JPM apingwa msimamo wake wa Zanzibar

pombe2

Siku moja baada ya Rais John Magufuli kusema hatoingilia mgogoro wa kisiasa Zanzibar kutokana na kuheshimu utawala wa sheria, vyama na watu wa kada mbalimbali wamepinga hatua hiyo ya Rais.

Katika hotuba yake ya dakika 55 juzi wakati akizungumza na wazee wa Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema uamuzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta uchaguzi wa Zanzibar na kisha kutangaza tarehe ya marudio, hauwezi kuingiliwa na mtu yeyote na kusisitiza kuwa wanaotaka tafsiri ya kisheria juu ya uamuzi wa ZEC, waende mahakamani.

Alisema Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ni huru kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar na kwamba tume yoyote ya uchaguzi duniani haiwezi kuingiliwa na Rais, hivyo ataendelea kukaa kimya bila kuingilia ila atahakikisha kuna utulivu.

CUF waja juu

Chama cha Wananchi (CUF) kimesema kiongozi huyo wa nchi ameikana kauli yake ya kumaliza mkwamo wa kisiasa visiwani humo aliyoitoa wakati akizindua Bunge la Kumi na Moja mjini Dodoma.

Wakati akihutubia bunge, Rais Magufuli aliapa kuulinda Muungano na akasema hata bila kiapo, yeye ni muumini wa Muungano na kwamba anaamini kwa dhati kuwa ndiyo amani ya Taifa.

Kutokana na kauli hiyo, jana CUF ilisema Rais Magufuli hawezi kukwepa sintofahamu iliyoibuka Zanzibar baada ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa rais, wawakilishi na madiwani.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Zanzibar, Kaimu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui alisema inashangaza kuona Serikali ikishiriki kutatua migogoro ya nchi nyingine na kushindwa kulimaliza suala la Zanzibar.

Alisema: “Kauli yake ya jana (juzi) imedhihirisha wazi kuwa Zanzibar ni koloni la Tanganyika. Ameonyesha wazi kuwa jambo lolote linalotokea Zanzibar haliwezi kuwa kinyume na watawala.”

Alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania unakandamiza demokrasia ya Zanzibar na kuwataka Wazanzibari kutafakari kwa kina kauli hiyo.

Naye kiongozi wa chama cha ACT­ Wazalendo, Zitto Kabwe amesema: “Nitoe wito kwa Rais (Magufuli), kuchukua hatua stahiki kwa mamlaka aliyopewa kikatiba kuhakikisha kuwa umoja na amani ya taifa vinaendelea kuimarika nchini.

“Kingine Rais Magufuli afanye kazi yake kikatiba katika sakata hili kwa sababu yeye siyo Rais wa Tanganyika, hivyo si vyema kulikimbia suala hilo kama alivyotamka jana (juzi) katika hotuba yake,” alisema Zitto baada ya kikao cha Kamati Kuu cha chama chake cha ACT Wazalendo.

Pia, Zitto alisema sasa ni wakati kwa Rais kusimamia msingi wa utendaji kazi baada ya kila mmoja kufahamu dhamira aliyonayo ya kutumbua majipu.

Jijini Dar es Salaam, vyama mbalimbali vilikutana jana huku baadhi ya viongozi wake wakizungumzia hotuba ya Rais Magufuli.

Vyama nane vya Chaumma, DP, Demokrasia Makini, Sau, Jahazi Asilia, NRA, UPDP na UMD, kwa mara nyingine, walitia mkazo msimamo wao wa kutoshiriki uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar.

Ikiwa ni siku tatu baada ya tarehe ya mwisho kwa vyama kuthibitisha majina ya wagombea, viongozi wakuu wa vyama hivyo, kwa kauli moja walijitokeza mbele ya vyombo vya habari na kusisitiza kutoshiriki uchaguzi huo.

“Tumeshaiandikia barua ZEC kuwa waondoe majina ya picha za wagombea wetu kwa sababu vyama vyetu havitashiriki uchaguzi wa marudio. Tunamuomba Rais Magufuli abadili msimamo wake na kuingilia kati mgogoro uliopo, kutofanya hivyo ni sawa na kuwatelekeza Wazanzibari ambao walimchagua,”alisema aliyekuwa mgombea urais wa Chaumma, Mohammed Massoud Rashid ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa chama hicho.

Katibu mkuu wa chama hicho, Ali Omar Juma alisema kwa msimamo wa Rais kutoingilia mzozo uliopo visiwani humo ni ishara ya kutoridhika na mfumo wa uendeshaji wa serikali ambayo anaiongoza.

Lakini, mbunge wa zamani wa Vunjo, Augustine Mrema alitofautiana na msimamo wa wengine na kumtaka Rais Magufuli kutolazimishwa kuingilia kati mgogoro huo kwa hofu ya kusitishiwa misaada na nchi za Ulaya.

Alisema Rais hapaswi kulazimishwa kujitosa kwenye mgogoro kuwaridhisha vibaraka wa wahisani na kumtaka asimame kwa nguvu zake zote kuhakikisha uchaguzi huo unarudiwa na anapatikana kiongozi anayestahili.

Mgogoro wa kisiasa Zanzibar uliibuka baada ya ZEC kufuta matokeo ya uchaguzi kwa maelezo kuwa sheria na kanuni zilikiukwa na baadaye kutangaza Machi 20 mwaka huu kuwa siku ya kupiga kura upya.

Wakati mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha akitangaza kufuta matokeo siku ambayo alitakiwa amtangaze mshindi wa kiti cha urais Oktoba 28 mwaka jana, tayari matokeo ya majimbo 31 yalikuwa yameshatangazwa huku majimbo tisa yakiwa yameshahakikiwa. Pia washindi wa viti vya uwakilishi na udiwani walishatangazwa na kupewa hati za ushindi.

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

One Reply to “JPM apingwa msimamo wake wa Zanzibar”

  1. Waliona juhudi zao tokea 1957 za kuimaliza Zanzibar zimeshindwa ndio maana wakafuta uchaguzi. Ili wamueka karagosi lao na hatimae kuifyeka Zanzibar . Kumbukeni enyi Watanganyika wazanzibari ni vyura vitavyoogelea katika tumbo la tembo na kupiga taarab zao taimu za jioni ama wakati wowote wakipenda. Jee tembo utaicheza rusha roho wakati wako wa malisho au mapunziko, maana vyura hawana wakati maalum wa buldani.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s