Kikwete na ukatili wa “mazombi”

Vikosi-vya-SMZ-620x308

Ahmed Rajab

KWA mara nyingine, baada ya kipindi kirefu, vitimbi vya ile inayojiita Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar vinaiaibisha Tanzania mbele ya ulimwengu.Vinawapa nguvu waliozoea kuitukana Afrika kuwa ni bara lisiloheshimu sheria, lenye viongozi vikaragosi wenye kuwanyima haki wananchi.

 

Vitimbi hivyo ni pamoja hatua ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, ya kuubatilisha uchaguzi, hatua ambayo inakwenda kinyume cha misingi ya kidemokrasia kwa vile, inakiuka sheria na Katiba ya Zanzibar. Hatua hiyo pia inahatarisha amani ya nchi na usalama wa wananchi.
Kitimbi kingine ni hatua ya kuwamimina wanajeshi wakiwa na vifaru vya kijeshi na askari wenye silaha nzito mitaani Unguja na Pemba. Lengo ni kuwatia hofu wananchi. Jumapili tulipata taarifa kuwa wale wanaoitwa “mazombi” waliingia katika eneo la Mtendeni, Unguja mjini, milango ya saa sita na dakika 20 za usiku. Hiyo ilikuwa ni mara yao ya tatu katika wiki moja.

 

Mtendeni ndiko kwenye makao makuu ya Chama cha Wananchi (CUF). Kwa mujibu wa walioshuhudia tukio hilo hao “mazombi” waliwapiga watu na walitaka kuvunja mlango wa makao hayo makuu ya CUF na walitishia kufyetua risasi.
Wiki iliyopita, vilevile katika saa za usiku waliingia katika mitaa ya Mwembetanga, Michenzani na huko huko Mtendeni. Walivunja nyumba za watu na wakawapiga wananchi.

 

“Mazombi” ndivyo vinavyoitwa mitaani vikosi vya washambulizi wasiojulikana wanaojifunika nyuso zao na ambao huingia mitaani kuwashambulia watu wakiwa na kila aina ya silaha. Labda wamepewa jina hilo kwa kuliigiza jina la Kiingereza “zombie”. Hivi ni viumbe vinavyoonekana katika filamu au riwaya za kutisha. Aghalabu huwa ni maiti wanaofufuliwa kwa uchawi.

 

Baadhi ya wataalamu wa lugha wanasema kwamba asili ya jina “zombie” ni jina la Kikongo “nzambi” lenye maana ya “Mungu” na “zumbi” lenye maana ya “mungu wa sanamu”.

 

Pengine wakazi wa Unguja wamewapa jina hilo kwa namna wanavyotisha kwa ukatili wao. Nasikia wiki iliyopita walimvua “zombi” mmoja barakoa aliyovaa usoni na wakamuona kuwa ni polisi wa ngazi ya juu wa kituo cha polisi cha Madema cha Unguja mjini.

 

Jina lake kamili tunalo na cheo chake lakini, kwa sasa, tunalihifadhi.

Vitimbi vya hao “mazombi” ni ukiukwaji wa haki za binadamu. Ni vitimbi vya kikatili vyenye kukirihisha.

 

Jumapili jioni, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu ya Dar es Salaam ilitoa taarifa ikisema imesikitishwa na madai ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kwamba amepuuzwa na kuwa amekataliwa kumuona Rais Jakaya Kikwete ili kuijadili hali ya kisiasa ya Zanzibar.

 

Ikulu imekanusha kuwa imepokea ombi lolote kutoka kwa Hamad la kutaka kumuona Rais tangu siku ya upigaji kura na kubatilishwa kwa uchaguzi (wa Zanzibar) na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, Jumanne ya wiki iliyopita.

 

Hata hivyo, Kurugenzi hiyo ilikiri kwamba Kikwete alipokea malalamiko ya CUF kuhusu vitendo fulani vya baadhi ya polisi wa Jeshi la Polisi la Zanzibar na alipokea ombi la kumtaka asaidie pawepo mazungumzo baina ya Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange na Hamad.

 

Taarifa hiyo iliongeza kwamba kufuatia hayo, Kikwete, ambaye pia ni Amiri Jeshi wa Majeshi ya Tanzania, alimpa amri Inspekta-Jenerali wa Polisi Ernest Mangu ayachunguze madai ya CUF na halafu ampelekee ripoti. Kadhalika, ameiamrisha ofisi yake isaidie pafanywe mazungumzo baina ya Jenerali Mwamunyange na Hamad.

 

Inasikitisha kwamba katika mgogoro mkubwa wa kitaifa kama huu ambao ni wa kisiasa, Rais amejitoa asisimamie yeye mazungumzo na Hamad na badala yake akakubali kumuachia mwanajeshi afanye mazungumzo hayo.

