Siasa za kale Zanzibar hazina tija

Babu Juma Duni Haji
                                                          Babu Juma Duni Haji

Na Juma Mohamed, Zanzibar

WIKI iliyopita iliwasili meli mpya ya abiria na mizigo inayomilikiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, iliyotengenezwa katika Mji wa Busan, Jamhuri ya Korea Kusini.

Mengi yamesemwa na kuandikwa, wapo waliosifu na kupongeza uamuzi wa Serikali kununua meli hiyo mpya na ya kisasa, lakini pia kama kawaida ya binadamu wapo wanaobeza na kupotosha ukweli kuhusu meli hiyo iitwayo “Mapinduzi II”.

Wapotoshaji wanadai meli hiyo si mpya, upotoshaji huo naweza kuunasibisha na kisa cha uvumi wa popobawa na siasa za Zanzibar kwa wakati ule na wapinga maendeleo waliojificha kwenye koti la kisiasa.

Haishangazi watu hao kuchupia hoja maana maisha yao yanategemea matone ya maji baada ya dripu kutowasaidia katika kutibu maradhi ya kusadikika kama ilivyosimuliwa na gwiji wa fasihi, Sheikh Shabaan Robert katika kitabu chake cha Kusadikika.

Watu hao ni vifuu tundu, wameselelea katika siasa za ukale na upingaji wa kila jambo huku ukasuku ukiwatopea, hawaoni, hawasikii zaidi ya kuamini ‘redio kifua’ na tumbaku wakiamini na kuacha kusikiliza vyombo vyenye uhakika.

Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, Juma Duni Haji akiwa Waziri wa wizara hiyo alieza kwa kina hatua ya Serikali kuamua kununua meli mpya na hatua zilizofikiwa za utengenezaji wa meli hiyo.

Hoja ya ununuzi wa ‘meli chakavu’ hii ni hoja dhaifu mno na ya kuvunja moyo maana wasemaji wanaegemea jina la mwanzo la meli hii ikiwa katika hatua ya utengenezaji wake pamoja na majaribio, ilipopewa jina la Posco Plantec kwa ajili ya utambuzi kulingana na taratibu za IMO.

Akifafanua suala hili, Naibu Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Issa Gavu, anasema jina la Posco Plantec ni jina la kampuni iliyotengeneza meli hiyo akiwa na mshirika wake Daewoo ambapo wao ndio walioomba namba za utambuzi.

“Namba hizo haziwezi kubadilika na kuonekana kwa Posco hapo haimaanishi kama Meli hiyo ni ya kwake na sisi tumeuziwa mtumba isipokuwa utaratibu wa kawaida, mjenzi kuomba namba na mkifikia hatua za kuweka jina mtafanya hivyo kama ambavyo tumeipa jina la Mapinduzi II na hakuna ukweli wowote juu yaupotoshaji unaofanywa na watu hao wasio na nia njema.”

Naibu Waziri Gavu anasema kuna mambo mawili makubwa anayopaswa kuyafanya Mjenzi , mosi kumpatia mteja wake IMO namba na daraja la meli na gharama zote na ambapo maombi yanafanywa na mjenzi kwa gharama zake huku suala la Bima litasimamiwa na mjenzi akitumia jina la Kampuni la Posco hadi atakapokabidhi meli kwa wamiliki .

Gavu anasema usajili uliofanywa ni wa muda na ni kwa mujibu wa mkataba kwa kiuwezesha Mv. Mapinduzi II kuweza kusafiri kutoka Korea Kusini hadi Zanzibar ambapo usajili utafanyika chini ya Mamlaka ya Usalama Majini ya Zanzibar.

Anasema bado kuna hatua kadhaa kama nyaraka nane za makabidhiano ya Meli hiyo ambapo jina la Posco linajitokeza.

Hii ina maana gani? Msingi wa kutumia jina la mjenzi ni kuwa meli hiyo inakuwa bado haijakabidhiwa katika dhamana za mnunuzi yaani Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kama hadi ujenzi wake unakamilika na kusafiri kutoka Korea Kusini hadi Zanzibar kwa usajili wa Mamlaka za hapa nchini, ingetokea kuzama kwa meli hiyo SMZ isingeweza kudai fidia.

Mv. Mapinduzi II ilianza kujengwa mwaka 2013 na imekamilika katikati ya mwaka 2015 na ina uwezo wa kubeba abiria 1,200 na mizigo yenye uzito wa tani 200 ambapo mwezi Machi mwaka huu ilishuhwa kwa rasmi baharini kwa majaribio (sea trials)

MV. Mapinduzi II imetengenezwa kwa dola za Kimarekani milioni 30.6 fedha ambazo zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Ni vizuri katika makala haya tukawafahamisha wasadikika hatua ilizopitia Meli hii hadi kukamilika kwake. Hatua ya mwanzo ilikuwa ni Milestone ukataji wa chuma kwa maana ya vyuma vinataarishwa kwa ajili ya ujenzi wa meli husika na hatua hio huwa inashuhudiwa na wahusika wote wa mradi yaani mmiliki na wajenzi wote pamoja na wasimamizi wa kimataifa.

MV. Mapinduzi II ilipitia hatua zote ikiwa pamoja na ile ya kukata vyuma vya kujengea meli ziliandaliwa Mjini Ulsani Korea Kusini na baadae kuhamishiwa Busan katika chelezo cha Kampuni Mjenzi kwa hatua ya pili ya kuunganishwa katika sherehe za ulazaji wa mkuku ambao ni hatua ya pili ya ujenzi wa meli na ilihudhuriwa na wahusika wote.

Hatua hizo zote lazima msimamizi ajiridhishe kama alivyo kwa mshauri wa miradi vyenginevyo mradi haupigi hatua bila ya msimamizi kuidhinisha hatua inayofuata.

Hatua hizi zote zimefanyika nchi kavu baada ya hapo kuunganisha mkuku na makuta yaani lile jengo lenyewe ndio inashushwa baharini kama vile mtumbwi bila ya kitu chochote na hapo huwa tayari lile umbile la meli yenyewe bila ya kitu chochote ndani yake.

Hatua ya nne ni kuweka vitu vyote vinavyohusika ikiwa pamoja na mashine, generata na samani zote pamoja na mfumo wa umeme na mitambo husika ya kuendeshea Meli.

Aidha, hatua hii ndipo panapofanyika majaribio yote ya Meli husika pamoja na safari za baharini kwa kuona ueleaji wake pamoja na mambo mengine ya kiufundi kwa chombo hicho.

Hoja ya kuwa meli ni chakavu haipo katika Mapinduzi II zaidi ya upotoshaji wa makusudi baada ya kuona Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein imetekeleza ahadi yake kwa wananchi.

Hatua nyingine kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya ujenzi wa meli ni kwamba meli inayojengwa ikifikia hatua za kushushwa baharini na kuijengea utambuzi ni lazima ipewe namba kwa ajili ya kujibainisha na hivyo namba ya IMO inayoonekana ni kama vile chansesi namba ya gari ni utaratibu wa kawaida.

 

CHANZO: RAI

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s