Mazombi ni nani, kwa nini wanatamba Zanzibar?

vikosi-vya-smz-620x308

Taarifa za kuwapo kwa vikundi vya watu wanaojifunika nyuso zao visiwani Zanzibar na kuwashambulia wananchi na mali zao, zimekuwa za muda mrefu na kuonekana kuongeza kasi.

Wahalifu hao wamepewa jina la ‘mazombi. Matukio ya kushambulia watu na mali zao hasa katika Kisiwa cha Unguja yaliibuka zaidi mwaka jana wakati wa kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia mfumo wa kielektroniki (BVR).

Wananchi walikuwa wakilalamika kushambuliwa na watu waliojifunika nyuso zao kwa kutumia soksi ambao awali, walipewa jina la ‘janjaweed’ wakifananishwa na wapiganaji wa kundi la kigaidi katika Jimbo la Darfur, Sudan.

Kundi hilo linatumia silaha za moto na zile za jadi, bunduki, mashoka, mapanga, nondo, mikuki na mishale. Kuonyesha kwamba kundi hilo ni hatari, wakati wa uandikishaji wa BVR mwaka jana, watu wawili waliuawa kwa risasi na wengine kujeruhiwa na kundi hilo. WaIiojeruhiwa walikaririwa wakisema kuwa waliowashambulia ni watu waliokuwa wamejifunika nyuso, wakitumia magari yanayoonyesha dalili kuwa ni mali ya baadhi ya vikosi vya Serikali.

Mwishoni mwa mwaka jana mazombi hao walivamia na kuharibu vitendea kazi vya kituo cha redio cha HITS FM kilichopo Unguja.

Lakini kundi hilo pia lilivamia Ofisi za Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na kutapanya makaratasi waliyoyakuta ofisini humo.

Hivi karibuni, waliripotiwa kuvamia Barabara ya Magogoni, Wilaya ya Mjini Unguja na kuvunja vibanda, kuharibu mali na kupiga watu ovyo.

Mashuhuda walisema watu hao walikuwa na silaha za moto na zile jadi wakati wakifanya unyama huo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, alisema alipewa taarifa na Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi kwamba watabomoa mabanda katika eneo hilo lakini hakuwa na majibu ya kwa nini kazi hiyo ilifanyika usiku na kwa staili hiyo.

Tukio jingine ambalo lina maswali mengi ni pale walipovamia usiku wa manane ofisi za CUF zilizopo Mtendeni na kuwateka walinzi wakilazimisha kuingia ndani kabla ya kutokomea kusikojulikana baada ya polisi kupata taarifa na kufika katika eneo hilo.

Swali letu kwa vyombo vya dola ni hili, mazombi hawa ni akina nani? Kwa nini wananchi wanahusisha vitendo vyao na masuala ya kisiasa?

Wakati wananchi wakisubiri kwa hamu kupata majibu ya maswali hayo, tunasema ipo haja kwa Serikali kusikia kilio hiki na kuchukua hatua kali kudhibiti mashambulizi hayo kwa raia kabla hali haijawa mbaya zaidi.

Ni imani yetu kuwa Polisi, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama, wataendesha operesheni maalumu kuwakamata wahusika na kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria.

Isitoshe, tunaamini kuwa Jeshi la Polisi Zanzibar litatoa taarifa ya kina kuhusiana na waovu hawa. Kwamba, kutokana na uchunguzi wao, wamebaini kuwa hao ni watu gani na wanafanya yote hayo kwa masilahi ya nani?

Hakika, maswali ni mengi na Serikali kukaa kimya pasi na kuyatolea majibu kunaacha wigo ambao unawafanya watu mitaani kuja na maelezo mbalimbali kuhusu mazombi hawa wanaoweza kufanya uhalifu bila kuguswa.

Chanzo: Maoni ya Mhariri Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s