‘Spirit’ ya Maridhiano ndio inayoongoza kikao cha Ikulu

IMG_1119

Salma Said

Viongozi wa kisiasa wanaokutana kwa ajili ya mazungumzo ya kuutatua mkwamo wa kisiasa Zanzibar wamekutana tena jana kwa mara ya sita Ikulu Mjini Zanzibar. Mazungumzo hayo yanawajumuisha wagombea urais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein na Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na marais wastaafu akiwemo Mzee Ali Hassan Mwinyi, Dk Salmin Amour Juma, Dk Amani Abeid Karume na Balozi Seif Ali Iddi.

Mazungumzo hayo ambayo yalianza Novemba 9 mwaka huu yamekuja kufuatia mgogoro wa kisiasa ambao umetokana na uchaguzi mkuu uliofanyika Octoba 25 mwaka huu kugubikwa na giza nene kutokanana na kufutwa kwa uchaguzi mkuu siku tatu baada ya wananchi kupiga kura zao na baadhi ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salum Jecha mnamo Octoba 28 alitangaza kuufuta uchaguzi mkuu wote wa Zanzibar kwa madai ya kuwepo kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi huo jambo mbalo limepingwa vikali na viongozi wa Chama Cha Wananchi (CUF) pamoja na  waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje ya nchi ambao walitoa tathmini zao za kufanyika uchaguzi huru, uwazi na haki.

Hata wanasheria kupitia Jumuiya ya Wanasheria ya Zanzibar (ZLS) walipinga hatua ya Mwenyekiti wa tume wakisema hana mamlaka ya kisheria ya kufuta uchaguzi kwa mujibu wa sharia No 11 ya Uchaguzi ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Hadi sasa hakuna kiongozi yeyote anayeshiriki mazungumzo hayo ambaye yupo tayari kuzungumzia nini khsa wanachojadiliana na mpaka lini watatoa taarifa kwa umma.

Lakini taarifa ndani ya kikao hicho zinasema kwamba kikao hicho tokea kuanza kwake licha ya changamoto za hapa na pale mazungumzo yanakwenda vizuri huku kila mmoja akiweka maslahi ya taifa mbele badala ya kuweka mbele mtazamo wa chama chake.

Viongozi wote wanaokutana ni kutoka Chama Cha Mapinduzi isipokuwa Maalim Seif ambaye ndiye kutoka chama cha upinzani cha CUF lakini licha ya kuwepo peke yake amekuwa akielewana vyema na wenzake kwa kuweka maslahi ya taifa mbele huku ‘spirit’ ya mazungumzo ikiwa imewekwa mbele kwa kuwa Dk Amani Karume naye ni mshirika wa karibu wa Maalim Seif na ndiye aliyeongoza mazungumzo ya kutafuta Mwafaka wa Zanzibar katika kipindi kilichopita cha uongozi wake. Mazungumzo yao yalihitimishwa kwa Maridhiano yalioidhinishwa rasmi na wananchi kupitia kura ya maoni kabla ya uchaguzi wa 2010.

Kikao hicho ambacho tokea kilipoanza Novemba kimeendelea na mazungumzo vizuri na ilipofika Novemba 17 Dk Shein aliondoka na kwenda kumuunga mkono Rais wa Tanzania Dk John Magufuli katika kuzindua Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo lilizinduliwa Novemba 20 uzinduzi ambao umefuatiwa na kuzomewa kwa Dk Shein na wapinzani wakisema sio Rais halali wa Zanzibar kwa kuwa muda wa kuwepo madarakani imemalizika.

Wiki moja baadae viongozi hao walikutana tena na kurejea pale walipoishia na kila upande kuwasilisha kile walichokubaliana katika kikao kilichopita ambapo walipeana kazi za kufanya na kuziwasilisha katika kikao kilichofuata ambapo baadhi ya maamuzi yamefikiwa pasi na kipingamizi chochote..

Kwa upande wa vyama vya siasa ambavyo viongozi wao wanashiriki mazungumzo hayo kutoka CCM na CUF nao hawakuwa tayari kuzungumza juu ya kinachoendelea huko Ikulu kwa madai kwamba mazungumzo hayo ni ya viongozi wa juu na hayajashushwa katika ngazi ya chama.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alipohojiwa na Mwananchi jana alisema chama CCM kimetoa baraza juu ya mazungumzo yanayoendelea huko Ikulu lakini kinachojadiliwa ndani ya kikao hicho wao kama chama hawajui.

“Sisi kama chama tumeyabariki mazungumzo yanayoendelea ya viongozi baina ya pande zote mbili kwani tunaamini yatakuja na muelekeo mzuri wa mustakabali mwema wa nchi yetu” alisema Vuai kwa njia ya simu.

Vuai alisema mazungumzo ya Dk Shein na viongozi wenzake  hayajafikishwa katika uongozi wa CCM na hivyo hana cha kuongea zaidi kwa kuwa bado mazungumzo hayo ni siri lakini wanampongeza Dk Shein kwa ujasiri wake wa kuendesha nchi katika utulivu na amani.

Vuai alisema licha ya mazungumzo lakini taratibu za uchaguzi kufanyika tena Zanzibar ipo pale pale na wanasubiri tume ya uchaguzi itangaze tarehe ili waweze kushiriki uchaguzi huo kikamilifu.

“Taarifa nilonazo uchaguzi upo na hatujapokea mabadiliko yoyote kwa hivyo sisi kama chama tunasubiri Tume itangaze siku ya uchaguzi na tunasubiri kama wanavyosubiri vyama vyengine watangaziwe” alisema Vuai Ali Vuai.

Kikao cha leo kinatarajiwa na wengi kuwa ndio kitakuwa cha mwisho na baadae kusubiri maamuzi yatakayoamua mustakabali mzima wa nchi ikiwemo kupata hatma ya uchaguzi ambao chama cha CUF kinashikilia kuwa kina ushindi mkononi.

Kwa upande Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF,  Ismail Jussa Ladhu alisema wanazo taarifa za kuendelea mazungumzo hayo lakini jambo la msingi ni kwamba umefika wakati mazungumzo hayo yakamilishwe na matokeo yake yaelezwe kwa wananchi.

“Mazungumzo haya yanahusisha viongozi wetu na makubaliano yao ni kwamba kama ni taarifa basi watatoa wenyewe kwa pamoja. Kwa hivyo, mimi siwezi kuzungumzia chochote kwa sasa”. Alisema Jussa.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s