Fatma Karume amshauri Dk Shein akae pembeni

Mwanasheria wa kujitegemea nchini, Fatma Karume akizungumza ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana. Picha: Mwananchi
Mwanasheria wa kujitegemea nchini, Fatma Karume akizungumza ofisini kwake jijini Dar
es Salaam jana. Picha: Mwananchi

Dar es Salaam: Mwanasheria wa kujitegemea nchini, Fatma Karume amemshauri Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein kuachia madaraka. “Dk Shein lazima aondoke kwa sababu kuendelea kubaki madarakani ni kuwanyang’anya Wazanzibari haki yao ya msingi,” alisema Fatma ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Fatma alisema kuwa mzozo wa Zanzibar umesababishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha kutangaza kufutwa matokeo yote ya Uchaguzi Mkuu visiwani humo wakati hana mamlaka kisheria kufanya hivyo.

Fatma alisema Jecha hana mamlaka kikatiba na kisheria kufuta matokeo hayo kwa kuwa maamuzi kama hayo yanatakiwa kufanywa na ZEC yenye mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe watano; watatu kutoka CCM na wengine wawili kutoka CUF.

“Akidi ya vikao vya ZEC ni mwenyekiti na wajumbe wanne. Kama kikao kilifanyika, akidi ilitimia na jambo hilo likakubaliwa na tume hiyo, basi waonyeshe ni wapi walipokubali wajumbe wengine. Hata makamu mwenyekiti hajashiriki kwenye maamuzi hayo kwa sababu kisheria uchaguzi hauwezi kufutwa bila kupata akidi hiyo,” alifafanua Fatma.

Mwanasheria huyo alisema kuwa amekuwa akiwasikia baadhi ya wana CCM Zanzibar wakisema kuwa Jecha ndiyo tume na tume ndiyo Jecha, hivyo ana haki ya kufuta uchaguzi.

Lakini Fatma alisema Jecha hana mamlaka kusema jambo ambalo halijakubaliwa na tume. Alipoulizwa ikiwa hatua ya aliyekuwa mgombea urais kupitia CUF, Seif Sharrif Hamad ya kutangaza matokeo aliyodai yalimpa ushindi si kosa, Fatma alisema, “Sikumuona Maalim Seif alipokuwa anatangaza matokeo hayo hivyo sijui kama alijitangaza kuwa mshindi au alitangaza matokeo kama yalivyobandikwa kwenye vituo.

“Katika nchi zilizokomaa kidemokrasia mgombea anaweza kuona mwelekeo wa matokeo na akampigia mwenzake kumpongeza. Nadhani Maalim Seif alisoma jumla ya matokeo ya uchaguzi kama yalivyobandikwa kwenye vituo, hivyo hilo si kosa ati,” alisema na kuongeza:

“Ninasikitishwa na tabia hii. Sikutegemea kama CCM watatumia nguvu kutaka kubaki madarakani kwa njia hii. Sikutegemea kama watavuruga katiba…ndiyo maana nina huzuni.”

Jambo jingine alilosema litazua mgogoro Zanzibar ni mamlaka yenye haki ya kuidhinisha fedha za uchaguzi wa marudio ikiwa watalazimisha ufanyike. “Kisheria fedha hizo ni lazima zikubaliwe na Baraza la Wawakilishi.

Baraza lipo wapi? Ili mtu awe waziri lazima awe mjumbe wa Baraza la Wawakilishi. Rais alivunja Baraza Agosti na kwa hiyo hadi ilipofika siku ya kuapishwa rais mpya, Zanzibar hakuna Baraza wala Waziri. Ina maana fedha za wananchi zinatumiwa bila idhini ya Baraza, ” alisema.

Alisema kinachofanyika Zanzibar ni ‘ukoloni’ wa watu weusi dhidi ya watu weusi ambao unawakosesha Wazanzibari haki yao msingi ya kumchagua kiongozi wanayemtaka. “Hali si shwari Zanzibar.

Watu wamekata tamaa kwa sababu unapokuwa na Serikali ambayo inanyang’anya haki ya wananchi ya kupiga kura, kuandamana, watu wanakosa imani na Serikali hiyo,” alisema.

Kurudia uchaguzi Kuhusu kurudiwa uchaguzi nchi nzima, Fatma alisema ulipofanyika uchaguzi mwaka 2000 ambao Amani Karume aligombea kwa mara ya kwanza, zilitokea dosari katika majimbo 10 ya Unguja.

CUF walipotaka uchaguzi urudiwe nchi nzima, CCM chini ya Benjamin Mkapa waligoma wakasema ni katika majimbo yenye dosari tu.

“Nini kimetokea mwaka huu? Kama dosari zilijitokeza Pemba kama wanavyodai kwa nini urudiwe Unguja? Kwa nini hawataki kutumia uamuzi wa mwaka 2000 wa kurudia maeneo yenye dosari tu?” alihoji.

“Mkapa alisema wazi kwenye kipindi cha Hard Talk cha BBC akihojiwa na mtangazaji Tim Sebastian uchaguzi hauwezi kufutwa ila utarudiwa tu katika baadhi ya majimbo. Kwa nini leo mambo yamebadilika na CCM inataka uchaguzi mpya?” alihoji.

Fatma ambaye alikataa kueleza msimamo wake kisiasa, alisema iwapo uchaguzi huru na wa haki utafanyika leo Zanzibar, CCM haiwezi kushinda kwa sababu Wazanzibari wanajionea yale ambayo wanafanyiwa na chama hicho.

