliyoisaidia ZEC kujenga uwezo wa usimamizi, yamejitoa na kutamka kutoshiriki uchaguzi huo.

Ni tume isiyonguvu za kisheria kwa sasa baada ya baadhi ya makamishna kujitenga na maandalizi ya uchaguzi huo wa marudio.  Ukakamavu wa makamu mwenyekiti Abdulhakim Ameir Issa, ambaye kitaaluma ni jaji, umembakisha Jecha na makamishna watatu watiifu kwa CCM, Omar Ramadhani Mapuri, Salmin Senga Salmin na Haji Ramadhan ambaye si mwanachama CCM.

Tume imejivunja yenyewe. Haingii akilini Tume kuitisha uchaguzi wa marudio miezi mitatu tangu ilipoufuta uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba, halafu wagombea wakawa ni walewale. Hakuna kampeni. Uchaguzi huu unatafuta kitu gani?

Makao makuu ya ZEC yamezingirwa na askari wa Jeshi la Ulinzi, picha inayojenga taswira kuwa demokrasia imetwaliwa na dola. Hapo hakuwezi kutolewa maamuzi ya kisheria isipokuwa kisiasa. Ndio maana Jecha amedhibitiwa.

Suala linajitokeza hapa kwamba ni nani hasa aliye nyuma ya Jecha hata afikie kufanya mambo ya kuichafua Zanzibar na Tanzania namna hii? Uovu wa kupuuza Katiba unapaswa kukemewa, sio kuchekewa na kuonekana ni jambo la kawaida.

Dk. Mahiga anaposema anawataka washirika wa maendeleo washawishi CUF kushiriki uchaguzi wa marudio ili kuwatendea haki wanachama wake ni hoja ya kipuuzi. Kumtaka Maalim Seif afute uamuzi wa CUF wa kutoshiriki uchaguzi huo ni mbinu ya kuhalalisha haramu iliyofanywa ambayo CCM wameiunga mkono.

Lakini akajitokeza Jaji mstaafu Lubuva, akiwaza hivyohivyo, tena huyu akamsihi na Rais John Magufuli asijishughulishe na kutafuta suluhu Zanzibar.

Anajua fika kilichotendeka. Anajua anaelekeza sivyo. Anajua Jecha hana mamlaka ya kisheria ya alichokifanya kwa hivyo kile hakiwezi kuwa halali. Basi na uchaguzi wa marudio hauwezi kuwa halali.

Hoja ya Jaji Lubuva sio tu inamuonesha alivyo msomi mchovu, bali pia anavyotekeleza dhamira ya wanasiasa wa Tanganyika, kuitenga Zanzibar na kuitelekeza. Rais mwenye majeshi ambayo yanaongezeka idadi kila uchao Zanzibar, hawezi kukosa wajibu wa kuondoa mgogoro wa kisiasa uliopo.

Mgogoro wa Zanzibar unahitaji usuluhishi mpana wa kudumu na zaidi, watawala wahafidhina wa CCM wabadilike na kuheshimu mila za demokrasia. Wasiende kama walivyokuwa kabla ya Sheria ya Usajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, 1992.

Chanzo: MwanaHalisi

Advertisements

2 Replies to “Balozi Dk. Mahiga amekwenda kombo”

  1. Wahafidhina musibabaike na Pemba, Nafuu yenu ni huyo maalim Seif ambaye hataki kutekeleza tunavyotaka sisi wapemba. Yeye anataka muungano wa haki baina ya Zanzibar na Tanganyika wakati sisi wapemba wakali hatutaki kabisaa hata kuusikia muungano huu. Kumbuka sisi hatupendi kutawaliwa na mtu, jueni tuliwaangamiza wareno hapa , tukawaondosha waengereza za kura na tulidhamiria kuuondosha usultani kwa sheria ila mulikuja kutuvamia nyinyi watanganyika na mukatutawala mpaka leo. Tunamsubiri Seif aachie uongozi ndipo mutapotutambua, jueni mutahama hapo Dar na kurudi mabara kwenye asili zenu. Kumbukeni Chama chetu sisi ni ZPPP, hatukuwa kamwe ASP maana hicho ni chama tulichokijua malengo yake tokea kilipokuwa Africa association , na kwa ghilba tu Mshenzi Julius akakiunganisha na tawi la Shirazi association lililokuwepo Unguja. Nyinyi Watanganyika pia kumbukeni ili kujenga umoja uchaguzi wa 1957 viti vyote vitatu vya Pemba vilichukuliwa na wagombea binafsi na baadae kwa mapenzi kabisa waliviunganisha na ASP. Viongozi wa ASP chini ya ushawishi wa Nyerere waliwachukia sana na kuwakejeli viongozi hawa waliojiunga kutoka Pemba , na sababu kubwa ya kuwapiga vita ni kwamba viongozi hawa ndio wazanzibari halisi , Kwa Upande wa ASP ni ukweli kwamba viongozi wake wengi hawakuwa wazanzibari wala hawkuwa na malengo ya wazanzibari wao waliabudu ubaguzi tu na kusingizia kunyonywa na utumwa, na wachache waliokuwa na upeo wa kimtazamo juu ya uzanzibari walipigwa vita na hasa wale waliotoka shirazi association hawakutakiwa, na baada ya mapinduzi maovu ya 1964 yaliouwa roho zipatazo 20,000 pia viongozi hawa hawakusalimika waliuliwa kinyama kwa mkono wa Karume pamoja na bwana wake Nyerere . Miongoni mwa viongozi aliyeuliwa kinyama zaidi alikuwa Mpemba aitwae Othman Sharif, ambae alipelekewa vijana jela kwa ajili ya kumnajisi chini ya amri ya mkatoliki anaeombewa utakatifu maluuni Nyerere pamoja na zumbukuku wake Karume. Othman Sharif aliuliwa kwa mkono wa Karume mwenyewe baada ya kumtesa kwa magumi sana jela Kinua miguu.
    Hivyo washenzi hawa viongozi wa CCM wanapokezana kuidhalilisha Zanzibar ili isiibuke na kustawi , wadudu hawa wana uhasidi saana ndani ya nyoyo zao. Nyinyi na nchi zilizomajirani nanyi kama vile Kenya muna udugu zaidi kuliko wazanzibari walio kilometer 40 mbona hammungani na Waafrica wenzenu munangangania wazamzibari ambao nyinyi hamuwajali kamwe kama ni waafrica.

    1. Safi sana lazima wajuwe Watanganyika kama msimamo wa Wapemba hauto badilika Masha ni walewale waumini wa ZPPP sio ASP mpaka mwisho wa Dunia

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s