Matokeo ya uhalifu Zanzibar

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Usiku wa kuamkia jana, tarehe 13/12/2015, nchi yetu Zanzibar imeshuhudia matukio ya uhalifu unaoratibiwa na kutekelezwa na makundi ya vijana wa CCM waliopatiwa mafunzo maalum katika makambi mbali mbali kwa lengo la kuendesha uharamia dhidi ya raia wasio na hatia huku wakilindwa na baadhi ya askari wa Vikosi vya SMZ.

Taarifa tulizozipokea zinaonesha makundi hayo ya vijana waliokuwa wakitumia magari ya Vikosi vya SMZ na magari ya Baraza la Manispaa Zanzibar (ZMC), na kulindwa na askari wa Vikosi vya SMZ wakiwa na silaha za moto, silaha za jadi: mapanga, marungu na misumeno yalivamia maeneo ya Mwanakwerekwe Meli nne, Fuoni Maharibiko na Michenzani, kisiwani Unguja.

Katika tukio la kwanza, kundi hilo la vijana lilivamia eneo la Mwanakwerekwe katika jimbo la Magomeni na kupiga watu wasio na hatia. Katika tukio hilo, Bwana Ali Salum wa mtaa wa Nyerere alikamatwa na vijana hao na kuwekwa chini ya ulinzi na kupigwa kupita kiasi. Kutokana na kipigo hicho alipata maumivu makali na kupelekea kufikishwa hospitali kwa ajili ya matibabu.

Aidha, katika tukio la pili, kundi hilo la vijana lilivamia Baraza ya CUF iliyopo eneo la Michenzani, maarufu kwa jina la ‘COMMONWEALTH’ na kufanya uharibifu mkubwa wa mali, kuvunja na kuiba, na kukata miti iliyopandwa na Baraza la Manispaa katika kuendeleza hifadhi ya mazingira. Katika eneo hilo la Michenzani, kundi hili la vijana limevunja kibanda cha kutoa huduma ya kupiga Simu na uuzaji wa kadi za mawasiliano cha Bwana Ali Kombo na kuiba mali na bidhaa mbali mbali zilizomo katika duka hilo. Inakisiwa kuwa vijana hao waliiba mali ya kiasi cha TSH Milioni nne na laki tano (4,500,000) zilizokuwa katika duka hilo.

Tukumbushe kwamba matukio haya ya kuvamia, kupiga, na kujeruhi watu sambamba na kufanya uharibifu wa mali za wananchi ni muendelezo wa nia mbaya ya baadhi ya watu kutaka kuhatarisha amani ya nchi yetu. Itakumbukwa kwamba matukio haya yalianza katika kipindi cha Juni na Julai mwaka huu na kufikia hatua mbaya wakati wa uandikishaji wa wapiga kura. Kukosekana kwa hatua madhubuti ya kukabiliana na uhuni na uonevu dhidi ya raia kunakofanywa na kikundi hichi cha vijana wa CCM kulipelekea kupigwa risasi na kujeruhiwa vibaya watu wawili wa kijiji cha Makunduchi, Julai 4, 2015 na tarehe 29, Oktoba 2015 kuliripotiwa taarifa za kuvamiwa, kupigwa watu na kuharibiwa kwa mali za wananchi wa kisiwa cha Tumbatu.

Hivi karibuni, usiku wa kuamkia tarehe 3 Desemba, 2015 makundi ya watu waliojifunika nyuso zao wakiwa na silaha (maarufu hapa Zanzibar kwa jina la MAZOMBI) walivamia na kuchoma moto kituo cha radio cha HITS FM kilichopo Migombani, mjini Unguja na kumjeruhi vibaya mwandishi aliyekuwepo hapo. Kabla ya hapo mwezi wa Juni mwaka huu, kikundi cha MAZOMBI hao hao wakitumia magari ya Vikosi vya SMZ walivamia kituo cha radio cha COCONUT FM na kumtisha mwandishi Ali Mohamed kwa kurusha kipindi kilichokuwa kikihoji matukio yaliyokuwa yakihusisha makundi hayo.

Mbali na ukweli kwamba matukio haya haramu ya uonevu dhidi ya raia wasio na hatia yameendelea kujaza khofu na kuwatia wasiwasi wananchi, pia yamezidisha taharuki na bila ya shaka yanapalilia mbegu ya chuki miongoni mwa jamii katika kipindi hiki muhimu ambapo nchi yetu inapita katika kipindi kigumu kufuatia kadhia ya uchaguzi mkuu na yanayoendelea sasa, ikiwemo mazungumzo yanayoendelea ya kuikwamua nchi yetu, baada ya hatua ya Bw. Jecha Salim Jecha kutangaza kwamba eti amefuta matokeo ya uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015.

