Kwaheri Bi Asha, Kapumzike salama

ashabakari

Salma Said.
Ni majira ya saa 11 Alfajiri nafungua simu yangu napata ujumbe ulioanza na Inna Lillahi Wainna Ilayhi Rajiuun,  Asha Bakari hatunaye tena ameshatangulia mbele ya haki, waarifu na wengine. Ujumbe huo ukitokea Dubai.

Nami nikasema pia Inna Lillahi Wainna Ilayhi Rajiuun Alhamdulillah, Mwenyeenzi Mungu ampokee na amlaze mahali pema, Allah amjaalie Marehemu kaburi lake liwe bustani miongoni mwa mabustani ya peponi. Amin. Baadae ndio nikaanza kufungua facebook yangu na kutuma ujumbe wa taarifa ya kifo baada ya kupata uhakika na kuthibitishwa kifo hicho na Katibu wa Umoja wa Wanawake (UWT) Salama Aboud Talib ambaye alisema wamepokea kwa mshituko mkubwa taarifa za kifo.
Kulipokucha tu taarifa zimeshaeneo kila sehemu nikatembea maeneo ya Soko Kuu la Darajani, taarifa zikawa ni hizo tu anazungumzwa Bi Asha Bakari Makame ambaye alifariki nchini Dubai baada ya kuugua muda mrefu ‘Kiharusi’ huku akitajwa kwa mambo mbali mbali kama ilivyo kawaida utatajwa kwa mambo uliyoyatanguliza.
Wapo ambao wakisema ameshatangulia tumuache alichotanguliza ni yeye na Mola wake lakini wapo ambao eti wakisema wanatoa joto wakaanza na kebehi, kejeli na maneno mengine wakikumbushia maneno yake ambayo alikuwa akipenda kuyatamka kila mara.
Kauli unayoisikia katika vinywa vya watu ni hii “Nakwambieni nchi hii haipatikani kwa karatasi sisi tumepindua labda na nyie mpindue….hatutoi hatutoi hatutoi” ni kauli ya Bi Asha Bakari wakati wa uhai wake ni kauli iliyompa umaarufu mkubwa katika siasa za Zanzibar ambayo imemalizia maisha yake.
Matamshi hayo ndiyo yaliompa umaarufu na kuonekana jasiri hapa Zanzibar sio mwengine bali ni Bi Asha Bakari Makame ambaye akijulikana zaidi kwa jina la ‘Mtama’ ambalo alipewa na Baba yake Mzazi Bwana Bakari Makame alikuwa ni Mwanamke aliyekuwa mstari wa mbele katika kukihami na kukitetea Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uhai wake wote.
Amekitumikia chama kwa muda mrefu na kukamata nyadhifa mbali mbali ndani ya chama hicho huku akiamini dhana ya uhafidhina ambao ni viongozi wachache waliobaki ndani ya Chama Cha Mapinduzi waliobakia kutetea msimamo huo wa uhafidhina ambao hawataki demokrasia kufuata mkondo wake na kungangania dhana ya Umapinduzi zaidi kuliko uhalisia au lengo la Mapinduzi yenyewe ambalo limeasisiwa na aliyekuwa Rais wa Kwanza Zanzibar, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.
Lengo la Mapinduzi ni kukataa ubaguzi wa aina yeyote na kuwepo usawa kwa wananchi wote katika kupata huduma za kijamii kama elimu, afya na huduma nyenginezo zitolewazo na serikali.
Bi Asha pamoja na kuwa akipingwa na wengi kutokana na msimamo wake lakini hakuvunjika moyo hata kidogo, licha ya kukabiliwa na changamoto mbali mbali hasa kwa kuwa akitokea katika Kijiji Cha Mtambwekijiji ambacho pia alichozaliwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad.
“Mimi mwanangu Mtama amejiunga na CCM muda mrefu tokea wakati wa ASP na anakipenda chama na anamaliza uhai wake akiwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi CCM lakini sio lazima na mimi nimfuate yeye mimi CUF na yeye ni CCM na hilo alilitambua awali” alisema Mzee Bakari ambaye ni Baba yake Bi Asha.
Ujasiri wa Bi Asha na msimamo wake thabiti ndio uliompa umaarufu mkubwa ndani ya siasa za Zanzibar ambapo alionekana kama ni turufu muhimu mbele ya wapinzani wao wa CUF kwa kuwa anatokea Kisiwani Pemba lakini jengine kutoka kijiji kimoja na Maalim pia ilionekana kama ni nguvu kubwa ambayo ikitumika wazi wazi katika kumdhoofisha Maalim Seif kutokana na kutoka ndani ya kijiji na familia zilizo na mahusiano ya karibu.
Asha Bakari ambaye alizaliwa Disemba 25, 949 na kupata elimu yake ya msingi katika Shule ya Utaani mwaka 1957 hadi 1964 na kujiunga na Sekondari katika shule ya Fidel Castro mwaka 1965 hadi mwaka 1968.
Baadae alijiunga na Chuo cha Uhazili mwaka 1970 kwa mwaka mmoja akisomea masomo ya sekretari katika ngazi ya cheti na kuongeza na miaka mengine miwili katika chuo hicho kwa kuendelea na kozi hiyo hiyo kwa ngazi ya Advence mwaka 1978 hadi 1979 na baadae kujiunga na kozi ya Diploma ya Political Science and Management mwaka 1984 hadi mwaka 1985 nchini Bulgeria.
