Watadanganya tu ili kung’ang’ania madaraka

Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein akiongea na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai.
Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein akiongea na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai.

Na Enzi T. Aboud

NDANI ya uzio wa siasa za kinafiki, chuki na laghai zinazotesa viongozi wa CCM Zanzibar kila unapofanyika uchaguzi, lengo hasa ni kung’ang’ania madaraka. Wataficha ukweli kwa vyovyote wanapoona maslahi binafsi yanaingia katika mtihani. Watadanganya tu bila aibu.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, Dk. Salmin Amour, aliyegombea kupitia CCM, hakushinda, na baada ya ukimya wa siku nne, kama kawaida Tume ya Uchaguzi (ZEC) ikaibuka na kumtangaza Dk. Salmini mshindi kwa asilimia 0.04 ya kura 165,271 alozipata, sawa na asilimia 50.2.

Mpinzani wake, Maalim Seif Shariff Hamad wa Chama cha Wananchi (CUF), alipata kura 163,706 (asilimia 49.8 ya kura za urais). Kwa upande wa viti vya Baraza la Wawakilishi, CCM ilipata 26 lakini haikupata kiti kisiwani Pemba. CUF ilipata 24, viti vyote, kasoro vitatu, kutoka kisiwani Pemba.

Kwa matokeo hayo, uchaguzi uliofuata ukawa ni CCM kunyimwa viti Pemba. Mwaka 2010 matokeo ya kura za urais yalifanana kwa ushindi mdogo mno alioupata Dk. Ali Mohamed Shein, na mshindani wake, Maalim Seif, alikubali kushindwa.

Kufutwa kwa uchaguzi 2015 kuliandaliwa baada ya CCM kujua imeshapoteza madaraka kwa kukosa kura ilizozitarajia kutoka Kisiwani Pemba licha ya kuwalipa viongozi kadhaa na kuahidi wangepata kura hizo na viti kadhaa.

Ni hatua iliyochukuliwa kibahati mbaya kwa kuwa kura zote Unguja na Pemba zilishahisabiwa na matokeo yake yote kutangazwa kwa mtindo wa kuyabandika vituoni baada ya kuthibitishwa na watendaji wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC). Mawakala wote walishapewa nakala za fomu za matokeo yote na wale wa CUF kufanikiwa kukabidhi kwa wakala mkuu wa Maalim Seif na ndio maana aliona atangaze mapema mwelekeo wa kura zake. Ni mbinu iliyozuia wapinzani wao kubadilisha matokeo kama inavyojulikana kiuzoefu kutokea.

Katika majimbo ya Pemba, kama kawaida CCM haikuambulia kiti hata kimoja, ushahidi usiopingika kuwa chama hicho hakina nafasi kisiwani Pemba, ambako ni ngome isiyoshindika ya CUF tangu asili. Watawala hawapati kura.

Kulikuwa hakuna njia nyengine ya kuinusuru CCM kwa kuwa utafiti umeonesha asilimia 90 ya wananchi wote Pemba ni watiifu kwa CUF. Katika hali hiyo CCM ikasaidiwa kucheza rafu na kutumia mabavu kulazimisha ushindi. Pale iliposhindikana, makada wake wakatunga madai ya kura zao kuibwa Pemba, kugombana kwa makamishna wa Tume na kuokotwa kwa kura mitaani.

Kwa kawaida uongo na dhihaka ni zao la uvivu wa kufikiri, na mara zote huzalisha migogoro na kwa watawala hutumia ubabe/mabavu kuhalalisha kile ambacho kwa asili yake ni cha uongo. Wakubwa wa CCM Zanzibar walipoona wameshindwa kihalali, wakaagiza uchaguzi ufutwe kinyemela na kitoto.

Mkaidi hafaidi mpaka siku ya Idi. Wakafanya jambo la ziada lililofedhehesha taaluma ya sheria, wakajivika utaalamu wa Katiba na Sheria kwa kutafsiri Katiba ya Zanzibar kimaslahi yao; pasina kuhofia wataalamu halisi ambao wamepinga kilichotendwa.

Hata wakati fulani aliyekuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa kuwa ni msomi wa sheria, alibainisha ukweli wa tafsiri ya Katiba na Sheria aliposema Zanzibar si nchi bali sehemu ya Jamhuri ya Muungano Tanzania. Kwa unafiki tu, viongozi wa Zanzibar, wakamshupalia na kumshutumu kuwa ameidhalilisha Zanzibar.

Viongozi wengine wakiwemo wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wakadiriki kusema “Pinda atuache tupumue.” Mwenyewe alijitenga nao kwa kutowajibu kitu, mpaka amestaafu uongozi.

