Walozoea dhulma waache yaishe

Vigogo-Zenji-620x308

SAUTI na Jabir Idrissa

WAZANZIBARI wamesubiri vya kutosha kupata majibu ya haki yao iliyodhibitiwa na viongozi wahafidhina. Wamesubiri huku wakionesha kiwango kikubwa cha uvumilivu na imani.

Wanamuamini kiongozi ambaye amekuwa ndio alama ya upiganiaji haki yao maisha yote tangu mfumo wa vyama vingi uliporudishwa mwaka 1992. Wanajua kwa kuwa yule wanayetaka aongoze Zanzibar, amesihi watulie, hakika wametulia.

Watu hawa wanaweza kuwa ni wajinga na malofa; lakini si wapumbavu. Tofauti na walio wapumbavu wanaoshupaa, wao wametulia huku wakisikiliza kinachoendelea. Hawajatekwa akili kama wapumbavu.

Wazanzibari ni watu watulivu na wenye fikra kubwa katika kuyaendea mambo yanayohusu maslahi yao, maslahi ya nchi yao. Wanaamini kwa hakika, na wanajua kuwa waliyempa imani hajawaacha, hajawapuuza. Wako naye na yeye hajabadilisha imani yake kwao; yuko nao kama vile alivyoahidi huko nyuma na tangu hapo.

Wamefanya uamuzi ambao bado wanaamini ni uamuzi sahihi na haki yao kuufanya kwa sababu ndivyo ilivyo katika kutekeleza maamuru ya Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984.

Katiba imewaridhia wachague kiongozi wamtakaye kwa kuwa nchi yao inatakiwa kuongozwa na mtu aliyepewa ridhaa nao kupitia uchaguzi mkuu unaosimamiwa na chombo kinachoundwa kwa mujibu wa mamlaka ya katiba hiyo.

Kwa hivyo, kwa vile katiba inawapa haki ya kuchagua, wananchi wanaokaribia 400,000 wameamua na wakachagua. Hakuna anayebisha Wazanzibari walichagua wanayemtaka aongoze Zanzibar. Ilikuwa tarehe 25 Oktoba.

Kila mtu aliyekuwepo aliona wananchi wamechagua kwa amani, licha ya kuwepo vitisho vya hapa na pale. Ni kweli hakuna uchaguzi Afrika unaokosa dosari, lakini si tumeamua kuziita “dosari za hapa na pale” au “ndogondogo?”

Lakini ndio ukweli kwamba uchaguzi wa Zanzibar, kwa safari hii umesimamiwa vizuri zaidi ya ilivyopata kuwa tangu 1995. Watu walitoka majumbani, wakafika vituoni, wakajipanga foleni, wakaingia vyumbani, wakapiga kura zao baada ya kupewa karatasi za kura walipothibitishwa ni wapigakura halali.

Watendaji vituoni, wakiwemo mawakala wa vyama na wagombea, walishiriki na kushuhudia kura zikihesabiwa, zikijumlishwa na hatimaye matokeo yake kuanza kutangazwa. Matokeo ya wawakilishi na madiwani yalitangazwa yote vituoni. Na ya urais yalibandikwa vituoni kama sheria inavyoelekeza.

Ah Afrika bado i Afrika tu. Haishi mazonge katika kuishuhudisha haki ya wananchi. Baadhi ya wanasiasa wenye dhamana ya kuongoza serikali, hawaipi nafasi haki kwa uzito uleule wa dhamana waliyopewa na wananchi kupitia uchaguzi. Wanajiachia na kuamini katika dhulma.

Akatokea kidudumtu na kuamua kuvuruga utaratibu, akisahau kuwa yeye mwenyewe alishatangaza matokeo ya kura za urais za majimbo 41. Alichukua hatua ya peke yake na kufuta uchaguzi wote.

Labda hakujua mapema athari za alichojiingiza kukifanya. Bali asijue kwa vipi mtu mzima na mwenye akili timamu? Alijua ila alidharau akidhani yatakwisha na kupita tu kama ilivyozoeleka.

