Balozi Amina ni yuleyule wa 2005

bb93435ae94cab2a53bdceee1231a583NIMEMSIKILIZA Amina Salum Ali ambaye siku hizi anahadhi ya kibalozi, akijitokeza kama mwanasiasa mwerevu, jasiri na anayefaa kuitwa Mama ushauri. Ameshiriki kipindi cha mahojiano kupitia idhaa ya televisheni ya Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), kufanya kazi maalum na ndio maana binafsi, nilikiona kipindi hicho kikirudiwa kwa mara ya tatu ndani ya wiki mbili.

Ndivyo inavyokuwa katika kusukuma propaganda yake nyeupe, Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakioni vibaya kuvitumia vyombo vya habari vya serikali kuandaa vipindi vya kimkakati kwa lengo la kuzubaisha umma pale kinapokabiliwa na wakati mgumu.

Amejitahidi kujenga hoja kwamba uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 Zanzibar umefutwa kihalali, na kwamba Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) inayo mamlaka ya kufuta uchaguzi wote nchi nzima.

Anasema kwa njia ya kushutumu viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) ambao amewaita “hawa wenzetu” kwa kuwa hawawaelezi wananchi ukweli wa kilichotokea.

Kupitia kipindi hicho anaaminisha wasikilizaji kuwa anayosema ndio sahihi na kuasa wananchi wasisikilize maneno ya ubabaishaji yanayotolewa na hao aliowaita “hawa wenzetu.”

Mbali na kujenga uhalali wa maneno matupu wa uamuzi wa kufutwa kwa uchaguzi mkuu kwa tangazo la Oktoba 28 mwaka huu alolitoa Mwenyekiti wa Tume, Jecha Salim Jecha, Bi Amina anasema wananchi wasubiri uchaguzi utakaofanyika tena kama “ilivyokwishatangazwa na Tume ya Uchaguzi.”

Hakuna hata wakati mmoja mwanasiasa huyu anayehangaikia nafasi ya kula baada ya kumaliza kazi Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, ametaja kifungu cha sheria kinachohalalisha hoja zake.

Huyu ni msomi wa uchumi, lakini kwa bahati mbaya anaingia katika kujivunjia hadhi kutokana na kutoeleza kwa ufasaha mambo ambayo kwa kiwango chake cha usomi, angejisikia vizuri tu kutaja vifungu vya sheria au ibara za katiba.

Kwa hivyo basi, sikuipata tofauti kubwa katika maelezo yake mwanamama huyu na kada wa kufa wa CCM, Baraka Mohamed Shamte, ambaye ni mmoja wa waliotoka na kubeba hoja za kishabiki tangu Jecha alipochukua uamuzi wa peke yake kufuta uchaguzi wote majimbo 54.

Kwa maana nyingine, Balozi Amina ameingia katika historia ya wanasiasa waliofuata mkumbo kwa kuridhia uvunjanji wa sheria kwa sababu tu alitaka naye kuonekana ameshiriki “kazi muhimu” ya kukitetea chama chao cha CCM.

Ni kazi adhimu iliyoshirikisha hata wanasheria, wanataaluma wanaotarajiwa kunyoosha mambo yaliyozusha utata kutokana na kutendwa katika mazingira ya shaka.

Hivi balozi Amina anaposema uchaguzi umefutwa kihalali kwa kuwa Tume imejiridhisha yalikuwepo matatizo, anaweza kueleza ni kwanini hasa ameshindwa kutaja angalau kituo kimoja ambako uchaguzi uliharibika?

Ni kwanini katika maelezo yake kwenye kipindi hicho kilichokosa ufundi na ujuzi wa kitaaluma upande wa mwendeshaji wake ambao ungesaidia wananchi kuelimishwa kinachodaiwa kutokea vituoni siku ya uchaguzi Oktoba 25, hakueleza kifungu kilichompa mamlaka ya kisheria Jecha kufuta uchaguzi?

 

Na kama aliposema uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein na serikali anayoongoza ni halali na sio kama inavyoelezwa na “hawa wenzetu” kuwa kikatiba ulikoma Novemba 2, alishindwaje kugusa Ibara ya 28(2) inayosema kipindi cha uongozi wa rais kitakuwa kimekwisha miaka mitano kutoka siku aliyoapishwa kushika wadhifa huo kwa kula kiapo cha uaminifu?

Hakugusa hapa, labda kwa kujua maelezo hayo yanamaliza nguvu ya hoja yake na kama inavyoelezwa na makada wenzake wa CCM kutaja Ibara ya 28(1) ambayo kwa hakika inahusu uhalali wa rais aliyepo kuendelea kushika wadhifa huo wakati akisubiri kuapishwa kwa kiongozi aliyepatikana kwa uchaguzi baada ya kipindi chake cha uongozi kumalizika.