Lakini kwa kuwa tamko hilo lilikuwa sahihi, ukimya wake ulikuwa kama laana na kuwaachia mzuka wa uwongo wenyewe viongozi wa Zanzibar, ambao unaendelea kuwatesa ikiambatana na matatizo ya kisiasa na hatimaye mgogoro mpya wa kisiasa waliousababisha kwa chuki tu, jeuri na ubinafsi.

Msimamo wao ni tofauti kwa mbali na CUF, baadhi ya viongozi wastaafu Zanzibar na hata waangalizi wa uchaguzi kutoka nchi za nje na Jumuiya za Kimataifa ambao wote sasa wanahimiza mgogoro upate ufumbuzi haraka na kisheria ili kuipa nafasi Zanzibar kuwa na uongozi uliochaguliwa na wananchi na unaofuata Katiba na Sheria, demokrasia na haki za binaadamu.

Ukweli Zanzibar imepoteza mamlaka yake na kwa hivyo haina hadhi kimataifa; si dola kama alivyoeleza Pinda wakati ule bungeni. Kwa kulijua hilo, ndio maana CUF na Maalim Seif wanapigania mamlaka yake kamili kurudishwa na kubakisha masuala machache ya ushirikiano na Tanganyika.

Ukaidi wa viongozi wa CCM kuyaeleza haya vizuri kwa wananchi wa Zanzibar hausaidii zaidi ya kuzidisha unyonge kwa nchi yao. Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano na haiwezi kujiunga na jumuiya yoyote ya kimataifa hata Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Hilo ni eneo moja tu, yapo maeneo mengi muhimu kwa uhuru wa nchi kujiendesha yenyewe: kuteua mabalozi wake nchi za nje ikiwemo katika wa kudumu katika Umoja wa Mataifa, na kujenga uhusiano wa kimataifa kwa lengo la kusimamia maslahi ya Zanzibar kama nchi nyengine wanachama zilizo huru.

Wazanzibari wana haki ya kujua hilo, na si sababu ya kuvunja muungano na Tanganyika; kazi inayofanywa kinagaubaga na CUF na vyama inavyoshirikiana navyo chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA). Wanachokifanya ni kuipa changamoto Serikali ya Muungano kutekeleza wajibu wake wa kisiasa na kiuchumi kuisaidia Zanzibar, sehemu ya Jamhuri ya Muungano, isonge mbele kimaendeleo.

Kusema ukweli huo kwa lengo la kuelimisha Wazanzibari kujitambua walivyo ndani ya Muungano, hakuwezi kuhusishwa kwa vyovyote vile na Uhizbu (ZNP) au Uafro (ASP). Ni haki ya msingi ya wananchi kujua mambo yanayohusu nchi yao, ili kudumisha umoja wa kisiasa zaidi kwa maelewano ya hiyari.

Kwa muktadha huo, vyama vya UKAWA wanaendeleza uelewa kwa wafuasi wao na wananchi kuthamini Katiba na kuheshimu ukomo wa Serikali wakati inapomaliza madaraka yake, kumbe kwa wenzao CCM wa Zanzibar, wanapinga kwa kujipa mamlaka ya kutawala kwa namna hata ya kudanganya dunia na kuikanyaga Katiba, ikiwemo kudharau maamuzi ya kidemokrasia ya wananchi katika uchaguzi.

Inakuaje Baraza la Wawakilishi halipo na hakuna wajumbe waliochaguliwa na wananchi kutokana na kufutwa uchaguzi, lakini Pandu Ameir Kificho aendelee kubaki Spika na kulipwa mshahara, posho na marupurupu?

Mawaziri wa CCM waendelee kufanya kazi lakini wale wa CUF wasiende kazini kwa kushikilia wanahofia kuikiuka Katiba ya Zanzibar kwa kuwa hawakuthibitishwa kuwa ni wawakilishi.

Nani hasa atawadhibiti watu wanaokwapua fedha za Serikali kulipana mishahara kwa kazi zisizonufaisha wananchi?

Hatima ya mgogoro inamsubiri Dk. Magufuli ategue kitendawili cha mvutano wa kimaslahi ambapo CCM inashikilia uchaguzi mpya huku CUF wakisema mshindi halali atangazwe ili yaishe kwa salama usalmini.

Ndio kitendawili hasa kwa Dk. Magufuli aliyeahidi kusimamia kutatua mgogoro kwa mazungumzo. Ataongozaje Serikali ya Jamhuri bila Zanzibar kuwepo Serikali iliyochaguliwa kihalali na wananchi?

Chanzo: MwanaHALISI

 

One Reply to “Watadanganya tu ili kung’ang’ania madaraka”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s