Ukawa wampa mkakati mzito Maalim Seif

Aliyekuwa mgombea urais Zanzibar kupitia CUF, Maalim Seif Sharif Hamad akiwa na aliyekuwa mgombea urais wa Tanzania Edward Lowassa
Aliyekuwa mgombea urais Zanzibar kupitia CUF, Maalim Seif Sharif Hamad akiwa na aliyekuwa mgombea urais wa Tanzania Edward Lowassa

Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umempa mgombea Urais wa Chama cha Wananchi (CUF) Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, mkakati mzito wa kupambana na serikali ili uchaguzi wa marudio usifanyike na badala yake atangazwe kuwa ndiye mshindi wa uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana.

Mkakati huo walimpa juzi usiku kwenye kikao cha siri kilichofanyika Dodoma baina ya viongozi wa Ukawa na wabunge wanaotoka kwenye vyama vinavyounda umoja huo.

Katika kikao hicho, alikuwapo pia aliyekuwa mgombea urais wa Tanzania wa Chadema, Edward Lowassa.

Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa Maalim Seif aliwaeleza wabunge hao hatua zote zilizopitiwa tangu kufutwa kwa uchaguzi huo.

Chanzo hicho kilisema Maalim Seif aliwaambia wabunge hao kuwa viongozi wa CCM waliokuwa wakishiriki mazungumzo hayo, walikiri kuwapo kwa makosa wakati wa kufuta matokeo ya uchaguzi huo.

“Alisema viongozi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na hata hao wengine wa CCM waliokuwa wajumbe, walieleza vikao vya usuluhishi na kukiri kwamba kufutwa uchaguzi ilikuwa ni makosa,” kilisema.

Kilieleza kuwa Maalim Seif aliwaambia wabunge hao kwamba muda wote alikuwa anasisitiza msimamo wa kutorudiwa kwa uchaguzi.

“Alisema hata alivyoenda Dar es Salaam kuonana na Rais (John Magufuli), alimwambia kabisa kwamba hayuko tayari uchaguzi urudiwe,” kilieleza chanzo kingine kilichokuwa kwenye mkutano huo.

Taarifa hizo zilidai kuwa baada ya kikao hicho walikubaliana kuwa ni vyema kwanza akakutana na Baraza Kuu la CUF ili kutoa msimamo wa pamoja.

“Lakini si CUF tu, tumekubaliana kuwa viongozi wakuu wa Ukawa na washauri wao nao pia wakutane ili kufikia muafaka wa pamoja,” kilieleza chanzo kingine.

Pia chanzo kicho kilieleza kwamba baada ya kutoa matamko hayo, wabunge wa upinzani watatumika zaidi kuongeza shinikizo kwa serikali.

Juhudi za kuweka shinikizo la jumuiya ya kimataifa, pia zitakuwa juu zaidi ili kuhakikisha muafaka visiwani humo unafikiwa.

MBOWE AFUNGUKA
Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, akiwaeleza waandishi wa habari kilichojiri kwenye mkutano huo, alisema wamepokea taarifa kwa kile kinachoendelea Zanzibar kuhusiana na mazungumzo ya usuluhishi yaliyokuwa yakiendelea visiwani humo.

Alisema maamuzi ya kilichojadiliwa yatatolewa Januari 28, baada ya  kikao cha utendaji  kitakachokaa Januari 27.

“Jambo moja ambalo ni zito la kuiambia Serikali ya Chama Chama Mapinduzi, hatima ya Zanzibar na watu wake watambue kwamba amani ya taifa letu haiwezi kuwa ya kudumu kama haki na demokrasia havitaheshimiwa katika mchakato mzima wa kiongozi katika taifa,” alisema Mbowe.

Alisema amani ya kudumu haiwezi kupatikana kwa nguvu za kijeshi, vitisho ama kuvaa nguo za kijeshi na badala yake amani itapatikana kwa kuzingatia maamuzi ya wananchi kupitia taratibu za kidemokrasia zitakapokuwa zinaheshimiwa.