Balozi Amina katika hali iliyothibitisha kuandamwa na dhamira mbaya ya kutetea kibubusa hoja zinazojengwa na CCM katika kampeni ya kutafuta uhalali usiokuwa nacho wa kushindikiza uchaguzi mpya, akasisitiza wananchi wasubiri uchaguzi utakaorudiwa.

Mbona hakueleza kwamba CCM imeshindwa hoja hiyo kuanzia pale viongozi wenzake walipolalamika mbele ya Tume ya Uchaguzi, baada ya kubaini chama wakipendacho kimepigwa mwereka katika uchaguzi?

Hakueleza kuwa malalamiko waliyoyawasilisha wenzake mbele ya makamishna wa Tume na waangalizi wa uchaguzi siku ile ya Oktoba 27 yalishindwa kuthibitishwa.

Anasemaje basi akiambiwa anaficha ukweli kwa kuwa kwa hadhi yake kiuongozi anajua hakuna rekodi hata moja katika kituo chochote cha uchaguzi ya kutokea fujo wala uharibifu wa taratibu za uchaguzi.

Lakini kama amejiaminisha kama wenzake kuwa kulikuwa na kituo ambako uchaguzi ulikuwa na vurugu, pia anaamini vurugu katika kituo kimoja inastahili kufutisha uchaguzi wa vituo vingine vyote vilivyobakia?

Na ilikuaje mawakala wa CCM hawakulalamika vituoni? Au ilikuaje wasijaze fomu kuwasilisha malalamiko kama utaratibu unavyotaka?

Balozi Amina amejidharau. Nasikitika unapokuwa na mwanamama unayemheshimu akaamua kujichafua kwa kuungana na watoa hoja za uongo.

Nachelea kumhesabu katika wanasiasa wanafiki, kusema usichokiamini, bali pia kueneza uongo kwa sababu ya kupalilia maslaha yako binafsi.

Kweli kwa wengi CCM, wapo katika kipindi cha kutafuta kuangaliwa kwa nafasi fulani ya kula. Na iwapo CCM itafanikiwa kushikilia mpini kama ifanyavyo kabla ya ukweli na haki kuchukua nafasi yake wakati wowote, basi ametimiza muradi.

Balozi Amina amekuja mwenyewe kuonesha hajabadilika kitu. Ni yuleyule tunayemjua siku zote tangu huko nyuma.

Yale matarajio kubadilika kifikra kwa kuwepo kwake nje ya siasa chafu za chama chao Zanzibar, na kukaa ughaibuni ambako nasadiki alipata wasaa wa kuzunguka sehemu nyingi za dunia akichanganyika na watu wenye upeo wa kufikiria kitaalamu na katika uhalisia wa mambo, kumbe sifuri.

Ninashawishika kuwa yungali mwanasiasa mhafidhina asiyethubutu kuamini ukweli unaokiumiza chama akipendacho na akitegemeacho kimaisha, badala ya usomi wake.

Anaitwa balozi sasa, awe mwanasisa aliyeshiba chembe za dhana ya diplomasia, hili nalo limempitia kwa mbali.

Nataka kuamini pale alipoulizwa na Ally Abdalla Saleh (Alberto) mwaka 2005 ndani ya duka maarufu la Masomo, kwamba anafikiria hali itakuaje ikitokea CCM imeshindwa uchaguzi na CUF, jibu lake halikuwa utani.

Alisema “hiyo haitatokea duniani.” Alishikilia maneno hayo hata aliponasihiwa aweke akiba kwamba Mwenyeezi Mungu ana kadari yake ya kuamua nani awe kiongozi wa wanadamu.

Ni kama kuamini kuwa katika uhai wake, haitapata kutokea CCM ishindwe uchaguzi na kulazimika kuachia madaraka. Kwa hivyo hakujishughulisha kamwe na kujiuliza ni kwanini CCM isishindwe uchaguzi wa ushindani?

Hivyo ndivyo walivyo CCM wahafidhina Zanzibar – hata uwaambie vipi, hawakubali CCM imeshindwa uchaguzi halali ndio maana ikamshika Jecha afute uchaguzi kinyemela, na sasa wanapata shida kuukubali ukweli huo usiopingika.

Hawa hawaeleweki. Mpaka wanamaliza kampeni, mgombea wao hakupata kutamka kuwa akishindwa uchaguzi atampongeza aliyeshinda. Hayo si katika maneno kwenye msamiati wao kisiasa.

Chanzo: Mwanahalisi

One Reply to “Balozi Amina ni yuleyule wa 2005”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s