Huku CCM chuki, kule Dk Shein king’ang’anizi

Vijana wa Chama cha Mapinduzi CCM wakipita mbele ya mgeni rasmi Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein wakiwa na bango lenye ujumbe wa ubaguzi
Vijana wa Chama cha Mapinduzi CCM wakipita mbele ya mgeni rasmi Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein wakiwa na bango lenye ujumbe wa ubaguzi

Tatizo la Zanzibar limejulikana. Wanachama wa CCM Zanzibar wameanika wazi. Vijana tena wenye akili timamu wameitangazia dunia tatizo la Zanzibar kwamba si uchaguzi wala matokeo yake, bali ubaguzi na chuki. Katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mapinduzi Zanzibar Januari 12, mbele ya viongozi wa kitaifa lilipitishwa bango lililoandikwa maneno kwa herufi kubwa: MACHOTARA HIZBU ZANZIBAR NI NCHI YA WAAFRIKA.

Kwa sababu ya chuki ujumbe ulilengwa kwa wapinzani lakini uligeuka kuwa mwiba kwa CCM ambako kuna machotara kibao ndani ya Serikali yake. Hesabu. Halafu pale Michenzani, umbali wa mita 200 hivi kutoka Kisiwandui yalipo makao makuu ya CCM, kuna kijiwe maarufu kiitwacho Sauti ya Kisonge.

Hapo huandikwa ujumbe uliojaa chuki, kejeli, dhihaka, dharau, ubaguzi. Ni mashambulizi dhidi ya wapinzani hasa CUF; mpinzani mkuu hasa Katibu mkuu wa CUF (mgombea urais wa Zanzibar) Seif Sharrif Hamad.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka jana kulikuwa na ujumbe uliokuwa unahamasisha uvunjwe mwafaka uliowezesha Seikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). Ujumbe ulisema: “Ole wao; Pemba iwe salama, Unguja zogo tumechoka. 2015 maridhiano yaishe Unguja iwe salama, Mapinduzi Daima”.

Siku nyingine waliandika: “Nendeni kwenu msiotaka tuacheni wapenda amani na maendeleo”. “Angalieni Sudani ya Kaskazini na Sudani ya Kusini, vereje Pemba na Unguja inawezekana.” Tawi hilo ndiyo kipindi cha kufanya marekebisho ya Katiba mwaka 2010 lilihamasisha kura ya hapana likisema: “Wana CCM mseto ni hatari, kura ya maoni tia hapana, hapana, hapana.”

Baada ya kuibuka mzozo wa mshindi wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015 na ikionekana wazi aliyeshinda uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 ni Maalim Seif waliandika: “Mtangazeni huyo Sefu tumeyataka wenyewe haya!” Sauti ya Kisonge inawakilisha hisia za chuki za wana CCM.

Huo ni mtazamo wa CCM ndiyo maana hakuna kiongozi wa Serikali wala chama anayethubutu kukemea hasa pale maneno yanapokuwa makali yaliyojaa ubaguzi na uchochezi.

Mfano, japokuwa viongozi wa ngazi ya chini wamejitokeza kukemea ujumbe wa bango la ubaguzi lililopitishwa mbele ya viongozi Siku ya Mapinduzi, viongozi wa ngazi ya juu wako kimya kama hawapo.

Wiki hii Sauti ya Kisonge imesema: “Hukulijua kaburi ya baba ako! Iweje uyatambue mapinduzi yetu? Mlaunga wewe, uchaguzi upo.” Ujumbe huu unashadidia ule wa Machotara Hizbu Zanzibar ni nchi ya Waafrika.

Tatizo si Pemba, tatizo ni CCM kuwaona wanasiasa wengine ambao si CCM kuwa hawafai kuongoza Zanzibar. Maana kama tatizo lingekuwa Pemba na watu wake, mbona Rais wa sasa wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein anatoka Pemba! Mbona Maalim Seif alipokuwa mwana CCM alikuwa akipendwa alipokuwa Waziri Kiongozi ilhali akitoka Pemba!

Tatizo ni CCM kumiliki visiwa vya Unguja na Pemba, kwamba wengine wasiotokana na CCM iliyozaliwa kutoka Tanu na ASP hawastahili kuongoza visiwa hivyo. Wazanzibari wanamjua Maalim Seif alivyokuwa mwanachama kindakindaki wa ASP na CCM, lakini leo anapakaziwa kuwa CUF anayoongoza inakataa kutambua Mapinduzi ya mwaka 1964 bali eti inataka historia itambue uhuru wa Zanzibar wa Julai 1963.

Tujikumbushe. Januari 1961 ulifanyika uchaguzi kugombania viti 22; ASP ilipata 11 na ZNP (Hizbu) pia 11. Juni 1961 ukafanyika uchaguzi mwingine kuwania viti 23. ZNP ikaungana na ZPPP na kunyakua viti 13 na ASP 10. ASP ililalamikia matokeo, vurugu zikazuka watu 68 wakauawa.

Julai 1963 vikaongezwa viti hadi 31; ASP ilishinda uchaguzi wa jumla kwa asilimia 54 lakini iliambulia viti 13 tu bungeni wakati ZNP/ZPPP vilinyakua viti vilivyosalia na kuongoza Serikali. Desemba 10, 1963 Zanzibar ilipata uhuru huku ZNP/ZPPP wakiongoza Serikali.

Januari 12, 1964 ASP ikafanya mapinduzi yanayohusudiwa hadi leo. Maalim Seif alikulia ndani ya ASP na CCM na akaja kuwa Waziri Kiongozi. CCM wanajua wamepoteza uchaguzi isipokuwa wanatumia mabavu, dola; polisi na jeshi vyote vyao. CCM wanajua kuwa Maalim Seif alishinda uchaguzi isipokuwa wanalazimisha ionekane anataka kuvunja Muungano.

Mara kadhaa amesema anaunga mkono Muungano lakini si wa muundo huu. Pia, wanajua Maalim Seif alishinda isipokuwa wanataka kumzuia asiwe mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Muungano.

Hivyo, njia pekee ni kulazimisha uchaguzi mpya ambao CUF watasusia. Katika mazingira kama haya unamwona Dk Shein akitamba ni rais halali. Rais wa kuongoza waliomkataa. Rais aliyepuuza misingi ya sheria ya matakwa ya wengi (mokcracy). Kichekesho kilioje?

Chanzo: Mwananchi

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s