Mzee Mwinyi alishajiondolea heshima

Mzee Ali Hassan Mwinyi
                                         Mzee Ali Hassan Mwinyi

Na Jabir Idrissa

MZEE Ali Hassan Mwinyi wa mwaka 1984, kwa hakika siye anayeonekana zama hizi machoni mwa wananchi wa Zanzibar. Wanamuona ni mtu tofauti kwa mbali. Wazanzibari wanajua fika kuwa Alhaji Mwinyi ndiye rais wa tatu wa Zanzibar aliyekaa uongozini kwa mwaka mmoja tu (1984/85) na kutakiwa kuondoka ili akachukue madaraka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wanajua ndiye yule kiongozi waliyempenda isivyomithilika alipokuwa akiongoza Zanzibar. Wanajua aliitoa kubaya Zanzibar na kuivusha ikajenga uchumi uliozalisha ajira nyingi hasa sekta binafsi na zikachochea pato zuri kifamilia.

Wanajua halkadhalika kuwa wakati ule mzee Mwinyi alikuwa si mwenye fikra za ndani ya moyo wake dhidi ya Zanzibar na watu wake, isipokuwa aliongozwa na dhamira njema ya kuonesha au kutoa mchango wake kujenga jamii.

Yeye alikulia kijiji cha Mangapwani, karibu na Bumbwini, kisiwani Unguja akiwa kijana aliyetokea Wilaya ya Rufiji, Mkoa wa Pwani.

Alifika Zanzibar kwa lengo la kupata elimu zote, ya dini (Uislam), na dunia (Sekula). Akawa miongoni mwa vijana wasomi wa il’mu ya dini yake. Akawa mwalimu.

Alipigiwa kura nyingi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akikaa kwenye jumba la Magogoni, jijini Dar es Salaam. Akaongoza kwa miaka 10 hadi alipostaafu na kumkabidhi kijiti Benjamin Mkapa.

Usiyejua ujuwe leo kwamba alipokuwa anaondoka Zanzibar kama rais aliyeongoza kwa mwaka mmoja tu lakini kwa mafanikio ya kupigiwa mfano, alikuwa bado anapendwa na kuheshimika sana.

Akipendwa hasa na Wazanzibari, tena wote, hata ndugu zetu Wazanzibari wa asili ya Pemba, kisiwa kinachoonekana na wakubwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama cha “shida tu” au “balaa tupu.”

Ni ni kisa cha viongozi wa CCM kuwaona watu wa Pemba siwo? Watu hao hawajawahi kutoa kura zao kwa raidhaa kwa watawala tangu asili yao.

Wazanzibari wengi leo wanajiuliza kwamba mzee Mwinyi waliyemjua kwa heshima zote, alijipotezea heshima ya kiwango kile baada ya kuanza kusikika hadharani akitoa maneno ya masimango dhidi ya watu wenye asili ya kisiwa cha Pemba, hata kuwafananisha na vijibwa vya santuri.

Wazanzibari wanajua vilevile kuwa mzee Mwinyi wa zama hizi haijali tena Zanzibar kama nchi inayohitaji kupewa mamlaka ya kujiendesha ili kurudisha hadhi yake ya kuwa kituo cha kielimu pamoja na eneo bora kibiashara na shughuli za kukuza utamaduni.

Hawamuoni tena kama mwenye kuifikiria ing’are na kupaa kimapato kama alivyoiongoza 1984; hataki kuiona inafaidi matunda ya uhuru wake  wa Desemba 10, 1964, basi hata kuiona inanufaika na matunda ya mapinduzi, ikiwemo watu wake kupata makazi bora, huduma bora za jamii na kwa jumla, maendeleo yanayoendana na wakati uliopo.

Mzee Mwinyi hasemwi vizuri Zanzibar, na hasa miongoni mwa wafuasi wa CUF ambao wanamuona kama kikwazo cha kupatikana Zanzibar yenye mamlaka kamili.

Kiongozi huyu hasemwi kwa ukakamavu kama alivyokuwa miaka ile. Siku hizi na tangu ilipovuja kuwa alikuwa na mtizamo wa kutoridhia Maalim Seif kukabidhiwa madaraka ilipothibitika kuwa alishinda uchaguzi mkuu tangu mwaka 2005.

Nimekuwa nikiwasikia wananchi baadhi yao wakisema Mzee Mwinyi alipata kusema kuwa kuruhusu Maalim Seif akabidhiwe kuongoza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni kuridhia viongozi wa CCM kujidhalilisha.

Kwamba watakuwa wanajidhalilisha kwa kuwa wanayekusudia kumkabidhi madaraka hayo, ni kiongozi mwenye uwezo na dhamira hasa ya kuibadilisha nchi iwe yenye maendeleo makubwa.

Kama hiyo haitoshi, wanamuona mzee Mwinyi leo kama kiongozi anayejali zaidi maslahi ya familia yake na kuwa tayari kwa vyovyote vile kusimamia watoto wake wapate nafasi kubwakubwa za uongozi kupitia jina la Zanzibar.

Wameshuhudia baada ya miaka kadhaa ya mtoto wake, Dk. Hussein Mwinyi kupata ubunge jimbo la Kwahani, safari hii mtoto mwingine, Abdalla Ali Hassan Mwinyi, naye ameunyaka ubunge.