 

Kuhusu majeshi yetu inafaa tujiulize: ilikwenda-kwendaje hata wanajeshi na polisi, kwa kiwango kikubwa, wakawa na nidhamu wakati wote wa kampeni ya uchaguzi Bara na Visiwani na halafu wakabadilika kuanzia siku ya uchaguzi? Kuanzia hapo walianza kufanya mambo utadhani nchi imo vitani.

 

Yote hayo yameitia dosari Tanzania pamoja na hatua ya mwenyekiti wa ZEC kuutengua uchaguzi wa Zanzibar.

 

Kwa hali ilivyo, inaonekana kama viongozi wa CCM wamechanganyikiwa. Dalili moja ni kuwa taarifa wanazozitoa hawazitoi kwa mpango. Mara hutolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM/Zanzibar, Vuai Ali Vuai, mara hutolewa na waziri katika ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud na wakati mwingine hutolewa na Makamu wa Pili wa Rais mwenyewe, Balozi Seif Ali Iddi, ambaye ndiye mwenye kuonekana anaiendesha Zanzibar.

 

Kinachosikitisha na kuzua maswali mengi ni ukimya wa Rais Ali Mohamed Shein na kutoonekana kwake hadharani tangu alipopiga kura. Hii ni ishara ama ya udhaifu au ya kutojali wakati nchi imo hatarini au labda kuna mengine ya ziada ambayo kwa sasa hatuyajui.

 

Tunachokijuwa ni kuwa CCM inakabiliwa na mtihani mkubwa kwani kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa Zanzibar jumuiya ya kimataifa imetamka kwa kauli moja kuupinga uamuzi binafsi wa Jecha kuufuta uchaguzi. Nchi na taasisi kadhaa za kigeni, pamoja na za ndani ya nchi, zimetaka zoezi la kuhesabu kura lirejelewe na uamuzi wa wapiga kura uheshimiwe.

Kiroja cha mambo, iweje hadi siku ya tatu baada ya uchaguzi kumalizika ndipo Jecha aseme kulikuwa na kasoro? Na kama kasoro hizo zilikuwa Pemba pekee kwa nini aliufuta uchaguzi mzima?

 

Ukweli ni kuwa CCM haiko tayari kuyaacha madaraka. Baadhi ya wanasiasa wake wa Zanzibar, akina Asha Bakari, wamelisema hilo mara nyingi, faraghani na hadharani. Kauli yao kwenye majukwaa ilikuwa “Hatutoi, hatutoi, hatutoi. Tumeipata serikali kwa bunduki hamtoweza kutuondosha kwa karatasi (za kura)”.

 

Wanasiasa fulani wa Bara nao wana kono lao kubwa katika mbinu za kutaka CCM iidhibiti Zanzibar. Tusisahau maneno ya Waziri William Lukuvi, aliyesema hadharani kwamba Serikali ya Muungano itafanya kila iwezalo kuidhibiti Zanzibar kwa sababu ya “kitisho cha ugaidi” kwa vile takriban asilimia 98 ya wakazi wake ni Waislamu. Ushahidi wa matamshi yake upo kwenye kanda za video mitandaoni.

 

Nilimsikia Rais Mteule Dk. John Magufuli akisema Kikwete anastahili sifa kwa kuiheshimu Katiba na kuondoka madarakani. Amesahau kuwa ulimwengu unamuangalia akiondoka madarakani akiacha Zanzibar katika hali ngumu sana.
Ulimwengu pia unazungumzia dosari zilizojitokeza katika uchaguzi huu wa 2015. Kubwa ni ukosefu wa uwazi na mazonge yaliyosababishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) huku ile ya ZEC ikifurutu ada. Kuheshimiwa demokrasia ni suala pana, zaidi ya Rais kuondoka madarakani muhula wake ukimalizika.

 

Ni wazi kwamba kuna viongozi wa juu wa CCM/Zanzibar wanaokerwa na demokrasia. Wangefaa wajifunze kutoka Benin. Huko, utawala wa kwanza wa kikomunisti barani Afrika wa mwanajeshi Mathieu Kérékou, aliyefariki dunia Oktoba 14 mwaka huu, ulirudisha mfumo wa vyama vingi ikiwa nchi ya kwanza Afrika kufanya hivyo.

 

Aliposhindwa katika uchaguzi, Kérékou aliyakubali matokeo, lakini akawa tena Rais baada ya kushinda uchaguzi mwingine miaka mitano baadaye. Benin ilifanikiwa kwa sababu ilikuwa na nia ya dhati ya kufuata demokrasia pamoja na ilifanya mkutano wa kitaifa ulioandaa Katiba mpya ya wananchi. Ikiwa Benin na Kérékou walifanikiwa Zanzibar na Shein wanahofia nini?

