Magufuli ana nguvu gani Zanzibar?

Magufuli
                                              Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli

Ahmed Rajab

KUNA msomaji wangu mmoja ambaye kwa muda mrefu nikifikiri ni mwanachuoni au, pengine, mhamiaji tu wa Tanzania anayeishi Afrika Kusini lakini mwenye shahada ya chuo kikuu. Sitolitaja jina lake kamili kwa vile sikumuomba ruhusa ya kufanya hivyo, lakini jina lake la mwanzo ni Hamidu.

Tumekuwa tukiandikiana kwa kipindi kirefu. Mara nyingi Hamidu amekuwa akiniandikia kutaka ufafanuzi wa mambo niliyokwishayaandika au hunidadisi kuhusu vipengele vya siasa na historia ya Afrika. Kutokana na maswali yake na mada anazozigusia ilinidhihirikia kwamba Hamidu ni mtu mwenye kufuatilia mambo kwa ukaribu sana.

Kadhalika, nilimuona kuwa ni mtu mwenye kipawa kikubwa cha kufahamu mambo, tena kwa haraka, na ni mwenye kutafakari kwa kina kabla ya kufikia maamuzi yake.

Siku moja, sijui ilinijia nini, kwa unyenyekevu nilimuuliza anafanya kazi gani Afrika ya Kusini. Jawabu yake kidogo ilinishangaza.

Ilinishangaza kwa sababu kama nilivyokwishagusia nikidhania kuwa yeye ni msomi wa chuo kikuu, kumbe alikuwa msomi wa aina yake. Wasomi wa aina hiyo aghalabu huwa ni wenye kuuona ukweli haraka kushinda wale wanaojidhania kuwa ni wasomi kwa kuwa wana shahada za vyuo vikuu.

Hamidu aliniambia kwamba yeye ni dereva tu wa masafa marefu ambaye, mara kwa mara, husafiri kutoka Tanzania hadi Afrika Kusini. Kuna nyakati ambapo hupiga kambi huko ugenini akijitafutia riziki kwa miezi kadhaa kabla hajarudi nyumbani.

Nilibahatika kukutana naye kwa mara ya mwanzo jijini Dar es Salaam miezi michache iliyopita na tulikuwa pamoja kwa siku mbili tatu. Kwa siku hizo chache nilijifunza mengi kutoka kwake.

Siku mbili baada ya kumalizika upigaji kura wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, Hamidu aliniandikia haya akiwa Dar es Salaam: “Tukiwa tunakaribia mwisho wa pilikapilika za uchaguzi wa mwaka huu, naomba nikiri kuna mambo makubwa mawili nimejifunza kutoka kwa wagombea wawili wenye upinzani wa hali ya juu kama ifuatavyo:-
“Edward Ngoyai Lowassa amenifundisha kutokata tamaa kwa kile ninachoona, ninachotamani au ninachokiamini kukifanya. Amenifanya niamini hata kama mlango mmoja utafungwa mwingine mzuri zaidi utafunguliwa.

“Pili, amenifundisha kujiandaa mapema kutimiza ndoto unayokuwa nayo kwenye maisha.Ikumbukwe alianza harakati za kwenda Ikulu tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990.

“Tatu, amenifundisha kuwa kukaa kimya ni busara zaidi hasa pale mambo mengi ambayo ukweli wake unahitaji muda yaweze kufahamika. Ni vigumu kuamini namna alivyoweza kubadilisha mawazo ya watu hasa wale waliokua wakimchukia.

“John Pombe Magufuli amenifundisha kufanya kazi kwa bidii muda wote. Kila unachopewa kifanye kwa akili na ubora wako wote. Kwa kufanya hivyo ipo siku sehemu kubwa ya watu wataona na wataweka tofauti zao pembeni na kutamani kukupa nafasi kubwa zaidi wakitumaini, kupitia wewe, malengo makubwa zaidi yatatimia…

Hii ndio sababu kwa sisi tuliobashiri mapema tulijua Bwana Pombe Magufuli angepitishwa na chama chake kule Dodoma.”
Nimekuwa nikiyatafakari sana maneno hayo ya Hamidu. Ni kweli kwamba Lowassa hajakata tamaa, yungali anaendelea na lengo lake.

