Nchi shwari, ndani ya hofu kuu

img-20150630-wa0009

Na Jabir Idrissa

KWA dakika kumi hivi, wakati naandika uyasomayo, nilikuwa naongea kwa simu na msomaji wangu, pamoja na wa safu ya Kalamu inayotoka kwenye gazeti la MwanaHALISI kila Jumatatu, aliyejitambulisha yuko mkoani Mtwara.

Maongezi yake yaligusia kutaka kujua ni kwanini hasa wanaosoma gazeti hili pamoja na MwanaHALISI ambayo yanaandaliwa na timu moja, “wanafuatwafuatwa” kwa kupigiwa simu na watu wasiojitambulisha kwa uwazi.

Anasumbuliwa kwa kupigiwa simu za vitisho tangu alipompigia simu mtu mmoja ambaye alitajwa katika moja ya habari zilizochapishwa na moja ya haya magazeti, kumuuliza sababu ya kukataa kueleza jambo aliloulizwa na mwandishi, ilhali lilikuwa ni suala la maslahi kwa umma.

Ni suala muhimu ambalo linahitaji mjadala mpana katika siku mahsusi na kwa wakati wake muafaka. Nitafanya hivyo katika nafasi nyingine ndani ya gazeti hili.

Suala la pili alolizungumzia ni kuniuliza kama ni kweli Zanzibar ni shwari; kama alivyosoma baadhi ya magazeti ya kila siku katika wiki iliyokwisha?

Akawa na nyongeza kuwa wakati anafurahi anavyonufaika anaponisoma kuhusu masuala ya Zanzibar hasa uchaguzi ulivyokwenda na mkwamo wake, ni lini ukimya uliopo utafikia kikomo.

Hili swali la pili nilitaka kulieleza kwa upana safari hii. Ninapokea simu nyingi kila siku za kutaka nieleze nini kinaendelea; mbona kimya kimezidi; hii hali tete itakwisha lini; mazungumzo ya viongozi wakubwa yanayofanyika Ikulu yatakwisha lini? Nini kinazungumzwa? Na mbona umma hauelezwi kinachoendelea?

Kadhalika, hivi katika hali hiyo, shughuli za kiuchumi za wananchi na serikali zinaendeleaje; na je kuna amani ya kweli au iliyowekwa kitanzini kutokana na matukio yanayoendelea?

Haya ni maswali muhimu na ya msingi kwelikweli. Watu wengine wanaonipigia, wapo nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wengi wao ni wazalia wa Zanzibar ambao wamelewea nchi mbalimbali za ughaibuni barani Ulaya, Marekani na Asia, wakitafuta uchumi huko.

Nitaeleza eneo moja tu la kama amani iliyopo Zanzibar ni ya kweli au iliyowekwa kitanzini.

Ulisoma taarifa za kituo cha redio cha Hits FM kuvamiwa na kuchomwa moto, na studio zake ambazo kabla tu zilipatiwa zana mpya za kiasi cha Sh. 70 milioni, kuteketezwa. Ni uvamizi dhidi ya haki ya watu kupata habari, na vilevile ukandamizaji uhuru wa vyombo vya habari.

Kwa hivyo, wakati mgogoro wa kisiasa unaohusu kuhujumiwa kihuni kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 haujafikiwa muafaka, vyombo vya habari vinalengwa na wanasiasa walioitia nchi kwenye fadhaa.

Niweke wazi haraka, ni wanasiasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao (i) ndio walioshindikiza uchaguzi wote ufutwe, na (ii) ndio wanufaikaji wakuu wa hilo kwa kudhani ingewasaidia kunusurika kuachia madaraka.

Zanzibar ipo chini ya serikali ambayo uhalali wake kisheria unatiliwa shaka na wanasheria wa ndani na nje kutokana na vifungu vya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Wanasema Ibara 28 Kifungu (2) imemvua uhalali Dk. Ali Mohamed Shein, wa kuendelea kuongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Lakini, kiongozi huyo aliyetangazwa mshindi na hatimaye kuapishwa kuwa rais tarehe 2 ya Novemba 2010 baada ya uchaguzi mkuu, anaendelea kushika hatamu za wadhifa huo, na anafanya hili na lile ingawa kwa mazingira yanayosikitisha sana.

Si katika mazingira ya kawaida kwa anavyoonekana hadharani; hata mara chache kwa wiki anavyofika ofisini Ikulu anaonekana amekosa uchangamfu, anajitokeza kama mtu aliyedhoofika kihali – na pengine ni hali inayotokana na kufikiria mazonge aliyoyazembea kuyazuia, na ikiwa ni vigumu kuyaondosha haraka.

