Miaka 52 ya Mapinduzi Zanzibar, hatma ya mkwamo wa kisiasa

 Abeid Amani Karume rais wa kwanza wa Zanzibar. Kwa ufupi Mtafaruku huu umekuwa tukiambiwa unatafutiwa ufumbuzi kwa kufanyika kwa njia ya mazungumzo ambayo yametawaliwa na usiri uliosababisha kutoa tafsiri ya kukwama.
Abeid Amani Karume rais wa kwanza wa Zanzibar.

Mtafaruku huu umekuwa tukiambiwa unatafutiwa ufumbuzi kwa kufanyika kwa njia ya mazungumzo ambayo yametawaliwa na usiri uliosababisha kutoa tafsiri ya kukwama.

By Salim Said Salim

Zanzibar iliyogubikwa na mtafaruku wa kisiasa kufuatia kufutwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu inaadhimisha miaka 52 tangu kufanyika mapinduzi, Januari 12, 1964.

Mtafaruku huu umekuwa tukiambiwa unatafutiwa ufumbuzi kwa kufanyika kwa njia ya mazungumzo ambayo yametawaliwa na usiri uliosababisha kutoa tafsiri ya kukwama.

Mazungumzo haya yamewakutanisha ana kwa ana wagombea wawili wakuu kwa uchaguzi wa rais. Nao ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ambaye kikatiba muda wa Serikali yake na aliyekuwa Makamu wake wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad ulifikia kikomo Novemba 2.

Hata hivyo, Dk Shein anaendelea kuongoza Serikali ambayo sasa ni ya chama kimoja cha CCM badala ya kuwa ya umoja wa kitaifa baada ya washirika wenzao wa CUF, akiwamo Maalim Seif kukaa pembeni kwa maelezo kuwa hawapaswi kuendelea kushika nyadhifa hizo kikatiba kwa vile muda wa maisha ya Serikali hiyo umekwisha.

Viongozi wastaafu wa Serikali ya Zanzibar, Muungano na wawakilishi wa kimataifa, akiwamo Rais wa zamani wa Nigeria, Goodluck Jonathan, aliyepewa kazi ya usuluhishi na Jumuiya ya Madola wameshiriki katika mazungumzo hayo kwa nyakati tofauti kutegua kitendawili hicho.

Kwa sasa wakati sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi zikiendelea, lakini siyo kwa kishindo na mvuto kama ilivyokuwa miaka iliyopita kutokana na mvutano kati ya CCM na CUF, haijulikani kilichopatikana au kukosekana katika mazungumzo hayo yaliofunikwa na usiri mkubwa.

Zanzibar njia panda

Kwa muhtasari wa Wazanzibari wanaadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi wakielewa walipotoka na walipo, lakini hawajui wanaelekea wapi na watarajie nini katika mvutano huu wa kisiasa ambao mbali ya kuigawa Zanzibar vipande viwili, umezusha hofu ya usalama na kutengwa kisiasa na kiuchumi na washirka wake wakuu wa maendeleo, miongoni mwao nchi za Marekani na Umoja wa Ulaya.

Hofu nyingine iliyopo ni uwezekano kwa washirika wengine wa maendeleo wa Zanzibar, hasa nchi za Kiarabu nazo kama hazikuitenga Zanzibar basi huenda zikapunguza kasi yao ya kutoa misaada.

Kwa vyovyote vile uamuzi wa kufuta uchaguzi uliotangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, umeipa Zanzibar mtihani mwingine katika historia ya miaka 52 ya Mapinduzi na kwa upande mwingine kuutikisa muungano wake na Tanganyika ulioundwa miezi mitatu baada ya kufanyika mapinduzi.

Tayari Rais John Pombe Magufuli aliyeingia madarakani baada ya uchaguzi uliofanyika pamoja na ule wa Zanzibar katika mazingira sawasawa, ameshaanza kuwekewa ngumu na baadhi ya mataifa yakiongozwa na Marekani kwa kuzuia fedha za misaada kwa miradi ya maendeleo.

Hali hii ni mtihani mgumu wa kisiasa, kiuchumi na kidiplomasia kwa Magufuli na kwa kutumia kauli yake maarufu, kilichopo Zanzibar ni “ Hapa kazi tu”, tena ngumu na pevu.

Kinachoonekana ni kwa Magufuli kuwa hana wa kumsaidia na zipo taarifa kwamba juhudi za Serikali yake isinyimwe misaaada na ipewe muda kushughulikia suala la Zanzibar zimegonga mwamba.

Taarifa za kidiplomasia zinadai kwamba jibu lililotolewa na baadhi ya washirika wa maendeleo ni kwa wao kutaka wapewe muda kufikiria kutoa fedha za kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo wakati wakisubiri hatima ya Zanzibar.

Marekani na washirika wengine wa maendeleo ya Zanzibar wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa mchakato wa uchaguzi kuendelea na mshindi kutangazwa, lakini pia kusikitishwa na taarifa za vitendo vya ukiukaji wa haki za binaadamu vilivyoshuhudiwa kabla na baada ya uchaguzi visiwani.

Hii ni pamoja na madai ya wapinzani na taarifa za vyombo vya habari juu ya kile kilichoelezwa kama matumizi mabaya ya vikosi vya ulinzi vya Muungano na vya Serikali ya Zanzibar katika siasa za visiwani.

Vitendo vya watu kupigwa hovyo mitaani na majumbani na mashambulizi ya vyombo vya habari, ikiwa pamoja na kuchoma kituo cha radio binafsi ya Hits FM vimetoa taswira mbaya kwa Zanzibar wakati huu ikiadhimisha miaka 52 ya mapinduzi yaliyoung’oa utawala wenye asili ya Omani wa

Historia ya Mapinduzi

Mapinduzi yalipofanyika watu zaidi ya 500, wakiwamo wanawake na watoto, waliuawa kwa kupigwa mapanga, mashoka, mikuki na bunduki katika Kisiwa cha Unguja, lakini hali ilikuwa shwari huko Pemba.