Aidha, Mbowe alisema kikoa cha juzi wote kwa pamoja wamepokea taarifa za viongozi wao na wamekubaliana wawe na subiri hadi Januari 28 maamuzi ya Baraza Kuu la CUF litakapotoa msimamo wao na baada ya hapo Ukawa watatoa tamko lao.

Mbunge wa Jimbo la Malindi (CUF), Ali Saleh, alisema Rais dk. John Magufuli ana jukumu la kushughulikia mgogoro wa Zanzibar, lakini kilichojitokeza ana uoga dhidi ya chama chake kwa kuwa ana haki ya kushughulikia tatizo hilo.

Alisema endapo mgogoro huo usipomalizika, kuna uwezekano mkubwa wa kushuka kiuchumi pamoja na kuzuiliwa kwa msaada wa dola milioni 900.

Alisema haiwezekani kurudiwa uchaguzi kwa kuwa kila kitu kipo wazi, hivyo mkutano wao umewajengea uwezo na watatoa msimamo.

Alipoulizwa kama CUF itasusia uchaguzi huo endapo msimamo wa serikali utabaki kama ulivyo, alisema uamuzi wa kususia au kutokususia, utatolewa na baraza kuu.

Alisema hata kama wataamua kususia, haitakuwa mara ya kwanza na hatua hiyo haiwezi kuiathiri CUF kwani waliwahi kufanya hivyo na kura za maruani zikapigwa ambazo ziliiathiri CCM.

LISSU ANENA
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, alisema kufutwa kwa uchaguzi huo ni kinyume cha sheria na haiwezekani kupinga mahakamani kwa kuwa katiba inakataza suala hilo.

“Hatuwezi kwenda mahakamani kwa kuwa katiba zetu mbili haziruhusu kuhoji matokeo ya urais mahakamani. Huwezi kuhoji chochote mahakamani kinachohusiana na uchaguzi huo,” alisema Lissu.

Alisema ufunguo wa mgogoro wa Zanzibar uko Dar es Salaam, kwa sababu tangu mwaka 1972 rais wa visiwa hivyo anapangwa Dar es Salaam.

“Kwa hiyo Magufuli akiamua kutoa jeshi lake Zanzibar mshindi wa uchaguzi atatangazwa,” alisema Lissu.

CUF KUJADILI UCHAGUZI WA MARUDIO LEO
Hatima ya CUF kushiriki uchaguzi wa marudio au kutoshiriki, itafamika Machi 28, mwaka huu, baada ya kukamilika kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la chama hicho.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Shehe, alipokuwa akizungumzia uamuzi wa ZEC kutangza tarehe ya kurudiwa uchaguzi tofauti na msimamo wa chama hicho.

Alisema vikao vya chama hicho vya kujadili mkwamo wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, vitaanza kufanyika leo na kesho vikitanguliwa na Kamati ya Utendaji ya chama kabla ya kukutana Baraza Kuu la Taifa la Chama.

“Msimamo wa chama juu ya kurudiwa uchaguzi kama tutashiriki au kutoshiriki utafahamika alhamisi baada ya kukamilika kikao cha Baraza Kuu,” alisema Shehe.

Hata hivyo, aliwataka wananchi kuendelea kuwa na moyo wa subra na kuimarisha amani na umoja wa kitaifa wakati jambo hilo likiendelea kujadiliwa na vikao vya chama.

Alisema msimamo wa CUF tangu mwanzo ni kwamba uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana, ulikuwa huru na wa haki, lakini Mwenyekiti wa ZEC aliamua kufuta matokeo baada ya kuona CCM wako katika hatari ya kuanguka.

Alisema chama chake kitaendelea kutetea na kupinga kitendo chochote cha uvunjifu wa sheria na katiba ikiwamo kufuta maamuzi halali ya wananchi waliyoyafanya kupitia uchaguzi huo.

Shehe alisema maazimio yatakayotolewa na Baraza Kuu la CUF ndiyo utakuwa msimamo wa wanachama wote na wagombea katika mpango wa kurudiwa kwa uchaguzi huo.

