Duni: Bila SUK, hakuna atakayetawala Z’bar

Aliyekuwa mgombea mwenza wa urais kwa tiketi ya Chadema, Juma Duni Haji
Aliyekuwa mgombea mwenza wa urais kwa tiketi ya Chadema, Juma Duni Haji

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CUF, Juma Duni Haji amesema kuwa bila Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), si Dk Ali Mohammed Shein wala Maalim Seif Sharif Hamad atakayeweza kuitawala Zanzibar.

Duni alisema hayo katika mahojiano maalum na Mwananchi alipokuwa akijibu swali kuhusu kauli ya Balozi Amina Salum, aliyesema kuwa anatamani SUK ivunjwe kwa kuwa baadhi ya viongozi hawana nia ya kuiendeleza, akimtaja Maalim Seif kuwa kikwazo. Amina, ambaye alishika nafasi ya pili kwenye kinyang’anyiro cha urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia CCM, alisema siasa za Zanzibar zitaendelea kuwa za vuta­nikuvute mpaka Maalim Seif atakapotambua maana ya maelewano kuwa ni nipe nikupe.

Lakini, Duni Haji alisema kauli hiyo ya Balozi Amina Salum imetokana na chama chake cha CCM kushindwa kwenye uchaguzi wa rais wa Zanzibar. “We mwambie Babu Duni kasema kwa sababu chama chake kimeshindwa,” alisema mwanasiasa huyo mkongwe.

Alisema suala la Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar si la Amina, bali la Katiba ambayo inataka maridhiano ya watu waishi kwa amani kama ndugu. “Hilo lilishawezekana, Shein katurejesha miaka kumi nyuma sasa.

Sijui wanaota wako karne ya 17? haiwezekani kabisa bila Serikali ya Umoja wa Kitaifa si Shein wala Maalim Seif atakayetawala,” alisema Duni. Alisema wakitaka kuiondoa SUK, ni lazima waende kwenye Katiba na pia ifanyike tena Kura ya Maoni kutaka maoni ya wananchi kuhusu serikali waitakayo.

Duni alisema kama CUF haitashiriki na vyama vingine vikashiriki, waendelee lakini haamini kama watafika popote. “Hivi bila CUF Zanzibar kuna uchaguzi?” alihoji Duni na kuongeza: “Hivyo vyama vingine vinavyosema vitashiriki, vimepata chini ya kura 80 halafu vinasema sisi tunakwenda kushindana?”

Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya 1984 iliyofanyiwa marekebisho 2010, Ibara ya 39(3) inayozungumzia muundo wa serikali hiyo, inasema: “Makamu wa Kwanza wa Rais atatakiwa awe na sifa za kumuwezesha kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na atateuliwa na Rais baada ya kushauriana na chama kilichotokea nafasi ya pili katika matokeo ya kura ya uchaguzi wa rais isipokuwa kwamba: Iwapo chama kilichotokea nafasi ya pili katika matokeo ya kura ya uchaguzi wa rais kimepata chini ya asilimia kumi (10) ya kura zote za uchaguzi wa rais, au endapo rais atakuwa hana mpinzani, basi nafasi ya makamu wa kwanza wa rais itapewa chama chochote cha upinzani kilichotokea cha pili kwa wingi wa viti vya majimbo katika Baraza la Wawakilishi.

Vyama vitano vya siasa vilivyotangazwa kuwa vitashiriki katika uchaguzi wa marudio wa Zanzibar, utakaofanyika Machi 20 mwaka huu, ni CCM, ADC, CCK, TLP na Sau. Mbali na CCM, vyama vilivyosalia havijawahi kupata hata asilimia moja ya kura zilizopigwa Zanzibar katika chaguzi zilizopita na havijawahi kushinda majimbo.

Hiyo ndiyo kusema kuwa chama kitakachoshiriki kuunda SUK ni lazima kipate angalau asilimia 10 ya kura za urais au kishinde viti vingi katika Baraza la Wawakilishi.

Akijibu swali kuwa hii si mara ya kwanza kwa CUF kususia uchaguzi Zanzibar, Duni alisema: “Jambo jipya ni kwamba Magufuli (Rais John) anakubali kuvunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano,” alisema Duni

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

One Reply to “Duni: Bila SUK, hakuna atakayetawala Z’bar”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s