Zanzibar sasa imeachwa rasmi gizani

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha

Nimefuatilia mwenendo wa mgogoro wa kisiasa na kikatiba Zanzibar katika wiki tatu zilizopita na kusikitishwa sana na hali ya mambo yanayoendelea huko.

Kwanza kuna kila dalili kuwa yale ambayo tunayafundisha katika taaluma ya utatuzi wa migogoro yanazidi kujidhihirisha visiwani Zanzibar.Yapo mambo mengi yanayonisikitisha kuhusu mgogoro huo ambao bado umekumbwa na kiza kinene cha lini na vipi utatatuliwa.

Natumia fursa hii kujadili mambo hayo kwa lengo la kuhamasisha Watanzanzania kuona hatari inayokuja mbele yetu na kushauri hatua za kuchukua ili kuimaliza sintofahamu hii iliyopo Zanzibar tangu tangazo la kufutwa uchaguzi wa Zanzibar, Novemba mwaka jana 2015.

Licha ya kufuta uchaguzi huo, lakini tayari Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar  (ZEC), imetangaza tarehe ya kurudiwa uchaguzi huo.

Kwanza, nianze na mambo makubwa kuhusu mgogoro wenyewe kwa kuwa nauona ukizidi kukua na kufikia mithili ya kidonda ndugu. Baada ya tangazo la Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha kumekuwa na mwenendo usioridhisha katika kushughulikia mgogoro huu.

Badala yake mgogoro umeendelea kuwagawa Wazanzibari kwa vigezo vya vyama, rangi na asili mpaka inatisha.

Kwa mfano, mwanzoni mwa Januari kulisikika kauli za viongozi wakuu wa Umoja wa Vijana wa CCM Tanzania, wakitaka Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume atimuliwe na kunyang’anywa kadi ya chama hicho.

Matamshi haya ya vijana hayakukanushwa wala kukemewa na ngazi yoyote katika uongozi wa CCM.

Katika kuonesha madhara ya kauli hiyo, kulitokea sintofahamu wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya Mapinduzi Zanzibar ambapo sehemu ya umati ulisikika ukimzomea Rais Karume wakati akiingia viwanjani.

Vitendo hivi ni hatari na vinaweza kuipasua Zanzibar vipande vipande.

Wakati hayo yakiendelea, kumeanza dalili za wazi wazi za ubaguzi wa rangi  Zanzibar.

Katika siku ya Mapinduzi matukufu ya visiwa hivyo, ilishangaza kuwa moja ya mabango yaliyoonekana viwanjani lilisomeka kwa maneno ya ‘Hatutaki Hizbu, machotara waondoke, Zanzibar ni nchi ya waafrika’

Bango hili lilionekana kupamba sherehe ambazo lengo lake ni kupingana na ubaguzi wa rangi na aina zote za udhalimu.

Mtu unaweza kujiuliza mambo ya Hizbu yametokea wapi tena? Na suala la machotara kutakiwa wasionekane Zanzibar linatokana na azimio gani na la wapi?

Na kwa nchi yenye mchanganyiko wa damu na kuoleana kama Zanzibar, uchotara na uafrika ni hoja inayoletwa na nani?

Siku za nyuma kidogo kuelekea uchaguzi mkuu visiwani Zanzibar, kulitokea pia maneno ya vijembe na kashfa yakilenga kuhamasisha kuenguliwa kwa viongozi wa CUF katika serikali ya umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Jambo hili nalo halijawahi kukemrwa ipasavyo ikizingatiwa kuwa suala la kuwepo CUF na CCM katika serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar siyo  la hiari tena tangu mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010 ambayo yameweka seikali ya umoja wa kitaifa kuwa matakwa ya kikatiba.

Iweje tena watu wanaibuka na kuwataka viongozi wa CUF kuondolewa katika serikali na Baraza la Mapinduzi pasipo kukemewa wakati kitendo hicho kingevunja katika ya Zanzibar?

Mbaya zaidi hakuna juhudi za kuridhisha kuelekea katika suluhu ya kudumu ya mgogoro wa Zanzibar. Tazama, baada ya ‘kutofahamiana’ na kupelekea tangazo la Mwenyekiti Jecha kufuta uchaguzi, Tume ya uchaguzi Zanzibar ni kama imesambaratika na haipo. Kufuatia kupigana kwa wajumbe wake ambako kulitaarifiwa na Jecha, hatujaambiwa endapo walikwishafanya juhudi za kukutana na kuanza kutafuta suluhu yoyote.

Kwa maoni yangu, usuluhishi wa mgogoro wa Zanzibar hauwezi kuanzia nje ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar.

Nikiamini kuwa sababu tisa za Jecha za kufuta uchaguzi ni za kweli, upatanishi wa kwanza lazima ufanyike ndani ya ZEC ili kurejesha uhai wa Tume hiyo kufanya kazi ikiwa chombo kimoja badala ya kubaki vipande vipande kama ilivyo hivi sasa.

