Shari inayomwandama John Magufuli

Rais John Magufuli "Ala kuli hali, hatua alizochukua mpaka sasa zimewatikisa walio karibu na hao vigogo na pia baadhi ya vigogo vyenyewe".
Rais John Magufuli “Ala kuli hali, hatua alizochukua mpaka sasa zimewatikisa walio karibu na hao vigogo na pia baadhi ya vigogo vyenyewe”.

Na Ahmed Rajab

KAMA kimya kinasema basi hichi kilichotanda miongoni mwa baadhi ya vigogo vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinasema mengi, tena kwa sauti kubwa.  Hichi ni kimya chao kuhusu hatua ambazo Dkt. John Magufuli amejaaliwa kuzichukua katika kipindi cha siku thelathini ushei tangu aapishwe awe Rais mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM.

 

Hadi sasa miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho ni Katibu wa Uenezi na Itikadi, Nape Nnauye, pekee aliyejitokeza akionekana kuwa yuko upande wa Magufuli.  Nnauye, ambaye naye alichaguliwa mbunge kwa mara ya mwanzo katika uchaguzi uliopita, amejigamba kwa kusema kwamba Magufuli anachofanya ni kutekeleza ilani ya CCM.

 

Juu ya hayo, hata naye pia amethubutu kuonya kwamba chama chake cha CCM kitaingilia kati endapo Magufuli atatenda mambo kinyume na chama hicho. Hilo ni onyo na tishio kwa Magufuli licha ya kuwa Nnauye hajawadhihisha ni kwa njia gani chama cha CCM kitaingilia kati pindi akikikiuka chama chao.

 

Jumapili hii iliyopita Ramadhan Madabida, mwenyekiti wa wenyeviti wa mikoa wa CCM alisema kwamba wenyeviti hao wanampongeza Magufuli kwa kasi yake ya kuwachukulia hatua watendaji wanaoshindwa kuyatekeleza majukumu yao.

 

Wakuu wengine wa CCM wamejikunyata. Ama wamepigwa na muhuma kwa mshtuko walioupata, na wasioutarajia, kutoka kwa Magufuli. Kama si hivyo, basi wamepigwa na bumbuwazi na hawajui Magufuli ana mizungu gani mingine ambayo baadaye atawaonyesha Watanzania.

 

Ala kuli hali, hatua alizochukua mpaka sasa zimewatikisa walio karibu na hao vigogo na pia baadhi ya vigogo vyenyewe.

 

Sitoshangaa waathirika hao wakimwagia Magufuli maganda ya ndizi ili ateleze akiwa njiani kupigana na ufisadi, ubadhirifu pamoja na uzembe uliozagaa serikalini.  Au huenda wakamwekea vizingiti ili ajikwae, wakitaraji kwamba ataanguka.

 

Uzuri wa Magufuli ni kwamba yeye pamoja na waziri mkuu wake, Majaliwa Kassim Majaliwa, wanaonekana kuwa wanayajali maisha ya Watanzania.  Hilo halina shaka. Pili, wamekuwa wakichukua hatua bunifu, hatua tusizowahi kuziona zikichukuliwa na marais waliopita wa taifa hili baada ya Mwalimu Julius Nyerere.

 

Tatu, kila moja ya hatua walizochukua ni kama yenye kumsuta au kumpiga kigongo Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete. Tunaweza labda kuzimithilisha hatua hizo na yale maneno ya Nyerere dhidi ya uongozi wa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi.

 

Mwaka 1994, Nyerere aliandika kijitabu alichokiita “Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania”. Kijitabu hicho kilikuwa na mengi ya kuukaripia na kuukosoa uongozi wa serikali ya wakati huo iliyokuwa chini ya Mwinyi na Waziri Mkuu wake, John Malecela, pamoja na Katibu Mkuu wa CCM wa wakati huo, Horace Kolimba.

 

Kwa vile Nyerere wa siku hizo hakuwa na madaraka serikalini hakuweza kufanya lolote ila kukemea.  Magufuli mwenye madaraka serikali hana haja sana ya maneno.  Kwa vile anao uwezo wa kikatiba wa kuchukua hatua basi amekemea kwa vitendo.