Abdalla ni mbunge wa Fuoni, aliyetangazwa mshindi kwa kupata kura zisizozidi 1,100 kati ya kura zisizozidi 1,400 za jimbo zima. Ni jimbo lililomegwa kutoka jimbo ambalo katika uchaguzi wa 2010, lilikuwa na zaidi ya wapigakura 6,000.

Wananchi wanasema wazi kwamba chaguo lao tangu waliposhiriki kura za maoni, alikuwa mtoto wao kipenzi, Mzee Yussuf ambaye ni msanii maarufu na mmiliki wa kundi la muziki la Jahazi Modern Taarab.

Ni kwa vipi Wazanzibari wakafikia kutomuamini tena mzee Mwinyi? Kauli tata zinazochochea mgawanyiko katika jamii, na zinazoviza demokrasia ya siasa za ushindani.

Mzee Mwinyi ameonekana akihutubia hadhara ya sherehe za Maulid ya Mtume Muhammad (SAW) yaliyoandaliwa na mbunge wa Mpendae, Salim Turky anayemiliki kituo cha televisheni cha Zanzibar Cable, miongoni mwa miradi ya mfanyabiashara na mwanasiasa huyo.

Amesifia amani iliyopo Zanzibar kwa sasa. Akahimiza wananchi waidumishe kwa kuwa inadhihirisha neema ya Uislam kwa Wazanzibari.

Huku akijinasibu kuwa Zanzibar ni raha tupu, alisema si vyema watu wakatafuta mambo mengine, badala yake waitazame Syria inavyovurugwa kwa vurugu.

Lakini akasema Tanzania kulikuwa na hofu kuwa ingeingia katika machafuko kutokana na uchaguzi. Akashukuru uchaguzi umekwenda vizuri japo kwa Zanzibar “yametokea matatizo madogomadogo ambayo yatamalizika.”

Kwa hivyo, kwake mzee Mwinyi yaliyotokea Zanzibar ni matatizo madogo, hayamshughulishi, na anaiona Zanzibar ina raha tupu. Hapa ndipo atapozidisha kuonekana mkorofi na kiongozi asiyeaminika.

Kama uzee ni dawa kwelikweli, basi hata hayo anayoyaita matatizo “madogomadogo” yasingetokea, hasa inapoaminika yamepangwa na kwa nafasi yake, bali na namna anavyoshiriki unapokaribia uchaguzi, na akiwa amesikika aliyoyasema wakati wa kampeni, aliridhia kwa kuwa yanampendeza kwa ilivyo dhamira yake.

Kama mzee Mwinyi anashiriki vikao vya Ikulu, halafu nje viongozi wenzake wa CCM wanasikika wakitoa kauli za ovyo, anajiondoaje katika uvundo huo? Ni dhahiri uzee haujamsaidia.

Na kwa kweli amejishushia hadhi na kujiondolea heshima na imani aliyokuwa nayo kabla. Nampa pole.

 

 

Advertisements

2 Replies to “Mzee Mwinyi alishajiondolea heshima”

  1. ndugu zangu wazanzibar mm ni mzanzibar lakini niwausieni amani amani ikivunjika mzanzibar atamdhuru mzanzibar mzanzibar atamdhuru mbara nasi sote ni ndugu ninavyofaham myenendo ya serikali kwa mawala kama haya nikutokuyumba rudieni uchaguzi simamieni kila mtu kura yake zanzibar ni ndogo nirahisi kuzibiti hali hiyo katika hilo cuf ambao wanadai kuonewa,waweke masharti ya usimamiaji uweje wasimamizi wa nje wajekwa wingi ngoma uwanjani,anaekufa safari hii kafa kweli,kweli zanzibar inamatatizo ya kiuchumi na ndio shida kubwa ya wazanzibar wanapenda biashara wanabanwa sana kazi hakuna kulikua na kiwanda cha sukari sigara wapi sasa uchumi pemba dhooful hali watu taabani viongozi hawa wanafanya nn?unashindwaje kuiweka zanzibar yenye watu 1m. na kidogo katika bora?kiongozi aliepo mh.shein hajui kama neema hupunguza upinzani?nikitu kidogo kinahitajika katika uongozi zanzibar kwanza kujua wazanzibar wanahitaji nini,pili kuiendesha kama nchi bila shinikizo la bara kama alivyoendesha komandoo.kufanya hivyo nchi itaenda vizuri na wazenj wataridhia.

  2. Kwa vile Maudhui ilikuwa inamuhusu Mzee Ali Hassan Mwinyi -na mm ningependa kuchangia kwa maneno yaliokuwa yakisikika zama hizo kule Dar —-Msikiti wa Magomeni unaoitwa MCHANGANI ..ilikuwa siku ya ijumaa nilipokuwa nikitoka kusali , nikaona vikundi vikundi vya waislaam vinaongelea kuhhusu KIBAO ALICHOPIGWA MHESHIMIWA HUYO AMBAYE RAIS WA TANZANIA …kumbe huko alipoalikwa ( SIKU YA HAFLA ZA MAULIDI ) alikwenda kutangaza CONDOMS badala ya kutoa neno la kumsifu Mtume (SAW) -Kijana mmmoja wa kiiislaam alinyanyuka na kumpiga kibao …mm naona heshima yake ilianza kumuondekea tokea siku ile

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s