Naona wakubwa CCM wamelielewa somo

Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho
Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho

INAFURAHISHA kubaini sasa viongozi wakuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameamua kutogeuka jiwe. Wanaendelea kuifanya kazi muhimu ambayo walitarajiwa waifanye tangu walipothibitisha kuwa mbinu waliyoitumia kutaka kubaki madarakani ilhali wameshindwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar, wa Oktoba 25, haitawavusha.

Wamelielewa barabara somo la haja ya kuwaelimisha wafuasi wao kuhusu ukweli na ukweli mtupu usio hata chembe ya dhihaka. Wamelielewa somo kwa sababu ninaamini sasa wamefika mwisho wa kusubiri wakati uwaangushe puu.

Na wangeanguka tu kama historia ya wakorofi wengine popote duniani inavyoonesha – wote wajitahidio kuamini kuwa wanaweza kuchezea muda adhimu kwa kushindana na wakati huanguka na vibaya.

Viongozi wa CCM wanakutana na wafuasi wao katika madaraja mbalimbali, wakiwaeleza kuwa ni lazima wakubali kwamba wakati wa chama hicho kuongoza, umepita angalau kwa Zanzibar. Baada ya zaidi ya robo karne ya kuwa juu ya kilele, sasa ni zamu ya Wazanzibari wenzao kukalia hatamu za uongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Tayari simulizi za vilio zinasikika kusawiri kote ambako viongozi wa CCM wanakutana na wanachama na kuwaeleza kinachotakiwa wakielewe.

Kwa kweli, hata kulieleza somo kwenyewe – kwamba CCM haikushinda uchaguzi mkuu ule na wala haikuibiwa kura zake – kumekuwa kwa shida, na sababu iko wazi.

Viongozi hao wanaifanya kazi hiyo baada ya kuifanya kazi ya kueneza uongo kwa muda mrefu, ambao umeingia ndani isivyo kawaida miongoni mwa wafuasi wa chama hicho.

Wana-CCM wanauliza sasa ni kwanini walifichwa ukweli wa mambo tangu kule mapema? Hapa ninawaachia viongozi wenyewe, wanaifanya hiyo kazi ya kueleza sababu. Wanajua maneno au lugha ya kueleza.

Ndio desturi haki itakapolazimu kusimama, hakuna wa kuizima. Haki inarejea njia yake baada ya Wazanzibari kuwa wamesubiri vya kutosha kuidhibiti.

Huku wakionesha walivyo na moyo wa subira na kiwango kikubwa cha uvumilivu, pia wamejenga imani kwa viongozi wao. Na hili ni jambo lililosaidia kuinusuru nchi na balaa la vurugu saa hizi.

Wamefanya uamuzi wanaoamini mpaka sasa ni sahihi na ni haki yao kuchagua wamtakaye kwa kuwa wanamuamini. Wamefanya hivyo kwa kujua wanalindwa na Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984.

Ukweli unabaki palepale: Uchaguzi wa Zanzibar ulifanyika kwa amani na kusimamiwa vizuri zaidi ya ilivyokuwa 2010. Wapigakura walitoka na kufika vituoni, wakapanga foleni na kupigakura kihalali.

Watendaji wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na mawakala wa vyama na wagombea wao, walishuhudia kura zikihesabiwa, kujumlishwa na wakajionea utangazaji wa matokeo.

Matokeo ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wajumbe wa Mabaraza ya Madiwani wa Halmashauri, yote yalitangazwa vituoni na nakala za matokeo kubandikwa. Kura za urais kila jimbo pia zilibandikwa vituoni kama sheria inavyotaka.

Kazi ya kujumlisha na kuhakiki kura za urais ikiwa iliyoshafikia majimbo 40, ambayo ni majimbo 14 kasoro ya majimbo yote 54 ya Zanzibar, ndipo Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha akalikoroga kwa kutangaza uamuzi wa peke yake kuwa “uchaguzi wote umefutwa.”

Hatua yake ilikuwa matokeo ya alichokifikiria siku zote baada ya kuteuliwa – kuihujumu haki ya wananchi. Haya ndiyo matokeo ya mwananchi kujifikiria zaidi yeye na anaowapenda; badala ya kuangalia maslahi mapana ya wananchi na nchi yao.

Kila kitu kiko hadharani safari hii au niseme hakuna kilichojificha. Zile nguvu za kupotosha ukweli, zimeshindwa.