 

Wakati maneno ya Nyerere yalikuwa yakikinzana na uongozi wa aliyemfuatia kwenye madaraka, vitendo vya Magufuli vinakinzana na uongozi wa aliyemtangulia kwenye madaraka.

 

Katika nchi nyingi Rais anayeondoka madarakani aghalabu hupendelea anayemrithi awe dhaifu kushinda yeye au asiwe mtu mwenye kung’ara kumpita yeye.  Bahati mbaya ya Kikwete ni kwamba amerithiwa kwenye madaraka na kiongozi anayeonekana kuwa mshupavu zaidi yake na ambaye, hadi sasa, kila hatua aliyoichukua imezidi kumnawirisha na kumfanya azidi kuwa kipenzi cha umma.

Kwa mujibu wa wananchi, Magufuli ni Rais mwenye kujiamini, mwenye uchungu na nchi yake na mwenye ari ya kizalendo. Hivyo ndivyo wamuonavyo.  Zaidi ya hayo, wanaamini kwamba anajuwa anasema nini na anajuwa anafanya nini.

 

Juu ya hayo yote, ameonyesha unyenyekevu kwa kusema, bila ya kubania, kwamba yuko tayari kujifunza asiyoyajuwa, kama alivyowaambia wafanya biashara aliokutana nao wiki iliyopita.

 

Mara kwa mara amekuwa akisisitiza kwamba serikali iliyopo sasa ni serikali yake yeye John Pombe Magufuli. Haitaji kuwa ni ya CCM, ingawa ulimwengu mzima unajuwa kwamba yeye ndiye aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho. Tusisahau kwamba mara mbili tatu wakati wa kampeni ya uchaguzi wa urais alisikika akitamka hadharani kwamba CCM ni chama chenye wanafik na kinachohitaji kusafishwa.

 

Kwa kusema hayo akimaanisha kwamba hicho chama ni kichafu, yaani uongozi wake wa juu ni mchafu na akijuwa kwamba chanuka kwa wengi wa wananchi.

 

Yote hayo yamewatia kiwewe wajionao kuwa ndio wenyewe wa kuiendesha nchi watakavyo, hata kama ni kwa kuzipinda sheria. Ndio maana vigogo vya juu ndani ya CCM vimekaa kimya vikimkodolea macho tu Magufuli badala ya kumshajiisha katika bidii zake za kizalendo.

 

Tunayahifadhi majina ya wawili watatu, mmoja akiwa katika ngazi ya juu kabisa, ambao tunasikia kwamba faraghani wanamkebehi na hata kumcheka wakimfanya kuwa kama ni mwehu. Wanaikebehi kauli yake ya “kupasua majipu” na wanazifanyia dhihaka ahadi alizotoa.

 

Ninazisikiliza hotuba zake, naiangalia ile iitwayo “lugha ya mwili” wake inavyosema na moyo unaridhika, unafarijika kwamba kweli huyu ni kiongozi mwenye kuyaweka mbele maslahi ya taifa na si ya chama chake au ya viongozi wa chama hicho.

Huyu ni mtu ambaye unaamini kwamba atakifanya anachosema atakifanya kwa sababu unahisi ya kuwa anakikusudia kwa dhati yake. Haonyeshi kuwa na ajizi wala muhali.

 

Magufuli ana sifa nyingine inayomzidishia haiba: anaweza kuyalainisha magumu kwa mizaha lakini katu si mcheka ovyo. Ukimsikiliza tu utajuwa kwamba kiongozi huyu hana mchezo. Hii ndiyo sababu inayowafanya wenye nguvu ndani ya CCM wawe wanamcha na, wakati huohuo, kumchukia.

 

Wameingiwa na wasiwasi mkubwa kwa sababu wanachelea asije akaamua kuyageukia na kuyafufua madudu yao waliyoyazika yakazikika. Kwa sasa hawawezi kumgusa kwani hagusiki kwa vile wananchi wengi wanamuunga mkono kwa hatua alizochukuwa.

