Mgogoro Zanzibar wakwaza muungano

Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein (kushoto) na Makamu wake wa Kwanza, Maalim Seif Shariff Hamad
Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein (kushoto) na Makamu wake wa Kwanza, Maalim Seif Shariff Hamad

Kuendelea kwa sintofahamu baada ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kufutwa imeelezwa kusababisha mikwamo ya kisiasa, ikiwamo kushindwa kukamilika utimilifu wa Bunge na sura ya baraza la mawaziri.

Tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha afute uchaguzi huo Jumatano ya Oktoba 28, zimetimia siku 36, na bado kuna mvutano kati ya CCM na CUF. Upande wa CCM wanaunga mkono huo tamko la kurudiwa kwa uchaguzi wa rais, wawakilishi na madiwani visiwani humo huku upande wa CUF ukisisitiza usirudiwe.

Tayari Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na Maalim Seif Sharif Hamad wamekutana mara kadhaa kwa kinachoelezwa mazungumzo ya kutafuta suluhu.

Dk Yussuf Suleiman ambaye ni mwanataaluma na mwanadiplomasia aliyewahi kushika nafasi za uongozi katika visiwa vya Seychelles na Mauritania, alisema tatizo ni vyama kushindwa kuwandaa wafuasi wao kisaikolojia kuhusu kushindwa au kushinda.

“Iwapo mshindi wa urais wa Zanzibar alishajulikana kabla ya ZEC kusitisha sehemu ya matokeo yaliyosalia, bila shaka chama kilichoshindwa au mgombea aliyeshindwa imemuwia tabu kuwakabili wafuasi wake na sura ya kukubali kushindwa au kuachia madaraka,” alisema Dk Suleiman.

Kwa upande wake, Mwalimu Ahmed Omar, akizungumzia mkwamo huo wa kisiasa Zanzibar, alisema inawezekana utamu wa ving’ora unasababisha watu kujisahau madarakani na tabia hiyo imejengeka kwa baadhi ya viongozi wa nchi za Afrika.

“Utawala una ladha yake, lakini siyo busara kung’ang’ania madaraka hasa iwapo umeshindwa na ulimwengu ukashuhudia,” alisema Omar ambaye ni mwalimu mwenye uzoefu wa muda mrefu na mkazi wa Kibweni, Wilaya ya Magharibi A Unguja.

Hivi karibuni CCM kupitia msemaji wake Zanzibar, Naibu Katibu Mkuu, Vuai Ali Vuai, walisisitiza umuhimu wa chama chake kujiandaa na uchaguzi wa marudio, huku CUF kupitia kwa Kaimu Mkurugenzi wake wa Habari na Mahusiano na Umma, Ismail Jussa Ladhu ukishikilia msimamo kwamba kwa upande wao uchaguzi wa marudio ni mwiko, wanachohitaji ni ZEC kumtangaza mshindi na kumuapisha Maalim Seif.

Kwa upande mwingine timu ya kimataifa ya maadili iliyojumuisha maaskofu, wanasheria, wanadiplomasia, viongozi wa madhehebu mbalimbali wa kidini, wakiongozwa na Profesa Adou-Aliy Suleiman kutoka Nigeria, walikwenda Zanzibar hivi karibuni na walitembelea majimbo yote 54 ya Zanzibar na baadaye walikutana na Dk Shein.

Timu hiyo katika ripoti yake waliyoitoa hadharani walipinga uamuzi wa kurudia uchaguzi, wakihoji kwa kusema, “mshindi amejulikana, kwanini asitangazwe! Katiba ipo kwanini isiundwe Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama inavyoelekezwa?

“Uchaguzi wa marudio unatawaliwa na vitisho na matumizi ya jeshi na kuendelea hata dola kuwapigania walioshindwa au ikibidi kupelekea machafuko na mapigano,” ilisema taarifa ya viongozi hao wa dini.

Pia imeelezwa mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar, umekwamisha ukamilifu wa baadhi ya masuala mengine ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwamo ukamilifu wa Bunge linalohitaji kutimizwa na wajumbe watano kutoka Baraza la Wawakilishi ambalo kimsingi kwa sasa halipo.

Jambo lingine linaloelezwa ni tishio la wafadhili wa kimataifa wanaochangia Bajeti ya Serikali, pia sura ya Baraza la Mawaziri la Muungano ambalo Rais wa Zanzibar ni mjumbe wake kwa mujibu wa sheria.

Chanzo: Mwananchi

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s