Shuwari inayoitumbukiza shimoni Z’bar

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salum Jecha na wajumbe wa tume hiyo
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salum Jecha na wajumbe wa tume hiyo wakitangaza matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Octoba 25 kabla ya kuchukua uamuzi wa kuufuta Octoba 28 akidai kumetokea kasoro katika uchaguzi huo

Na Enzi T. Aboud

SIKU 90 zilizohalalishwa katika Katiba ya Zanzibar ya 1984 zinakwisha, nchi ikiongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein ambaye kuwepo kwake kunatetewa na wasaidizi wake baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 kufutwa kimaajabu.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaongoza peke yake tangu hapo baada ya kuunga mkono tamko la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta uchaguzi na kushikilia kuwa ni halali Dk. Shein kuongoza mpaka rais mpya atakapoapishwa.
Dk. Shein anajitokeza kutekeleza shughuli za urais ndani ya mgogoro wa kisiasa unaoendelea huku akikutana na mshindani mkuu wa urais, Maalim Seif Shariff Hamad pamoja na marais wastaafu Zanzibar.

Kule wananchi kunyamaza wakiendelea na maisha kama vile hakuna kilichotokea; kunapumbaza mgeni asione tatizo. Wenyeji wanaviona viashira vya hatari ya mgogoro kuzaa balaa kwa kukosekana ufumbuzi haraka.

Mshindi wa uchaguzi hajatangazwa miezi miwili uchaguzi ulifanyika. Wanaojua sababu ni watawala wa CCM.
Kabla ya hapo, maisha ya kisiasa Zanzibar yamekuwa ya kushuhudia Maalim Seif akigeuzwa jamvi la kutupiwa matusi ya nguoni na maneno ya kibaguzi kwa watu wenye asili ya Pemba kama yeye.

Zanzibar kwa sababu ya siasa za chuki, imekuwa kijiwe cha siasa chafu na ubarakala wa kutukanana. Hakuna heshima tena sio tu kwa viongozi wa vyama vya siasa, Serikali ama wananchi mitaani, matusi imekuwa nyimbo kila mahali.

Wingu la siasa chafu, na hofu ya usalama kwa raia limeathiri uhusiano wa mtu na mtu na hata ule moyo wa kuhurumiana na kusaidiana.

Kama vile mgogoro huo unavyoathiri Tanzania Bara kwa kuzuiwa msaada wa fedha na Marekani kupitia mpango wa MCC kwa kile Marekani, Ulaya na Jumuiya za Kimataifa zinavyotoa shindikizo na husisitiza mshindi wa urais Zanzibar atangazwe ili kuinusuru na kutumbukia katika vurugu kama ilivyotokea Ivory Coast au Burundi kutokana na watawala kung’ang’ania madaraka.

Huu ni mgogoro zaidi ya riwaya ya mfalme wa Misri Ramases au Farau na Mtume Mussa au Mkombozi wa Wanaisraeli (Wayahudi wa kale). Dk. Shein mshikilia madaraka makubwa ya urais wa Zanzibar bila ya kikomo anajivuna kwa kubebwa na makada wa CCM na serikali ya muungano. Wanamlinda kwa nguvu, na kweli, nani wa kumuondoa kwenye kiti alichokalia?

Na kwa upande wa Maalim Seif, Katibu Mkuu wa CUF, chama chenye nguvu kubwa Pemba na hata Unguja kama ilivyotokea uchaguzi uliofutwa, ameongeza nguvu. Ni nguli kisiasa, asiyeshikika. Nani wa kumkamata na kumuweka gerezani kama ilivyokuwa huko nyuma? Demokrasia ya vyama vingi inamhifadhi.
Lakini, kajitokeza Jaji Mstaafu Mark Bomani akijigamba kuwa mshauri; anamuoneshea kidole kwa kujitangaza mshindi, anataka akubali uchaguzi urejewe kwani “alivunja Sheria ya Uchaguzi,” bila ya mwanasheria mkuu wa kwanza wa Tanganyika huru huyu kutaja Mahakama iliyomtia hatiani na kumhukumu kwa kosa hilo.

Anamdhihaki anaogopaje uchaguzi anaotamba ameshinda? Aina ya kumuunga mkono Mwenyekiti wa Tume, aliyeufuta uchaguzi wote akidai ulikumbwa na matatizo mengi.

Anashiriki kusaidia kumfunika shuka usoni Jecha kwa uhuni alioutenda. Anakingwa, hajapelekwa Mahakamani kwa kutaka kuingiza Zanzibar katika maafa makubwa ya kufuta uchaguzi kinyemela kama wanasheria wanavyothibitisha.

Kama hilo halitoshi, Jaji Bomani akatoa ushauri liundwe jopo la wataalamu na watu wenye kuaminika, liwe chini ya Jaji Mkuu mstaafu mmoja na kuishirikisha Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (NEC) na kupata wataalamu wa uchaguzi kutoka nchi chache rafiki na za Jumuiya ya Madola au Umoja wa Afrika (AU) kuja Zanzibar kutatua mgogoro.