Nje ya Tume ya uchaguzi Zanzibar, tunaambiwa juu juu kwamba kuna mazungumzo ya kiusuluhishi yanayoendelea kati ya pande mbili za mgogoro wa Zanzibar.

Kibaya zaidi mazungumzo yaliyokuwa yanaendelea kati ya vyama vya Cuf na CCM yamevunjika rasmi.

Wakati tukisikia hayo, tunasikia pia kuwa mazungumzo hayo yanahusisha viongozi wapatao nane (8) wa CCM kwa upande mmoja na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif kwa upande mwingine.

Tunaambiwa pia Mwenyekiti wa mazungumzo hayo ni Dk. Ali Mohammed Shein. Nilipata mshangao kusikia jambo hili kutoka katika hotuba ya Dk. Shein siku ya Mapinduzi.

Hivi kweli mazunguzo yanayohusu mgogoro wa kisiasa na kikatiba Zanzibar yanaweza kuwa chini ya uenyekiti wa Dk. Shein au hata Maalim Seif? Hivi ndivyo usuluhishi wa migogoro unavyofanyika siku hizi?

Ukiacha mazungumzo hayo ya kupoteza muda yanayoendelea na ambayo yamekuwa hayana mtoa taarifa za kinachoendelea, kuna habari kuwa Maalim Seif ameamua kumwandikia Baba Mtakatifu, papa Francis kumjulisha kuhusu mgogoro wa Zanzibar. Je lengo la barua hiyo ni nini? Je hii inaleta picha gani kwa ‘mazungumzo’ yanayoendelea? Je tutarajie matunda gani kutokana na mawasiliano hayo kati ya Maalim Seif na kiongozi huyo wa kiroho duniani?

Nimetoa hoja siku zilizopita kuwa utata wa suala la Zanzibar ni pamoja na ugumu wa kutekeleza yanayofikiriwa kupendekezwa kama suluhu ya sakata hilo. Kwa mfano, nadhani itakuwa ngumu kurudia uchaguzi hata kama itakubalika hivyo kwa sababu mbili.

Kwanza, Tume huru tena mpya inayoaminika na kuheshimika na wazanzibari wote itatoka wapi ije isimamie uchaguzi wa marudio Zanzibar? Je uchaguzi utasimamiwa na Tume iliyoshindwa kufahamiana, ikatofautiana na kuanza kuvua mashati na kupigana? Je nini kitazuia Tume hiyo kutofautiana na kuanza kupigana tena wakati wa uchaguzi wa marudio. Sambamba na hilo, kuna suala la kikatiba linalohusu bajeti ya kurudia uchaguzi

Kwa kuwa suala hili la kurudiwa uchaguzi halikuwa limefikiriwa kabisa katika minajiri ya bajeti ya Zanzibar, bajeti hiyo mpya itatoka wapi na nani ataiidhinisha?

Hatma ya uchaguzi na masuala mengine ya kibajeti? Nini kinazuia kuitishwa kwa Baraza la Wawakilishi kama inavyoelezwa katika Katiba ya Zanzibar? Je hakuna anayeona fursa hii kutoka pande zote za mgogoro wa Zanzibar au kuna kitu kinachoogopwa?

Je wadau wengine wa demokrasia ya uchaguzi Zanzibar kama Asasi za Kiraia, Mashirika ya dini, wanasheria na wanahabari wako wapi katika hili? Kwa nini tunasikia kauli na ushiriki wa vyama vya Siasa pekee bila wadau wengine? Je wanawake na wasichana sauti zao ziko wapi? Je watu wenye ulemavu visiwani wana maoni gani kuhusu mgogoro huu?

Ninashauri tujitafakarishe kama taifa ili tupate mahali pa kuanzia katika kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro huu unaovitafuna visiwa vya unguja na pemba kwa hivi sasa.

Nje ya hapo tutajikuta tunapoteza muda na kama nilivyokwishaeleza katika makala zangu nyingine za safu hii, ‘Zanzibar isipoziba ufa wakati huu, itakuja kulazimika kujenga ukuta!’

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Zanzibar!

Deus Kibamba Ni mtafiti Na mchambuzi jamii aliyebobea katika maeneo ya uhusiano wa kimataifa, katiba na demokrasia ya uchaguzi. Amekuwa mwangalizi na mwezeshaji wa michakato, midahalo na mijadala katika nchi mbalimbali ikiwemo Burundi, Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Malawi, Zambia, Ghana, Sudan na Sudan ya Kusini. Pia, Kibamba ni mhadhiri wa masuala ya uhusiano wa kimataifa na utatuzi wa Migogoro. Anapatikana kwa nambari: +255 788 758 581 na barua pepe: dkibamba1@gmail.com

Chanzo: Nipashe

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s