 

Habari tunazozisikia ni kwamba wapinzani wake ndani ya uongozi wa CCM-Taifa wanaungwa mkono, chini kwa chini, na baadhi ya viongozi wa CCM-Zanzibar walio wahafidhina na wanaong’ang’ania madaraka kwa kukataa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar isiyatangaze matokeo yaliyosalia ya Uchaguzi Mkuu huko Visiwani. Pande la viongozi hao linaongozwa na Balozi Seif Ali Idi na mpaka sasa hakuna hata mmojawao aliyejitokeza kuiunga mkono kasi ya Magufuli na hatua anazozichukuwa.

 

Pale ambapo kasi za Magufuli hazijaonekana bado ni katika kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar. Mgogoro huo umesababishwa na hatua ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kukataa kumaliza kuyatangaza matokeo yaliyosalia ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wa Urais wa Zanzibar. Pamoja na hayo aliubatilisha uchaguzi Mkuu wa Zanzibar isipokuwa ule wa wabunge na wa kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano.

 

Hatua hiyo imeipelekea Marekani kuonya kwamba itainyima Tanzania msaada wa dola za Marekani milioni 472 lau mgogoro huo wa kisiasa wa Zanzibar usipotanzuliwa.  Marekani, pamoja na mataifa mengine yaliyo wafadhili wa Tanzania, yanataka mgogoro huo umalizwe kwa kukamilisha zoezi la kutangaza matokeo yaliyoyabaki ya uchaguzi na kutangazwa kwa aliyeshinda urais wa Zanzibar.

Tuna taarifa kwamba Muungano wa Ulaya (EU) umekwishaanza kufikiria ni hatua gani za kiuchumi unazoweza kuchukuwa dhidi ya Tanzania pindi ZEC isiporejelea zoezi la kutangaza matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar.

 

Kasi ya Magufuli pia imepwaya kwa kutowaondosha Zanzibar wanajeshi waliopelekwa huko kutoka Bara tangu siku za uchaguzi.  Kutawanywa wanajeshi hao mitaani kunawatia watu hofu hasa kwa vile Zanzibar haimo vitani wala hakuna hata fujo. Watu wanajiuliza kwa nini wanajeshi hao wametawanywa mitaani ilhali Bara wanajeshi wameondoshwa mitaani baada ya kumalizika uchaguzi mkuu?

 

Mwenye kuweza kuwatuliza wananchi wa Zanzibar kuhusu suala hilo ni yeye Magufuli akiwa Amiri Jeshi wa majeshi yote nchini kwa kuamrisha kwamba vikosi vilivyopelekwa Zanzibar virudishwe Bara.

 

Asipochukuwa hatua za kuyatatua matatizo hayo ya Zanzibar Magufuli atakuwa anajitafutia uhasama wa bure na wengi wa Wazanzibari wanaotaka utawala wa kisheria uheshimiwa Visiwani.  Huu si wakati wa kujipatia maadui zaidi ya wale walio katika uongozi wa CCM.

 

Hao viongozi wa CCM waliokaa kimya na wanaokerwa na miondoko yake ya uongozi hawana hila ila waendelee na kimya chao na labda waendelee pia kumperemba Magufuli na kutamani ajikwae.

 

Magufuli atafanya kosa kubwa akikipuuza kimya cha wasiomtakia yeye, na taifa, mema. Kimya chao ni cha shari na ni cha hatari. Ajue namna ya kupambana na wenye kimya hicho.

 

Kwa sadfa, Nyerere alitanguliza kijitabu chake kilichoushambulia uongozi wa Mwinyi kwa shairi kuhusu ukimya lililoandikwa na malenga wa mwambao wa Kenya, Muyaka bin Haji Ghassany (1776-1840).  Inafaa Magufuli ayakumbuke maneno ya ubeti wa mwanzo wa shairi hilo:

 

“Kimya mshindo mkuu, ndivyo wambavyo wavyele

Kimya chataka kumbuu, viunoni mtatile

Kimya msikidharau, nami sikidharawile

Kimya kina mambo mbele, tahadharini na kimya!”

Baruapepe: ahmed@ahmedrajab.com

 

Chanzo: Raia Mwema

 

 

 

 

 

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s