 

Viongozi wa CCM/Zanzibar wamedai kuwa CCM ilinyimwa ushindi kwa dosari zilizotokea Pemba. Ukweli ni kwamba sio Pemba inayowashughulisha. Huko wanajuwa si rahisi kupata ushindi. Ni Unguja wasikotaraji kushindwa na walikoshindwa. Ndani ya nyoyo zao wanajuwa kuwa wameshindwa tena kihalali.

Mara hii wafuasi wao wa Unguja hawakwenda kupiga kura. Ni asilimia 75 tu ya wapiga kura waliopiga kura zao, kwa kawaida huwa baina ya asilimia 85 na 90. Hii inaonesha kuwa wafuasi wao wa Unguja safari hii walichoshwa na vitimbi vya CCM. Mwishowe watakuwa kama Wapemba na huenda wakaikataa kabisa CCM.

Kwa hivo inafahamika kwa nini CCM wanataka uchaguzi urejewe kote. Ingekuwa kweli kulikuwa makosa Pemba basi wangeurejea huo wa Pemba.
Lakini huko hakutowasaidia. Ni Unguja tu watakoweza kuiba na wizi wao ukawasaidia. Kwa hivo njia ya kuurejea uchaguzi Unguja ni kuubatilisha uchaguzi wote wa Zanzibar nzima.

Naamini uongozi wa CCM/Taifa, Dodoma, umo katika hili. Haielekei kuwa majeshi yaivamie Zanzibar bila ya kuamrishwa na Amiri Jeshi Mkuu, Kikwete.
Inashangaza viongozi wa CCM kuwa hawaoni hata haya kuivunja amani ya nchi kwa makusudi kwa maslahi ya chama chao.

Tangu 1964 kila kosa la CCM au ASP limekuwa likitupiwa Wapemba. Kwa kufanya hivyo, viongozi hao hawakuweza kuelewa kwa nini kila kwenye uchaguzi Wapemba wanawakataa. Na hao vyura wanaokichupia kisingizio cha uarabu kila unapotokea mgogoro Zanzibar ndio kweli hawajui kuwa asilimia 97 ya Wapemba, akiwemo Maalim Seif na Dk. Shein, si Waarabu?
Bila ya shaka wanajuwa lakini wanahisi ni bora wauvuruge ukweli.

 

Tatizo lililoikumba CCM safari hii ni kuwa si Wapemba peke yao walioikataa. Waunguja nao, ambao miaka yote walikuwa wakiipigia kura kwa mkururo CCM, mwaka huu waliamua vingine.

Kura Unguja: (chaguzi tatu zilizopita; takwimu za Zec)
2005 CCM 64%; CUF 33%
2010 CCM 59.6%; CUF 39.6%
2015 CCM 57.8%; CUF 40.6%

Kura Pemba:
2005 CCM 24%; CUF 79%
2010 CCM 25.2%; CUF 72.5%
2015 CCM 18% ; CUF 80.9%

Mwaka huu Waunguja walibaki nyumbani kwa wingi kwa sababu walipungukiwa imani na CCM. Kwa upande mwingine, Wapemba walikwenda kupiga kura kwa mkururo.

Tangu 2005 kura za CUF zimekuwa zikipanda Unguja na zimebaki vile vile Pemba. Kura za CCM zilipanda Pemba 2010. Katika uchaguzi huo Wapemba walihisi walimpata Mpemba mwenzao, Shein, ndani ya CCM na wakampigia kura. Hata hivyo, 2015 walimwacha mkono Shein kwa sababu ya msimamo wake kuhusu Katiba.

Unguja kura za CCM zimekuwa zikipungua na za CUF zikipanda licha ya kuwa Unguja ndio kwenye ngome ya CCM. Sababu ni msimamo wa CUF kuhusu Katiba. Hakuna jengine.

\Na ukija uchaguzi mwingine na ukafanywa kwa haki kama huu kura za CCM Unguja na Pemba huenda zikazidi kupunguka. Hapo watamlaumu nani? CCM/Zanzibar ni mahodari wakulaumu na ndio maana halikuwa jambo la ajabu kwamba wameilazimisha Zec ijilaumu.

Shein anajuwa vilivyo kuwa yanayopitishwa na vichwa mchungu wa chama chake ni machafu lakini uchu wa utukufu unamfanya asione junaa kuchezea tope na kujiaibisha.

Akiamka, akilala, akila, akitia saini nyaraka za serikali, akipigiwa saluti, akiswali, atagubikwa na wingu la aibu. Aibu ya kumyang’anya ushindi aliyeshinda.

 

CHANZO: RAIA MWEMA

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s