MAASKOFU ZANZIBAR WAHAHA
Wakati wananchi wa Zanzibar wakiwa wamegawanyika makundi mawili wanaotaka kufanyika uchaguzi wa marudio na wasiotaka, makanisa matatu Zanzibar yamewataka waumini wake wajitokeze na kushiriki uchaguzi uliopangwa kufanyika Machi 20, mwaka huu visiwani humo.

Msimamo huo umetangazwa na  Viongozi wa Kanisa la Romani Katoliki, Kanisa la Angilikana na Kanisa la Katoliki katika ibada ya pamoja ya mwaka iliyofanyika Mkunazini Mjini Zanzibar juzi.

Akihubiri katika ibada hiyo, Askofu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Zanzibar,  Michael Hafidh, alisema haki ya kupiga kura ni ya kikatiba ya kila mwananchi na kuwataka waumini kujitokeza wakati wa uchaguzi wa marudio kutekeleza haki yao.

Hata hivyo, alisema kila mwananchi yuko huru kupiga kura bila uhuru wake kuingiliwa na mtu yeyote katika uchaguzi huo. Pia  alisema wananchi wanapaswa kutii mamlaka ya dola lakini na mamlaka inapaswa kutii wananchi wake na kuwathamini.

“Uchaguzi umetangazwa, kama sisi viongozi wenye dhamana na watu, hatuhitaji kuona damu ya watu ikimwagika kwa ubabe.”alionya Askofu Hafidh.

Kwa upande wake Askofu wa Kanisa la Katoliki Zanzibar,  Augustino Shayo, alisema maendeleo ya Zanzibar yanahitaji amani na mshikamano kwa wananchi wake.

Alisema haki ya kupiga kura ni ya kikatiba ya kila Mtanzania na kutaka wananchi kuwa huru katika kufanya maamuzi katika kuwapata viongozi wao.

Askofu Shayo alisema kuwapo kwa maelewano ya pamoja kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio ni jambo la msingi baina ya pande  zinazovutana katika mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar

Hata hivyo, aliwapongeza waumini wa makanisa hayo kwa kufanyika ibada ya pamoja ya mwaka na kuwataka viongozi kuanza kufikiria umuhimu wa kufanya ibada ya pamoja ya Ijumaa Kuu ya kila mwaka.

Tangu ZEC kutangaza tarehe ya kurudiwa kwa uchaguzi mkuu kumekuwapo na mjadala mkubwa katika Manispaa ya mji wa Zanzibar huku wananchi wengine wakiunga mkono na wengine wakipiga kufanyika uchaguzi huo.

Chanzo: Nipashe

3 Replies to “Ukawa wampa mkakati mzito Maalim Seif”

  1. Hizo kura za mlafi kibaraka Shein alipigiwa na makanisa, maana ccm ndio chama chao kwani wao ndio waafrika. Kwa vile maelewano hayapo na kura za marudio tayari zimeshapangwa mezani matokeo yake, na watakaodhulumiwa zaidi ni wapemba ikiwa maalim yeye hataki basi sisi wapemba hatuna haja na Zanzibar ni vyema zaidi kila Kisiwa kikawa na serikali yake ,hili litaleta kuheshimiana na litaharakisha maendeleo ya kila kisiwa. Hili lazima litendeke kwa sababu lilianzishwa na Nyerere na kupaliliwa na CCM ya sasa.

    1. Kabisa kaka bora tugawane visiwa unajuwa ccm haina maana kwet yan yasaidia unguja tu bora watuachie kisiwa chet cha pemba trudi na raisi wet atakuwa maalim seif bora tumtafute maalim atowe msimam0 uwo kwa awo wahafidhina ccm kuwa tgawane visiwa

  2. Ccm ukisema haiwafanyii kitu wapemba ni uongo, hizo barabara, maji safi, umeme maskuli nk. vyote hivyo kavitengeneza Maalim Seif shukurani tu ndogo, sijui mufanywe kitu gani hata mujuwe kuwa mumefanyiwa kitu, hata huyo Maalim Seif mapenzi ni mwanzo tu mwisho yatakuwa kuliko haya (fadhila za punda mashuzi) dkt shein anajitahidi kwa Pemba lakini hamna shukurani.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s