Dk Magufuli anapomtaka Maalim Seif ‘apige kazi’ tu Zanzibar

Dk John Magufuli akisalimiana na Maalim Seif Sharif Hamad
Dk John Magufuli akisalimiana na Maalim Seif Sharif Hamad

By Ndimara Tegambwage

Wiki iliyopita ilikuwa “Wiki ya Zanzibar.” Kwa nini? Kwa sababu wapinzani wakuu wawili kisiasa visiwani walikuwa Dar es Salaam. Hao ni Dk Ali Mohamed Shein na Maalim Seif Shariff Hamad. Walikuwa Dar es Salaam kumweleza Rais John Magufuli jinsi mazungumzo ya kumaliza mgogoro wa Zanzibar yanavyoendelea na hatua iliyofikiwa.

Oktoba 28, mwaka jana, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha alitangaza kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu na matokeo yake Zanzibar. Wakati Jecha anatangaza kufutwa kwa uchaguzi na matokeo yote, tayari matokeo ya majimbo 33 yalikuwa yameshatangazwa.

Hadi tangazo la kufuta uchaguzi, kila chama kilikuwa na viti 27 vya uwakilishi. CCM haikuwa imepata hata kiti kimoja kisiwani Pemba. CUF ilikuwa imenyakua viti tisa Unguja. Ngome kuu ya CUF ni Pemba.

Sasa kwa nini mwenyekiti wa ZEC alifuta uchaguzi? Alidai kwamba kulikuwa na vurugu katika maeneo mbalimbali; kwamba yalijitokeza mazingira yaliyofanya uchaguzi usiwe huru na wa haki; kwamba Maalim Seif alijitangazia ushindi. Sheria ya uchaguzi inatoa adhabu kwa mtu anayetangaza matokeo badala ya Tume. Je, Maalim Seif ameshtakiwa? Hajashtakiwa.

Sheria ya uchaguzi inatoa mamlaka kwa Tume kusimamisha au kuahirisha uchaguzi katika eneo ambako kuna tatizo. Je, kuna hatua yoyote iliyochukuliwa kule ambako inadaiwa kutokea vurugu? Hapana.

Jecha alifuta uchaguzi wote ambako inadaiwa kuwa na vurugu na kule ambako kulikuwa na utulivu na usalama.

Sasa hili lina uhusiano gani na kwenda Dar es Salaam kwa wagombea wa vyama hasimu? Kuna mambo mawili makubwa:

Kwanza, mgombea wa CUF Maalim Seif anashikilia kuwa uchaguzi ulifutwa baada ya yeye kuonekana ameshinda.

Maalim anabeba ‘makabrasha muhimu’ yenye taarifa mbalimbali kuthibitisha ushindi wake na chama chake. Anadai kufuta uchaguzi ni njama za kutaka kupora ushindi wa chama chake na wapigakura wa Zanzibar.

Pili, CCM inadai kuwa ufutaji matokeo ilikuwa hatua sahihi. Inataka uchaguzi urudiwe. CUF inakataa kurudia uchaguzi. Inadai siyo haki wala sahihi. Inataka ujumuishaji matokeo uendelee kutoka pale zoezi lilipositishwa.

CUF wanadai kuwa na matokeo sahihi. King’ang’anizi chao kinatokana na kile wanachoita ‘zana za ukweli’ ambazo ni fomu za matokeo na zilizosainiwa kutoka vituoni. Kuna madai kuwa CCM imekwishajiimarisha kwa kuongeza idadi kubwa ya wapigakura visiwani na ndiyo maana inataka uchaguzi urudiwe.

Katika mazingira haya, CCM imebanwa. Ina kitu mdomoni. Ikikitema itakuwa imetema utamu. Ikikimeza itakuwa imemeza moto. Kote kuna madhara.

Lakini ni kweli kwamba uchaguzi na matokeo yake yote vilifutwa? Hapana. Siyo kweli. Baadhi ya matokeo, ingawa yalitamkwa kufutwa, hayakufutika. Kuna walioyakingia kifua.

Baadhi ya waliochaguliwa kuwa wabunge wa Bunge la Muungano, walikwenda Dodoma na kuapishwa. Ni hao waliombeba mgombea urais wa Muungano kutoka upande wa pili wa Muungano.

Je, katika mazingira haya, uchaguzi ukirudiwa Zanzibar ina maana na hao walioko bungeni Dodoma watarudi kwenye kinyang’anyiro? Kurudi katika uchaguzi ni kubatilisha ubunge wa Wazanzibari waliokwishaapa. Ni kumwacha rais katika mgogoro mkubwa kisiasa na kikatiba, ambamo yumo tayari.

Kuendelea kuwa wabunge katika Bunge la Muungano; huku Zanzibar wakirudia uchaguzi, ni kujinyima uhalali na hivyo kuonekana mamluki waliochukuliwa rasmi kuhalalisha matakwa ya CCM.

Rais Magufuli hawezi, kama ambavyo hastahili, kukubaliana na hili na bado akabaki kuonekana mwadilifu mbele ya Watanzania na jumuia ya kimataifa.

Kwa nini? Kwa sababu uchaguzi uliobatilishwa hauwezi kuzaa wachache ambao si batili. Na ili ‘waliobatili’ wawe halali, ingawa awali walifanywa halali kwa shabaha maalumu, sharti ujumuishaji kura za uchaguzi wa Oktoba uendelee kutoka pale ulipositishwa.

Hii maana yake ni kwamba huwezi kurudia uchaguzi Zanzibar. Ama uchaguzi uendelee kwa kujumuisha matokeo au majumuisho yaliyopo (hadi kusitishwa kwa uchaguzi) yachukuliwe kuwa ndiyo matokeo sahihi na halali ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.

Je, Rais Magufuli anaona ‘ukora’ huu wa kisiasa Zanzibar? Je, anaweza kutema wabunge waliompa ‘uhalali’ kwa kuwarejesha katika kukurukakara za kuomba kura?

Sikiliza kauli za marais Magufuli na Shein baada ya kikao cha Dar es Salaam.

Vyombo vya habari vilimnukuu Rais Magufuli akisema amehakikishiwa na Maalim Seif kuwaa wanaendelea vizuri katika mazungumzo; na kwamba amemtaka “…wakamalize majadiliano yao na apige kazi.” Ikulu haijakanusha.

Naye, Dk Shein alinukuliwa akiwaambia waandishi wa habari, “…mazungumzo yanaendelea vizuri na yatakapomalizika tutatoa taarifa kwa umma kuwaeleza maafikiano yaliyofikiwa.”

Kauli hizi mbili hazitofautiani. Kama Magufuli ana maana ya anachosema, na kwa misingi iliyoelezwa hapo juu; basi siyo tu hakuna sababu wala haja ya kurudia uchaguzi; bali hakuna uchaguzi.

Chanzo: Mwananchi

 

Advertisements

One Reply to “Dk Magufuli anapomtaka Maalim Seif ‘apige kazi’ tu Zanzibar”

  1. hao CCM wamenaswa na MTEGO mkubwa wa MWENYE ENZI MUNGU , na wala sio juhhudi za CUF au UKAWA au wengine wakadhani ni ushujaa wa Maalim Seif …..bali M/Mungu alitaka kuudhihirishia ulimwengu juu ya lmaovu na dhulma za CCM zinazofanyika

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s