Jaji mstaafu Bomani yumkin anaumwa, mgonjwa wa maradhi ya uzee ya kupoteza kumbukumbu. Amesahau huu si mgogoro wa kisiasa wa kwanza Zanzibar, ni zaidi ya mmoja na kwa visiwani migogoro ya kisiasa ni kama utamaduni wake kutokana na migawanyiko ya wananchi wa asili ya Unguja na wale watokao Pemba.

Lakini wanaoishi Unguja kwa mchanganyiko wao ni wengi zaidi na wanaitikadi tofauti za kisiasa hasa vyama vyao vya CCM na CUF zinatokana na vyama vya kistoria – Afro Shirazi Party (ASP), Zanzibar Nationalist au Hizbu (ZNP) na Muungano wa Watu wa Pemba na Unguja (ZPPP) vinavyozidisha ugumu wa siasa zenyewe na utatuzi unapotokea mgogoro.

Yote anayoyashauri yalifanyika wakati wa mgogoro uliotokea kwa Dk. Salmin Amour Juma na Maalim Seif baada ya uchaguzi mkuu wa 1995. Dk. Salmin alitangazwa mshindi wa urais na kupingwa na Maalim Seif na CUF; na kutangaza kutomtambua. CUF ilishikilia kuwa imeporwa ushindi.

Kwa historia ya siasa ilivyo, Zanzibar hakujatulia na kule kushuhudia wafadhili wakisitisha misaada huku mataifa yakishinikiza Tume ikamilishe kumtangaza mshindi wa uchaguzi, na safari za kitalii zikifutwa na kampuni za uwakala za Ulaya na Marekani, kunathibitisha.

Zanzibar chini ya Dk. Salmin ilifutiwa misaada yote ya maendeleo na kuathiri huduma nyingi za kijamii ikiwemo afya na elimu. Kulizuka upungufu mkubwa wa bidhaa, kukatokea mfumuko wa bei na hatimae Serikali kushindwa hata kulipa mishahara ya watumishi wake.

Ndani ya madhila yote hayo, mgogoro uliodumu kwa miezi 34 ulibaki ukiwashinda Dk. Moses Anaf na Chief Emeka Anyaoku kutoka Jumuiya ya Madola, mpaka Dk. Salmin akamaliza miaka mitano Oktoba 2000 akiwa dhoofu wa afya na mwishoni akapoteza uwezo wa kuona.

Hizo ndizo siasa za Zanzibar za mizengwe na vurugu zinazoshupaliwa na watawala wahafidhina ambazo sijui kama ni kweli Jaji Bomani amezisahau. Fikra zake zinafanana na za Samuel Sitta alipokuwa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba mwaka 2014 alipoamini angeweza kuiburuza Zanzibar kwa kubuni uongo wa kupatikana theluthi mbili ya wajumbe kutoka Zanzibar na kuipitisha Katiba Inayopendekezwa.
Kwa kuwa kulifanyika uongo na dhulma, Katiba hiyo haikupigiwa kura ya maoni na wananchi.

Sitta kwa sababu ya kufanya dhambi na dhulma, ameporomoka kisiasa kwa kupuuzwa hata na CCM aliyoinufaisha kwa matendo yake. Hayo pia ni malipizo kwa dhulma na maonevu aliyomfanyia Edward Lowassa alipokuwa Waziri Mkuu na kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni. Watawala wa CCM hasa wa Zanzibar wamekuwa na tabia ya kukandamiza wananchi na kuonea wakiamini hawataondoka madarakani.

Kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar na Rais Dk. Shein kuendelea kubakia madarakani wakati muda wake kikatiba umemalizika, ni ushahidi tosha wa kiburi cha kung’ang’ania madaraka. Mgogoro hautoamulika kwa kurejewa uchaguzi ila ni kuzidisha migogoro zaidi ya hasa pale itakapotokea uchaguzi kurudiwa na CCM kutangazwa mshindi.

Sina shaka CUF hawatakubali kuutambua ushindi huo na ndipo Zanzibar itapotumbukizwa shimoni, na sasa kutarajiwa ukandamizaji viongozi wake na wafuasi wao, bali ikawa chanzo cha mauaji ya kisiasa.

Kwa kuwa wananchi wa Zanzibar ni wamoja na imejitokeza wanataka mamlaka kamili ili waweze kujiamulia mambo yao, lazima Dk. Magufuli asimame imara kuona haki ya Maaliam Seif kutangazwa mshindi na kupewa nafasi kuunda serikali inatekelezwa.