Kama tulivyowahi kueleza siku zilizopita, CUF inaamini kuwa kuwepo kwa matukio haya ya kuvamiwa, kupigwa, kuharibiwa na kuibiwa mali za wananchi ni muendelezo wa mipango miovu ya baadhi ya viongozi muflis wa CCM kutaka kupandisha jazba za wananchi wanyonge na kuchochea machafuko katika nchi kwa lengo la kuhalalisha mpango wa viongozi hao wa kuvunja amani na usalama na kuvuruga misingi ya haki za binadamu na utawala wa sheria.

Kutokana na kubainika kwa njama na mbinu hizo chafu za CCM za kuchochea uvunjaji wa amani na ukiukwaji wa sheria za nchi, uonevu, na hujuma dhidi ya raia wasio na hatia na mali zao, hata baada ya juhudi kubwa za Viongozi wa CUF za kuwasiliana na Mamlaka zinazohusika na Ulinzi na Usalama wa nchi yetu, kwa lengo la kuviza juhudi za kutatua mgogoro wa uchaguzi nchini ambao kimsingi unatokana na CCM kutokuwa tayari kuheshimu maamuzi ya wananchi waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015, tunapenda kueleza yafuatayo:

• CUF kinawaomba Wazanzibari wote kuendelea kuwa watulivu na kutokubali kuingia katika mtego wa CCM na kwamba kwa gharama yoyote wapuuze mbinu chafu za kuwachokoza wananchi zinazopangwa na kuratibiwa na viongozi wa CCM kwa kushirikiana na makundi ya vijana wasiokuwa na maadili na baadhi ya maofisa wa vyombo vya ulinzi walioamua kuasi viapo vyao vya kazi na kujipa jukumu la kuhujumu wananchi wasio na hatia. CUF inawataka wananchi wote kutambua na kuweka katika makini yao nasaha za kiongozi wao Maalim Seif Sharif Hamad kuwa ni muhimu kwa wananchi wote kuwa watulivu katika kipindi hiki mbali na hujuma nyingi zinazopangwa na kuratibiwa kwa lengo la kuwatoa wananchi katika malengo makubwa na ya muda mrefu ya kujenga enzi mpya za utawala utakaojali maslahi ya Zanzibar na wananchi wake wote bila ya kujali itikadi zao na historia ya mambo yaliyopita.

• CUF kinawanasihi Vijana wa Zanzibar, hasa wale wanaotumika na viongozi wa CCM kushambulia na kudhuru wananchi wenzao kinyume na Sheria za nchi, kuacha mara moja unyama huo kwani wao ndio watakaobeba lawama na hakuna atakaweza kuwasaidia kuwajibika kisheria. CUF inawataka Vijana hao kutambua kuwa siasa za Ulimwengu wa sasa ni tafauti na miaka iliyopita. Mfano wa yanayoendelea katika nchi za jirani na Zanzibar kama vile Kenya ni ushahidi unaotosha kubainisha kuwa sheria za kimataifa zinaweza kuchukua mkondo wake wakati wowote na kwa mtu yoyote bila ya kuzingatia na kujali nafasi yake.

• CUF kinatoa wito kwa Wakuu wa vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama hapa nchini, hasa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), kusimamia amani nchini na kuchukua hatua stahiki pasi na kuegemea upande wowote wa kisiasa ikiwa ni pamoja na kuwakamata na kuwafungulia mashitaka wale wote waliohusika na matukio yanayoendelea nchini. CUF kama taasisi makini, inalishauri Jeshi la Polisi kupitia na kutumia taarifa mbalimbali zilizokwisha kuwasilishwa kwa Jeshi hilo kwa nyakati tafauti kubainisha maeneo na wahusika wa matukio yaliyotajwa.

• CUF kinamkumbusha Dk. Ali Mohammed Shein kwamba pamoja na kumaliza muda wake wa kikatiba wa kuendelea kutumikia nafasi ya Urais, lakini kwa kule kuendelea kushikilia nafasi hiyo kunamfanya abebe dhamana na kuwajibika kwa matendo yote haya.

• CUF kinawaambia viongozi wa CCM wanaoshiriki kuandaa na kuchochea matukio haya na mengine ambayo yanapangwa muda huu kwamba kinawatambua wote na kitafikisha taarifa zao kwa IGP na kwa taasisi za kimataifa zinazosimamia uhalifu na makosa ya jinai.

• Tumalizie kwa kuwaambia CCM kwamba kwa hali ya mambo inavyokwenda, muda huu si wa kuvunja madaraja baina yetu, bali ni muda wa kujenga madaraja yatakayotuwezesha kufanya kazi pamoja katika Serikali mpya ya Umoja wa Kitaifa itakayoundwa na vyama vya CUF na CCM chini ya Rais mpya aliyechaguliwa tarehe 25 Oktoba, 2015. Zanzibar Mpya tunayotaka kuijenga ni yetu sote. Tusifanye njama za kuivuruga bali tuunganishe nguvu kuijenga.

HAKI SAWA KWA WOTE

ISMAIL JUSSA
KAIMU MKURUGENZI WA HABARI NA MAWASILIANO – CUF
14 DESEMBA, 2015

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s