Katika nafasi ambayo ameshikilia ndani ya serikali ni pamoja na uwalimu kuanzia mwaka 1969 hadi mwaka 1970, sekretari wa wizara ya elimu kuanzia mwaka 1970 hadi mwaka 1974, sekretari wa wizara ya habari mwaka 1974 hadi mwaka 1980, na kisha kuwa sekretari wa baraza la wawakilishi ambapo aliitumikia mwaka 1983 hadi 1985.
Baadae akateuliwa kuwa mjumbe wa baraza la wawakilishi kuanzia mwaka 1985 hadi mwaka 1990 wakati huo akiwa Naibu waziri wa Usafiri na Mawasiliano mnamo mwaka 1990 hadi mwaka 1995 na baadae kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii, Vijana na Wanawake, mnamo mwaka 1995 hadi mwaka 2000 alikuwa Waziri wa Wanawake na Watoto na Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi akitokea kwenye jumuiya za wanawake wa CCM Zanzibar.
Mbali na nafasi hizo za serikali lakini Bi Asha alikuwa mstari wa mbele katika kukiendeleza Chama ambapo mnamo mwaka 1964 alikuwa ni Mjumbe wa Vijana wa Paunia kupitia Chama Cha ASP na baadae mwaka 1972 alijiunga na Afro Shirazi Youth League hadi hapo mwaka 1977 vyama vya TANU na ASP vilipoungana na kuzaliwa  Chama Cha Mapinduzi (CCM) yeye akawa miongoni mwa wajumbe wa mwanzo wa chama hicho.
Tokea hapo mwaka 1978 kwenye jumuiya ya wanawake wa CCM kisha kuwa mjumbe wa JUWATA na baadae kuwa mjumbe wa Wazazi wa chama hicho cha CCM mwaka 1980 na akaanza kukamata nyadhifa nyengine mbali mbali ndani ya chama ikiwemo Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na 1992 hadi 2010 Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) mwaka 2007 hadi anamaliza uhai wake yeye ni Makamo Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mwaka.
Katika uhai wake Bi Asha amaekabiliwa na changamoto mbali mbali lakini zaidi kwa wapinzani wake wa Chama Cha Wananchi (CUF) ambao alikuwa ni mpinzani wao mkubwa katika siasa.
Bi Asha ambaye maarufu anajulikana kwa msimamo wake wa maneno alitokuwa akiyatoa mara kadhaa kuhusiana na Maalim Seif kushika dola yeye ni miongoni mwa wahafidhina wachache waliokuwa wakipinga na kusema kwamba “Hii ni nchi ya kimapinduzi na haitoki kwa karatasi”.
Matamshi yake hayo yakimaanisha hata mkipiga kura hamuwezi kushinda “Labda na nyie mfanye Mapinduzi mpindue kama tulivyopindua lakini hatutoi..hatutoi…hatutoi” hizo ndo kauli zake ndani ya baraza la wawakilishi na hata katika Bunge Maalumu la Katiba.
Mbali ya ujasiri wake huo wa kusimamia uhafidhina lakini Bi Asha pia alikuwa ni mtetezi mzuri wa maslahi ya Zanzibar kwa muda mrefu amekuwa akisimamia na kutetea suala la Zanzibar katika Muungano lakini kilichokuwa kikimponza na kuitwa msaliti ni kushikilia uhafidhina na umapinduzi tu.
Inawezekana wengi wakamuona Bi Asha ni mtu aliyekuwa anasimamia dhana isiyokubalika na wengi katika ulimwengu huu wa sasa lakini ni miongoni mwa wanawake wachache ambao wameweza kusimama imara na kutetea kile wanachokiamini katika maisha yao.
Bi Asha kwenye Umapinduzi hajawahi kukengeuka hata siku moja ni miongoni mwa wengine walioipigia debe serikali ya umoja wa kitaifa kwa wakati ule ingawa kwa baadae akaungana na wenzake na kutaka kura ya maoni ya kuivunja kutokana na dhana ile ya uhafidhina na umapinduzi mbele.
Badhi ya wakati alikuwa na uzalendo na kuipenda nchi yake na linapokuja suala la kuitetea Zanzibar kwenye Muungano yeye ilikuwa kama anajifunga kibwebwe na kuanza ‘kucharura’ khasa akipaza sauti yake akisema na kutetea haki za Zanzibar na wakati mwengine aliungana na back benchers kwa kuikosoa serikali na kutaka kamati teule ziundwe katika kuwafichua wenye kufanya badhirifu ndani ya serikali.
Ukiacha ya kwenye siasa pia alikuwa ni mcheshi, mtu mwenye kupenda watu hodari na ni mzungumzaji mzuri na daima akipenda kutania muda wote ambaye nimejuana naye akiniita ‘Mwanangu’ na kunitaka nimwite ‘Mama’ kutokana na mahusiano na urafiki wake na Baba yangu tokea wakiwa wadogo ambapo walicheza pamoja.
Kama ilivyo kwa binaadamu wengine hawakosi kuwa na makosa na kasoro katika maisha yake lakini tusahau yale mabaya yake na tumkumbuke kwa mema yake ni binaadamu kinachotakiwa sasa ni kumuombea katika safari yake hiyo nzito Mwenyeenzi Mungu awatume malaika wake wampokee kwa mikono ya rehma na wamlaze mahali pema peponi. Amin.
Advertisements

One Reply to “Kwaheri Bi Asha, Kapumzike salama”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s