Magufuli naye tangu aushike urais ameonyesha kwamba akitaka anaweza. Hatua chache alizozichukuwa hadi sasa zimewatia moyo wananchi kwamba uongozi wake ni uongozi wa aina mpya utaoweza kuzinyanyua hali zao.

Ili kutimiza lengo hilo haoni taabu kuzidokoa baadhi ya sera za upinzani na kuzifanya ziwe zake. Magufuli ana pupa ya kuonyesha kwamba anatenda haki na anawahudumia wananchi.

Wapo wenye kumkejeli wasemao kwamba nguvu alizozionyesha hadi sasa ni sawa na povu la soda.

Juu ya hayo, ni taabu kuipuuza, kwa mfano, hotuba aliyoitoa wakati wa ufunguzi wa Bunge la 11. Ilikuwa hotuba iliyowafanya wananchi waamini kwamba kweli serikali yake itawapatia matilaba yao.

Katika hotuba hiyo Magufuli aliugusia uchafu uliofanyika katika utawala wa awamu ya nne, uchafu ambao umeifikisha Tanzania hapa ilipo kiuchumi na kijamii.

Kwa kufanya hivyo, kama alivyokuwa akifanya wakati wa kampeni za uchaguzi, Magufuli amekuwa akijitenga na utendaji kazi wa serikali iliyopita. Wakati wa kampeni alikuwa akijitenga hata na chama chake mwenyewe, Chama cha Mapinduzi (CCM).

Magufuli aliahidi kulishughulikia tatizo la ulaji rushwa. Pia alisisitiza juu ya ukusanyaji wa kodi na aliahidi kwamba atahakikisha ya kuwa wamiliki wa viwanda vilivyobinafsishwa wanawajibika. Watakaoshindwa watapokonywa hivyo viwanda na watapewa wengine.

Mengine yaliyomfanya aonekane kama anajitenga na Kikwete ni ahadi alizozitoa za kupunguza idadi ya mawaziri katika Baraza la Mawaziri na, kadhalika, kuzipunguza safari za nje ya nchi za watendaji wa serikali. Wengi waliona kama anampiga kijembe Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliyekuwa hatulii nchini mara nyingi akiwa safarini nje ya nchi.

Masuala mengine mazito ni pamoja na mgogoro wa Zanzibar na Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Magufuli ameahidi kuyashughulikia yote hayo mawili. Ni matarajio ya wengi kuwa atayashughulikia bila ya utashi wa kichama.
Kwa kuizingatia kauli yake, “msema kweli ni mpenzi wa Mungu,” masikio ya Watanzania yatakuwa wazi kusikiliza kama kweli ahadi hizo zimetoka moyoni mwake.

Wakati wa hotuba yake, Kikwete alikuwa ameketi akimsikiliza aliyekuwa waziri wake na sasa kiongozi wake akiyachambua na kuyafichua maovu yaliyofanyika katika utawala wake.

Pengine Bwana Mkubwa wa awamu ya nne hakutegemea kuwa Magufuli angekwenda umbali huo wa kufanya kama anamkashifu hadharani. Bila shaka kuna watakaouliza, kwani yeye mwenyewe Magufuli si alikuwemo katika serikali ya Kikwete?
Ndio lakini labda Mafuguli huenda ikawa aliisoma namba. Alikwishatambua kwamba msamiati wa kukosoa na kujikosoa haumo ndani ya CCM. Magufuli si mjinga, alijuwa kwamba wakati haukuwa muwafaka.

Sasa hali imegeuka na inampa uwezo awe na ujasiri alionao kwa vile ndiye yeye mwenye kushika mpini.

Kwa sasa mtihani mkubwa unaomkabili Magufuli ni ule wa Zanzibar. Daima amekuwa akisisitiza kwamba amemtanguliza Mungu mbele na atawatendea haki wananchi wote bila ya upendeleo. Amejigamba kuwa yeye si mtu wa mzaha. Kama kauli hiyo ni ya kweli basi tutaraji mengi hasa tukizingatia kwamba alikula kiapo kizito alipokuwa anakabidhiwa urais.