Chanzo: Mawio

Advertisements

3 Replies to “Shuwari inayoitumbukiza shimoni Z’bar”

  1. Kwa maoni na mtazamo wangu.bado Utendaji na ufuatiliaji wa Jumuiya ya Madola za nchi za magharibi inaonekana wazi kupuuza mgogoro wa uchaguzi wa Zbar. Zile taasisi tunazozifahamu zinazosimamia Haki za Kibinaadamu duniani zikiwa chini ya Umoja wa Mataifa .pamoja na ile tume ya EU Observers iliokuja huko TZ kwa shughuli maalum ya kusimamia Uchaguzi …zote hizo zinaonekana kutojali tena kuendelea kutatua mgogoro huo baada ya kuonekana Uchaguzi Utarudiwa. Napenda ifahamike kwamba Taasisi hizo kwa upande mwengine wana mvutano wa wao kwa wao kuingilia suala hilo…na zaidi pale wanapothibitishiwa kwamba uchaguzi utarudiwa. Lakini kwa upande wa siasa za Nchi za Africa..inapotokeya Uchaguzi kurudiwa na chama tawala kikawa ndicho kilichopoteza nafasi uchaguzi wa awali..ni sawa na kuipa ushindi mkubwa chama hicho kwenye uchaguzi wa marudio ..hali ambayo itasababisha chama au vyama vya upinzani kukosa majimbo mengi waliokuwa wakiyategemea.Hii ndio hali halisi za uchaguzi ndani ya nchi za Afrika. Na bila shaka kwa watawala wa Zbar tayari wameshajipanga vizuri kwa kuzielewa kasoro zao hivyo ni rahisi mno kwa upande wao kuzirekebisha hata kama Nguvu ya Dola itatumika….Ndipo ningewashauri tena Jumuiya ya Madola za Nchi za Magharibi pamoja na Taasisi za Umoja wa Mataifa wasidharau kuacha kutatua mgogoro huo au kuupuza..kwani Msemo wetu tunasema ( USIPOZIBA UFA UTAJENGA UKUTA )

  2. Kwa maoni na mtazamo wangu.bado Utendaji na ufuatiliaji wa Jumuiya ya Madola za nchi za magharibi inaonekana wazi kupuuza mgogoro wa uchaguzi wa Zbar. Zile taasisi tunazozifahamu zinazosimamia Haki za Kibinaadamu duniani zikiwa chini ya Umoja wa Mataifa .pamoja na ile tume ya EU Observers iliokuja huko TZ kwa shughuli maalum ya kusimamia Uchaguzi …zote hizo zinaonekana kutojali tena kuendelea kutatua mgogoro huo baada ya kuonekana Uchaguzi Utarudiwa. Napenda ifahamike kwamba Taasisi hizo kwa upande mwengine wana mvutano wa wao kwa wao kuingilia suala hilo…na zaidi pale wanapothibitishiwa kwamba uchaguzi utarudiwa. Lakini kwa upande wa siasa za Nchi za Africa..inapotokeya Uchaguzi kurudiwa na chama tawala kikawa ndicho kilichopoteza nafasi uchaguzi wa awali..ni sawa na kuipa ushindi mkubwa chama hicho kwenye uchaguzi wa marudio ..hali ambayo itasababisha chama au vyama vya upinzani kukosa majimbo mengi waliokuwa wakiyategemea.Hii ndio hali halisi za uchaguzi ndani ya nchi za Afrika. Na bila shaka kwa watawala wa Zbar tayari wameshajipanga vizuri kwa kuzielewa kasoro zao hivyo ni rahisi mno kwa upande wao kuzirekebisha hata kama Nguvu ya Dola itatumika….Ndipo ningewashauri tena Jumuiya ya Madola za Nchi za Magharibi pamoja na Taasisi za Umoja wa Mataifa wasidharau kuacha kutatua mgogoro huo au kuupuza..kwani Msemo wetu tunasema (( USIPOZIBA UFA UTAJENGA UKUTA ))

  3. Kulazimisha kurudiwa kwa uchaguzi huu Zanzibar,ndio kitakuwa chanzo kikubwa cha umwagaji damu Tanzania, maana hayo hayataishia Zanzibar tu. Pia inaweza kusababisha Bunge la muungano kuparaganyika kwasababu ya wabunge kutoka Zanzibar na wale wa UKAWA kwa ujumla wanaweza kujitoa kama walivyotoka katika Bunge la Marekebisha ya Katiba. Kutokana na vurugu hilo ambalo linaweza kuepukika litaipelekea Serikali ya Magufuli kufanyakazi kiTanganyika Zaidi kuliko Jamhuri ya muungano, Tukifika hapo muungano utakuwa umekwisha. Niafadhali wengelifanya busara ya kuheshimu matakwa ya wananchi nakuheshimu haki ya kumpa ushindi aloshinda.
    Kama walizoe kupora ushindi katika vipindi vilivyopita wasitegemee hata kidogo mara hii kufanya hivyo pakawa salama. PATACHIMBIKA.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s