Zinahitajika amri za Magufuli waziwazi

wazanzibari wakiwa wanatafuta majina yao kwa ajili ya kupiga kura Octoba 25 mwaka huu wa 2015
wazanzibari wakiwa wanatafuta majina yao kwa ajili ya kupiga kura Octoba 25 mwaka huu wa 2015 uchaguzi ambao baadae ulifutwa Octoba 28 na Mwenyekiti wa ZEC

 

SITAKI kuwa mnafiki kujitia kumpongeza; lakini ningependa kuona Dk. John Magufuli, aliyemrithi Dk. Jakaya Kikwete katika hatamu za uongozi wa jamhuri, pia anatekeleza kaulimbiu yake ya “hapa kazi tu” kwa upande huu wa Zanzibar.

Zanzibar, sehemu ya hiyo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoingia kuiongoza, Dk. Magufuli ataonekana wa maana sana na wananchi akisikika anatoa amri hadharani kwa viongozi wa CCM ambao zipo dalili nyingi kuonesha walimtuma Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 kuukubali ukweli kuwa chama hicho kimepoteza madaraka kihalali.

Nasema viongozi wa CCM wamemtuma Jecha afute uchaguzi, katika kitendo kinachothibitika ni cha kuvunja sheria na hivyo kuitumbukiza nchi kwenye dimbwi la ukosefu wa serikali halali kisheria inayoongoza kwa sasa, kwa sababu ni CCM peke yake walionufaika na kitendo hicho.

Aliyoyaeleza Jecha katika kujenga hoja ya kufuta uchaguzi, yamesikika midomoni mwa viongozi wakuu wa CCM Zanzibar peke yao; hayajatamkwa pengine popote, si katika vyama vingine wala wasimamizi wa uchaguzi vituoni na majimboni.

Ni viongozi hao wa CCM peke yao, wanaotetea uamuzi wa Jecha, ambao wenyewe umeshathibitishwa si uamuzi wa Tume ya Uchaguzi aliyoteuliwa mwaka 2013 kuiongoza. Makamishna wawili walimkana haraka baada ya tangazo lake, na wengine hawajajitokeza kumuunga mkono.

Isitoshe, uamuzi halali wa Tume kwa mujibu wa sheria, huwa ni ule uliofanywa kupitia kikao kilichomshirikisha Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti, pamoja na makamishna angalau wanne. Jecha alinunua vazi kabla ya mtoto kuzaliwa.

Kwa kutambua alivunja sheria, Jecha alihangaika kule alikojificha au alikohifadhiwa chini ya ulinzi wa waliomtweza akili, na kujitokeza Novemba mosi, kwa kuwaita makamishna pamoja na Makamu Mwenyekiti, Jaji Abdulhakim Ameir Issa, na kutaka wamuunge mkono kwa uamuzi haramu alioufanya.

Nausema ni uamuzi haramu kwa sababu yeye mwenyewe alipokutana nao siku hiyo, ikiwa ni ya nne tangu alipoharibu mambo, alitangulia kuwaomba radhi kuwa alilazimika “kusema uongo” eti “ili kuokoa nchi kuingia katika balaa.”

Yaangaliwe hayo mazingira ya uchaguzi kufutwa na Mwenyekiti akiwa makali alikodhibitiwa, halafu siku nne baadaye, ndipo atoke alikokuwa na kukutana na makamishna na kuwaomba wamuunge mkono kwa uamuzi huo. Huu ndio uamuzi ninaousema haramu kisheria hata kama kungekuwa na kifungu cha sheria kinachoipa tume mamlaka, si yeye Jecha.

Sasa, kwa kuwa Zanzibar imegubikwa na mgogoro wa kisiasa uliotokana na kitendo haramu cha Jecha, panataka Dk. Magufuli, kama vile anavyotoa amri hadharani kuhusu kushughulikiwa kwa ufisadi serikalini, atoe amri hadharani kutaka viongozi wa CCM waliomtweza akili Jecha, wajirudi na kurekebisha tatizo.

Kila ninavyoyaona mambo yanavyoendelea, ninaridhika kabisa kuwa mara tu viongozi wa CCM watakaposema “imetosha” basi Zanzibar itapata rais wake halali, yule ambaye wananchi walimpigia kura kwa wingi Oktoba 25.

Nieleza kwa undani ninachomaanisha. Tangu uchaguzi ulipoingizwa kwenye uharibifu, ni viongozi wa CCM walioonekana wakilalamika kuwa uchaguzi uliharibika, kura ziliokotwa mitaani, mawakala wake hawakupewa vitambulisho, makamishna wa Tume walikaribia kuchaniana mashati, ikimaanisha walipigana ngumi, na kulikuwa na maeneo, ambayo hayajatajwa, idadi ya kura ilizidi wapigakura.

Malalamiko haya hayapo popote isipokuwa yanatamkwa na viongozi wa CCM, na ndiyo haya yalilalamikiwa na Jecha siku aliyosikika tangazo lake la kufuta uchaguzi wote Zanzibar. Malalamiko haya yamesikika yakipaishwa na baadhi ya wanasheria, ambao kwa kila hali wanajulikana ni watoto wa CCM. Tunajua hata namna walivyofadhiliwa kujitokeza kwenye vyombo vya habari kutetea kufutwa kwa uchaguzi.