Naona Wazanzibari wapo katika kile ambacho Ali Mohamed Ali Nabwa, aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa gazeti halisi la Dira (sio linalojitahidi kujipa sura ile), alisema, “iko siku itakuwa kweli.”

Haiwezekani wasio na haki wakapewa. Inayowastahili ndio wa kupewa. Daima haki haipotei, bali huweza tu kucheleweshwa na waliozoea kudhulumu.

Zanzibar inahaki ya kutulia na maisha ya watu wake yapewe nafasi ya kuendelea kama kawaida ya siku zote. Yanakuwepo maisha baada ya uchaguzi. Wagumu baada ya kuridhika wameshindwa uchaguzi, ni muhimu waachie haki waliyoizuia.

Waliozoea kuzuia haki kusimama mahali pake, wametambua lazima kuridhia matakwa ya wengi badala ya kuendelea kuzuia kikatili. Hawataki tena kuzikufuru neema za Mola muumba.

Rafiki yangu aliyeko Makunduchi ameniambia baada ya tambo nyingi na kauli za kuvunja moyo wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) pamoja na wapenda mabadiliko ya uongozi Zanzibar, kuwa uchaguzi utarudiwa, viongozi wa CCM wanasema, “tutafanya uchaguzi mwingine baada ya miaka mitano.” Ni kweli, uchaguzi mwingine ni mwaka 2020, ndivyo Katiba inaelekeza.

Anayeshikilia uspika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho alikwenda kumwaga siri nyumbani kwao huko. Pamoja na kuchafua hali ya hewa kwa maneno mabaya, aliusema ukweli, “chama chetu kimepoteza madaraka.”

Yeye si kwanza. Wasaidizi wengine wa Dk. Ali Mohamed Shein, katika nafasi yake ya umakamu mwenyekiti wa CCM Zanzibar, wameeleza ukweli huu mara mbili-tatu.

Wote viongozi waandamizi waliopo Ofisi Kuu Kisiwandui wakiongozwa na naibu katibu mkuu Vuai Ali Vuai, wameeneza neno.

Ukweli huu umeshasemwa katika namna mbalimbali kwenye wilaya za Unguja na umesambaa wilaya za Pemba. Awali ukweli nusu, sasa ukweli wote ikiwemo “hakuna uchaguzi tena.”

Wana-CCM wanaelezwa sasa kuwa wasubiri Tume itatangaza. Na katika kusubiri, wasubiri wasichokitarajia kitatangazwa – ushindi wa CUF na Maalim Seif Shariff Hamad. Wanaambiwa wajumuike katika kushiriki hatua zitakazofuata baada ya hapo.

Somo limeeleweka kwa viongozi wakuu, likaenezwa kwa wasaidizi wao, na baada ya wote kujiridhisha wakati umefika, sasa linafikishwa kwa wananchi. Ni hatua ya kupongezwa walioamua kuipa nafasi yake haki. Na kwa kutambua hilo, waliofanikisha wanayo malipo ya ahsante kwa umma, bali kwa hakika watalipwa na Allah kwa kuishuhudisha haki.

Hawakosi kujua hatua yao imeepusha vurugu. Imeepusha kuudidimiza uchumi wa familia na uwezo wa kiuchumi upande wa Serikali.

Vyote hivyo havina nafasi ya kunawiri ndani ya jamii iliyojaa chuki, fitna na majungu; huku viongozi wake wakizidisha mizaha, ulaghai, vitisho, mabavu na wakitafuna raslimali za wananchi.

Maendeleo huja pale penye amani ya kweli, umoja wa kweli miongoni mwa wananchi, na viongozi waliosimamisha uongozi mwema. Ni dhahiri, huko ndiko Wazanzibari walikoamua Zanzibar ielekezwe kupitia Civic United Front.

Chanzo: Mwanahalisi

 

Advertisements

4 Replies to “Naona wakubwa CCM wamelielewa somo”

    1. ok ila mbona mm nilichohuzuria hayakuzungumzwa haya mbona hii nchi imekua na waongo wengi hemu tutumieni video za hao watu walichokizungumza na ziwekeni wazi kwenye mitandao na wao wenyewe tupate tuwaulize watujuze kuwa ndicho walchokisema maana nilkokwenda mm tuliambiwa tujiandae na uchaguzi na cuf hawawezi kuishinda ccm ilitokea kwa kuiba kura tu na hlo tunalikubali kwan wezetu wa kisiwa cha pli hushi ni ktu ha kawaida tu hasa tunapokua nao vyuoni tunawaona hvyo inatufanya tuamini kuwa wamewaibia ccm.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s