“CCM imeshindwa Zanzibar kwa sababu ilishindwa kuwashawishi watu wake na badala inawakemea, ikawanyima haki zao. Kisaikolojia wapiga kura wanataka haki zao na wasibaguliwe lakini ukiwapelekea jeshi na vifaru, unazidi kuwapoteza,” alisema.

Sherehe za Mapinduzi Wakati zikiwa zimesalia siku nne kufikia kilele cha maadhimisho ya miaka 52 ya Sikukuu ya Mapinduzi ya Zanzibar, Fatma alisema kwa hali ilivyo haina maana kutokana na CCM kung’ang’ania kukaa madarakani kwa nguvu.

“Ninajisikia kusalitiwa. Madhumuni ya Mapinduzi haikuwa kuiweka CCM madarakani milele bali kurejesha madaraka kwa wananchi,” alisema.

Alisema aliambiwa kuwa waliofanya mapinduzi (wakiongozwa na Abeid Amani Karume) walitabiri kuwa ipo siku Zanzibar itakuwa na uchaguzi au Serikali ya Umoja wa Kitaifa lakini CCM hawataki.

“Wakati hao waliofanya mapinduzi wakisema hivyo, CCM haikuwepo, ilikuwepo ASP. Hao ASP hawakuwa wakijiaminisha kuwa watakaa madarakani milele,” alisema.

“Wakati tunaadhimisha mapinduzi ya Zanzibar, ni vyema Watanzania wakafahamu kuwa malengo ya mapinduzi hayo yalikuwa ni kuondoa ubaguzi wa aina yoyote na kuweka misingi ya kidemokrasia lakini CCM wamevuruga,” alisema Fatma.

Chanzo: Mwananchi

2 Replies to “Fatma Karume amshauri Dk Shein akae pembeni”

 1. Nadhani anachokieleza Bi Fatma Karume ni marudio na msisitizo wa kauli zake za awali …Jopo la wanasheria kutoka VISIWANI na BARA pia walikutana na kuongelea kadhiya hiyo ya matokeo ya uchaguzi, Taasisi za Nchi za Jumuia ya madola nazo pia zimekerwa na kusikitishwa na Hujuma inayofanywa na serikali ya CCM.
  Kwa ujumla jitihada nyingi zikichangiwa na vikao vya viongozi wakuu wa Nchi ziliffanyika , na kauli nyingi zilitolewa na ahadi kadhaa kuhusiana kutangazwa kwa mshindi wa uchaguzi 2015 …Hata hivyo, Hakuna lolote lililofanyika ktk kutanzua mgogoro huo zaidi kusikia kauli za viongozi kutoka kambi zote wakilumbana kwa maneno ya kejeli na ushindani.
  SISI WATANZANIA TUNAJIULIZA NINI HATMA YA ZANZIBAR ? NA WAZANZIBAR WANAPELEKWA WAPI? AU KUNA AGENDA ZA SIRI ZA KUANDAA MACHAFUKA YA UMWAGAJI WA DAMU BAINA YA WAZANZIBAR WENYEWE KWA WENYEWE WATU WENYE ASILI MOJA NA DINI MOJA ?

  1. Ukweli ni kwamba F.Karume,hana hoja shikika kwenye
   suali la uhalali wa Urais wa Shein ,hadi atakapo apishwa
   “aliyejitangazi Ushindi kinyume na taratibu za uchaguzi
   au tangazo la ukakiki la nani mshindi na aliyeshindwa “.

   Pili,mbali na kwamba huyu mtoto wa Karume Jr.mjukuu
   wa Mzee Karume ,anayoyasema yote ni yenye lengo la
   kujitafutia umaarufu na ni uendelevu/endeleza ushabiki
   wa urafiki wa babaye na aliyejitangazia ushindi kwa ile
   ile misingi ya Maridhiano ya Siri yaliyokosa radhi za
   wengi ndani ya CCM Na CUF.

   Tatu,Tamko la F.Karume kwamba eti ” kinachofanyika
   Zanzibar ni ukoloni wa watu weusi dhidi ya watu weusi
   unawanyima Wazanzibari haki msingi ya kumchagua
   kiongozi wamtakaye “.Hili ni tamko lenye ulofa wa hali
   juu kabisa la wenye ” akili za samaki “.

   Kubwa zaidi la kipotoshi ni pale aliposema ” Nnajisikia
   kusalitiwa ,madhumi ya Mapinduzi haikuwa kukipa
   chama cha ASP/CCM Madaraka ya milele,bali ni
   kurejesha madaraka kwa wananchi ..”.Hivi kweli
   huyu mama ndani ya `mindset yake,yeye alikuwa
   ananijisemea hayo kihovyo hovyo,yeye kama Nani ;
   na kwa niaba ya Nani ?.
   Hivi kweli,hajuwi kwamba Mapinduzi ya January
   1964 ndiyo pekee yaliyorejesha madaraka kwa
   wananchi ?.Anataka madaraka yarejeshwe kwa
   kwa wananchi gani ?.

   Madhumuni gani mengineyo kinyume na hayo hayo yaliyotendeka kwa kuupindua Usultani na serikali yake
   ya kikaragosi ?.

   Au F.Karume ,anataka kudanganya kuwa Mapinduzi
   yalikuwa na lengo la kuwarejeshea madaraka kundi
   lile-lile la wale-wale wa tabaka lenye itikadi za wale
   wale za waliopinduliwa ?.

   Kufikiri Na Kujiamnisha Hivyo Ni Ishara tosha ya ule Ulofa
   Wa Ziada Ambao Ni Kinyume Na Madhumuni Jumla Ya Mapinduzi Ya Kila Leo Tokea 1964 MAPAKA HII LEO.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s