Waandishi wa habari waonywa

DSC_2196

Khelef Nassor

 Waandishi wa habari visiwani Zanzibar wametakiwa kutumia taaluma yao katika kuandika habari kwa weledi mkubwa ili kulinda amani iliyomo visiwani humo hususan katika kipindi hichi cha mkwamo wa kisiasa uliotokana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kufuta matokeo ya uchaguzi kwa madai kuwepo kwa kasoro nyingi kwenye uchaguzi huo.

 

Wito huo umetolewa hapo jana mjini Zanzibar katika semina iliyoandaliwa na ofisi ya Mufti ambayo iliyowakutanisha waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali nchini kwa lengo la kujadili nafasi ya vyombo vya habari katika kukuza na kuendeleza amani ndani ya visiwa vya Zanzibar.

Akizungumza katika semina hiyo, Naibu mufti wa Zanzibar, Mahmoud Mussa Wadi aliwataka waandishi wote waliohudhuria semina hiyo kutorusha au kuchapisha taarifa yoyote ambayo inaonekana kutokuwa na ishara ya kuleta amani nchini.

“Ni vizuri nyinyi waandishi kuitathmini habari kwanza kabla ya kuifikisha kwa wananchi, na jambo ambalo mutakuwa munamashaka nalo basi ni vizuri kuliwacha” Alishauri.

Kwa upande wake Katibu wa Mufti Sheikh Fadhil Suleiman Soraga amesema waandishi wa habari wanamchango mkubwa katika kutunza amani ya nchi hivyo wanapaswa kutumia taaluma yao katika kufanikisha wajibu huo.

“Nyinyi waandishi wa habari munaweza kuitunza amani ya nchi yetu, hivyo wajibu wenu ni kutoa taarifa za kweli na ambazo hazitawagawa wananchi” Alisema.

Aidha amewataka waandishi hao kuzifanyia uchunguzi habari zao kabla ya kuziwasilisha kwa wananchi kwani kutofanya hivyo kunaweza kusababisha machafuko na mifarakano katika nchi hali ambayo itaifanya amani ya nchi kusambaratika.

Akitolea mfano wa vyombo vya habari nchini Rwanda katika kipindi cha mauaji ya Kimbari, Soraga amesema mauaji hayo kwa kiasi kikubwa yalichangiwa na vyombo vya habari kutokana na kuhubiri chuki kati ya makabila mawili maarufu ya Wahutu na Watusi hatua ambayo ilipelekea kuwagawa wanachi hao hadi kufikia hatua ya kuuana kinyama.

“ Tunatakiwa tujitahidi sana, vyombo vyetu vya habari visiwe ni sehemu ya kuigawa jamii na badala yake viripoti habari za vyama na makundi ya aina yote bila ya upendeleo” Aliongeza.

Hata hivyo aliongeza kwa kusema kwamba vipindi vingi vya redio vinavyorushwa hewani, kwa kiasi kikubwa huwa vinachochea uvunjifu wa amani kwani vipindi hivyo hutoa fursa kwa wasikilizaji kutoa maoni yao kupitia ujumbe wa simu ya mkononi ambapo amesema sehemu kubwa ya ujumbe huo unaotumwa huwa na ishara ya uchochezi na uvunjifu wa amani.

Semina hiyo ya Waandishi wa habari iliyofanywa na Ofisi ya Mufti mkuu wa Zanzibar, ni muendelezo wa jitihada mbali mbali zinazofanywa na ofisi hiyo katika suala zima la kutunza na kuendeleza amani ya nchi ya Zanzibar ambapo kabla ya semina hiyo, Ofisi ya Mufti Mkuu ilishafanya mazungumzo mbali mbali na baadhi ya viongozi wa kisiasa akiwemo Makamo wa Kwanza wa Rais, Maalim seif Sharif Hamad na Makamo wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi na Marais Wastaafu wa Zanzibar.

 

 

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s