Viongozi wa CCM ndio peke yao wanadai kuwa Dk. Ali Mohamed Shein, rais wa awamu ya uongozi iliyoingia Novemba 2010, bado angali kiongozi halali wa nafasi hiyo hata sasa kunapotokea wanasheria wajuzi wakitilia shaka uhalali wake. Ni wao pamoja na hao wanasheria watoto wa CCM wanahalalisha kukaa kwa Dk. Shein madarakani baada ya Novemba 2, siku ambayo miaka mitano iliyopita, aliapishwa kuwa rais.

Kwa hili, Ibara ya 28(2) inasema wazi, “Rais ataacha madaraka yake baada ya kumalizika miaka mitano kuanzia tarehe (ambayo) (a) kama yeye ni mtu ambaye ndiye mara ya kwanza amechaguliwa kuwa Rais chini ya Katiba hii alipokula kiapo cha uaminifu na kiapo cha kuwa Rais., na (b) kwa sababu nyenginezo mtu wa mwisho kushika madaraka hayo kwa mujibu wa Katiba hii alipokula kiapo cha uaminifu na kiapo cha kuwa Rais, au pasingelikuwa na sababu ya kifo chake, basi angelikula kiapo hicho.”

Kadhalika, ni viongozi wa CCM peke yao wanaoshikilia kwamba uamuzi wa Jecha kufuta uchaguzi ni halali, na wanasubiri Tume ya Uchaguzi itangaze tarehe ya uchaguzi wa marejeo. Ni CCM peke yao, licha ya jitihada kubwa za kujenga hoja kutaka wapate kuungwa mkono. Hawajaungwa mkono popote pale ndani na nje ya nchi.

Kwa hivyo, kwa kuwa hawa viongozi wa CCM ndio walionufaika na uamuzi wa Jecha kufuta uchaguzi, hasa kwa kuwa ndio waliomtweza akili na kumrubuni mtu mzima huyu na kutenda jinai, na sasa kuwa ndio wanaoshikilia kueneza propaganda kuwa kutakuwa na uchaguzi mwingine baada ya uliokwishafanyika bila ya malalamiko halali, basi Dk. Magufuli ataonekana wa maana kweli na Wazanzibari iwapo atawashika na kuwaambia waache umajununi wao na kuingia katika ukweli.

Dk. Magufuli kweli aliahidi kuwa atashirikiana na Makamu wake wa Rais, Bi Samia Suluhu Hassan na Dk. Shein, kutatua tatizo la Zanzibar. Kweli aliahidi, na aliahidi hadharani katika hotuba yake kwa taifa ya uzinduzi wa Bunge la 11. Lakini ahadi yake itakuwa na maana iwapo atatoa amri za wazi na wananchi wazisikie za kutatua tatizo lililopo.

Nashikilia umuhimu wa Dk. Magufuli kutoa amri za wazi sasa, kwa sababu kumekuwa na vikao vya viongozi wakubwa pasina kuwaeleza wananchi wanachokijadili na lini watamaliza kujadiliana. Hakuna taarifa za vikao hivi vinavyoshirikisha viongozi wa CCM na Maalim Seif Shariff Hamad, ambaye anashikilia kuwa ana ushindi mkononi wa urais.

Nashikilia hapo kwa sababu pia: wakati vikao vinaendelea faraghani, viongozi wa CCM wanaeneza propaganda ikiwemo ya kuandaa taarifa na kuzikana zikishatoka. Wanasema weshakubaliana kutakuwa na uchaguzi au mazungumzo yanayoendelea hayafuti ukweli kuwa uchaguzi umefutwa.

Bali pia nashikilia hapo kwa kuwa ndani ya ukimya huo wa wanaokutana kutojulisha wananchi kinachoendelea, kwenye mitandao ya kijamii kunazuka uvumi mwingi kila siku na kusema la haki, unaumiza mno hisia za wananchi wa Zanzibar.

Wakiendelea kuishi katika uvumi namna ilivyo, iko siku watapasuka kwa hisia za unyonge, hofu na kuzugwa.

Chanzo: Mwanahalisi

 

One Reply to “”

  1. Kwa hali inayoonesha na ukimya unayoendelea ni wazi kwamba TANZANIA hakuna WAPINZANI ijapokuwa UPINZANI upo na umesajiliwa…Labda kwa wale wasioweza kunifahamu ninachokikusudia ni Muonekano wa WAPINZANI ambao wangechukua uamuzi badala ya kusubiri NYIRADI za kila siku tunazozisoma magazetini / vyombo vya habari pamoja na vijiwe vya maskani -huku watu wakipewa moyo kumbe hawajui kinachopikwa na siku zinazidi kusonga mbele …..Naamini kama WAPINZANI wangekuwa wajasiri na kuchukua Hatua bila ya kusubiri ushauri wa viongozi wao ambao kwa namna moja au nyengine wamekuwa kama WAMEROGWA ….au wamepewa vidonge vya Fluouxetine …Na kwa hali hii iliokuwepo WAZANZIBAR wasitarajie kuwepo na MABADILIKO yyte …

Leave a comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.