Kazi inayopigwa Z’bar wananchi hawaijui

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad
                                         Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad

 Na Jabir Idrissa

AMIRI Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Dk. John Magufuli anampa moyo Maalim Seif Shariff Hamad, kuendelea kujadiliana na viongozi wengine wa kisiasa katika jitihada za kutatua mgogoro wa kisiasa Zanzibar.

 

Kwingineko, Jeshi la Ulinzi (JWTZ) linaondoa askari wake maeneo ya serikali iliyokuwa ikiyalinda tangu mapema Oktoba.

 

Hizi habari zinasukuma wananchi katika tafakuri jadidi hasa kwa kuwa ni kama vile zimetokea katika mpangilio ulioandaliwa kwa ustadi na maelewano kwa wahusika.

 

Siku alipokuwa akizindua Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mjini Dodoma, Dk. Magufuli aliahidi kuchukua hatua ya kutatua mgogoro wa Zanzibar kwa kushirikiana na viongozi wengine akiwemo Makamu wake, Samia Suluhu Hassan, mwanamama kutoka jimbo la Makunduchi, Wilaya ya Kusini, Unguja.

 

Lakini wakati hajaonekana hadharani kuchukua hatua tangu hapo, Jumatatu wiki hii, alishuhudiwa akiwa katika mazungumzo ya faragha na Maalim Seif, mwanasiasa wa enzi anayepigania haki yake ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa Oktoba 25, iliyowekwa katika mtihani na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kwa kutoa tangazo la uamuzi wake kuufuta uchaguzi wote wa Rais, Wawakilishi na Madiwani wa Zanzibar.

 

Jecha alitangaza uamuzi huo Oktoba 28, siku tatu baada ya Wazanzibari kupigakura, na tangu hapo, hajaonekana hadharani na haijulikani bado yuko wapi hasa. Lakini Novemba mosi, alifika ofisi kuu za Tume, Maisara, na kuwaita makamishna wa tume kwa kikao cha ghafla.

 

Uamuzi wake huo wa kufuta uchaguzi umefurahisha na kuendelea kufurahiwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), bila ya shaka kwa kuzingatia ukweli kuwa wamenufaika na uamuzi huo, tofauti na washindani wao wa kihistoria kisiasa, Chama cha Wananchi (CUF) wanaendelea kuupinga na kutaka Tume ikamilishe kazi ya kuhakiki kura za mwisho za urais na kumtangaza mshindi wa uchaguzi.

 

CUF inaamini hata Jecha hakuzuka tu na kutoa tangazo la kuufuta uchaguzi, isipokuwa aliandaliwa hata kama kwa pupa, kwa vile alitoa tangazo wakati akiwa hakutokea zilipo ofisi za kutangazia matokeo ya urais, ndani ya ukumbi wa Salama, katika Hoteli ya Bwawani.

 

 

Dalili zinaonesha wazi kuwa alichokisoma Jecha na kurekodiwa kwanza kabla ya kurushwa hewani kupitia Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), huenda hakukiandika mwenyewe, labda alipewa kusoma, baada ya kushurutishwa kuweka saini yake.

 

Jecha alijua fika hakuna kifungu katika Sheria ya Uchaguzi Na. 11 ya Zanzibar ya Mwaka 1984 kinachompa mamlaka kisheria ya kufuta uchaguzi. Hata Tume yenyewe, kisheria, haina mamlaka hayo.

 

Na ni hapo panapojengeka mazingira mazuri ya mtu kuamini kuwa waliomtweza nguvu na akili Jecha, anawajua, hata akiamshwa usiku wa manane, kwa vile labda ni wenzake katika CCM, chama ambacho alitumia kuomba kuteuliwa kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu wa 2010. Hakubahatika kuteuliwa.

 

Wala haikushangaza alipotajwa jina lake mwaka 2013 kwamba ametuliwa na Rais Dk. Ali Mohamed Shein kuwa mwenyekiti wa Tume. Sanasana ilijulikana tu kuwa aweza kutoa nafasi nzuri ya kukibeba chama chao kibakie madarakani.