Mpaka sasa viongozi wa CCM/Taifa wameonyesha makuruhu kila wanapotakiwa walitanzue tatizo la Zanzibar ambalo, kwa kweli, ni tatizo la wachache walio viongozi wenziwao huko Visiwani.

Tatizo la Zanzibar ni la mgogoro wa kikatiba uliozushwa na hatua ya Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), kuufuta Uchaguzi Mkuu wa Visiwani isipokuwa ule wa wabunge.

Ninaamini kwamba kwa dhati ya nafsi yake Magufuli anajuwa kwamba hatua ya Jecha ni ya kiharamia yenye kuipora demokrasia.

Ninaamini pia kwamba kwa vile anajigamba kwamba yeye ni mtu wa Mungu atataka kulitanzua tatizo hilo kwa njia za haki. Swali ni kuwa je, wahafidhina ndani ya CCM na ndani ya vyombo vya usalama watamruhusu?
Uhakika wa mambo ni kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar hakuna mtu binafsi, hata akiwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, mwenye uwezo wa kuzifusahi sheria za uchaguzi.

Kwa hivyo, Jecha hana uwezo wa kuutengua uchaguzi. Kitendo chake ni haramu, kinaweza hata kutafsiriwa kuwa ni cha uhaini. Katika hali kama hiyo, mtu kama huyo aliyehalifu sheria huchukuliwa hatua za kisheria.

Kabla ya hapo, kuna haja ya kufanywa uchunguzi rasmi kuhusu yanayodaiwa kutokea usiku ule Jecha alipoubatilisha uchaguzi. La kwanza kuchunguzwa ni hatua ya askari/wanajeshi walioingia Hoteli ya Bwawani ambamo Tume ya Uchaguzi ilikokuwa ikiendesha shughuli zake na kumchukuwa Jecha. Amri ile aliitoa nani na kwa sababu gani?
Ni wazi kwamba hapakuwa na kusukumana seuze mchafuko wowote ule. Tena kulikuwako mashahidi wa ndani ya nchi na waangalizi wa uchaguzi wa kigeni wanaoweza kuthibitisha yaliyotokea.

Mjadala ungali ukiendelea kuhusu hatua ya wabunge wa vyama vilivyo chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ya kufanya rabsha na sokomoko bungeni wakati Magufuli alipokuwa analifungua Bunge. Wabunge hao wakipinga kuwepo hapo kwa Dk. Ali Mohamed Shein, anayeshikilia kiti cha urais wa Zanzibar licha ya kuwa muda wake wa urais umeshamalizika.

Kuna wanaoipinga hatua hiyo ya wabunge wa Ukawa akiwemo Magufuli mwenyewe. Wao wanadai kwamba walichofanya wabunge hao kilikuwa kitendo cha aibu, hasa kwa kuwa walikifanya mbele ya wageni. Wanachosahau ni kwamba miongoni mwa hao wageni walikuwemo wanaokubaliana na Ukawa kwamba hatua ya Jecha si halali.

Kukiita kitendo hicho kuwa cha kihuni ni kujitoa kimasomaso, kwani aibu iliyosababishwa na Jecha ni kubwa zaidi. Ni aibu kwa ZEC, kwa Zanzibar na kwa Tanzania, kwa jumla, mbele ya macho ya ulimwengu.

Aibu ya kichekesho cha kuyapindua juu chini maamuzi ya walio wengi ni aibu kwa CCM kinachojinata kuwa ni chama chenye kuheshimu matakwa ya umma na misingi ya uhuru na haki. Aibu kubwa zaidi ni kwa Mwenyekiti wa CCM na viongozi wakuu wa Muungano waliokaa kimya.

Magufuli anawajibika kuwashurutisha wajumbe wa ZEC waiheshimu Katiba na warejee kukamilisha kazi iliyobaki ya kutoa matokeo yaliyosalia na kumtangaza mshindi wa uchaguzi wa urais wa Zanzibar. Akishindwa kufanya hivyo basi itathibitika kwamba vile viapo vya kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano ni mapambo na mbwembwe tu za kufungulia Bunge.

Raia Mwema

 

 

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s