Tuseme Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha alirukwa akili kweli? Mmh, siamini kama ilikuwa hivyo. Alijiachia na kujitakia.

Hatua yake ilikuwa matokeo ya alichokifikiria siku zote baada ya kuteuliwa. Ndivyo hivyo alivyodhamiria – kuihujumu haki ya wananchi. Sikitiko ni kuwa aliangalia zaidi maslahi yake na siasa zake; badala ya kuzingatia maslahi ya wananchi na nchi yao Zanzibar.

Inawezekana hakujua angesababisha mashaka hata kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alijua yatakwisha na kupita mfano wa ngoma ya kitoto, haikeshi. Hasara yake, ile ngoma ni ya watu wazima, sio watoto.

Kosa moja limezaa makosa yasopungua 11 na madhara yake yanaendelea. Zinasikika sauti za waliomo na wasiokuwemo. Wenyeji ndani ya nchi, nje ya nchi (diaspora), na wageni walioko ndani na wenzao wa huko kwao. Maswali na hoja. Majibu magumu.

Mimi naamini mjumuiko huu ndio uliosaidia kutuliza jazba za wananchi wanaoamini kuwa haki yao inalindwa na wanasubiri idhihirishwe kusimama. Kila kitu kiko hadharani safari hii, hakuna kilichojificha. Zile nguvu za kupotosha ukweli, zimeshindwa. Siku ya kweli imefika.

Baada ya kucheleweshwa kwa zaidi ya mwezi mmoja, haki ya wananchi inakaribia kutoka na kushuhudiwa inalalia upande inakopaswa ilalie. Haiwezekani wasio haki kupewa. Inayowastahili ndio wa kupewa. Hainyimiki, hainyimwi daima, hucheleweshwa tu. Walioichuma wapo, wapewe yaishe.

Zanzibar inahaki ya kutulia na maisha ya watu wake yapewe nafasi ya kuendelea kama kawaida ya siku zote. Yanakuwepo maisha baada ya uchaguzi. Wagumu baada ya kuridhika wameshindwa uchaguzi, ni muhimu waachie haki waliyoizuia.

Shughuli za kiuchumi ziendelee na kiongozi aliyepewa ridhaa apewe nafasi ya kuonesha aliyodhamiria kuyatenda kwa wananchi na nchi yao. Wananchi wanajua waliozuia haki kuwa mahali pake wanajisikia vibaya kwa kuizuia, lakini kule kuridhia kwao tu kuwa haiwastahili wao, ni funzo tosha.

Ukweli, dunia ya leo popote pale, hata penye udhalimu uliopitiliza mpaka, haki inazingatiwa tu inapolazimu baada ya kucheleweshwa. Waliozoea kuzuia haki kusawiri, hujikuta hawana uchaguzi ili kuridhia. Kuendelea kuweka zuio, haiwezekani tena. Ni kuzikufuru neema za manani.

Makosa amehulukiwa binaadamu si ng’ombe au punda. Akishatambua alipokosea hata kama kifitna tu na kichuki, anajirudi kwa kuukubali ukweli. Wajue subira huvimba na anayesubiri akapasuka; si vizuri ikafikia hapo.

Nimekuwa nikipita mitaa na vitongoji kupima upepo, mote ninatoshwa kuwa waliozoea kuishi kwa kudhulumiwa ni watu wastaarabu; hawana kinyongo, watawasamehe wadhulumati, ingawa hawatasahau yaliyotokea.

Basi na wao waliozuia haki kwa mikwara, mizaha, ulaghai, vitisho na mabavu huku wakitumia vyombo vya dola kujenga hofu nyoyoni mwa umma, kibri hicho; wasahau yote yale, waungame kabla ya kuungamishwa.