 

Sasa wakati Jecha alishalikoroga, kwa kuwa hana mtu hata mmoja nje ya CCM anayemuunga mkono kwa kuufuta uchaguzi badala yake akishutumiwa kusababisha hali mbaya ya kisiasa nchini, ameshindwa kuisaidia tume kusawazisha alipopakoroga.

 

Ni yeye mwenyewe alitangaza katika uamuzi wake kuwa uchaguzi utarudiwa katika tarehe itakayopangwa baadaye, na ikathibitika iwe ndani ya siku 90, lakini mpaka sasa hakuna tarehe iliyotajwa kuwa uchaguzi utafanyika.

 

Je, huyu Jecha amejivuruga bila ya kubashiri kitakachoweza kutokezea baadaye, au ndio ile inayolazimu kueleweka kuwa kwa sababu haikuwa amri yake, utashi wake, haikuwa pia kazi yake kujua nchi itawekwa katika mkwamo wa kisiasa kwa vile hakutakuwa na uongozi halali wa serikali maana uliopo ambao unajilazimisha tu kwa mabavu, ulikoma uhalali wake Novemba 2.

 

Ni kwa vipi ukiambiwa usiamini kuwa kuufuta uchaguzi kwa staili ile ya kishetani ilikuwa ndio mbinu iliyobakia katika mfuko wa mbinu tele wa CCM ili kuzuia kupoteza madaraka kwa mara nyingine?.

 

Hebu fikiria ilikuaje muda mfupi mno kabla ya adhuhuri siku ile ya Oktoba 28, kwenye geti la Bwawani kulijazwa askari wa JWTZ na ikaonekana pia askari kanzu wengi wamehanikiza ndani ya eneo kwenye ukumbi wa Salama?

 

Ni nani aliagiza kamanda wa JWTZ aliyepo Zanzibar aruhusu askari wake kutoka kambini na kumdhibiti Jecha, na angalau komandoo wawili wa jeshi hilo, wakatumwa kumchukua – hakika ni kumteka nyara – Makamu Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Abdulhakim Ameir Issa?

 

Jaji huyu alifanyiwa mbinu ya kijasusi akatoka ofisini na kuacha makamishna aliokuwa akiwaongoza katika kazi ya kuhakiki kura za urais, wakati Jecha ilishathibitika alikuwa ametoweka makusudi kuwezesha chama chao kutimiza azma yake ya kuhujumu haki ya wananchi kuchagua kiongozi wamtakaye.

 

Basi matumizi ya jeshi ni mbinu kwa CCMa kupata watakacho kila unapofanyika uchaguzi. ilitokea miaka yote, lakini ya mwaka 2000 yalikuwa kiboko. Makundi ya wanajeshi wenye silaha walimwagwa vituoni na kuyapora masanduku ya kura yaliyokuwa katika udhibiti wa mawakala na kupotea nayo wanakokujua.

 

Haikuchukua muda, wananchi wakatangaziwa na Tume kuwa uchaguzi wa majimbo 17 ya Mkoa wa Mjini Magharibi, umefutwa. Ukisikia uchaguzi wa marudio leo, ujue ni marudio kweli; Novemba 5 ya 2000, ulifanywa na kususiwa na upinzani, na kutoa mwanya kwa CCM kujitangazia ushindi usio shida.

 

Safari hii pia, askari walijazwa maeneo nyeti ya taasisi za serikali – Radio Zanzibar, Televisheni ya Serikali Karume House, Ikulu, Bandarini Malindi, kwenye Mnara wa Kumbukumbu ya Mapinduzi, Michenzani.

 

Ni juzi tu waliondoshwa. Ni kwanini waliondoshwa wiki hii, CCM wanajua. Tatizo isije ikawa wanajua na kupanga hata kitachoweza kutokea siku chache zijazo.

 

Rais Magufuli anampa moyo Maalim Seif ili iwe nini? Na pale anapomwambia akapige kazi, hivi ni kazi ipi hiyo? Ni bahati mbaya wananchi hawajui chochote. Tena hawa waliochagua kiongozi, hawajui kitu.

 

 

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s