Watu zaidi ya 2,000 waliwekwa kizuizini na wengine gerezani bila ya kufunguliwa mashtaka.

Kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10 tangu kufanyika mapinduzi, Zanzibar iliendelea kuwa katika hali iliyoshuhudia watu wengi kuuawa kwa kudaiwa kuhusika katika njama ya kuipindua Serikali.

Mara baada ya mapinduzi mamia ya watu walifukuzwa Zanzibar na kupelekwa au wenyewe kwenda nchi za Kiarabu, Comoro na India au kukimbilia Bara, nchi jirani, Ulaya, Marekani na Canada kutafuta usalama au kuanza maisha mapya.

Serikali iliyopinduliwa ilikabidhiwa madaraka na Uingereza iliyotoa uhuru kwa visiwa hivi Desemba 10, 1963. Kila pakifanyika sherehe za mapinduzi familia nyingi za watu wa visiwani na jamaa zao waliopo nje huwa katika maombolezo ya kupoteza wazee, ndugu na marafiki.

Wengi wao hawajui jamaa zao waliuawa katika mazingira gani na wapi miili yao ilifukiwa.

Taarifa za kufanyika mapinduzi zilipatikana asubuhi ya Januari 12 kupitia Sauti ya Unguja, siku hizi inaitwa Zanzibar Broadcasting Corporation (ZBC). Aliyesoma taarifa hiyo alikuwa mmoja wa waasisi wa Afro Shirazi Party (ASP), Mdungi Ussi, aliyeuawa miaka michache baadaye kwa tuhuma za kupinga mapinduzi aliyofurahia kufanyika kwake akiwa madarakani mwaka 1964.

Tangazo hilo lilifuatiwa baada ya kila dakika chache na vitisho vilivyotolewa na John Okello, raia wa Uganda aliyehamia Zanzibar na kufanyakazi za kibarua.

Mpaka wiki chache kabla ya mapinduzi, Okello alikuwa fundi muwashi mjini Unguja na kabla ya hapo alikuwa akivunja mawe Micheweni, Kaskazini Pemba.

Aliletwa Unguja kutoka Pemba na rafiki yake, Ali Lumumba, ambaye alikuwa miongoni mwa waliovamia kambi ya Polisi ya Ziwani (siku zile ikijulikana kama Bomani) kufanya mapinduzi usiku wa Januari 11, 1963.

Mzee huyo aliyefariki dunia akifanyakazi ya kuosha magari eneo la Welesi, mjini Unguja, alikuwa mmoja wa waanzilishi wa chama cha CUF kutokana na kuamini malengo ya mapinduzi yalipotoshwa na kusikitishwa na ubaguzi waliofanyiwa Wapemba.

Okello ambaye msaidizi wake alikuwa Absalom Engine, raia wa Kenya, aliamuru kukamatwa mawaziri wa Serikali iliyopinduliwa na kukataza watu kutembea usiku.

Baadaye wote wawili walifukuzwa Zanzibar bila ya maelezo na taarifa zilizofuata zilieleza kuwa waliwekwa mbele ili kama mapinduzi yasingefanikiwa ionekane waliotaka kupindua ni wageni.

Karume alishiriki?

Baadhi ya wanasiasa wakongwe wa ASP wamesema mzee Abeid Amani Karume aliyekuja kuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar ndiye aliyeongoza mapinduzi. Upo uthibitisho, pamoja na wa mke wake mama Fatma, kuwa mzee Karume alikuwapo Unguja yalipofanyika mapinduzi, lakini yapo mashaka kama alijua kwa undani mpango huo.

Mzee Karume alikwenda Dar es Salaam siku ya pili baada ya kufanyika mapinduzi kwa kuhofiwa kukamatwa kama mapinduzi yasingefaulu.

Karibu kila siku kabla ya kufanyika mapinduzi nilimuona mzee Karume kwa vile nyumba yake na ile niliyozaliwa mpaka leo zinatazamana katika Mtaa wa Kismamajongoo, mjini Unguja.

Mapinduzi yalipofanyika nilikuwa ninakaribia miaka 18 na nilimuona mzee Karume asubuhi ya Januari 10 akinywa kahawa kwa mzee wa Kiarabu, Sheikh Salim (jina lake la utani Mtefutef, yaani mtu asiyeeleweka) katika baraza iliyokuwa karibu na nyumbani kwetu na nyumba ya mzee Karume.

Siku ile Karume akiwa na majirani na marafiki zake, mjomba wangu marehemu Suleiman Omar Kombo, marehemu Aboud Maalim na marehemu baba yangu alininunulia kashata mbili na kuniambia moja yangu na nyingine ya mdogo wangu.

Nilimuomba mzee Karume aniazime baiskeli yake ya aina ya Raleich na alinitaka nikachukue ya mjomba wangu aliyeishi nyumba iliyokuwa nyuma ya baraza la kahawa.

Wapo waliosema mwanasiasa aliyehusishwa na kuuliwa Karume mnamo Aprili 7, 1972 na kushtakiwa kwa uhaini, Abdulrahman Babu, alikuwa miongoni mwa waliopanga mapinduzi, lakini Babu alikuwa Dar es Salaam mapinduzi yalipofanyika.

Baada ya Karume kuuawa Mwalimu Julius Nyerere alimuweka Babu kizuizini katika gereza la Ukonga katika eneo wanaokaa watu waliohukumiwa kunyongwa.

CHANZO: MWANANCHI

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s