Ghadhabu za Mwenyeezi Mungu aliyeumba mbingu na ardhi na vyote vilivyomo ndani yake, kwa wale wasioungama, zinazaa dhoruba nzito. Yarabbi wape wepesi walio wazito kuridhia yasiyowapendeza, bali yale ambayo ndiyo ya haki kwa waja wako wema.

Chanzo: Mwanahalisi

Advertisements

3 Replies to “Walozoea dhulma waache yaishe”

  1. Daima nikisoma makala zinazohusu Uchaguzi wa Zbar wa mwaka 2015 ..Wengi humtaja Bwana Jecha..na kila malalamiko ya kufutwa kwa hayo matokeo bado anatupiwa Lawama hizo Mzee wetu Jecha…lakini tumeshswahi kumfuata yeye mwenyewe Bwana Jecha kumuuliza juu ya scandal hiyo?Je tumeshafanya utafiti wa ndani wa kujua nani alieweza kumpa amri ile Bwana Jecha ya kufuta matokeo ?..Mm naona Mzee Jecha pamoja na dhamana na wadhifa aliopewa kuhusiana na uendeshaji wa Uchaguzi …bado yeye anabaki ni mamluki tu . Asiekuwa na ubavu wa kufuta na wala kutangaza .isipokuwa Mzee huyo itakuwa ameamrishwa na akashurutishwa kufanya alichofanya pengine hata na yeye asingependelea iwe hivyo.Ni bora kuelekeza lawama zetu kwa wale waliojuu yake …na inasemekana ni Mmoja asietokana na wao.

    1. Kwanini iwe kila leo ni “… Jecha Wee !! Jecha Wee !! “. Hivi kweli kichonga baa ni yeye tu ?. Kwanini watu wanalifumbia macho na midomo kosa sugu lilofanywa na Seif Sharif ,kufanya kiburi cha kujitangazia Ushindi kabla uhakiki ukatangzwa na waliohusika kama utaratibu wa sheria uchaguzi unavyosisitiza ?.Ni Ubgauzi Na Unafiki Kumuandama Jecha ,pekee au kulirahisisha kosa la Seif Sharif.

      1. Jecha alifanya kosa kubwa kuliko yote unayoyajua wewe. Haijatokea uchaguzi uliokwishafanyika na matokeo kuanza kutangazwa ukafutwa, kwa ufahamu wangu sijaona wala kusikia dunia nzima. Najuwa uchaguzi waweza kuahirishwa tena wakati unaendelea, na wala haujafikia hatua ya kutangaza matokeo. Kwa hiyo alilofanya mzee Jecha ni kosa kubwa sana, halina mfano. Labda nitakubaliana na mchangiaji alietangulia hapo juu kuwa mzee Jecha alifanya maamuzi yale pekee? tena bila kushurutishwa? hilo linatia shaka. Kwa maana hiyo kama wapo waliomshurutisha kufanya maamuzi yale wao wanastahili lawama zaidi kuliko yeye, lakini hilo halimtowi na yeye lawamani.

        Kosa la maalim Seif kujitangaza kama mshindi, ndiyo lilikuwa kosa lakini haliwezi kuwa ndiyo sababu ya kuhalalisha uamuzi uliofanywa na mzee Jecha. Lile ni kosa na adhabu yake inajulikana, aliyekuwa na mamlaka ya kumuadhibu angemuadhibu kwa mujibu wa sheria. Hakuna mahali sheria yoyote ya Zanzibar inasema kuwa mgombea akijitangaza kabla tume kumtangaza basi uchaguzi husika utafutwa, hakuna. Hata hivyo angalia mazingira baada ya Maalim Seif kujitangaza bado watu walikuwa na amani na shughuli za kutangaza matokeo zinaendelea sawia. Baada ya mzee Jecha kutangaza kufuta matokeo hapo hapo hali ikabadilika na mtafaruku ukaanza, kwa hiyo kosa la mzee Jecha huwezi kulifanananisha na lile la Maalim Seif, la mzee Jecha ni kubwa mno na ndiyo limewafikisha wazanzibari katika mkwamo unaoendelea mpaka sasa.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s