Anajua hajashinda uchaguzi maana aliridhia mapema, lakini ikatokea kuidharau dhamana na kujenga moyo mgumu wa kutojali lolote, akashindwa kutekeleza hatua muhimu aliyopaswa aitekeleze alipojulishwa matokeo usiku uleule wa uchaguzi mkuu, lakini amekuwa akistahamili yanayotendwa au kuagizwa kutendwa na wasaidizi wake kichama Zanzibar.

Hatua aliyokosa kuifanya ni aliyoelezwa na Goodluck Jonathan, alipoamua kumpigia simu na kumpongeza haraka Muhammadu Buhari, aliyeshinda uchaguzi wa rais nchini Nigeria uliofanyika Machi mwaka huu; na akawa amezima mbinu chafu za wanasiasa wahafidhina waliotaka asiridhie kushindwa bali ang’ang’anie madaraka.

Jonathan ambaye aliongoza kundi la waangalizi wa uchaguzi wa Jumuiya ya Madola, amefanya kazi kubwa ya kuelimisha wanasiasa nchini kujifunza kukubali kuachia ngazi iwapo wameshindwa uchaguzi hata wanapokuwa madarakani. Yeye aliridhia na anaishi kwa furaha na heshma. Anashawishi Waafrika wengine wamuige.

Zanzibar kweli shwari, lakini ni kwa vile tu hakuna mapigano. Watu hawapigani, si raia wenyewe, wala wao na askari. Hakuna mapigano.

Kilichopo ni hofu kuu, na wala si wale tu wanaoamini kuwa kiongozi waliyemchagua kwa raha zao, anahujumiwa kwa hila za CCM, bali hata kwa wana-CCM walioaminishwa na viongozi wao kuwa kura zao ziliibwa. Ni hofu tupu.

Hata wao hawana amani kamili. Wangekuwa nayo, wasingekuwa wanalizana leo kila wanapokabiliwa na viongozi wao na kunasihiwa wastahamili matangazo – ambayo wanaambiwa waziwazi si uchaguzi kurudiwa – yatakapotolewa siku chache zijazo.

Uthibitisho wa kuwepo hofu kuu kwa wananchi unaonekana kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo iliyoanzishwa mara tu uchaguzi ulipofutwa kihuni na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, mchana wa 28 Oktoba.

Washiriki wanaulizana, wanajibizana, wanadhihakiana, wanakasirikiana huku wakishutumiana; mwishoni kwa maneno ya kuoneana huruma unaona wanafarijiana, wanaelekezana na kuombana radhi kwa kuhisi baadhi yao walipitiliza mpaka wa mipasho au dhihaka.

Kwa sababu hiyo, Wazanzibari wamejenga msamiati kwa kusemezana, “hebu nipe dripu nipate kulala vizuri. Ona namna wananchi walivyogeuka wagonjwa wa muda kutokana na kutoijua hatima ya tafrani iliyopo?

Maswali ya msingi kila siku ni lini Maalim Seif Shariff Hamad atatangazwa na kuapishwa kuwa Rais wa Zanzibar? Niweke vizuri suti yangu au niivae maana kama kawaida yetu tushadhulumiwa?

CCM nako hakuna utulivu; wanaulizana lini uchaguzi utarudiwa (hawajaisikia tarehe kutangazwa), Dk. Shein ndo anaendelea kiunyonge hivi mpaka lini, au kama walivyopata kusema Muembekisonge, “Basi wamalize tu kwa kumtangaza Maalim, tumeyataka wenyewe.”

Wakati kuna kupeana dripu “wagonjwa” vijana waliofundishwa uharamia (Mazombi) wakiwa chini ya ulinzi wa askari wa vikosi vya SMZ, wanaingia mitaani mchana na usiku wakijeruhi wananchi hasa maeneo maarufu kukaliwa na wanaoonekana ni wapinzani wa CCM.

Mazombi waliivamia barza maarufu ya Commonwealth kando ya mzunguko wa Michenzani, wakavunja viti vya chuma, wakang’oa mlingoti wa bendera ya CUF na miti iliyopandwa kwa ruhusa ya Baraza la Manispaa, wakavunja kabati mlimohifadhiwa televisheni, king’amuzi na vifaa vingine na kuviiba; na kutoweka na kibanda cha kuuzia vocha mkiwa na fedha nyingi.

Ni maharamia wapatao 50, wala hakuna aliyekamatwa ingawa operesheni ilichukua karibu saa nzima kukamilishwa. Makao makuu ya Polisi mkoa wa Mjini Magharibi, yapo mita 200 hivi kutoka hapo.

Chanzo: MwanaHalisi

One Reply to “Nchi shwari, ndani ya hofu kuu”

  1. Vipi Salma / jabir kuna taatifa gani Benn haidar ametushituwa nyoyo zetu kwa taarifa yake kwenye facebook saa hii tusaidieni taarifa sahihi.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s